Habari za Jumapili mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA. Ni matumaini yangu kuwa mpo salama , ni wakati mwingine tena tunakutana kwa ajili ya kuzidi kujifunza na kukumbushana namna sahihi ya kuangalia mambo. Ndugu yangu napenda nikukumbushe kuwa wewe umeumbwa ukiwa na uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo, ulipewa akili na uwezo wa kufanya kile unatakiwa kufanya hapa duniani.

UNAWEZA.

 
Kuna wakati unakutana na mambo ya kusikitisha na kuumiza pale ambapo mtu anakuwa kama amezipeleka akili zake likizo, au naweza sema amejisahau au kujipoteza kabisa , haelewi hata ni nani, anaenda wapi?, kwa nini yupo? n.k. Baadhi ya watu wapo tu kwa kuwa wapo. Baadhi ya watu hawaelewi hata uwezo walio nao, hawajui kusudi la wao kuwepo hapa duniani, mwingine anafikiri alikuja hapa ili aishie kutamani kuwa kama wengine, hajui kama naye ikiwa atatembea na kukaa kwenye ile nafasi yake anacho kitu cha maana , cha kumfanya na wengine watamani kuwa kama yeye, japo ukweli ni kwamba hakuna mtu awaye yote duniani hapa anaweza kuwa kama wewe ndugu yangu, wewe ni wewe, ni wa peke yako, uliumbwa hivyo kwa kusudi maalumu, Kama ulikua haujui hilo ndio nimekujulisha leo na ikiwa ulisahau basi nakukumbusha tu kuwa hakuna aliye kama wewe, usijifananishe na mwingine wala usitamani kuwa kama yule maana hauwezi kuwa vile, utakuwa unajichosha na kujichelewesha kufika kule unaenda tu, tafuta na tamani kuwa kama wewe yule Muumba alikukusudia uwe, tafuta kujua na kuona ule uwezo umeumbwa nao ndugu yangu, tambua zile akili umepewa ndugu yangu.
SOMA; Hizi Ndizo Fikra Zinazokuzuia Kufikia Viwango Bora Vya Mafanikio!
Ni jambo la kusikitisha pale unapokutana na mtu anasema kwa kujiamini kabisa kuwa hawezi kufanya jambo fulani na ukitaka kujua ni kwa nini atakuambia eti kwa kuwa fulani alijaribu akashindwa, yaani kwa kuwa tu yule alishindwa naye anaamini atashindwa, anakubali kushindwa bila hata kujaribu kufanya kile kitu, anajipima kwa kumwangalia mtu yule, anajiona yeye hawezi kufanya zaidi ya yule, ndugu yangu tambua kuwa katika maisha haya usitumie kushindwa kwa mwingine kama kipimo cha kwamba nawe huwezi kwenda zaidi ya pale, kwamba hauwezi kufanya zaidi yake, tambua utofauti uliopo miongoni mwetu wanadamu wote, tuna uwezo tofauti wa kufanya mambo, hata namna ya kufikiria tunatofautiana.
Mwingine anashindwa kwa kuwa tu kachagua kushindwa, ninasema kachagua kushindwa kwa maana ya kwamba kama mtu unatumia kigezo cha kwamba kama na yule kashindwa basi na mimi siwezi, mtu huyu ameamua na kuchagua kushindwa lakini angeamua kuangalia kushindwa kwa mwenzie kwa namna tofauti angeweza kufanya vizuri zaidi. Badala ya kukubali kushindwa kwa kuwa yule kashindwa au alishindwa unaweza kuamua kumfuata yule aliyeshindwa na uweze kuchunguza na kuelewa ni kwa nini alishindwa na kuanzia hapo unaweza kupata vitu vya kukufanya wewe hata ukiamua kufanya hilo ufanye kwa uzuri na usahihi zaidi, maana unajua wapi mwenzio aliangukia, unakuwa na nafasi ya kurekebisha.
SOMA; Una Uwezo Wa Kufanya Mambo Makubwa Sana, Anza Kuutumia Sasa.
Lakini pia ukitambua kuwa wanadamu tunaomba mambo yale yale kwa utofauti hautalinganisha uwezo wako na wa yule, utatambua kuwa wewe ni wewe na yule ni yule, lakini ukielewa kuwa muumba wako amekupa uwezo , akili na nguvu za kufanya kile anataka ufanye hautajilinganisha na wengine, hautajipima kwa kuangalia yule kafanya nini. Maana cha muhimu ni wewe kutambua uwezo wako, nafasi yako na kusimama hapo, kufanya kila jambo kuendana na nafasi yako, kujiona wewe kama wewe na kuona kuwa unao uwezo wa kufanya kile umeumbwa uje kufanya, ni vyema kuuliza, kuomba ushauri kwa wengine lakini katika hayo usisahau akili zako, au kuna ule usemi unasema ukiambiwa changanya na zako, pima , jihoji angalia kama ni kweli, kinafaa kwako, usiwe ni mtu wa ndio kila wakati, chunguza mambo, pima, amua.
Ndugu yangu hata ukiambiwa kitu usiwe ni mtu wa kukubali tu, kubali ikiwa kweli kinakubalika na una sababu ya msingi ya kukubali ikiwa kinyume kuwa mkweli na uonyeshe kile unaona na kuamini, usiogope kusema ukweli, usiogope kusimamia kile akili yako inakuridhisha kuwa ni kweli na sahihi hata kama hakuna mtu anayekuelewa lakini ikiwa dhamiri yako haikuhukumu uwe na amani na kusimamia hapo, usifanye jambo kwa kufuata mkumbo, fanya kwa kuwa una uhakika ndicho kitu unahitaji na ni kitu sahihi.
Makala imeandikwa na Beatrice Mwaijengo
+255 755 350 772