Wiki iliyopita nilipata nafasi ya kwenda Mafinga Iringa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kampuni ya MATANANA INVESTMENT. Nikiwa huko Mafinga nilipata nafasi ya kukutana na John Matiku Magori, ambaye ni msomaji na mchangiaji mzuri wa makala kwenye AMKA MTANZANIA.

Nimekuwa nikiwasiliana na kushirikiana na John kwa muda mrefu ila wakati huu ndio nilipata nafasi nzuri ya kuzungumza nae kuhusu kile anachokifanya. John ni mmoja wa vijana wa kitanzania ambao wamefanya mambo makubwa sana kwa wakati mfupi.

Mwaka 2011, John aliingia Mafinga na kuanza biashara kwa mtaji wa tsh milioni nne na laki sita(4,600,000/=), na mpaka kufikia sasa biashara yake ina mtaji wa zaidi ya milioni mia moja.

magori2(picha; nikiwa na John nyumbani kwake Mafinga)

John aliwezaje kufikia mafanikio haya makubwa?

Hapa John atatueleza kwa kifupi historia ya maisha yake na kwenye makala nyingine zijazo atatushirikisha njia alizotumia kuweza kufikia mafanikio hayo makubwa na pia atatushirikisha changamoto alizokutana nazo na jinsi gani aliweza kuzikabili.

John anatokea musoma ambapo alizaliwa tarehe 23/03/1988 na kupata elimu ya msingi. Baada ya kumaliza elimu ya msingi hakuweza kupata nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari kutokana na hali ngumu ya kifamilia kwa wakati huo. Mwaka 2004 akiwa na miaka 16 John aliamua kwenda Mwanza ambapo hakujua anakwenda kufanya nini. Alipofika mwanza alifanya kazi ya umachinga kwa miaka mitatu(2004-2006). Kazi hii ya umachinga ilikuwa ngumu sana kwake na hakuweza kupata fedha za kutosheleza kujikimu, hivyo aliamua kurudi nyumbani na kwenda kufanya kilimo na ufugaji.

Akiwa nyumbani Musoma alipewa taarifa kwamba kuna mtu alikuwa anatafuta mfanyakazi wa dukani mkoani Mbeya. John alikubali kwenda mbeya kufanya kazi hiyo na tarehe 17/07/2007 alisafiri kwenda mbeya na alipofika alipewa majukumu ya kazi atakayofanya. Aliambiwa atalipwa mshahara wa tsh elfu arobaini(40,000/=) kwa mwezi. John alikubali mshahara huu kidogo na kujitoa kufanya kazi ile kwa moyo mmoja.

Wakati anafanya kazi hii John alijiwekea malengo ya kuifanya kwa miaka mitano na baada ya hapo aweze na yeye kuanzisha biashara yake. Kutokana na lengo hili John alijibana na kuwa na matumizi kidogo sana ya fedha zake ili aweze kuweka akiba itakayomsaidia kufikia lengo lake.

Mwaka 2011(kabla hata ya miaka mitano kufika) John aliomba kuacha kazi ili aweze kwenda kuanzisha biashara yake mwenyewe. Wakati huo mshahara wake ulikuwa umefikia tsh 350,000/=, watu wengi ikiwemo ndugu zake walimshangaa anawezaje kuacha kazi hiyo inayomlipa vizuri ukizingatia kwamba ana elimu ya msingi tu. John hakuzingatia hayo kwa sababu alikuwa anajua malengo makubwa aliyojiwekea na alijua bila ya kuyatekeleza hataweza kupata uhuru aliokuwa anategemea.

Mwaka huo 2011 alifika Mafinga akiwa na fedha taslimu 4,600,000/=. Hakuwa na ndugu yeyote hapo Mafinga na hivyo alitegemea fedha hii kwenye kuishi pamoja na kuanzisha biashara. Baada ya kuzunguka na kutafuta alifanikiwa kupata eneo la biashara ambalo pia ilimlazimu kulifanyia marekebisho hivyo akaanza biashara kwa kununua mali za duka zenye thamani ya milioni mbili. Biashara aliyoanza na ambayo mpaka sasa anafanya ni ya kuuza vifaa vya ndani kama tv, magodoro na vifaa vingine vya kielektroniki.

magori(picha;wiki ya kwanza ya biashara)

Mwanzo biashara ilikuwa ngumu sana na kwa wiki moja ahakuweza kufanya mauzo kabisa. Hii ilimsukuma kubadili mawazo yake ya ufanyaji wa biashara na kuweka ubunifu zaidi. Ubunifu alioweka ulimpatia wateja wengi sana ambao mpaka sasa anauhusiano mzuri na wamemletea wateja wengi zaidi. Ubunifu mkubwa aliofanya ni kukopesha bidhaa zake kwa makubaliano na pia kujenga urafiki mkubwa na wateja wake.

Kwa miaka hii mitatu John ameweza kufikia mafanikio makubwa kwani sasa ana maduka mawili, duka jingine liko Mkuranga, nje kidogo ya Dar es salaam na ameajiri vijana sita. Pia ameweza kununua nyumba ya kuishi huko Mafinga, ameweza kununua gari la biashara na biashara yake kwa sasa ina mtaji wa zaidi ya milioni mia moja.

Kuna mengi sana utaendelea kujifunza kwa John kwenye makala atakazoendelea kutushirikisha hapa AMKA MTANZANIA.

Mambo makubwa ambayo nataka ujifunze kupitia hadithi hii ya John ni haya;

1. John aliweka malengo makubwa ambayo alifikiri njia za kuyafikia kila siku. Hakuwahi kujishusha na kuona haiwezekani kufikia malengo yake.

2. John alikubali kuanzia chini ili kujifunza na kukua. Najua utakuwa umevutiwa na kutoka milioni 4 mpaka milioni 100 kwa miaka mitatu, ila habari haianzii hapo. Vitu vilivyomwezesha John kupata mafanikio haya ya sasa ni elimu ya biashara aliyoipata wakati anafanya umachinga na wakati ameajiriwa.

3. Licha ya mshahara kidogo, John alipenda kazi aliyokuwa anafanya. Ni muhimu sana kupenda kile unachofanya, kwa njia hii ndio unaweza kujifunza na kukua zaidi.

4. John aliweza kuwa na udhubutu wa kuacha kazi ambayo ilionekana kuwa inalipa kulingana na hali yake na badala yake kwenda kuanza biashara kwenye eneo ambalo hana uzoefu wala ndugu.

Kuna mambo mengi sana ambayo kila mtanzania anaweza kujifunza hapa. Na kama mpaka sasa unalalamika maisha yako ni magumu basi jua umejiamulia mwenyewe. John hakuwa na vitu ambavyo wewe unalalamika huna. Hakuwa na elimu kubwa, hakuwa na ndugu aliyempa mtaji wa kuanzia biashara. Alikubali kufanya kazi kwa mshahara kidogo sana ila akiwa na lengo lake ambalo baadae limefanikiwa.

Ni kipi kinakuzuia wewe? Elimu? Mtaji? Au hujaamua? Jibu moja naloweza kukupa ambalo unaweza kulikataa ni kwamba hujaamua. Kwa mambo mengi ambayo umejifunza kwenye AMKA MTANZANIA kama utaamua kuyatumia sasa utafikia mafanikio makuwa sana.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia MAFANIKIO MAKUBWA SANA. Karibu sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA ambapo utajifunza kila kitu unachotakiwa kujua ili kufikia mafanikio makubwa.

TUKO PAMOJA.

KAMA NA WEWE UNA KITU KIZURI CHA KUTUSHIRIKISHA WATANZANIA ILI TUWEZE KUBORESHA MAISHABYETU ZAIDI TAFADHALI WASILIANA NAMI KWA 0717396253/amakirita@gmail.com