TUPO PAMOJA?
Nataka kujua tu kama bado tupo pamoja na kama bado unafanyia kazi yale ambayo unajifunza kila siku kupitia mitandao inayoendeshwa na AMKA CONSULTANTS. Kuna wengi wanayafanyia kazi na wamekuwa wakitoa shuhuda nzuri sana ni jinsi gani maisha yao yamebadilika. Bado wewe hujatuambia ni jinsi gani maisha yako yanabadilika kwa kutekeleza haya ambayo unajifunza. Tafadhali usisite kutushirikisha hilo kupitia email makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Leo nataka tuongelee kitu kimoja muhimu sana kwenye maisha yetu sote, kitu ambacho tunaweza kujifunza kutoka kwa viumbe hai wenzetu ambao tumekuwa tunawaona ni viumbe wa kawaida tu lakini wana somo kubwa la kutufundisha. Japo viumbe hawa hawawezi kuongea na sisi moja kwa moja, ila vitendo vyao vinaonesha wazi wazi na hivyo mtu unaweza kujifunza na kuboresha maisha yako sana.

 
Viumbe hawa ni ndege, ndio ndege wanaoruka angani. Nakusikia ukisema, kweli Makirita leo umekosa vya kuandika kabisa mpaka unatuandikia kuhusu ndege? Naomba usiwe na wasi wasi, endelea kusoma mpaka mwisho na kama hutakuwa umejifunza kitu cha kubadili maisha yako, funga huu mtandao na usiusome tena kuanzia sasa. Lakini kama kuna vitu utakuwa umejifunza vifanyie kazi haraka sana kwa sababu kadiri unavyochelewa ndivyo maisha yako yanavyozidi kuwa mabaya pia.
Kwenye kitabu cha biblia, usiwe na wasi wasi kama hutumii biblia ni mfano tu, kuna mfano ambao umetolewa kwamba ndege wa angani hawalimi, hawavuni lakini wanakula. Na huu ni ukweli kabisa, ni lini umeona ndege wanakwenda shamba kulima? Lakini umewahi kuona ndege mwenye utapiamlo? Au aliyekufa kwa njaa? Nafikiri wote huwa tunawaona ndege wakiruka kwa furaha huko angani.
Sasa sijui kama umewahi kutafsiriwa mstari huo ulitafsiriwaje na ukafundishwa nini, mimi leo nataka nikupe tafsiri ambayo itakusukuma zaidi na uamue kuyachukua maisha yako kwenye mikono yako kama lilivyo lengo la mtandao huu wa AMKA MTANZANIA.
Ndege wa angani hawalimi, hawavuni ila wanakula na maisha yao yanasonga mbele. Na wewe unaweza kusema kwamba kumbe hakuna haja kubwa ya kuhangaika na kuweka juhudi kwa sababu hata nisipofanya hivyo bado nitakula na kuishi. Kama umewahi kufikiria hivi, na wengi ndio wanafikiria hivi ndio maana hawaweki juhudi kubwa kwenye kile wanachofanya, basi umepotoka. Umepotoka kwa sababu kuna mambo mengi sana ambayo unatakiwa kuyafanya na huyafanyi.
Ngoja tuanze na huu mfano wa ndege ambao hawalimi ila wanakula na tuone ni jinsi gani ni wajanja kuliko wewe.
1. Chakula cha ndege hakitokei kwenye kiota chao.
Ndio ndege halimi, wala havuni ila pia chakula chao hakitokei pale pale kwenye kiota chao. Ni lazima watoke wakatafute na hata kwenye kutafuta hawakutani nacho kirahisi tu. Wanapitia mazingira magumu sana, wengine wanakoswa koswa kuliwa na ndege wanaokula ndege, wengine wanakoswa koswa kuwindwa lakini wanachukua hatari yote hiyo ili wapate chakula.
Lakini wewe ndugu yangu haupo tayari kuchukua hatari yoyote ili kuboresha maisha yako, haupo tayari kuingia kwenye biashara ambayo unaweza ukashindwa lakini pia unaweza ukafanikiwa. Unajaribu kidogo na ukiona hatari unakimbia haraka sana na kukata tamaa. Hapa ni sawa na ndege akoswe na mwindaji siku moja na aseme sitaenda tena kutafuta chakula, nakaa hapa kwenye kiota changu tu.
Somo la kujifunza; kama unataka mabadiliko kwenye maisha yako ondoka hapo kwenye kiota chako leo. kama utaendelea kungangania hicho kiota jua hakuna kitakachobadilika. Kiota chako ni hali yoyote ambayo imekuridhisha kwa sasa. Hali ambayo inakufanya uogope kuchukua hatua kwa kudhani ni hatari mno. Maisha yote ni hatari hivyo usiogope kufanya jambo ambalo ni muhimu kwako kwa sababu unaogopa kushindwa.
SOMA; Matatizo Yote Ya Mahusiano Yanaanzia Hapa… Sehemu Ya Pili(2)
2. Mwanga ukishatoka na ndege wameamka.
Sasa hivi ninapoandika hapa ni saa kumi na moja na nusu asubuhi na nimeshasikia ndege wanalia huko nje. Hivi umewahi kukuta ndege amelala mpaka saa mbili? Sawa, hata wewe huwa hulali mpaka saa mbili, labda nikuulize hivi tena. Umewahi kukuta ndege amelala mpaka saa mbili kwa sababu siku hiyo ni siku ya jumapili? Au siku ya sikukuu?
Haijalishi ni siku gani kwenye dunia yao, mwanga ukishaonekana tu ndege nao wameamka na wanaendelea na mchakato wao wa kuboresha maisha yako. Sijui kama kuna ndege ambaye huwa anajishauri mara mbili mbili kwamba aamke au asiamke. Na sijui kama kuna ndege ambaye ana alarm anayoweza kuizima na kulala kidogo, dakika tano tu ila anakuja kustuka nusu saa baadae, kama unavyofanya wewe mara kwa mara.
Unakumbuka usemi kwamba ndege anayewahi kuamka ndiye anayepata wadudu wazuri wa kula. Nafikiri hilo halina ubishi, kama kuna mdudu alichelewa kujificha basi ndege anampata kwa urahisi kabisa anapokuwa ameamka mapema.
Somo la kujifunza; amka mapema kila siku, haijalishi ni jumatatu au jumapili, haijalishi ni siku ya sikukuu au msiba. Kuwa na utaratibu wa kuamka mapema kila siku na tumia muda huo kutafakari maisha yako, kupangilia siku yako, kujisomea na hata kufanya kazi zako, kama kazi zako zinawezekana kufanya kwenye muda huo. Usiache hata siku moja kuamka mapema na usiamke halafu ukaanza kujishauri. Kama unatumia alarm kuamka ikishaita tu, ruka kutoka kitandani na unapoanza kupata mawazo kwamba urudi kulala, jiulize je ndege angefanya hivyo? Kama jibu ni hapana ondoka kitandani na kawahi wadudu wazuri. Wadudu kwako ni zile shughuli muhimu kwako.
3. Ndege wa kishua.
Sijawahi kuona ndege wa kishua, kama huelewi neno kishua maana yake nini, kwanza samahani, ila kishua maana yake ni ya kitajiri. Sasa swali ni je umewahi kumuona ndege wa kishua? Yaani ndege ambaye wazazi wake ni matajiri? Na je juhudi zake zinatofautiana na ndege ambaye ni wa kimasikini? Nafikiri tunakubaliana kwamba hakuna ndege anayekaa chini na kusikitika kwamba leo siwezi kwenda kutafuta chakula kwa sababu wazazi wangu hawajanisaidia. Au ndege analalamika kwamba wazazi wake hawakufanya kitu fulani ndio maana maisha yake sio mazuri. Au ndege anawaambia wazazi wake wampe uruthi!!
Somo la kujifunza; kama unasoma hapa, ni marufuku kutoa sababu ya kijinga kama hiyo eti maisha yako sio bora kwa sababu wazazi wako hawakukusomesha, au hawajakupa mali, au ni masikini. Kama umeweza kuwa na akili ya kufikiria hiki, jua kwamba chochote unachotaka kipo kwenye mikono yako. Acha kuwalaumu wazazi wako na anza kufanyia kazi kile ambacho unakitaka. Wazazi hawakukusomesha? Vizuri unaweza kujisomesha sasa, huoni ni vizuri?
4. Malalamiko ya ndege kwa serikali.
Labda ndege wana serikali yao, na wana CCM yao au CHADEMA yao, mimi sijui lakini ninachoweza kusema ni kwamba sijawahi kuona ndege ameacha kwenda kutafuta riziki yake kwa sababu CCM au CHADEMA yao imewaahidi maisha bora. Sijawahi kuona ndege ameacha kuweka juhudi kwenye kutafuta riziki yake na kutumia muda huo kulalamika kwamba serikali yao imefanya hiki, mara imefanya kile na kuitumia kama sababu ya kutokupata riziki.
Somo la kujifunza; kama unaamini CCM ndio itakuletea wewe maisha bora umepotoshwa na ukakubali kupotoka. Kama unaamini CHADEMA ndio jibu la matatizo yako umepotoka pia. Laini mbona niliahidiwa maisha bora na kuhakikishiwa hivyo? Sawa uliahidiwa, je umeyaona maisha hayo bora/
Maisha bora yapo kwenye mikono yako. Usidanganyike kwamba kuna serikali itakuja kukuletea wewe ugali ukiwa umekaa unabishana au kusifia kwamba serikali ni nzuri. Hivi unajua serikali inakutegemea wewe ndio iende. Yaani wewe usipofanya kazi hakuna mshahara wa kumlipa raisi. Tunahitaji serikali nzuri lakini hilo sio jawabu la matatizo ya maisha yako.
SOMA; Kama Umewekeza Kwenye Majengo Yafahamu Magonjwa Sugu Yanayo Athiri Majengo.
5. Ndege ni wajasiriamali.
Sijui kama kuna ndege mmoja ambaye ameajiri ndege wengine au kuna ndege ambao wameajiriwa na matumaini yao yote wameweka kwa yule ndege aliyewaajiri. Ndege wanajua juhudi zao ndio zitafanya maisha yao yaendelee kuwepo.
Somo la kujifunza; ajira ni sehemu ndogo sana ya mafanikio ya maisha yako. Unahitaji kuweka juhudi nyingi binafsi ili kuweza kufanikiwa kwenye maisha yako. Kama unafanya kile tu ambacho umeajiriwa kufanya na wakati mwingine unafanya kwa kiwango cha chini sana, umekwishapotea.
Nimetumia mfano huu wa ndege ili tuweze kujifunza mambo haya matano muhimu sana kwenye maisha yako. Ndio ndege ni kiumbe mdogo sana, huwezi kumlinganisha na sisi binadamu, sawa kabisa, je kwa hayo anayofanya hajakuzidi ujanja? Hebu anza kuyafanyia kazi hayo mara moja na yafanyie kazi kila siku kama wanavyofanya ndege halafu uone kama maisha yako yataendelea kuwa kama yalivyo sasa.
Nakutakia kila la kheri katika jukumu hili kubwa na zuri uliloamua la kuboresha maisha yako.
TUPO PAMOJA? Hapo kuna alama ya ulizo, tafadhali nijibu kwenye makirita@kisimachamaarifa.co.tz na niambie unafikiriaje kuhusu maisha ya ndege na ya kwako? Nasubiri kusikia kutoka kwako.