Kwa sababu zao binafsi, kuna watu ambao wangependa kuajiriwa maisha yao yote. Au wangependa kuajiriwa kwa kipindi fulani kwenye maisha yao. Au kama ni mhitimu basi ungependa kuajiriwa kama sehemu ya kuanzia kujijenga ili baadae uweze kuingia kwenye kujiajiri au kufanya biashara ukiwa na uzoefu zaidi ya sasa.
Hakuna mtu mwenye tatizo na hilo, iwe unataka kuajiriwa maisha yako yote au iwe unataka kuajiriwa kwa kipindi tu, kama ndio kitu unachopenda kufanya, basi ni vyema. Mafanikio hayaji kwa kufanya biashara au kuwa mjasiriamali tu, mafanikio yanakuja kwa wewe kufanya kile ambacho unakifanya kwa ubora wa kipekee na kwa utofauti sana. Mafanikio yanakuja pale unapotoa thamani kubwa kwenye jambo lolote unalofanya.

FANYA KITU CHAKITAALAMU KITAKACHOONGEZA SIFA YAKO NA KIPATO PIA

 
Lakini pamoja na wewe kutaka kuendelea kupata kazi nzuri au kutaka kuingia kwenye ulimwengu wa kazi, soko la ajira limechafuka vibaya sana. Nafasi za ajira ni chache na wanaohitaji ajira hizo ni wengi mno. Kama ni sifa kila mtu anazo, elimu kila mtu anasoma. Hivyo wasifu wenu wote waombaji, yaani cv ni kama zinafanana. Ni vigumu sana kusimama katikati ya kundi la wengi na ukawa tofauti na kupata kazi bora kwa sababu tu cv yako umeiandika wewe ni mchapa kazi, unajituma na maneno mengine kama hayo ambayo kila mtu atayaandika.
Leo nataka nikushirikishe njia moja ambayo hakuna watu wengi wanaoweza kuipita. Kwa wewe kupita njia hii utaongeza kitu kimoja kwenye cv yako ambacho watu wengi hawana. Kitu hiki kitakusimamisha wewe na kukutofautisha na kundi kubwa la watu wengine wanaotaka kazi unayotaka wewe. Endelea kusoma na utajua kitu hiko muhimu sana.
 
Kama mmekwenda kuomba kazi, na sifa za mfanyakazi anayehitajika ni kuwa na shahada ya kitu fulani, watakaoenda ni wengi sana. Kwa sababu watu wengi sasa hivi wana shahada. Kwa wote kuwa na shahada wanaofanya usahili watakuwa na wakati mgumu wa kuchagua ni nani apewe kazi, kwa sababu kama ni kujieleza, kila mtu anaweza kuyapanga maneno yake vizuri sana na akajieleza mpaka wanaofanya usahili wakasema huyu ndio mwenyewe. Lakini akiondoka na kuja mwingine ambaye na yeye ameyapangilia maneno, wataona huyu naye yuko vizuri. Mwisho wa siku, wanabaki na makaratasi ambayo karibu yote yanafanana na maneno mazuri waliyoambiwa. Hivyo wanaweza kuchagua tu mtu yeyote. Na wewe ukakosa kwa sababu tu ulikosa kitu cha kutofautisha.
 
Vipi kama ungekuwa na kitu cha kukutofautisha wewe na hawa watu wengine. Vipi kama usingekuwa na haja ya kuongea sana bali kuonesha. Unapofika kwenye usahili ukawaambia pia ninafanya kitu hiki na hiki kinachoendana na kazi hiyo ambayo unaiomba? Na kuwa makini hapo nimekwambia unawaambia unafanya, sio ulifanya. Maana hapa hatuleti zile hadithi kwamba nilikuwa kiranja, au nilikuwa mchezaji mzuri shuleni, ni hadithi nzuri lakini kila mtu anaweza kuzisema pia. Wasahili hawataenda kwenye kila shule kuuliza kama mtu fulani alikuwa kiranja kweli.
 
Kwa hiyo nataka wewe uwe na kitu cha kuonesha, na unapoenda kwenye usaili wa kazi unawaonesha, nimefanya na ninaendelea kufanya kitu hiki kinachoendana na kazi hii ninayoomba kufanya. Ninachoweza kukuhakikishia kwamba kama unachoonesha ni kitu kizuri, tayari kazi utakuwa nayo, wengine watafanyiwa usaili ili kukamilisha tu zoezi ila wewe utakuwa tayari na kazi. Unajua ni kwa nini? Kwa sababu ni wewe pekee utakayekuwa na kitu cha kuonesha. Wengine watakuwa wavivu sana kuweza kuandaa kitu cha kuonesha, na hata wewe binafsi huenda hutafanyia kazi kitu nitakachokuambia uende nacho kuonesha.
 
Sasa ninaweza kuonesha nini?
Taaluma niliyosomea sina cha kuonesha, labda mpaka nifanye kazi ndio nitakuwa na kitu cha kuonesha. Kama huu ndio utetezi wako basi huna utetezi. Kama kuna taaluma yoyote uliyosomea, au kama kuna kitu ambacho unapenda kufanya unaweza kuongeza hatua moja ya ziada tu na ukawa na kitu kikubwa cha kuonesha. Kitu hiki wala hakihitaji uwekeze fedha za ziada, kitu ambacho utaniambia huna, bali kinahitaji juhudi na maarifa yako ya ziada.
Kitu hiko ni nini? Kitu ninachotaka kukuambia hapa ni kwamba uanzishe blog. Nianzishe blog? Ndio anzisha blog, hii itakutofautisha wewe na watu wengine wengi watakaokwenda kuomba kazi na wewe. Blog ninayokuamia uanzishe sio ya kuandika habari za udaku za dimond na wema, bali blog itakayokuonesha wewe kama mtaalamu kwenye eneo lile ambalo umesomea au unalopenda kufanyia kazi. Labda nitoe mifano michache ambayo itakupa mwanga.
 
Kama umesomea taaluma yoyote ya afya, anzisha blog inayowasaidia wananchi kwenye eneo la afya. Kuna changamoto nyingi sana eneo hili, kuna magonjwa mengi yangeweza kuzuilika, ila watu hawana elimu, anzisha blog na wapatie elimu hiyo.
Kama umesomea mambo ya elimu, anzisha blog na andika kuhusu elimu. Elimu yetu sasa hivi ina changamoto kubwa, eleza ni jinsi gani inaweza kuboreshwa, waeleze wazazi ni pi nafasi yao, wanafunzi na serikali pia eleza nafasi yako kwenye ukuaji wa elimu ni ipi. Hakikisha kwa mtu kusoma pale anatoka na kitu kitakachomsukuma kuboresha elimu.
Umesomea uafisa wa jamii? Aisee wewe ndio unahitajika sana kwenye nchi hii. Tuna matatizo mengi sana ya kijamii, kuna unyanyasaji wa kijinsia unaoendelea, kuna malezi mabovu ya watoto yanayopelekea taifa kukosa maadili na mengine mengi. Anzisha blog yako na toa elimu hii ya kijamii.
 
Umesomea sheria? Hongera sana, kama utafungua blog utakuwa mkombozi wa wengi, mimi binafsi kuna sheria nyingi sana ningependa nizijue, kila siku natafuta blog nzuri ya sheria sipati, ukianzisha nitakuwa msomaji wako mzuri na pengine mteja wako pia. Ukweli ni kwamba wananchi wengi wanahitaji msaada wa kisheria.
Chochote ulichosomea kuna maeneo mengi unayoweza kuandikia. Kama hujaona ni wapi unapoweza kuandikia niandikie email kwenye makirita@kisimachamaarifa.co.tz na niambie umesemea nini au unapenda kufanya nini na nitakupa maarifa ya vitu vingi sana unavyoweza kuandikia.
 
Kuna vitu vingi mno unavyoweza kuandika na kutoa elimu kwa wengine. Unaweza hata kuandika mambo yanayofanyika hovyo kwenye eneo fulani ambalo unalijua vizuri, au mambo yanayofanyika vizuri au njia mbadala za kufanya kitu.
Na utakapokwenda kwenye usaili mwingine utawaambia pia mimi ni mwanzilishi wa www.mimihapa.blogspot.com au www.mimihapa.com ambayo ni blog inayotoa elimu kwenye eneo fulani la taaluma yako. Siku hizi kila mtu ana simu janja (smartphone) wataichungulia na wakiona vitu vizuri pale, tayari kazi unayo.
 
Ufanye nini sasa.
Fungua blog, nenda www.blogger.com na fungua blog yako. Huna haja ya kuiremba sana, huna haja ya kuifanya kubwa sana. Kikubwa anza kuandika vitu vizuri ambavyo vitawasaidia watu. Na kadiri siku zinavyokwenda utaendelea kuboresha. Kikubwa ifanye blog yako iwe ya kitaalamu zaidi, yaani profesional, usiandike kitu chochote ambacho hakiendani na dhumuni la blog, hata kama unaona wengi wangependa kukisoma, yaani acha usiandike kabisa. Habari kama Lowasa ahamia CHADEMA ni nzuri kwenye masikio ya watu, lakini usiweke kwenye blog yako, wewe ni mtaalamu, fanya mambo ya kitaalamu.
 
Sijui chochote kuhusu blog au kuandika.
Kama hii ndio sababu unayojipa, usihofu kabisa. Kwa sababu yote hayo tayari yameshafanyiwa kazi. Kuna kitabu kinaitwa JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG. Kitabu hiki kina maelekezo yote hatua kwa hatua, kwa lugha ya kiswahili na kimewekwa picha pia. Kupitia kitabu hiki utajifunza jinsi ya kutengeneza blog, jinsi ya kuifanyia marekebisho, jinsi ya kuandika makala nzuri na zenye kuvutia na pia jinsi ya kuigeuza blog yako kukuletea kipato? Umeipenda hii, basi unaweza kutumiwa kitabu hiki hapo ulipo sasa hivi. Unachotakiwa kufanya ni kutuma fedha tsh elfu 10 kwenye namba 0717 396 253 au 0755 953 887 na kisha utume email yako na utatumiwa kitabu. Kitabu ni soft copy yaani pdf na kinatumwa kwa email. 

Kumbuka sio lazima ununue kitabu hiki, unaweza kufanya kila kitu mwenyewe, kama ni mjanja wa kutumia kompyuta. Ila kama utataka kufanya mambo yako kitaalamu zaidi, basi jipatie kitabu hiko. Na kama hakitakusaidia chochote, utaniandikia kwenye namba hizo nikurudishie fedha uliyolipia kitabu. Nakupa kitu ambacho kitaleta mabadiliko kwenye maisha yako, ndio naamini hivyo na wengi waliokipata kitabu hiki wameshakuwa na blog zao na wanaziendesha vizuri.
 
Unasubiri nini?
Unapomaliza kusoma hapa usisubiri kesho, sasa hivi nenda www.blogger.com bonyeza create blog, andika jina la blog, unaweza kutumia jina lako au hata jina lolote, ila liashirie kitu cha kitaalamu au kile unachoandika na baada ya hapo weka makala yako ya kwanza, ya kuwasalimu wasomaji, kuwaambia blog hiyo inahusu nini. Na endelea kuandika kila siku, NDIO KILA SIKU.
Samahani, nilisahau swali moja muhimu ambalo huenda unajiuliza au unajipa sababu, SINA MUDA wa kuendesha blog. Sawa sio sababu hiyo. Fanya hivi unahitaji kama nusu saa mpaka saa moja kwa siku kuendesha blog yako. Unaipata wapi sasa, punguza kuzurura kwenye mitandao na acha kabisa kuangalia tv, lala mapema na amka saa kumi na moja au hata saa kumi asubuhi na andika kisha upost. Hivyo tu, kila siku. Kama ungependa kuwa unaandika asubuhi ila ni mvivu sana tuwasiliane, ninaweza kukusaidia kwenye hilo pia.
Asante na naomba ufanyie kazi hili tulilojadili leo, au kama hujajifunza chochote unisamehe kwa muda wako.
 
Rafiki na kocha wako,
Makirita Amani
TUPO PAMOJA.