Kuna wakati huwa inatokea tunajikuta tukiwa kwenye hali ambayo kwa ujumla hatuipendi. Tunajikuta tukiwa hatuna furaha, tumepumbaa na tunahisi mambo Fulani kutokuwa mazuri mahali, ingawa hatuyajui. kwa kawaida huwa tunasema leo niko hovyohovyo, sijui naumwa au vipi. Na huwa hatelewi tunafanye nini tunakuwa tupo tupo tu ili mradi.

Kuna wengine wanapokuwa kwenye hali kama hiyo, kama ni asubuhi, huanza kufikiri, au wamejenga kuamini kwamba, huenda siku haitakuwa nzuri, kutakuwa na matatizo huko mbele, kwa wengine inakuwa tu ni kero. Kujihisi vibaya, kuhisi kama vile kuna jambo Fulani linatokea au limetokea na linakera ni hali ambayo kwa kiasi Fulani, inaweza kuwa taarifa ya mambo mabaya baadae.

Kwa wale wenye nguvu za ziada, kuna uwezekano wa siku hiyo kutokuwa nzuri kwao au kwa watu waliokaribu yao. Kuna watu ambao, kama litatokea jambo baya muda mfupi ujao, huanza kujihisi hovyo, kujihisi vibaya na kukera bila sababu ya msingi. Kama  wameshabaini kwamba, hali hiyo kwao ina maana ya kutokea jambo baya, hukereka zaidi.

Hukereka zaidi kwa sababu, pamoja na kujua litatokea jambo baya, huwa hawajui ni jambo gani. Lakini kwa waliowengi hali hii hutokea kufuatia kupata taarifa, kuona jambo au kuhisi kutokea kwa jambo baya, ambavyo huwakera. Lakini kwa bahati mbaya, kupata taarifa, kuona au kuhisi jambo, ni vitu ambavyo vinakuwa haviko wazi wazi kwao.

Mara nyingi kujisikia vibaya kihisia ni matokeo ya kuchokozeka kwa hisia zetu bila wenyewe kujua ni nini kilichozichokoza. Hebu fikiria kwamba, biashara yako ni juisi na siku hiyo asubuhi mawingu yametanda na dalili ya mvua kubwa iko wazi. Inaweza ikatokea ukajikuta tu unajihisi vibaya.(Unaweza ukasoma pia Jinsi Unavyoweza Kuendelea Kuwa Na Hamasa Kubwa Kila Siku)

Ni vigumu mara nyingi kujua kwamba unajihisi vibaya kwa sababu ya hali ya hewa, kwa sababu ya hofu kwamba, hutaweza kuuza juisi. Wakati mwingine tunajihisi hovyo asubuhi kutokana na ndoto tulizoota usiku, ingawa tunaweza tusingamue jambo hilo kwa kirahisi. Kuna ndoto ambazo hututisha, hutukera au kutusumbua sana usingizini.

Ndoto hizo,  tunapoamka asubuhi tunakuwa tumezisahau, ingawa athari zake kwenye mfumo wetu wa kufikiri bado zinakuwepo. Tunaweza kutwa nzima tukajihisi hovyo tu kwa sababu ya ndoto tu. Mpaka hapo unaweza ukaona kuwa suala la kujisikia vibaya huwa linakuja tu bila sisi kujijua, ingawa huwa zipo sababu zinazosababisha itokee hivyo.

Inashauriwa kwamba, kama mtu anajihisi hovyohovyo au anajisikia vibaya bila kujua sababu zake, ni vizuri atulie na kuanza kujiuliza kuhusu mambo ambayo amekutana nayo kwa siku hiyo. Inawezekana ikawa ni ndoto, kwa hiyo ajiulize kuhusu alichoota usiku uliopita pia. Pengine inaweza ikawa mtu jana yake alikukera, hilo nalo unapaswa kujiuliza.

Kwa kujiuliza mambo ambayo tumekutana nayo, iwe watu, iwe hali ya hewa, iwe kauli Fulani, iwe tukio Fulani, hiyo inaweza ikatusaidia kubaini ni kwa nini tunajihisi vibaya. Tunachotakiwa kujua ni kwamba, kujihisi kwetu vibaya bila kujua sababu, ni matokeo ya hali zinazoenda nje au ndani mwetu na kwamba, tunaweza kuzigundua tukianza kufuatilia.

Tukigundua kile kinachotufanya sisi tujisikie vibaya ni rahisi kukikabili na kukishinda. Ukiweza kujua sababu ya nini kinachokufanya ujisikie vibaya, hiyo itakusaidia wewe kutokujiuliza maswali mengi kichwani kwako ya ‘kwa nini leo niko hovyohovyo au kwa nini sijisikii vizuri’, kwani utakuwa unajua kwa sehemu hasa sababu au chanzo ninini.

Nakutakia maisha mema yenye furaha tele, karibu sana katika mtandao huu wa AMKA MTANZANIA, uendelee kujifunza vitu vitakavyobadilisha maisha yako kabisa.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.

IMANI NGWANGWALU