Habari za Jumapili wapenzi wasomaji wa AMKA MTANZANIA, ni wakati mwingine tena tunakutana kwa katika ukurasa huu ili kuzidi kujuzana na kukumbushana mambo mbalimbali na kuzidi kufanya dunia kuwa mahala pazuri pa kuishi. Ni matumaini yangu kuwa kwako wewe ambaye tumekuwa tukikutana hapa kila Jumapili yapo mambo ambayo umeyapata mahali hapa na kwa namna fulani yanakusaidia kuweza kuyatazama mambo kwa mtazamo mwingine.

 
Mara nyingi tumesoma na kusikia watu wakisema kuwa maisha yanaanza mtu anapofikisha miaka arobaini , na kwamba labda ikitokea umefikia umri huo na haujafanya lolote la maana basi ni kwamba wewe unakuwa umeshashindwa maisha na pengine inaonekana uwezekano wa wewe kufanikiwa unakuwa mdogo sana. Ndugu yangu inawezekana kuna ukweli kwenye sentensi hii kwa kiwango fulani lakini si kweli kwamba haiwezekani mtu kufanikiwa hata baada ya kufikia umri fulani, kitu cha msingi hapa ni wewe unavyopokea taarifa hizi, ikiwa mtu atakuambia wewe huwezi hiki nawe ukakubali kuwa huwezi itakuwa ngumu sana kwa wewe kuweza kufika pale ulikusudia mwanzoni, maana inakuwa hauna kitu ndani kinachokufanya uendelee kufanya kile unafanya, mfano hata mtu akija akakuambia labda unakaribia miaka arobaini na bado hakuna lolote la maana umelifanya , na wewe ukaipokea taarifa hii na kuikubali , ukairuhusu ikae kwenye akili yako au mawazoni mwako basi hii itakuwa ni sumu tosha ya kukufanya ushindwe kufika pale unatakiwa ufike, maana tayari unakuwa umekubali kushindwa, umekubali kwamba wewe kwako jua limezama na ni ngumu kwa wewe kuweza kufikiria zaidi na pengine kuweza kufikia malengo yako maana tayari wewe ushajiweka kwenye kundi la walioshindwa.
SOMA; Si Lazima Wakukubali Ndio Uendelee, Songa Mbele Ndugu Unaweza.
Ndugu yangu leo naomba niseme na wewe uliyefikia hatua hiyo katika maisha , ndugu tambua kuwa wanadamu kwa vipimo na viwango vyao wanaweza kukuambia lolote maana wao wanaona hivyo, na uwezo wao wa kuona unaishia mahali fulani tu, kuna vitu vinavyokuhusu hawavijui na hawawezi kuviona kamwe. Tambua yupo mtu wa ndani yako ambaye yeye haendeshwi na taratibu za hapa nje, yeye ana uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo, anaweza kufanya mambo makubwa sana ya kukufanya uushangaze ulimwengu hata wakati ambao kila mtu alikuwa amekukatia tama kama unaweza lolote, lakini tambua huyo mtu wa ndani hawezi kufanya lolote bila wewe kutambua hilo na kumruhusu akuendeshe, mara nyingi wengi tunakubali kuendeshwa na mambo ya nje, tunasikiliza sana tunayoambiwa na watu wa nje, tunakuwa wepesi wa kuamini tunayoambiwa na watu wengine. Lakini imekuwa ni vigumu sana kwa wengi kuweza kukubali na kugundua kuwa wanao uwezo mkubwa sana wa kufanya vitu hata kama kila mtu anawaambia vinginevyo.
SOMA; Mambo 6 Yatakayokufanya Uzidi Kuwa Bora Na Mwenye Mafanikio Makubwa.
Hebu kaa fikiria ni vitu vingapi umeshindwa kufanya kwa kuwa tu kuna mtu au watu walikuambia hauwezi , au waliona kwa umri wako wewe hauwezi kufanya jambo hilo, ni mambo mangapi umeshindwa kuyakamilisha kwa sababu hizo? Na je umechagua kuishi kwa kuendeshwa na watu wa nje maisha yako yote? Je hautambui uwezo mkubwa uliopewa na muumba wako? Ndugu yangu una uwezo mkubwa sana, hata hao wanaokuambia kuwa hauwezi hawajui huo uwezo ulio nao, wanakuhukumu kwa namna wanavyokuona tu. Usiwape ushindi kwa kukubali wanayosema, endelea kufanya kile unaona ni sahihi ili mradi unakifanya kwa usahihi na hata kama hakieleweki leo, ipo siku ikifika watakuelewa vyema tu na kukubali kuwa inawezekana kufanya lolote kwa wakati wowote ili mradi iwepo nia ya dhati na kuweza kutambua uwezo ulio nao, wakati mwingine usikubali kuzuiwa na mifumo ya duniani hapa, pia usitake kuwa mtu wa kawaida na kufanya kama wengine, wewe ni wa peke yako, na njia aliyopitia yule si lazima nawe uipitie hiyo ili uweze kufika kule uendako. Ndio maana ili uende Mbeya waweza kusafiri kwa ndege, gari moshi au hata gari la kawaida na mwisho wa siku wote utafika tu kuwahi kwako kufika kutategemea na aina ya usafiri utakaochagua na kuumudu. Hata sisi wanadamu kila mtu ana njia yake anayotumia kufikia mafanikio, usikariri wala kuiga, kuwa wewe daima utafika pale unaelekea.
Makala imeandikwa na Beatrice Mwaijengo.
+255 755 350 772