Moja ya sababu kubwa ambayo watu wengi husema kwamba inawazuia kufanya biashara ni mtaji. Mimi huwa nakataa sana sababu hii kwa sababu haiwezekani leo huna mtaji, mwaka kesho huna mtaji na hata miaka mitano ijayo huna mtaji. Nasema mtaji ni kigezo tu ambacho watu wengi hutumia kuficha sababu halisi ya kutokuingia kwenye biashara ambayo ni kutokujipanga na kutokuwa tayari.

Leo nakushirikisha siri moja ambayo itakuwezesha kufikia mafanikio makubwa sana japo utaanza kidogo. Kupitia siri hii unaweza kuanza na tsh elfu moja na baadae ukapata mtaji ambao utakuwezesha kufanya biashara kubwa. Pia tutaangalia kama ukianza na kiasi kikubwa kidogo itakavyokuwa bora zaidi.

ANGALIZO; Mambo utakayoyasoma hapa yatabadili kabisa maisha yako kama ukiyatumia. Ila kama utayasoma na kupita utaendelea kuwa na maisha magumu huku ukilalamika bila ya msaada wowote. Hivyo chukua hatua, huu ndio ukombozi wako.

Siri kubwa nitakayoizungumzia hapa ni kuweka akiba kidogo kidogo kila siku na kwa muda mrefu ili kuweza kuondoka kwenye tatizo la fedha uliloko nalo sasa. Na akiba hii hitaiweka benki ambako utawafaidisha sana na hela yako kuliwa na mfumuko wa bei, bali utaiweka kwenye mfuko wa dhamana ambao una uhakika wa kukua kwa asilimia sio chini ya kumi kwa mwaka. Mfano wa mfuko wa dhamana ni Umoja Fund wa UTT(Unit Trust of Tanzania) maarufu kama mfuko wa umoja au vipande vya umoja.

Kupitia mfuko huu unanunua vipande ambavyo vinakua kwa thamani kadiri muda unavyokwenda. Kwa mwaka vinakua sio chini ya asilimia kumi na mara nyingi inakuwa zaidi ya hapo. Hivyo hii ni njia nzuri sana ya wewe kukuza mtaji wako hata kama unaanzia sifuri.

Sasa tuone maajabu ya kuweka fedha kwa muda mrefu.

1. Kama utaanza kuweka tsh elfu moja kwa siku.

Naamini kama unasoma hapa huwezi kukosa tsh elfu moja kila siku. Hata uwe ni mmachinga, mama ntilie, au mpiga debe unaweza kupata tsh elfu moja kila siku. Usiidharau elfu moja hiyo maana ni njia yako ya kuelekea kwenye utajiri.

Kama kila siku utaweka tsh elfu moja, kwa mwezi itakuwa tsh elfu 30, kwa mwaka itakuwa tsh 360,000/=. Kama utaweka fedha hii kwenye mfuko unaokua kwa asilimia 10 kwa mwaka, kwa miaka mitano itakuwa tsh 2,997,403.20 hii ni sawa na tsh milioni tatu. Hiki ni kiasi ambacho huenda hujawahi kukipata kutoka kwenye vyanzo vyako mwenyewe ndani ya miaka mitano iliyopita.

Kama utaweka elfu moja hiyo kila siku kwa miaka kumi itakuwa tsh 7,244,967.43, milioni saba ni fedha ambayo huenda hujawahi kuota kuishika.

Kama bado ni kijana na ukaiweka fedha hii kwa miaka 20 itakuwa tsh 25,102,799.78(milioni 25) na ukiiweka kwa miaka 30 itakuwa tsh 71,421,417.80(milioni 71). Yaani kama wewe una miaka 35 au chini ya hapo, kama utaanza kuweka tsh elfu moja kila siku na ukaiweka fedha hii kwenye mfuko wa umoja utakapokuwa na miaka 60 utakuwa na tsh milioni sabini.

compound

2. Kama utaanza na tsh elfu hamsini kwa mwezi.

Kama unafanya kazi ila una mshahara kidogo sana bado unaweza kujikusanya na kupata mtaji wa kutosha kukuondoa hapo ulipo. Kwa mfano kama mshahara wako uko kati ya laki mbili mpaka laki tano, kwa njia yoyote ile unaweza kujikaza na ukaweka pembeni tsh elfu 50 kila mwezi. Kama fedha hii utaiweka kwenye mfuko wa umoja, kwa miaka mitano itakuwa tsh 4,995,672.00(milioni 5), miaka kumi tsh 12,074,945.71, miaka 20 tsh 41,837,999.64 na miaka 30 tsh 119,035,696.34. Milioni tano kwa miaka mitano, 12 kwa miaka kumi, 41 kwa miaka 20 na 119 kwa miaka 30 ni fedha ambazo unaweza kuanzia nazo na ukafanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.

3. Kama utaanza na laki moja kwa mwezi.

Kama unafanya kazi na mshahara wako ni kati ya laki tano na milioni moja kwa mwezi, unaweza kujibana na kuweka pembeni tsh laki moja kila mwezi. Kama utaiweka fedha hii kwenye mfuko wa umoja unaokua kwa asilimia 10 kwa mwaka mambo yatakuwa hivi; Miaka mitano tsh 9,991,344.00(milioni 10), miaka 10 tsh 24,149,891.43, miaka 20 tsh 83,675,999.27 na miaka 30 tsh 238,071,392.67. Milioni kumi kwa miaka 5, 24 kwa miaka 10, 83 kwa miaka 20 na hata milioni mia mbili na arobaini kwa miaka 30 ni fedha ambayo inaweza kubadili kabisa maisha yako kama utaanza kuweka tsh laki moja kila mwezi.

Hii ndio siri kubwa ninayokushirikisha leo na kama utaanza kuitumia leo, namaanisha leo hii utaona mabadiliko makubwa sana. Kama usipoitumia naomba unitafute tarehe 10/10/2019 (miaka mitano ijayo) na uniambie ni kipi kikubwa ulichofanya. Miaka mitano sio mingi kabisa rafiki yangu, kama unafikiri ni mingi kumbuka ni lini ulifanya uchaguzi mkuu na mwaka kesho ni uchaguzi mwingine.

Hoja yangu kubwa ni kwamba kama umeweza kuteseka kwenye kazi kwa miaka zaidi ya kumi na huoni mabadiliko makubwa kwa nini usijipe miaka kitano tu au kumi tu na uweke kiasi fulani cha akiba na baada ya hapo upate mtaji wa kuanzia?

Na katika miaka hii mitano au kumi ambayo mtaji wako unakua na unaendelea kuuweka, jifunze kuhusu biashara unayotaka kufanya. Jifunze kwa kujisomea, jifunze kwa kufanya utafiti na pia jifunze kwa kufanya kazi inayohusiana na biashara unayotaka kuja kufanya. Kama kila siku kwamiaka motano au kumi utajifunza kuhusiana na kitu unachotaka kufanya utaona fursa nyingi sana za wewe kutoka.

Uanzie wapi?

1. Leo hii nenda katika ofisi za UTT(kama upo dar nenda sukari house ghorofa ya kwanza, unaweza kutembelea tovuti yao http://www.uttamis.co.tz), jiandikishe kuwa mwanachama na watakupa utaratibu wa kuwa unatuma fedha zako hata kwa mpesa, hivyo huna haja ya kwenda benk au ofisini kila mara. Ukisema unasubiri jumatatu au mwisho wa mwezi tayari fursa hii imekupita, na miaka mitano ijayo utajuta sana.

2. Baada ya hapo weka tsh elfu moja pembeni kila siku, unaweza kuwa unaiweka kwenye mpesa halafu kila mwisho wa mwezi unatuma UTT tsh elfu 30. Pia unaweza kutuma zaidi ya hapo kulingana na mipango yako, hiyo 30 kwa mwezi ni kiwango cha chini ambacho kila mtu ambaye yuko makini na maisha yake anaweza kukiweka. Kama unataka kuweka kiwango tofauti na nilivyotumia hapo juu au kwa miaka tofauti bonyeza maandishi haya na utakuta fomula niliyotumia.

3. Wakati unaendelea kuweka fedha hizi na kuzikuza endelea kujifunza kuhusiana na biashara unayotaka kufanya, Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA, hili ni kundi muhimu kwa watu wote wanaotaka kupiga hatua kwenye maisha na kufikia mafanikio makubwa. Ndani ya kundi hili utajifunza mengi kuhusu BIASHARA, MAFANIKIO, FEDHA NA UWEKEZAJI. Kujiunga bonyeza maandishi haya kupata maelekezo.

Chukua hatua sasa hivi, kama unafikiri haiwezekani kaendelee kulalamika. Kama umechoka kulalamika huu ndio wakati wa kushika hatamu ya maisha yako.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.

TUKO PAMOJA.

kitabu-kava-tangazo432