Kuna msemo ‘usemao mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’. Ni msemo ambao mara kwa mara huwafundisha wazazi umuhimu wa kulea watoto wao katika maadili mema na ya kimafanikio. Mara nyingi ikumbukwe kwamba wazazi huwa ndio wenye jukumu kubwa sana la kulea watoto wao tofauti na watu wengine kama walimu, madaktari na jamii, jukumu la kwanza huwa lipo kwa mzazi.
Hapa mzazi huwa ana kazi kubwa sana kumbuka tu si tu ya kumlea huyu mtoto katika mazingira hatarishi peke yake yatakayomdhuru, lahasha bali huwa ana jukumu pia la kuhakikisha mtoto huyu anakulia katika malezi bora ambayo yatampelekea awe na mtazamo chanya katika maisha yake siku zote.
Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya walezi ya watoto wanadai kwamba msingi mkubwa wa maisha ya binadamu huwa unajengwa kuanzia miaka 0-12. Hiyo ikiwa na maana kama mtoto wako utamlea vizuri kwenye umri huu basi elewa atakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa tofauti na yule ambaye atalelewa katika maadili mabovu.
Mpaka hapo unaweza ukawa umeona kwamba umri wa kuwa makini na mtoto wako ni umri huu ambao upo chini ya miaka 12. Katika umri huu, hapa wengi ndipo wanapoharibu au kutengeneza watoto wao. Kama unafikiri natania jaribu kufatilia wale watoto ambao wamevuka umri huu. Kwa tabia yoyote atakayokuwa nayo msingi wake mkubwa umetokea kwenye miaka 0-12.
Kwa kulifafanua hili vizuri, nikiwa na maana kama mtoto wako unaona ana tabia mbaya basi elewa kabisa ulimharibu tokea akiwa chini ya miaka 12 na wala usisingizie kitu chochote nje ya hapo. Na ndiyo maana ni hatari sana kwa mzazi kumpeleka mtoto wake chini ya umri huu shule za boarding kwa sababu huu ndiyo umri ambao mtoto anatakiwa apewe msingi bora wa maisha ikishindikana hapo basi tena.
Kwa hiyo kitu cha msingi katika umri ni kumpa mtoto malezi bora yatakamfanya ajitambue zaidi. Malezi haya kwa bahati mbaya tofauti na wengi wanavyofikiri hawezi kupewa na mwalimu au na mtu mwingine yoyote kwa ubora wa hali ya juu zaidi ya mzazi. Kwani ni  kipindi ambacho unatakiwa umfundishe mtoto wako juu ya mambo mengi kama upendo, kujali, utunzaji mzuri wa fedha, utu, kuokoa muda, kutoa, kujiamini na mambo mengineyo mengi.
Kwa kukosa mambo hayo baadae hupelekea mtoto huyu kuanza kuteseka kujifunza upya na tena kwa tabu lakini kumbe wakati alitakiwa kujifunza akiwa mdogo tena kwa urahisi . kwa kulijua hili leo unaweza ukaanza na kumfundisha mtoto wako namna ya kumjengea mtazamo chanya ambao utamfanya ajiamini na kufanya vizuri katika kila eneo la maisha kwa ubora wa hali ya juu.
Je, unawezaje kumjengea moto wako mtazamo chanya?
1. Msifie.
Jijengee tabia ya kumsifia mtoto wako kwa yale mambo madogo anayoyafanya. Acha kumkosoa na kiasi cha kwamba kujiona hafai. Hakikisha unampa sifa. Sifa hizo itakuwa nzuri sana kama utakuwa unampa hadharani mbele ya wenzake. Hilo litamfanya ajiamini zaidi na kujiona yeye anaweza. Kwa kadri utakavyoendelea kumsifia atajikuta mtoto wako anazidi kuwa mwenye uwezo mzuri wa kujiamini sana.
MSIFIE MTOTO WAKO  KWA KILE ANACHOFANYA.
2. Mwamini.
Mbali na kumpa sifa, lakini pia unaweza kumjengea mtoto wako tabia nzuri ya kujiamini kwa wewe kumwamini pia katika yale mambo anayofanya. Kama ni kazi umemwachia, mwache aifanye akiwa peke yake huku ukiwa unamfatilia sio sana ili kuona anafanyaje. Kwa kitendo cha kumfanyia hivyo atajiona kuwa yeye kumbe anaweza kufanya mambo makubwa na hivyo atajikuta akiwa anajiamini.
3. Mpe majina mazuri.
Weka utararibu wa kumpa mtoto wako majina mazuri yatakayomfanya ajiamini. Kila unapokutana naye mbali na kumuita jina lake halisi unaweza ukamuita ‘Pilot, shujaa, mshindi, mtaalamu’ na mengineyo mengi yatakamfanya ajiamini na kujiona bora kuliko. Epuka kumpa ‘lebo’ za kumuita majina kama vile ‘mjinga wewe, kichwa maji we’. Hiyo itamkatisha tamaa na itamfanya ashindwe kujiamini.
4. Mpe mazoezi ya kuongea mbele za wenzake.
Anapokuwa na wenzake tafuta kitu cha kuongea na kumfanya aongee mbele za wenzake. Hata kama anaona aibu mpe moyo wa kumfanya aendelee kuongea. Kwa kitendo hicho kitamfanya azidi kujiamini sana na itampelekea kweli kuongeza uwezo wake mkubwa wa kujiamini siku hadi siku. Hata wakati mwingine hata kuwa na ule woga mkubwa ndani yake wa kuzungumza.
Unaweza ukafanya mambo mengi yatakayomfanya mtoto wako azidi kujiamini. Lakini kwa leo fanyia kazi kwanza hayo na hakikisha mtoto wako anaweza kujiamini kwa namna yoyote ile. Hiyo itamsaidia sana kwa maisha yake yote ya baade.
Kwa makala nyingine nzuri pia tembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa ujifunza na kuhamasika kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Simu; 0713 048 035,