Makala iliyopita nilizungumzia sauti zilizopo ndani yetu ambazo zimekuwa zikitukatisha tamaa na kuturudisha nyuma.(kama hujaisoma isome hapa; ukiweza kushinda sauti yako ya ndani hakuna kitakachokushinda.). Uliona jinsi ambavyo sauti hii imekuzuia wewe kufanya mabadiliko makubwa na kuboresha maisha yako.

Kuacha sauti hii ya kukatisha tamaa iliyopo ndani yetu, kuna sauti nyingine pia ipo ndani yetu. Sauti hii inatuambia ni nini cha kufanya na kutupa moyo kuweza kufanya. Lakini kutokana na umaarufu ulioipa sauti inayokatisha tamaa, umeidharau kabisa sauti hii ya kukutia moyo.

         sikiliza

Leo tutazungumzia sauti iliyopo ndani yetu ambayo inatupa moyo kufanya mambo makubwa kwenye maisha yetu. Naomba usizichanganye sauti hizi mbili, kuna sauti inayokuambia nini cha kufanya na kukupa moyo na kuna sauti inakukatisha tamaa usifanye mabadiliko.

Mpaka hapo ulipo nina hakika kabisa kwamba unajua ni kitu gani unatakiwa kufanya ili ubadili maisha yako na ufanikiwe. Unajua kabisa kwamba kuna tabia unatakiwa kuziacha na kuna tabia nyingine mpya unatakiwa kujifunza. Na kama wewe umekuwa msomaji wa AMKA MTANZANIA kwa muda mrefu basi umeshajifunza vitu vingi sana ambavyo vinaweza kuyabadili maisha yako.

Pamoja na kujifunza yote hayo mbona maisha yako hayabadiliki? Mbona uko vile vile?

Katika jambo lolote unalofikiria au kujifunza ili liweze kuleta mabadiliko kwenye maisha yako ni lazima uchukue hatua na kuanza kufanya matendo. Na ili uweze kufanya matendo ni lazima ukubaliane na nafsi yako kwamba hiki ndicho utakachokwenda kufanya kwenye maisha yako. Kama ni hivyo tu vinavyotakiwa kwa nini hufanyi?

Sababu kubwa inayokufanya mpaka sasa hujachukua hatua ni kwa sababu hujisikilizi wewe mwenyewe. Kuna sauti inakupigia kelele kwamba sasa ni muda wa wewe kuboresha maisha yako. Kuna sauti inakuambia kila siku sasa ni muda wa kuanzisha biashara yako. Kwa nini unaipuuza hii sauti? Kama unashindwa kujisikiliza wewe mwenyewe unategemea ni nani atakayekusikiliza?

Kibaya zaidi unaacha kusikiliza sauti hii yenye manufaa na unaamua kufuata sauti ya kukatisha tamaa. Kwa wewe kupuuza sauti hii ya manufaa na kuchagua kusikiliza sauti ya kukatisha tamaa umekosa mambo makubwa sana kwenye maisha yako.

Kama ungekuwa unaisikiliza sauti hii ya kuleta mabadiliko na kukupa moyo ungekuwa umefanya mambo makubwa sana maishani mwako.

Hebu fikiri tokea ulipoanza kusema unaongeza kipato chako kwa kuanzisha au kukuza biashara yako kama ungeanza kipindi hiko leo ungekuwa wapi?

Hebu fikiri muda uliopita kwanzia ulipofikiri kuna haja ya wewe kuongeza ujuzi wako, kama ungefanya hivyo ungekuwa kwenye ngazi gani mpaka sasa?

Hebu fikiri tokea ulipopata wazo kwamba inabidi uboreshe mahusiano yako na familia yako na jamii nzima kama ungefanya ungekuwa umesaidia mambo gani?

Mambo yote haya mazuri ambayo uliyafikiri miaka miwili, mitano au kumi iliyopita kama ungeanza utekelezaji wake mara moja leo ungekuwa mbali sana. Huenda ulijipa sababu za kutokuyafanya wakati huo, je sasa huna sababu? Mara zote huwezi kukosa sababu kwa kuwa sababu nyingi unazojipa ni za uongo(bonyeza hapo kuzijua).

kitabu kava tangazo

Unalalamika kama watu hawakusikilizi unachosema? Unajisikia vibaya pale unapowaambia watu kitu ambacho ni kizuri lakini wao wanakipuuzia? Maumivu unayoyapata kwenye hali hii ndio nafsi yako inayapata, na ndio maana baada ya muda unashindwa kabisa kufanya jambo kubwa kwenye maisha yako.

Habari njema kwako.

Hujachelewa. Kama umekuwa ukiipuuza nafsi yako kwa muda mrefu leo acha kabisa huo mchezo. Fanyia kazi mawazo yote mazuri yanayokujia kuhusu kuboresha maisha yako. Sikiliza sauti zinazokupa moyo na kukuongoza kufanya mabadiliko kwenye maisha yako na zipuuze sauti ambazo zinakukatisha tamaa na kukurudisha nyuma kwenye maisha yako.

Wakati mwingine unapomwambia mtu kitu kizuri halafu akapuuza kabla ya kulalamika fikiria ni mara ngapi umeipuuza sauti ya kukupa moyo kutoka kwenye nafsi yako. Utaona kabisa huna haki ya kulaumu wale ambao hawakusikilizi kwa sababu hata wewe mwenyewe hujisikilizi.

Maisha ni ya kwako, mpaka sasa unajua nini cha kufanya na nini cha kuacha. Acha kupoteza muda na anza mara moja.