Katika kazi yoyote inayofanywa na binadamu, kuna watu ambao wanafanikiwa na kuna wengine hawafanikiwi. Hata kwenye kazi ambazo zinapewa kipaombele cha mafanikio kama urubani, uanasheria, udaktari na nyinginezo kuna watu wanaofanikiwa na wengine wanakuwepo tu kusukuma siku. Pia kwenye kazi ambazo zinaonekana ni ngumu kufikia mafanikio kama biashara ndogo ndogo, kazi za usaidizi na nyinginezo bado kuna watu wanafanikiwa na wengine wanaenda wakilalamika maisha yao yote mpaka kufa.

  Ni kitu gani kinaleta utofauti huu wa mafanikio baina ya watu wanaofanya kazi ya aina moja?

kwa nini

  Tulishazungumza mengi sana yanayochangia mafanikio kwenye kazi yoyote inayofanyika na binadamu. Baadhi ya tuliyosema ni

1. Kufanya kazi kwa bidii na maarifa.

2. Kupenda unachofanya.

3. Kuwa na mipango madhubuti juu yamaisha yako na kazi zako.

4. Kutumia ubunifu na uwezo mkubwa ulioko ndani yako.

  Unaweza kuwa unafanya yote hayo lakini bado mafanikio yakawa magumu kwako kufikia. Pamoja na hayo yote kuna swali moja la msingi sana unalotakiwa kujiuliza na kujijibu kila siku kama kweli unataka kufanikiwa kwenye kitu unachofanya.

  Kwa kushindwa kujiuliza na kujibu swali hilo unajikuta unashindwa kutimiza hayo hapo juu ili kufanikiwa. Kama hujui swali hilo itakuwa vigumu kwako kufanya kazi kwa bidii na maarifa, kupenda unachofanya na hata kuweka mipango ya maisha yako kutakuwa kugumu.

  Swali muhimu unalotakiwa kujiuliza ni KWA NINI UNAFANYA UNACHOFANYA?

  Unaweza kuona ni swali rahisi ila ni swali la msingi sana kwenye maisha yako.

  Kila mtu anajua ni NINI ANAFANYA, na wengi wanajua ni JINSI GANI YA KUFANYA ila wachache sana wanajua KWA NINI WANAFANYA WANACHOFANYA.

  Wachache wanaojua kwa nini wanafanya wanachofanya ndio wanaofanikiwa kwenye chochote wanachoshika. Wengi wasiojua kwa nini wanafanya wanachofanya ndio wanaishia kuwasindikiza wengine huku wakilalamika kila siku ya maisha yao.

  Jiulize kwa nini leo umeamka kitandani na kwenye kwenye shughuli zako? Kwa nini uchoke kwa kazi na wakati mwingine unyanyaswe? Ni nini hasa kinakusukuma ufanye hicho unachofanya?

  Kama huwezi kujijibu swali hilo nasikitika kukuambia kwamba mafanikio kwako itakuwa ndoto.

  Kama sababu pekee iliyokufanya uende kwenye kazi zako leo ni kwa sababu jana ulienda, hakuna tofauti yoyote utakayoileta kwenye kazi yako. Utaishia kufanya uliyofanya jana na mafanikio yatakuwa magumu sana kwako.

  Kama jibu lako ni unafanya unachofanya ili kupata fedha bado upo katika hali mbaya kwa sababu hakuna mtu amewahi kuridhishwa na fedha, hivyo utajikuta kila siku unashindwa kufikia lengo ulilojiwekea(soma; kama unafanya ili upate fedha maisha yako yatakuwa magumu sana).

  Kama hujui kabisa kwa nini unafanya unachofanya unaweza kuchukua sababu moja kuu nitakayokushauri hapa na uangalie jinsi unavyoweza kuitumia kwenye kazi zako.

  Fanya kutoa huduma kwa watu, badili maisha ya watu kupitia kazi unayofanya. Saidia kuboresha maisha ya watu kwa kazi unazofanya. Amua kuleta mabadiliko kwenye jamii na hata dunia kwa ujumla kupitia kazi unayofanya. Amua kuwa mtu bora na mwenye mchango chanya wa maendeleo kwako mwenyewe na kwa watu wengine.

  Kama ukianza kutumia moja ya sababu hizo au nyingine yoyote ambayo unaona inakufaa kutokana na kazi zako utaanza kuona mabadiliko makubwa kwako binafsi, kazi zako na kwa wanaokuzunguka. Utapata mafanikio makubwa kwenye kazi zako na maisha kwa ujumla.