Ndugu msomaji wa JIONGEZE UFAHAMU ni siku nyingine tena nzuri aliyoipanga mwenyezi Mungu kutukutanisha pamoja katika makala hii ili tuweze kujifunza pamoja. Wahenga walisema elimu ni kama bahari na haina mwisho. Hakuna hata mtu mmoja ambaye ataweza kujua kila kitu mpaka kufikia mwisho wa maisha yake kwani duniani na hata nje ya dunia kuna mambo mengi ya kujifunza. Hii ni fursa nyingine ambayo unapata kuisikia sauti yangu ikiongea na wewe kupitia maandishi haya. Ni matumaini yangu unaendelea kujifunza kila siku na ndiyo maana huwa napata mrejesho (feedback) kutoka kwenu kupitia simu na barua pepe. Niwashukuru sana kwani mnanipa nguvu ya kuendelea kuwapa makala nzuri na za kufundisha. Pia usisite kutembelea mtandao wa Life Adventures kwa mambo mengine mazuri kwako.
Baada ya utangulizi huu mfupi nipende kuanza moja kwa moja kwa kueleza kuhusu maisha yetu ya hapa duniani. Ni ukweli usiofichika kwamba kila mtu anahitaji watu. Huwezi kuishi bila watu. Kuna wakati unakutana na mtu haelewani na asilimia kubwa ya watu na kujiuliza tatizo ni nini, ni ule msemo kwamba ana damu ya kunguni au lah! Ukweli ni kwamba kuna tabia huwa zinatatiza mahusiano baina ya watu. Baadhi ya tabia hizo nimejaribu kuzieleza hapa chini. Twende sasa
1.     Usiwe mwepesi wa kukosoa, kulalamika au kulaumu
Ndugu msomaji wangu najua utakubaliana na mimi kuwa hakuna binadamu aliyekamilika na kila  mtu ana udhaifu wake. Kwa kujua hilo hata wewe mkosoaji una mapungufu na madhaifu yako pengine makubwa kuliko yeye. Usijaribu kutoa kibanzi kwenye jicho la mwenzako na wakati huo kwako kuna boriti. Usiwe wa kwanza kurusha jiwe kwa mwenzako kwa sababu tu makosa yake yamewekwa hadharani ili hali ya kwako yakipata nafasi ya kujulikana utatamani ardhi ipasuke uingie. Pia usiwe mtu wa kulalamika na kulaumu kwa kila kila kitu hata ambayo wewe ndiye msababishi. Usiwe mtu wa kukashifu na kutoa maneno ya ovyo. Beba msalaba wako mwenyewe na uupeleke Goligotha, acha kuhukumu, kukosoa na hata kulaumu wengine. Amini usiamini hakuna mtu anayependa mtu mwenye tabia hizo na mara nyingi watu wa hiyo huogopwa na kukwepwa kama ukoma.  Kama mtu kakosea tafuta namna ya kumwambia makosa yake naye kama ni muungwana atakuelewa.
2.     Toa pongezi za dhati
Kila mtu huhitaji pongezi pale anapofanya kazi nzuri. Mathalani nimpongeze Makirita Amani, Deogratius Kessy, Esther Ngullwa, Goodluck Moshi, Beatrice, Mahundi, Daudi na waandishi wengine wa JIONGEZE UFAHAMU nitakuwa natoa pongezi za dhati kutoka moyoni. Kumbuka ninaposema pongezi za dhati namaanisha zile pongezi ambazo kweli zinatoka moyoni mwa mtu na si zile za kumvisha mtu sifa zisizofaa ambazo waswahili wana msemo wao wa ‘’Kuvika kilemba cha ukoka’’ au ‘’kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa. Naamini waandishi hawa ni mahiri na hivyo hawataona kama nawasifia bure. Pia usisahau kuwa pongezi za kinafiki hazisaidii ila kama umedhamiria kutoa pongezi zitoe moyoni hata kama huyo mtu humkubali lakini jaribu kuikubali kazi yake. Kwa jinsi hii utaweza kukaa na kila mtu na kuishi vizuri na watu na hata kupunguza idadi ya maadui na kuongeza marafiki. Faida ya marafiki nilishaiandika siku za nyuma, kama hujaisoma Makala hiyo usisite kutembelea Life Adventures.
3.      Toa msaada kwa watu wengine kufikia malengo yao
Kila mtu duniani ni msafiri na katika safari yake anategemea kufika kituoni siku moja. Kwa kuwa njiani kuna dhoruba nyingi huhitaji msaada wa watu wengine. Kama wewe ndiye uliyefikwa na wajibu huo usisite kutoa msaada. Mtu anayesaidia wengine huwa na mahusiano mazuri na watu na hata yeye kusaidiwa pale anapopata majanga. Kumbuka msaada mzuri ni ule unaoutoa bila kutegemea malipo yoyote, na kama unataka kusaidia basi msaidie yule ambaye unajua hana uwezo wala jinsi ya kukulipa. Hii itakupa faraja na utajenga jina lako na wasifu wako kwa watu. Neno msaada lina maana pana sana, linaanzia katika vitu mpaka hali. Kuanzia hela, ushauri, kufundisha, kuelimisha na mambo yanayofanana na hayo.
4.     Toa faraja kwa watu
Kuwa mtu mwenye kufariji na kutia moyo wengine. Usiwe mtu mwenye kukatisha tamaa watu wengine.  Usiwe mtu wa kuumiza mioyo ya watu wengine, usiwe mtu wa kunyooshewa vidole kila kona kwamba una hasara nyingi kuliko faida. Kuna msemo unasema kama huwezi kuwapa faraja kwa watu basi usiwaumize. Kama mtu amekuambia jambo na unaona huwezi kumshauri au kumpa faraja yoyote ni bora umpe pole na ujiondokee zako na si kumuumiza kwa kumwambia maneno yenye kujeruhi. Kumbuka kuwa ukisha sema neno halirudi tena kinywani, hivyo basi fikiria kwanza kabla ya kuongea na pia jaribu kuvaa uhusika wa unayemwambia. Kumbuka watu wengi wamekuwa wakijiua kila siku kwa kukosa faraja na maelfu wakiokolewa kutoka kifo kwa faraja tu. Nenda na kauli mbiu hii ‘’Toa faraja, okoa maisha na jenga undugu’’
Ni faraja yangu kuwa umefika mwisho wa Makala hii, ni matumaini yangu kuwa utafanyia kazi kila nililoandika hapa mtandaoni. Yatakuwa ni masikitiko kwangu kama umesoma mpaka hapa halafu ukashindwa kubadilika kwani utakuwa umepoteza muda wako, muda wangu na hata gharama zako kusoma Makala hii. Naamini wewe ni wa tofauti na utabadilika kuanzia sasa.
Nikutakie siku njema yenye mafanikio tele.
Makala hii imeandikwa na Nickson Yohanes Unaweza kuwasiliana na nae kwa kwa: simu: 0712 843030/0753 843030 e-mail: nmyohanes@gmail.com
Pia unaweza kutembelea blog yake:  www.lifeadventurestz.blogspot.comkujifunza zaidi.