Merina anaishi ndani ya jiji la Dar es Salaam pia ni mwalimu wa shule ya msingi katika sekta ya umma, ni mwaka wake wa tatu toka alipoajiriwa na kuwa mwalimu katika shule moja ya umma wilaya ya kinondoni. Merina hakuwa tofauti na mimi miaka miwili iliyopita, pia hakuwa tofauti na wengine ambao kila siku hawaishi kuwalaumu wengine, walio kata tamaa ya maisha, asiyeipenda kazi yake na kipato chake ni duni kulingana na hali ya maisha yanavyokwenda. 
Merina kila alipotafakari miaka mitatu ijayo atakuwa kwenye hali gani kiuchumi na kiafya hakuwa na jibu lenye kutia matumaini ukizingatia majukumu yanaongezeka siku hadi siku. Msongo wa mawazo ulimtesa sana, aliishi kwenye gereza la utumwa wa maisha. Ni mwaka mmoja sasa Merina haamini kinachotokea kwenye maisha yake toka alipokutana na kufahamiana na mimi. Amekuwa ni mtu wa tofauti sana ukilinganisha na alivyoishi kipindi cha nyuma. Ni mtu mwenye furaha, hamasa na tumaini kubwa la nyakati zijazo. Ukiacha mambo mengine anayoyafurahia, 
Hivi sasa Merina anajenga nyumba ya kupangisha (apartment) yenye ghorofa tano eneo la bagamoyo mkoa wa pwani yenye gharama ya shilingi milioni 900,000,000 za kitanzania.

 
SOMA; Kitu Kimoja Kitakachoongeza Wasifu Wako(Cv) Na Kukuongezea Kipato Pia.
1. Chanzo cha mabadiliko
Nilikutana na Merina kwenye moja ya matamasha ya vijana lililoandaliwa na shirika moja la kanisa maeneo ya Bunju mkoa wa Dar es Salaam. Katika kufahamiana aliniambia kwa unyonge sana na katika hali ya kutojikubali kuwa yeye ni mwalimu, ila mimi nilimpongeza sana kwa yeye kuwa mwalimu na nilimpa sababu nyingi za kumpongeza. Baada ya siku kadhaa kupita alinitembelea ofisini na kunikuta naandaa makisio ya nyumba ya mteja wangu. Baada ya salamu na mazungumzo mengine kupita alihoji uzuri wa ramani ya nyumba ile na kuhoji gharama za ujenzi wa nyumba ile yenye ghorofa mbili juu. Nilimweleza kuwa itagharimu milioni mia tano za kitanzania hadi itakapokamilika. Alishtuka sana na kuhoji ‘’daaah, nchi hii ina mafisadi haswa, fedha zote hizo anazipata wapi’’. Nilimwambia hata yeye kama atapenda atafanya makubwa zaidi endapo ataamua kufanya hivyo. Alicheka na kuhisi kuwa namtania na kumkejeli, nilimwambia kuwa niliyomweleza ni kweli na hakika, kwenye maisha chochote kinawezekana kama utajiamini na kuchua hatua stahiki, pia ilinilazimu nianze kazi ya kumuelimisha na kumshawishi kuwa hata yeye anaweza, hata hivyo haikuwa rahisi kama nilivyofikiri kwa muda tuliotumia, hatimaye tuliagana.
2. Amefikaje hapo alipo sasa
Merina anaishi na mumewe pembezoni mwa wilaya ya kinondoni, na walifanikiwa kujenga nyumba wanayoishi sasa, aliolewa mwaka mmoja baadae baada ya kuhitimu chuo cha ualimu vikindu, hivi sasa ana mtoto mmoja anayeongeza chachu ya maendeleo kwa familia hiyo. Merina kwa sasa haamini kama maamuzi aliyoyafanya hatimaye yanatimia miezi mitatu ijayo.
Merina alichukua mkopo wa kununua kiwanja miongoni mwa viwanja vingi vilivyopimwa na kampuni moja ya upimaji na uuzaji wa ardhi. Masharti ya mkopo huo ni kwamba mkopaji anapaswa alipe asilimia ishirini ya gharama ya kiwanja atakacho chagua kutoka kwenye ramani hizo. Bei ya kiwanja kiliuzwa shilingi elfu sita na mia tano kwa kila mita za mraba [6500/Sqm] alichagua kiwanja cha 25m x30m ni sawa na mita za mraba 750 kwa thamani ya sh 4,875,000. 
Merina alilipa kiasi cha shilingi 975,000 tu kama asilimia ishirini ya gharama ya kiwanja hicho na fedha zilizobaki taasisi ya fedha ililipa na kuingia mkataba na Merina kuwa anapaswa alipe kupitia makato ya mshahara kwa muda usiozidi miezi 18 pasipo na riba endapo hatamaliza ndani ya muda huo ataongezewa tena miezi 18 itakayokuwa na riba. Na hati ya kiwanja hicho itamiliki taasisi hiyo hadi atakapo fikisha malipo ya asilimia hamsini. Merina alimaliza deni hilo ndani ya miezi nane na kumiliki ardhi yenye hatimiliki kwa mtaji wa shilingi 975,000 tu.
SOMA; Huyu Ni Kijana Wa Kitanzania Aliyeanza Biashara Kwa Mtaji wa Milioni Nne na Baada Ya Miaka Mitatu Ana Zaidi Ya Milioni Mia Moja.
Hatimaye nilimkumbushia tena ndoto yake ya kumiliki “nyumba kali” angali yeye ni mwalimu. Hatimaye Merina aliingia ubia na taasisi nyingine ya fedha kwa kugharamia ujenzi wa nyumba ya kuishi na kupangisha[apartment] baada ya kuandika proposal iliyokubaliwa na taasisi hiyo. Makubaliano hayo yalikuwa ni namna gani Merina atarejesha fedha za gharama hizo za ujenzi. Makubaliano yaliyofikiwa ni kwamba taasisi hiyo itagharamia gharama za ujenzi huo, baada ya ujenzi kukamilika Merina atamiliki ghorofa tatu za chini zitakazompatia kipato na taasisi hiyo itamiliki ghorofa za juu zilizosalia hadi itakaporejesha gharama hizo na faida ya asilimia kumi ya uwekezaji huo. Baada ya kupiga hesabu tuligundua kuwa taasisi hiyo itakuwa imerejesha gharama zote pamoja na faida yake ni ndani ya miaka saba baada ya ujenzi kukamilika. 
Baada ya kurejesha fedha hizo kwa njia yakupangisha kama apartment hatimaye jengo hilo litamilikiwa rasmi na Merina na kuliendesha kibiashara kwa kipindi chote cha uhai wake pia ataendelea kupata faida ya uwekezaji huo ambao wakati wa ujenzi hajatoa hata senti yoyote ya fedha. Hivi sasa mkandarasi yupo kwenye hatua ya mwisho kumalizia ujenzi huo na amelipwa fedha stahiki kutoka kwa Merina kupitia taasisi hiyo ya fedha. Watu wa karibu na Merina hawaamini kama yeye asivyokuwa akiamini hapo awali, aliwaita “mafisadi” watu waliofanikiwa kuishi ndoto zao, leo hii yeye anaitwa “mchawi”, lakini yeye anamalizia kuwa ni “mchawi wa maendeleo”.
Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.
Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma na mshauri wa ujenzi.
Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888,
Email: kimbenickas@yahoo.com