Habari rafiki, ni matumaini yangu waendelea vizuri. Wiki hii tunaendelea na utaratibu wetu wa kushirikishana mambo 20 niliyojifunza kwenye kitabu. Leo tunaangazia kitabu kinachoitwa THE SECRET CODE OF SUCCESS . Kitabu kimeandikwa na mwandishi anaitwa NOAH ST. JOHN. Kitabu kinazungumzia mambo mengi sana kuhusu mafanikio, na ni moja ya vitabu vya tofauti sana na vingine. Kwa kweli kitabu hiki kinatoa changamoto za hali ya juu. Hata kama umesoma vitabu zaidi ya 100 ukikutana na kitabu hiki lazima uanze kufikiri upya kwa kweli. Haya hapa ni machache tu ambayo nimeweza kujifunza.
Karibu tujifunze
1. Unahitaji kujua kwanza kwa nini (Why) ufanikiwe kabla ya kujua jinsi gani (How) ufanikiwe. Kwa bahati mbaya vitabu vingi na walimu wengi wanajikita kufundisha njia za kufanikiwa kabla ya kufundisha sababu za kufanikiwa. Maana tatizo kubwa haliko katika jinsi gani kufanikiwa bali kiini cha tatizo kipo kwenye kwa nini kufanikiwa. Na bahati mbaya tatizo la kwa nini haliwezi kutatuliwa kwa suluhisho la jinsi gani kufanikiwa.
2. Unahitaji mtu atakaye kuamini kuliko wewe unavyojiamini mwenyewe. Tumekua tukiaminishwa kwamba tunatakiwa kujiamini kabla ya kuaminiwa, lakini uhalisia ni kwamba kujiamini kwetu kunajengwa kwanza na mtu kutuamini. Huwezi kujiamini kama kila mtu hana imani na wewe. Anapotokea mtu anayekuamini kuliko wewe unavyojiamini, hii inaongeza imani yako juu yako mwenyewe. Kwanza: Unaaminiwa Pili: Unawaamini wengine Tatu: Unajiamini mwenyewe sasa
3. Tunaishi katika zama za wimbi kubwa la taarifa. Taarifa zipo kila kona, nyingi sana, mara kwenye radio, tv, magazeti, email, website, blogs, mitando ya kijamii ndio balaa. Wingi wa taarifa hizo husababisha usumbufu na hii hupelekea kuwa na machaguo mengi sana, na hivyo kufanya watu kua katika wakati mgumu wa kufanya uchaguzi sahihi wa taarifa sahihi.
4. Kujaribu kufanikiwa bila support kutoka kwa wengine ni sawa na kusimama kwenye mgodi wa dhahabu huku ukichimba madini kwa kutumia kijiko cha chai. Mafanikio yanahitaji support za watu wengine, maana huwezi kua vizuri kila sehemu, utahitaji watu pia wa kukushika mkono.
5. Akili ya mwanadamu imegawanyika sehemu kuu mbili yaani conscious mind na Subconscious mind. Conscious mind inachukua asilimia 10 tu ya kazi zote za ubongo, wakati subconscious mind inawakilisha asilimia 90 ya shughuli za ubongo. Kila mtu anapenda kufanikiwa kwenye conscious mind yake. Ila kwenye subconscious mind ana sababu nyingi sana zinazomzuia kufanikiwa. Hii inafananishwa na kuendesha gari la maisha huku mguu mmoja upo kwenye breki.
SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Kinachoitwa FLIGHT PLAN The Real Secret Of Success.
6. Hofu ya kufanikiwa. Haujizuii kufanikiwa kwa sababu haujui jinsi ya kufanikiwa, unajizuia kupata mafanikio ambayo yako ndani ya uwezo wako kabisa, kwa sababu kwenye subconscious mind yako unazo sababu nyingi kwa nini usifanikiwe kuliko sababu za kufanikiwa ulizo nazo kwenye conscious mind.
7. Kuna ngazi 4 za uwezo (competency)
· Unconscious incompetency – Hujui kwamba hujui….
· Conscious Incompetency – Unajua kwamba hujui
· Conscious competency – Unajua kwamba unajua
· Unconscious competency – Unafanya bila kujua. Hujui kama unajua
8. Asilimia kubwa ya watu waliofanikiwa ni Unconscious competent (wana uwezo ambao wenyewe hawaujui). Tatizo linakuja pale wanapowafundisha watu jinsi walivyofika hapo walipo, wanachowafundisha watu unakuta mara nyingi si hicho kilichowafikisha hapo japo wao wanadhani kwamba wamefikia hapo kwa sababu ya hivyo wanavyofundisha. Tatizo ni kwamba wao wenyewe hawajui maana ukiwa katika level ya Unconscious competency katika jambo fulani unakua hujui hata huwa unalifanyaje. Secret code ya mafanikio haipo katika conscious mind, bali ipo katika unconscious mind ndiyo maana hata hao waliofanikiwa inakua ngumu wao kujua kama hiyo secret code kama ipo.
9. Akili ya binadamu inafanya kazi kwa kutumia maswali zaidi kuliko misemo. Mawazo ya binadamu ni mchakato wa kuuliza maswali na kutafuta majibu ya maswali.
10. Muda ndio bidhaa yenye thamani kuliko zote. Sababu ni kwamba muda ndio rasilimali pekee ambayo haiwezi kurudishwa baada ya kutumiwa. Mabilioni yote aliyonayo Bill Gates hawezi kununua hata dakika moja ya jana. Hivyo tumia muda wako vizuri
11. Tabia zetu ni kama nguvu ya uvutano (gravity) ambayo inataka tuendelee kukaa katika hali tuliyoizoea. Ndiyo maana ukijaribu kufanya kitu cha tofauti na ulivyozoea tabia zako hazitakuruhusu, au unaweza kufanikiwa katika hatua za awali lakini baada ya muda unarudishwa palepale na nguvu ya uvutano (tabia). Tunaona ndege ili iweze kuruka juu inahakikisha nguvu ya kuruka ni kubwa zaidi ya nguvu ya uvutano.
12. Mawazo mazuri yanakuja wakati umetulia. Wapo wengine mawazo mazuri (good ideas) huwajia wakati wa kuoga, wengine wakati wakiomba, wengine wakati wakitafakari n.k Tambua ni muda gani kwako mawazo mazuri yanatiririka akilini mwako. Tenga muda kwa ajili ya kuipa nafasi akili yako kutoa mawazo mazuri. Hakikisha unaandika mawazo unayoyapata. Ukijenga utaratibu huu utakua ni mtu wa tofauti, fursa kibao utaziona.
SOMA; Ushauri Kwa Waajiriwa Wapya Wote Wa Mwaka Wa Fedha 2014/2015
13. Ubora wa maisha yako unategemea vitu viwili: Ubora wa mawasiliano yako na ulimwengu wako wa ndani, na ubora wa mawasiliano yako na ulimwengu wako wa nje.
14. Watu hawafuti wafuasi, bali wanafuata viongozi. Ili watu wakufuate lazima uwe kiongozi na si kua mfuasi (follower). Unaweza kua huyo kiongozi lakini kufanya hivyo lazima kwanza ujue sababu ya wewe kuwepo hapa duniani.
15. Watu wengi hawajui sababu/kusudi la wao kuwepo hapa duniani, na kwa kutofahamu sababu ya wao kuwepo hupelekea kuwa na hisia tofauti kama kuchanganyikiwa, kupata msongo wa mawazo, kuhisi kua na hatia fulani, na hata kukata tamaa. Ukiona mtu anapitia mambo hayo sababu kubwa na ya msingi ni kutokufahamu sababu ya yeye kuwepo duniani. Ukitambua kusudi lako utachukua hatua muhimu ambazo zitakupelekea kua mtu asiyezuilika, maana mtu anayelitumikia kusudi lake anaweza kupunguzwa kasi kwa muda tu lakini hawezi kuzuilika. Tambua kusudi lako na anza kulitumikia kusudi, you will become unstoppable.
16. Ukitaka kua tajiri huwezi kua kikawaida kawaida tu. Watu wanaotengeneza mamilioni ya hela sio watu wa kawaida tu, kwa sababu wanafanya vitu ambavyo watu wa kawaida hawavifanyi. Kwani idadi kubwa (majority) ya watu ni matajiri? La hasha, matajiri ni sehemu ndogo sana ya watu wote. Hii ina maana kwamba ukichagua kufanya kama idadi kubwa ya watu wafanyavyo, tegemea kupata matokeo wanayoyapata. Ila kama unataka kua mtu asiye wa kawaida, basi huna budi kufanya vile vitu ambavyo wale wachache (matajiri) wanavifanya.
17. Pindi maoni yako (opinion) kuhusu wakati uliopita, wakati ulionao na wakati ujao yanapokua chanya utakua mwenye furaha. Ila pale maoni yako ya jana yako, leo yako na kesho yako yanapokua hasi (negative) utakua usiye na furaha. Hata kama jana yako haikuwa nzuri usipende kukumbatia maoni mabaya kuhusu hiyo jana, chukua yale masomo mazuri uliyoyapata kwenye hayo mabaya yatumie hayo kujiboresha.
18. Kitu pekee tunachopaswa kufanya kwa past (wakati uliopita) zetu ni kusamehe. Samehe jana yako, samehe kwa yale ambayo si mzuri yalikupata. Jana imepita na haitarudi kamwe, usiposamehe jana yako unakua umefungwa na minyororo imara kuliko chuma. Samehe wote waliokukosea jana, samehe yote yaliyokupata jana, hii ndiyo njia rahisi ya kukufanya kua mwenye furaha.
SOMA; Usikubali jua lizame leo kabla hujafanya kitu hiki muhimu.
19. Ndoto za watu wengine au malengo ya watu wengine. Watu wengi kwa kujua au kwa kutokujua tumejikuta tukiishi ndoto za watu wengine na kutekeleza malengo ambayo wala si ya kwetu. Aidha wengine ni kwa ushawishi wa wazazi au ndugu, Mfano mtoto anasomea udaktari kwa sababu baba yake ni daktari, au mtu unaambiwa usome kozi fulani kwa sababu ndiyo yenye soko zuri la ajira. Hata wakati mwingine unakuta malengo unayotekeleza uliyaona kwa rafiki yako ukayapenda na wewe ndio unafanya hivyo. Lengo au Ndoto uliyonayo kama si original kwako basi itakusumbua mahali tu, kuna viwango hutaweza fika maana ndoto si yako. Kama wewe ni moja ya watu ambao wamejikuta wakitumikia ndoto za watu wengine, jipange kutambua ndoto yako original ni ipi, halafu ifanyie kazi.
20. Nani unayetaka kumfurahisha? Kwa kawaida tunapenda kuwa level moja na wenzetu, tukiogopa kwenda hatua ya juu maana tunaona kwamba tutapoteza marafiki zetu, wakati mwingine unaogopa kufanikiwa kuliko marafiki zako maana watakusema vibaya, kwamba unaringa n.k Hivyo tunaona ni bora kuwafurahisha hawa marafiki kwa kutokufanikiwa. Mbaya zaidi hii inajengeka kwenye subconscious mind ambayo ndiyo yenye nguvu kubwa na usiyokua na maamuzi nayo.
Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com