Ilikuwa miezi kumi na mbili, ukaiona mingi sana, na ukapanga kufanya mambo mengi sana. Sasa yamebaki masaa machache kabla ya mwaka huu 2014 kuisha. Ni jambo la kushukuru sana kwa mpaka sasa kuwepo hai na kuweza kuendelea na malengo na mipango yako. Hata kama malengo uliyojiwekea yote yameshindikana kwa asilimia 100, yaani hujafanikisha chochote bado una mambo mawili makubwa ya kufurahia.

Jambo la kwanza, upo hai. Sio wote walioanza mwaka huu wameweza kuiona siku ya leo, wakati wewe unasoma hapa kuna mwenzako anakata roho. Hivyo ni jambo la kushukuru na kufurahia uwepo wako mpaka leo hii.

Jambo la pili umejifunza mengi kutokana na kushindwa kwako. Kama umeshindwa maana sasa umeshajua ni njia ipi inaleta majibu mazuri na ni njia ipi inaleta majibu mabaya. Kama unaendelea kuchukulia kushindwa kwako kama kisirani au bahati mbaya unakosa somo zuri sana. Hivyo furahia kwamba mwaka huu umepata nafasi ya kujifunza mengi kupitia yale uliyoshindwa na hata yale uliyofanikiwa.

Baada ya kukumbushana hayo machache ya muhimu sasa tuzungumze kubwa kabisa unalotakiwa kulifanya kwenye masaa haya machache yaliyobakia. Kuna mambo unatakiwa uyaache kabisa kabla hujaingia mwaka 2015, yaani usipoyaacha unakwenda kuwa na mwaka wa kawaida utakaokuletea majibu ya kawaidia na maisha yako kuendelea kuwa kawaida. Sio vibaya kuwa kawaida ila wewe una uwezo mkubwa wa kufanya zaidi ya unavyofanya sasa, una uwezo mkubwa wa kufanikiwa zaidi ya ulivyofanikiwa sasa. Ila kuna mambo umeyang’ang’ania ambayo yanakuzuia wewe kufikia viwango vikubwa unavyoweza kufikia.

Mambo hayo kumi unayotakiwa kuyaacha kabisa ni haya yafuatayo;

1. Acha kujidanganya.

Umekuwa ukijidanganya kila siku na kila mara kwamba kinachokuzuia wewe kufanikiwa ni kwa kuwa huna mtaji wa kuanza, au huna mtaji wa kutosha, au huna elimu ya kutosha au huna mtandao wa kutosha. Hizi zote ni njia ambazo umekuwa unatumia kuepuka kubadili maisha yako. Ndio unaweza kuwa huna mtaji lakini ni jitihada gani umezifanya za kuhakikisha unapata mahali pa kuanzia? Au unakaa ukisubiri kuna mtu atakuletea mtaji. Ndio kazi yako inaweza kuwa inakupa msongo wa mawazo kila siku, kazi nyingi na kipato kidogo, lakini je ni jitihada gani ambazo umezifanya mpaka sasa? Acha kujidanganya, chukua hatua.

2. Acha kukwepa majukumu yako.

Maisha yako yako chini yako, usifikiri kuna mtu atakuja kubadili maisha yako. Usifikiri serikali, au bosi au ndugu yako atakuja kubadili maisha yako. Maisha yako yako chini yako na wewe ndio unaweza kuyabadili. Unapokwepa majukumu na kusema maisha yako ni magumu kwa sababu serikali haijakujali unajidanganya wewe mwenyewe. Mwaka 2015 kubali jukumu kubwa la kuboresha maisha yako, na fanya kazi kwa bidii na maarifa huku ukiendelea kujifunza kila siku ili uweze kuboresha maisha yako.

3. Acha mahusiano yanayokurudisha nyuma.

Tulishajadili tena hapa ya kwamba maisha yako ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka. Hivyo mahusiano uliyoendekeza mpaka sasa yanaweza kuwa ni sumu kubwa sana kwa mafanikio yako. Una marafiki zako ambao kila ukiwapa mipango yako mikubwa wanakwambia huwezi, acha kujisumbua, kula maisha na mengine mengi. Hawa ni wa kuwaacha kabisa mwaka 2015, usiwaache kwa ugomvi, ila kwa nia njema tu ya maendeleo ya maisha yako. Endelea kuwaendekeza na utaishia kuwa na maisha ambayo huyapendi.

Karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA upate nafasi ya kuzungukwa na watu ambao wana mtizamo chanya na wana kiu kubwa ya kuboresha maisha yao.

4. Acha hasira, kinyongo.

Kuna mtu amekutapeli au amekusababishia hasara, una haki kabisa ya kukasirika na hata kumwekea kinyongo. Ila unafikiri ni nani anayeumia kwa hasira yako na kinyongo chako? Mzazi wako alikukataa, alikutesa, alikutelekeza, hakukujali, una haki kabisa ya kuwa na hasira nae na hata kuwa na kinyongo. Lakini unafikiri ni nani anayeumia kwenye kinyongo hiki?

Ukweli ni kwamba wewe mwenyewe ndiye unayeumia, unapokuwa na hasira na unapoweka kinyongo inakuzuia katika sehemu nyingi sana kwenye maisha yako. Achana na hasira, achana na vinyongo, msamehe kila aliyekukosea kwa njia moja au nyingine na kazana kuboresha maisha yako.

5. Acha uvivu.

Makirita, mimi sio mvivu, naenda kazini kila siku, nafanya kazi mda mrefu na narudi nyumbani nimechoka. Najitahidi sana, lakini basi tu mambo hayaendi. Mambo kutokwenda ndio yanadhibitisha uvivu wako. Kuenda kazini na kufanya kazi siku nzima haikufanyi wewe kuwa sio mvivu. Unafanyaje kazi zako? Unazifanya kwa kiwango gani? Je una kiu ya kuwa tofauti, kuwa mbunifu? Kama unafanya kazi kidogo, mara unaanza kupiga soga, mara unapiga simu, au unajibu meseji, au unajibu email, mara unaingia facebook, unatoka hapo unapitia kidogo instagram, halafu unarudi jioni umechoka kumbe nusu ya muda wako wa kazi ulikuwa unaruka ruka kufanya mambo ambayo hayana uzalishaji kwako. Mwaka 2015 acha uvivu, fanya kazi kwa juhudi na maarifa ili uweze kuboresha maisha yako, hakikisha kazi yako inaonekana ni ya tofauti na ya kipekee, hata kama unafanya kazi ya kuosha vyombo, kuna njia nyingi za kujitofautisha.

6. Acha kupoteza muda wako.

Hapa sitaandika sana maana niliyoandika hapo kwenye namba tano yanaingia hapa moja kwa moja. Naomba niongeze sentensi mbili tu;

i/. Muda una thamani kubwa kuliko fedha, unaweza kupata fedha zaidi lakini huwezi kupata muda zaidi, yaani ukipoteza fedha unaweza kutengeneza nyingine, ukipoteza muda ndio umeupoteza moja kwa moja, hutakuja kuupata tena.

ii/. Binadamu wote tuna muda sawa, yaani kila mtu ana masaa 24 kwa siku, lakini kwa masaa haya haya wengine wanafanikiwa wengine wanaishia kusukuma maisha. Sasa fanya hizi 2015, kila baada ya saa moja simama na ujiulize, je hiki ninachofanya sasa kinaendana na malengo yangu? Kitafanya maisha yangu kuwa bora zaidi? Kama jibu ni hapana, kiache mara moja na fanya kile ambacho unapaswa kuwa unafanya. Usipoteze hata dakila moja ya maisha yako, utajutia sana baadae.

7. Acha tabia ya kuahirisha mambo.

Nitafanya kesho. Ngoja mambo yakiwa mazuri nitafanya hivyo. Ngoja matatizo niliyonayo yakiisha nitaanza biashara. Ukweli ni kwamba keho haitafika, maana kesho nayo ina kesho yake, mambo hayatakuwa mazuri na wala matatizo uliyonayo hayataisha, yakiisha hayo yanaanza mengine.

Kama kuna kitu chochote unachotaka kufanya fanya sasa, la sivyo hutokifanya milele na unapoteza nafasi ya wewe kuboresha maisha yako. Yale yote uliyopanga kufanya mwaka 2014 na ukashindwa kufanya unafikiri ni nini kilisababisha? Tabia ya kuahirisha mambo, ulisema ngoja january ipite, januari ni ngumu sana ikapita, ukasema mwezi wa pili bado haujachangamka sana nao ukapita, ukasema sasa ngoja pasaka ipite, ikipita tu naanza, ikapita, ukasema pasaka imesisha ila mambo hayajakaa vizuri. Umeendelea kujidanganya mpaka leo unasema ngoja mwaka uishe 2015 ikianza tu na mimi naanza. Kwa bahati mbaya sana unaweza usianze.

Anza sasa, NIKE wanasema JUST DO IT, hii iwe ndio kauli mbiu yako mwaka 2015.

8. Acha kutumia maneno hasi.

Maneno yanaumba, unalijua hili ila hulifanyii kazi.

Siwezi kufanya kitu fulani, Kila ninachofanya nashindwa, Nilijua tu nitashindwa, Kila nikifanya biashara na watu wananidhulumu, Huu ni mwaka wa shetani. Yote haya ni maneno hasi ambayo umekuwa unajiambia kila mwaka. Sasa usiyapeleke maneno haya 2015, utaendelea kuteseka maisha yako yote. Kama kuna kitu huwezi kufanya, jifunze jinsi ya kukifanya.

9. Acha kufanya mambo ili kuonekana.

Tunaishi kwenye jamii ambayo tunalazimika kufanya mambo kwa sababu kila mtu anafanya. Au ili tuonekane na sisi tupo.

Unanunua gari kwa sababu marafiki zako wana magari, unanunua simu toleo jipya kwa sababu watu wengine wananunua. Unanunua nguo fulani kwa sababu ndio fasheni mpya na kila mtu ananunua.

Mwaka 2015 acha kabisa kufanya mambo ili uonekane, fanya mambo kutimiza malengo na mipango yako. Acha kukimbizana na matoleo mapya ya simu, acha kukimbizana na matoleo mapya ya nguo, kimbizana na jinsi ya kukuza kazi yako au biashara yako, kimbizana kuboresha maisha yako.

10. Acha kufikiri kwamba furaha inatokana na vitu au watu.

Nikipata mume/mke anayenipenda nitakuwa na furaha, sio kweli.

Nikipata watoto wenye tabia nzuri nitakuwa na furaha, sio kweli.

Nikiongezwa mshahara na nikanunua gari ninalolipenda nitakuwa na furaha, sio kweli.

Kama unafikiri nakudanganya, subiri mpaka upate vitu hivyo ndio utajua kwamba furaha haitokani na watu au vitu badi inatoka ndani yako mwenyewe.

Nyongeza; ACHA KUTAKA KUBADILISHA WATU, BADILIKA WEWE.

Ukitaka kuwabadilisha watu utachoka sana na hawatabadilika, anza kubadilika wewe na wao watabadilika.

2015 ndio hii hapa imeshakaribia kabisa, acha mambo hayo ili uweze kuwa na maisha bora kuanzia 2015 na kuendelea.

Kujifunza mengi zaidi kuhusu kuufanya mwaka 2015 kuwa bora kwako jiunge na semina ya siku 21 itakayofanyika kwa njia ya mtandao ambapo kila siku utatumiwa email ya mafunzo. Imebaki siku moja tu ya kuweza kujiunga, changamkia nafasi hii sasa maana hutoipata tena kwa mwaka 2015. Kujiunga tuma fedha tsh elfu 10 na utume jina na email yako kwenye namba 0717396253/0755952887.

Nakutakia kila la kheri kwenye masaa machache yaliyobakia na kwa mwaka ujao 2015.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

kitabu-kava-tangazo4322