Watu wengi sana, au tunaweza kusema kila mtu anapenda kuwa na maisha bora. Hatua yoyote ambayo mtu anachukua ni kwa sababu anafikiri maisha yake yatakuwa bora zaidi kwa yeye kuchukua hatua hiyo kuliko kutokuchukua hatua.

Tunafahamu kwamba ili uweze kupata matokeo ya tofauti na unayopata sana ni lazima ubadilike. Lazima kuna vitu utakavyohitajika kubadili kwenye maisha yako ili yawe tofauti na yalivyo sasa.

Tunajua pia kuboresha maisha na kufikia mafanikio kunaanza na mtu mwenyewe. Kama mtu hatokubali ndani ya nafsi yake kwamba yupo tayari kubadilika na kuboresha maisha yake hakuna kinachoweza kumbadili mtu huyo. Na mafanikio yoyote yanaanza na mabadiliko kwenye maisha ya mtu.

Kwa hiyo ni rahisi, kama unataka kuwa na mafanikio, boresha maisha yako kwa kubadilika. Sasa kama ni rahisi hivi kwa nini watu wengi hawawezi kufanya hivyo? Kwa nini watu wengi hawawezi kubadilika na hatimaye kufikia mafanikio?

Jibu ni moja tu, watu wanabaka mabadiliko, hawaendi hatua kwa hatua, wanaparamia kubadilika na mwishowe wanashindwa kuendelea na mabadiliko waliyotaka yatokee kwenye maisha yao. Ndio maana mwanzoni mwa mwaka watu huweka malengo mengi sana ya mabadiliko, lakini muda mchache baadae wanarudi kwenye maisha yao ya kawaida.

SOMA; KAWAIDA Ni Tafsida Ya HOVYO…

Leo tutajadili hatua sita muhimu za wewe kuweza kubadili maisha yako na kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kwa kufuata hatua hizi utaweza kuona mabadiliko ya kweli kwenye maisha yako.

HATUA YA KWANZA; Unapobadili mawazo yako unabadili imani yako.

Kila kitu kwenye maisha yako kinaanza na mawazo unayoweka kwenye akili yako kwa muda mrefu. Matokeo unayopata sasa ni zao la mawazo yako, hivyo kama unataka kupata matokeo tofauti ni lazima uanze kubadili mawazo unayoweka kwenye akili yako. Unapoweka mawazo kwenye akili yako kwa muda mrefu, taratibu yanaanz akujenga imani. Kama kila mara utakuwa unawaza kushindwa tu, utaanz akuwa na imani kwamba wewe ni mtu wa kushindwa.

SOMA; Fikra TANO Zinazoua Mafanikio Na Jinsi Ya Kuziepuka.

HATUA YA PILI; Unapobadili Imani yako/zako unabadili matarajio yako.

Kila kitu tunachokifanya kwenye maisha tunakifanya kutokana na matarajio tuliyonayo. uUnafanya kitu kwa sababu unatarajia kupata majibu ambayo yatafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Ili kubadili na kuboresha maisha yako unahitaji kuwa na matarajio bora. Na matarajio haya bora yanatokana na imani ambayo unayo. Kama imani yako ni kwamba wewe ni mtu wa kushindwa, unavisirani, au bahati mbaya, jambo lolote unalokuwa unafanya utatarajia kupata matokeo yanayoendana na imani yako hiyo. Kwa upande mwingine kamaunaamini wewe ni mtu wa kushinda, utatarajia kupata ushindi kwenye kile aunachofanya.

HATUA YA TATU; Unapobadili matarajio yako unabadili mtizamo wako.

Mtizamo wako unatokana na kile unachotarajia.Kama unatarajia kushinda, kufanikiwa, kuwa bora utakuwa na mtizamo chanya ambao utakusukuma wewe kuweza kufanya vizuri zaidi. Kama unatarajia mikosi, balaa, visirani utakuwa na mtizamo hasi ambao utaendelea kukuletea mambo haya kila mara. Mtizamo wako ni muhimu sana kwani huu ndio utakaokuwezesha wewe kuziona na kuzitumia fursa mbalimbali zinazokuzunguka. Na kama mtizamo wako sio sahihi basi utashindwa kuziona fursa hizo muhimu sana kwako.

SOMA; UKURASA WA 10; Umetengeneza Ulimwengu Wako Mwenyewe.

HATUA YA NNE; Unapobadili mtizamo wako unabadili tabia yako.

Hii ndio sehemu ambayo watu wengi hurukua wanapotaka kubadili maisha yao. Hufikiri waishabadili tabia tu, mambo yamekwisha. Hii sio kweli kwa sababu hatua hizo tatu zilizopita ni muhimu sana kwenye kuweza kubadili na kutengeneza tabia ambayo itadumu. Unapokuwa na mtizamo sahihi hata tabia zako zinaendana na mtizamo ulionao. Na tabia zako ndio zinachangia asilimia 90 ya mafanikio yako kwenye maisha. Unafanya unachofanya sasa kutokana na tabia ulizojijengea tokea zamani. Tabia zako kwenye fedha, nidhamu binafsi, kuchapa kazi, ubunifu zote hizi zinaweza kuwa bora kama utakuwa na mawazo mazuri, imani sahihi na mtizamo mzuri.

HATUA YA TANO; Unapobadili tabia zako unabadili utendaji wako.

Kama una tabia ya kutokupenda kujituma, ukiibadili ni nini kitatokea? Kujituma.

Kama una tabia ya matumizi mabaya ya fedha ukiibadili ni nini kitatokea? Kuondokana na matatizo ya fedha.

Kwa vyovyote vile unapobadili tabia yako, moja kwa moja utendaji wako nao unabadilika. Na unapobadilisha utendaji ndio unaelekea kwenye mafanikio makubwa.

SOMA; Fanya Mambo Haya Matatu Na Usipokuwa Tajiri Ndani ya miaka 10, sahau kuhusu utajiri kwenye maisha yako.

HATUA YA SITA; Unapobadili utendaji wako, unabadili maisha yako.

Utendaji wako, uzalishaji wako ndio utakaobadili maisha yako. Kwa kuongeza tu ufanisi wenyewe sio rahisi kubadili maisha yako. Ndio maana kuna watu ambao wanafanya kazi kwa juhudi na maarifa sana ila bado maisha yao ni magumu sana. Hii ni kwa sababu wanakuwa hawajapitia hatua nyingine muhimu za kuleta mabadiliko ya kweli kwenye maisha yao.

Hizi ndio hatua sita muhimu za kubadili maisha yako na kuweza kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha.

Kama kweli unataka kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yako, usiruke hatua hata moja. Kwa sababu hatua hizi sita muhimu zinategemeana sana. Mawazo yako, imani yako, matarajio yako, tabia yako, utendaji wako vyote vinahitaji kuwa kwenye mrengo mmoja ili maisha yako yaweze kubadilika na kuwa bora zaidi.

Nakutakia kila la kheri katika mabadiliko ya maisha yako.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

kitabu-kava-tangazo4322