Katika wiki mbili zilizopita tuliona uhusiano kati ya uchawi na mafanikio na pia kwa nini waganga wanaweza kuwasaidia wengine kuwa matajiri wakati wao ni masikini. Katika makala hizi tuliona ni jinsi gani hata wewe unaweza kutumia mbinu hizo za kisaikolojia bila hata ya kuwa mchawi na ukaweza kufikia mafanikio makubwa. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hizo bonyeza hizo link kuzisoma.

mganga1

Leo tutajadili kwa nini watanzania wengi wanaamini uchawi unaleta mafanikio. Kwa nini tunashuhudia mauaji ya vikongwe na albino yakiendelea? Kwa nini kila siku tunaona mabango ya waganga wakijinadi kuweza kuwapatia watu utajiri na bahati? Na kwa nini kwenye jamii kila anayeonekana kuwa na mafanikio makubwa anaambiwa ni freemason?

Kuna sababu kubwa tano zinazosababisha watu wengi kuamini kwenye uchawi na ushirikina.

1. Mila na desturi.

Katika makabila mengi ya kitanzania kwa muda mrefu kumekuwa na mila ambazo watu hufanya ibada tambiko. Pia makabila mengine yana asili ya imani hizi za uchawi hivyo mtu anaingiziwa mawazo haya tangu akiwa mtoto mdogo na anakua akiamini hivyo.

2. Ukosefu wa elimu.

Kukosa elimu hasa ya kujitambua kumewafanya watu wengi kuendelea kuwa na imani hizi potofu. Kuna watu wenye elimu za vyuo vikuu ila bado wanakwenda kwa waganga wapate mafanikio. Watu hawa wamekosa imani ya kujitambua wao wenyewe na kuweza kutumia uwezo mkubwa ulioko ndani yao. Hii inawafanya watu kuwa watumwa wa imani hizi za kishirikina.

3. Hali ngumu ya uchumu na kukosa matumaini.

Kutokana na hali ngumu ya uchumi watu wengi wamekuwa wako tayari kufanya chochote kinachowezekana wapate fedha. Na pia kutokana na wananchi kukosa matumaini ya kwamba wanaweza kupata mafanikio kama watafanya kwa bidii na maarifa imefanya watu wengi kuamini imani hizi ndio msaada kwao.

4. Kukosa nidhamu binafsi.

Hili ndio tatizo kubwa kuliko yote. Watu wengi sana wamekosa nidhamu binafsi na hivyo kushindwa kujiongoza na kuvumilia vikwazo ili kufikia mafanikio. Ndio maana wanapokwenda kwa waganga na kupewa masharti huyaamini ni ya kweli na kushindwa kuelewa kwamba wanatengenezewa nidhamu binafsi ambayo wangeweza kutengeneza wenyewe.

5. Hadithi za mitaani na vijiweni.

Kitu kingine kikubwa kinachofanya watu wengi waamini imani hizi za kishirikina ni hadithi nyingi ambazo zimekuwa zinasambaa mitaani. Hadithi hizi zinaweza kuwa zimetengenezwa au mtu kazipata kutokan na ugonjwa na watu kuzipokea na kuendelea kuzisambaza. Kwa mfano kuna hizi habari za freemason, tumeona zikipewa nafasi hata kwenye vyombo vya habari. Ni habari za upotoshaji ila zinaendelea kusambaa. Mfano mwingine ni zile hadithi za kupokea kwa mfano mtu anakuambia huko sumbawanga kuna mwewe wanabeba ng’ombe. Asilimia kubwa sana ya watu wanaamini hivyo japokuwa hawajawahi kuona. Au mtu anakuambia Kigoma mtu anaweza kukutumia radi, kitu ambacho sio kweli bali mazingira ndio yanayochangia.

Ufanye nini ili uweze kufikia mafanikio makubwa bila ya kutumia uchawi.

Kwanza inawezekana kabisa kufikia mafanikio makubwa bila ya kutumia uchawi au kwenda kwa waganga. Fanya mambo haya sita na utafikia mafanikio makubwa;

1. Tambua kwamba una uwezo mkubwa sana ulioko ndani yako. Na hujaweza hata kutumia robo ya uwezo huo. Wewe ni wa pekee na una ubunifu na vipaji vingi sana. Vijue na uanze kuvitumia kufikia mafanikio makubwa.

2. Weka malengo na mipango ya maisha yako na ni mafanikio gani unataka kufikia.

3. Jifunze kila siku kuhusiana na kile unachofanya. Pia soma sana vitabu mbalimbali vya kukuhamasisha na kukuongezea ujuzi.

4. Fanya kazi kwa juhudi na maarifa. Tumia akili nyingi sana unapofanya kazi yako na pia fanya kazi zaidi ya watu wengine. Kama unategemea kuanza kazi saa mbili asubuhi na kumaliza saa kumi jioni baada ya hapo unapoteza tu muda sahau kitu kinaitwa MAFANIKIO MAKUBWA, utaendelea kusukuma tu siku.

5. Jenga nidhamu binafsi. Hii ndio itakayokuwezesha wewe kuendelea kusonga mbele hata kama mambo yamekuwa magumu. Kuwa na nidhamu binafsi ndio ucawi wako mkuu utakaokupatoa chochote unachotaka kwenye maisha yako.

6. Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Kisima cha maarifa ndio kitakuwa kama mganga wako kwani humo utajifunza kila kitu unachotakiwa kujua kuhusu kufikia mafanikio makubwa. Kupata maelezo ya JINSI YA KUJIUNGA NA KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi.

Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa. Najua unaweza na kama ukizingatia haya utafikia mafanikio makubwa sana.

TUKO PAMOJA.