Karibu kwenye kipengele hiki cha USHAURI WA CHANGAMOTO mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Naamini uko vizuri sana rafiki yangu na licha ya changamoto unazokutana nazi, bado unaendelea kuweka juhudi. Nina hakika bado hujakata tamaa na ndio maana sasa hivi unasoma hapa. Nakupongeza sana kwa hilo na nakusihi uendelee kuwa imara kwani kadiri unavyozidi kuzivuka changamoto ndivyo unavyozidi kukua na kuyakaribia mafanikio makubwa.
Leo katika ushauri wa changamoto tutaangalia changamoto moja kubwa sana na inayowaathiri watu wengi. Changamoto hii imewarudisha nyuma wengi, wengi wamekata tamaa na kuachana kabisa na malengo na mipango yao mikubwa. Hii ni kwa sababu changamoto hii ni kubwa sana, kwa kuwa inatokana na watu ambao wana ushawishi mkubwa kwako. Changamoto tutakayoangalia leo ni kukatishwa tamaa na watu wako wa karibu.

 
Kabla hatujaingia ndani zaidi kwenye changamoto hiyo na kujadiliana kwa kina ni hatua zipi za kuchukua, tupate kusoma maoni ya msomaji mwenzetu ambaye ametuandikia kuomba ushauri;

Changamoto kubwa ni magonjwa ya mazao na mifugo pia familia na ndugu wananikatisha tamaa ya kujiajiri wanataka niajiriwe. Efrem E. M.

Hayo ndiyo maoni aliyotuandikia msomaji mwenzetu kuomba ushauri juu ya changamoto hizo anazopitia.
Tukianza na changamoto ya kwanza ambayo ni kuhusu magonjwa ya mazao na mifugo, hapa unahitaji kujua kwa undani kuhusu mazao au mifugo unayoweka na kujua ni dawa gani zinahitajika ikiwa ni pamoja na chanzo. Pia jua kwa eneo unalofanyia kilimo ni magonjwa gani yaliyopo sana na njia za kuondokana nayo au kuyazuia.
Unaweza kujifunza hayo kupitia wataalamu wa kilimo hasa wa eneo husika au pia kutoka kwa wakulima wengine wanaofanya vizuri kutoka kwenye eneo hilo. Kama umelima au kufuga mara ya kwanza na magonjwa yakakuletea hasara, usikate tamaa hapa sasa ndiyo unahitaji kuendelea kwa sababu tayari umeshajifunza kwamba kuna magonjwa na hivyo ni muhimu kuchukua hatua mapema.
SOMA; Kanuni Ya Uhakika Itakayokusaidia Kutimiza Ndoto Zako Zote.
Kukatishwa tamaa na ndugu.
Tukiingia kwenye changamoto ya pili, ambayo ni kukatishwa tamaa na ndugu, hii ni changamoto kubwa sana ambayo unahitaji maarifa na juhudi kubwa ili kuweza kuivuka. Hii ni kwa sababu ndugu zako ni watu wako wa karibu sana na chochote wanachosema kinaweza kuwa na athari kubwa sana kwako.
Ili kuondokana na changamoto hii ya kukatishwa tamaa na ndugu, zingatia mambo haya muhimu sana.
1. Siyo kosa lao kukukatisha tamaa.
Ndugu zako wanapokukatisha tamaa kuhusu kujiajiri na kukushawishi uajiriwe, siyo kosa lao, bali hiko ndio kitu ambacho kimezoeleka na wao ndio wanajua hiyo ndiyo njia pekee ya mafanikio. Kwa muda mrefu jamii zetu zimekuwa zikiona ajira kama njia pekee ya kuwa na maisha bora na hivyo yeyote anayeiacha ajira amekuwa anaonekana kama hayupo sawa.
Ndugu zako wanapokukatisha tamaa kuhusu kujiajiri wao wanaona wanakusaidia sana kwa sababu wanaona unapotea na kama kuna wengine ambao walishajiajiri na wakashindwa, basi wanaona moja kwa moja na wewe utashindwa. Waelewe ndugu zako kwenye hili na jua sio kosa lao bali nao pia wamelibeba hili kutoka kwenye jamii.
2. Wasikilize.
Ndugu zako wanapokukatisha tamaa kuhusu kujiajiri, wasikilize kwa makini. Zisikilize sababu zao kwa nini wanafikiri utashindwa iwapo utajiajiri. Wakati mwingine wana hofu ambazo zinaweza kuwa kweli. Kwa kuwasikiliza vizuri utajua ni mambo gani muhimu ya kuzingatia ili usishindwe kwenye kujiajiri.
Labda wana mfano wa mtu ambaye aliwahi kujiajiri ila akashindwa, waulize mswali zaidi juu ya mtu huyo, taka kujua sababu hasa za yeye kushindwa, ili na wewe usiishie kama yeye. Kwa kuwasikiliza utajifunza mambo mengi sana.
3. Usikubaliane nao na waoneshe kwa vitendo.
Ukishawasikiliza ndugu zako juu ya hofu walizonazo kuhusu wewe kujiajiri, usikubaliane nao na wewe ukaacha kujiajiri. Kama kweli unajua ni nini unafanya, na umeshajitoa kwamba ni lazima upate kile unachotaka, basi endelea na mipango yako, weka juhudi kubwa kuhakikisha unapata kile unachotaka.
Ni vizuri sana kama utawaonesha kwa vitendo kwamba inawezekana badala ya kubishana nao kwa maneno. Hivyo kuwa mtu wa vitendo, wakati wanasema haiwezekani wewe kazana kufanya, watakapoanza kuyaona majibu mazuri watanyamaza wao wenyewe. Ila kama utataka kushindana nao kwa maneno, utachoka bure na watakushinda kwa sababu huenda wana mifano mingi sana ya waliojiajiri na wakashindwa.
SOMA; Tabia 7 Zitakazo Kufanya Uendelee Kuwa Maskini, Hata Kama Una Kipato Kikubwa.
Kwa ujumla unachotakiwa kujua ni kwamba hakuna kitu ambacho hakina changamoto kwenye maisha, na changamoto hazipo kwa ajili ya kutukatisha tamaa, bali kutukuza na kutukomaza ili tuweze kufika ngazi za juu zaidi. Pale ndugu zako wanapokukatisha tamaa, mara nyingi wanaongozwa na hofu zao. Usikubali kununua hofu hizi, wasikilize na weka juhudi kwenye kile ulichochagua kufanya. Hakuna mtu anayekujua wewe kama unavyojijua wewe mwenyewe. Hivyo licha ya watu kuwa na mifano mingi ya walioshindwa, bado hawakujui wewe, na huwezi kuishia kama wengine walivyoishia.
Nakupa moyo kuendelea na safari uliyochagua, hata kama dunia nzima ipo kinyume na wewe. Kama ni sahihi kwako na unajua itawasaidia wengine pia, weka juhudi na usikubali kurudishwa nyuma. Utakapofanikiwa wale waliokuwa wanasema huwezi au utashindwa, watakuwa wa kwanza kupiga makofi na kusema walijua utaweza.
Nakutakia kila la kheri kwenye safari ya kujiajiri ambayo umechagua.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.