Wiki iliyopita kulitokea kitu ambacho kiliibua hisia za watu wengi sana. Idara ya uhamiaji iliita waombaji zaidi ya elfu kumi(10,000) kwenye usaili wa nafasi za ajira zipatazo sabini(70). Kutokana na wingi huu wa waombaji ilibidi zoezi la usaili lifanyike uwanja wa taifa.

Kitendo hiki kimeibua hisia za watu wengi sana na wengi kulaumu utaratibu huu mbovu wa kuita watu wengi ambao hawana uwezekano wa kupata kazi. Yaani uwezekano wa muombaji kupata kazi ni chini ya asilimia moja.

Kwa upande wangu badala ya kulalamikia swala hili nalipongeza kwa sababu litaleta mabadiliko kwenye vichwa vya watu wengi. Tatizo la ajira hapa Tanzania limekuwa sugu na linaendelea kukua kadiri siku zinavyokwenda. Pamoja na tatizo hili kukua bado hakuna hatua kubwa zinazochukuliwa na serikali, mamlaka husika na hata watafuta ajira wenyewe. Kwa utaratibu huu wa kuita maelfu kwenye uwanja utaweza wazi kwamba uwezekano wa kuajiriwa ni mdogo na hivyo baadhi ya waombaji wataangalia njia nyingine za kujipatia kipato. Pia mamlaka husika zitahamaki zaidi kutokana na mshtuko wa watu wengi linapotokea swala kama hili.

Nina imani kabisa ya kwamba katika watu elfu kumi waliohudhuria usaili ule zaidi ya mia moja wamekata shauri la kuacha kutegemea kuajiriwa na kuangalia njia nyingine za kupata kipato.

Katika barua hii ya wazi kwa wahitimu ambao bado wanazunguka na bahasha nitazungumzia mambo matano muhimu unayotakiwa kufanya au kujua ili kuweza kuvuka wakati huu mgumu kwenye maisha yako. Pia nitazungumzia aina tano za biashara unazoweza kuanza kufanya kwa mtaji kidogo na kuweza kujenga mafanikio makubwa.

Najaribu kukushauri baadhi ya hatua ambazo mimi nilipitia kipindi kidogo kilichopita na kuweza kutengeneza njia nyingine za kipato tofauti kabisa na ajira.

Kama unataka kufikiri zaidi na upo tayari kubadili mtazamo wako juu ya elimu na ajira nakukaribisha uendelee kusoma hapa na ujifunze machache.

Kama bado unaamini serikali inalo jukumu la kukuhakikishia wewe kupata ajira na unaendelea kuilaumu nakushauri uishie hapa na usiendelee kusoma kwa sababu utakereka na kushindwa kujifunza chochote.

kitabu kava tangazo

Nimewahi kuzungumzia mengi sana kuhusiana na kusoma na uhakika wa ajira. Soma makala; kabla hujaanza kuzunguka na bahasha soma hapa na utajifunza vingine vingi kuhusiana na soko hili la ajira.

Baadhi ya mambo muhimu sana unayotakiwa kujua wakati unaendelea kutafuta kazi ni haya hapa;

1. Tatizo la ajira ni tatizo la dunia nzima.

Kuanzia kuyumba kwa uchumi duniani mwaka 2008/2009 soko la ajira limeshafuka sana dunia nzima. Watu wengi walipoteza kazi zao na wengi hawajawahi kuzipata tena. Yaani idadi ya waliopunguzwa na kufukuzwa kazi wakati wa tikisiko la uchumi ni kubwa kuliko walioajiriwa baada ya pale. Hali hii imeleta tatizo kubwa sana kwenye ajira. Pia utumiaji mkubwa wa mashine kama kompyuta na maroboti umepunguza sana uhitaji wa rasilimali watu kwenye uzalishaji. Japo haya hayajafika kwetu moja kwa moja ila yapo njiani yanakuja hivyo hali inazidi kuwa mbaya.

2. Mwezi ujao wanaingia wengine zaidi elfu arobaini.

Kama vile idadi ya wahitimu wanaotafuta ajira haitoshi mwezi ujao vyuo vingi wanafunzi wanahitimu masomo yao hivyo soko la ajira linategemea kupokea waska ajira wengie zaidi ya elfu arobaini. Hii inazidi kufanya hali iwe mbaya na uwezekano wa kuajiriwa kuzidi kuwa mdogo.

3. Mfumo wa elimu ni mbovu, umekuharibu.

Mpaka sasa umeshajua ya kwamba mfumo wetu wa elimu ni mbovu sana na umekuandaa wewe kuajiriwa wakati ajira hazipatikani. Baada ya kujua haya unafanya nini? Unaendelea kukaa na kulaumu mfumo huu wa elimu au unaangalia mpango mwingine wa kuboresha maisha yako?

4. Muda unakwenda kasi sana na kazi zimekuwa na thamani ndogo.

Inawezekana umeshakaa nyumbani zaidi ya mwaka mmoja ukifanya maombi ya kazi sehemu mbalimbali. Na kama bado hujazinduka unaweza kukaa mwaka mwingine tena na tena huku ukiamini siku moja mambo yatakuwa mazuri. Yanaweza kuwa mazuri kweli ila muda uliopoteza haulingani kabisa na kitu ulichokuwa unasubiri. Ajira zimekuwa na thamani ndogo sana siku hizi ukilinganisha na zamani. Kazi zimewachosha wengi na hazina hamasa kubwa. Wengi wa walioko kwenye ajira wanafanya kila juhudi waweze kuondoka na kwenda kujiajiri.

5. Chagua moja sasa.

Baada ya yote haya na usumbufu wote ulioupata kwa kuhangaika kutafuta kazi umefika wakati sasa wa wewe kufanya maamuzi. Chagua moja kati ya haya mawili; kuendelea kulaumu na kulalamika kusoma kwako ila unakosa ajira au kuamia kuchukua hatua ya kujiajiri wewe mwenyewe.

Unayo kila haki ya kulaumu serikali na mamlaka husika kwa kila kinachoendelea, lakini je pamoja na kulaumu ni hatua gani unaona zinachukuliwa? Kama unalaumu na hakuna hatua zinazochukuliwa unachukua hatua gani juu ya maisha yako?

Mwisho wa siku hautaitwa shujaa kwa kulalamika bali utaitwa shujaa pale utakapoweza kusimamia na kuboresha maisha yako hata kama hujapata nafasi ya kuajiriwa.

Kama unaendelea kualumi serikali na mamlaka nyingine nakuomba uishie hapa kwa sababu nitakayokwenda kuandika hapa chini yanaweza yasiwe na maana kwako. Kama unaona umefika wakati wa wewe kuchukua mustakabali wa maisha yako nakusihi uendelee kusoma na uchague kitu cha kufanya kati ya hivi nitakavyoshauri hapa chini.

Unaweza kuanzia wapi katika safari ya kujiajiri au kufanya biashara?

Najua kabisa ya kwamba nikikuambia fanya biashara au jiajiri cha kwanza utakachoniambia ni nitapata wapi mtaji? Sina dhamana ya mkopo na maneno mengine mengi. Lakini nilichojifunza kutokana na majibu hayo ni kwamba ni njia ambayo wengi wetu tunaitumia kama sababu ya sisi kutokutaka kuchukua hatua.

Hapa nitapendekeza biashara au shughuli ambazo unaweza kuanza na mtaji kidogo sana na ukaendelea kuukuza mpaka kufikia kuweza kufanya biashara kubwa. Sehemu kubwa ya mafanikio kwenye biashara hizi itatokana na juhudi zako wewe binafsi. Kama bado utanihoji mtaji huu kidogo utaupata wapi nakushauri ufikiri kwa kina na uangalia kila kona ya maisha yako hutakosa fedha kidogo za kuanza biashara hizi.

Biashara au kazi ninazopendekeza ni zifuatazo;

1. Kilimo na ufugaji wa kisasa.

Kilimo na ufugaji ni sehemu nzuri sana ya wewe kuanza kwa mtaji kidogo. Kama upo maeneo ya shamba au kijijini unaweza kupata eneo zuri sana ambalo utafanya kilimo au ufugaji wa kisasa ambao utakuwa na tija. Kwa elimu uliyopata unaweza kuendelea kujifunza mbinu bora zaidi za kuboresha kilimo au ufugaji wako. Kama upo mjini unaweza kutafuta maeneo ya nje ya mji kidogo na kuanza kufanya shughuli hizi.

Kuna changamoto kubwa sana kwenye kilimo na ufugaji ila haimaanishi unashindwa kufanya. Kila kitu kina changamoto, hivyo usiweke changamoto kama kizuizi cha wewe kufanya bali weka changamoto kama kitu cha kukufanya ufikiri zaidi. Upatikanaji wa maji, magonjwa ya mimea na mifugo ni vitu ambavyo unatakiwa kuwa makini navyo la sivyo vitakurudisha nyuma.

Kuna wasomi wenzako wengi sana ambao wamejiajiri katika kilimo na maisha yao yanakwenda vizuri sana. Kama upo tayari kufanya kilimo cha kisasa wasiliana na mimi na nitakuunganisha na watu hawa ili uweze kujifunza zaidi.

2. Fanya biashara ya mtandao.

Biashara ya mtandao(network marketing) ni biashara ambayo unaweza kuanza na mtaji kidogo sana ila baada ya muda ukatengeneza biashara kubwa sana yenye kipato kikubwa na faida kubwa. Biashara hii inahitaji juhudi zako na kujifunza kwako ili uweze kufanikiwa. Hakuna kikomo cha kiwango cha fedha unachotakiwa kutengeneza na hakuna gharama za kuendesha biashara unazotakiwa kulipa.

Kwa mfano kama una mtaji kidogo na unapanga kuanza kufanya biashara inabidi ulipe pango la chumba cha biashara kwa miezi sita au mwaka, inabidi ulipie leseni ya biashara, inabidi ulipie kodi kabla hata hujaanza biashara. Kwa vitu hivyo tu tayari umekwishatumia zaidi ta tsh milioni moja ili kuweza kuanza biashara eneo zuri. Hapo bado hujanunua vitu vya biashara husika. Ila unapojiunga na kampuni zinazofanya biashara kwa njia ya mtandao unaweza kufanya biashara kubwa bila ya kuweka gharama zote hizo.

ANGALIZO; Kuna watu wengi sana watakukatisha tamaa na kukuaminishwa kushindwa kwenye biashara hizi. Kama unataka kuzifanya nakushauri sana upate maelezo sahihi kutoka kwa wanaofanya au usome vitabu vilivypchammbua aina hii ya biashara. Kwa sababu wewe ni msomi unaweza kufanya maamuzi sahihi baada ya kupata maelezo yote hayo. Kuna wahitimu wengi ambao wanafanya biashara hii na wana mafanikio makubwa. Kama unataka kujua zaidi kuhusu biashara hii wasiliana na mimi na nitakuunganisha na mtu anayefanya biashara hii na atakuelekeza vizuri kisha utafanya maamuzi wewe mwenyewe.

3. Ujasiriamili wa Taarifa.

Hii ni aina ya ujasiriamali ambapo unakuwa unatoa huduma ya taarifa. Unatafuta na kutoa taarifa muhimu ambazo watu wako tayari kulipa fedha ili kuzipata. Biashara hii unaweza kuianza bure kabisa kama tayari una kompyuta yako uliyokuwa unatumia chuoni. Au kama huna unaweza kununua kompyuta ya bei ndogo na kuanza ujasiriamali huu. Hii ni biashara ambayo mimi nimeifanya kwa kuanza na mtaji sifuri ila sasa imefikia kuwa na kipato kikubwa sana. Unachohitaji kwenye ujasiriamali huu ni wewe kuwa na kiu ya kujifunza na kuwashirikisha wengine taarifa ambazo zitarahisisha au kuboresha maisha yao.

Kama taarifa hizo zitaweza kufikia vigezo hivyo watu watakuwa tayari kukulipa ili wapate taarifa zaidi kutoka kwako.

Kama utapenda kujua zaidi kuhusu aina hii ya ujasiriamali tafadhali wasiliana na mimi na nitakupa maelezo zaidi.

4. Biashara ya uchuuzi.

Kama unaona aina hizo hapo juu za biashara haziendani na malengo yako au mitazamo yako kimaisha unaweza kuanza kuingia kwenye biashara kwa kufanya uchuuzi. Kwa uchuuzi hapa namaanisha kununua vitu kwa bei ndogo na kuviuza kwa bei kubwa kidogo itakayokutengenezea wewe faida. Angalia ni kitu gani watu wanakosa kwenye eneo unaloishi na angalia jinsi unavyoweza kukipata na kuwapatia kwa bei ambayo wanaweza kumudu na wewe unaweza kupata faida.

5. Endeleza vipaji vyako.

Kuna vipaji vingi ambavyo unavyo na kama ukiweza kuviendeleza unaweza kutengeneza biashara kubwa sana. Unaweza kuwa muimbaji mzuri, mwandishi mzuri, mbunifu na mengine mengi. Angalia jinsi unavyoweza kutumia vipaji ulivyonavyo kutengeneza kipato na kuweza kujiajiri.

Kama mpaka sasa hujajua vipaji vyako soma hapa na utajua jinsi ya kutambua vipaji vyako.

Umefika wakati wa wewe kuchukua hatua juu ya maisha yako, weka kulalamika pembeni na anza kuyakabili maisha yako. Zipo njia nyingi sana za wewe kuweza kutengeneza kipato hata kama hujapata nafasi ya kuajiriwa.

Kikubwa unachohitaji ni kupenda kile ulichachagua kufanya na kuwa na juhudi kubwa kwenye kukifanya. Pia kuwa na ubunifu mkubwa na fanya kazi kwa juhudi na maarifa. Itakuchukua muda kidogo kuanza kuona matunda katika njia hizi nilizoshauri hapa ila utakapoanza kufaidi matunda haya utafurahi sana kukosa ajira kwa sababu utaona tofauti kuwa ya maisha yako na ya wenzako ambao wameajiriwa. Utaona maisha yako yakiwa bora na ukiwa na uhuru mkubwa wa maisha yako kushinda mtu ambaye ameajiriwa na kufanywa kuwa mtumwa wa kutengeneza ndoto za wengine.

Mambo haya ninayokuandikia hapa nina uhakika yanawezekana kwa sababu yamewezekana kwangu na kwa watu wangu wa karibu. Nakupa nafasi hii ya kujifunza kutoka kwangu na kwa wengine ambao wapo tayari kushirikiana na wewe. Kwa mawasiliano zaidi tafadhali nitafute kwa simu 0717396253 au email amakirita@gmail.com Ukiandika email itapendeza zaidi na uniambie ni kipi ulichochagua kufanya.

Nakutakia kila la kheri na nakupa moyo kwamba yote yanawezekana hata kama hukupata ajira.

TUKO PAMOJA.