Habari mpenzi msomaji wa Amka Mtanzania? Na karibu katika makala yetu ya leo ambapo tutazungumzia umuhimu wa kuwa na shukurani katika maisha yako. Shukurani ni neno dogo lenye maana kubwa sana katika maisha yetu sisi wanadamu. Nini maana ya neno SHUKURANI?
Shukurani ni neno au ishara inayoonesha kuridhika na wema aliotendewa mtu. Hii ni kulingana na Tuki toleo la 3, shukurani ni asante kwa maana ya kawaida pia. Shukurani ni falsafa ambayo kila binadamu huwa anaitumia katika maisha yake ya kila siku na ni falsafa yenye maana sana katika maisha yetu kila siku.
Ili uweze kufanikiwa kifuraha na kusonga mbele kimaendeleo huna buni kuanza kuwa na shukurani katika maisha yako ya kila siku. Huwezi kufurahia maisha kama wewe huna shukurani na hali ambayo unayo sasa. Unakosa shukurani na maisha yako ndio maana unaanza kuishi maisha ambayo siyo yako maisha ya utumwa. Shukurani inakupa shauku ya kusonga mbele, inaponya majeraha ya nafsi yako. 

 
Unatakiwa kuwa na shukurani na siyo kulalamika na kutoa maneno yenye laana katika maisha yako na kutokuwa na shukurani katika maisha yako itakupelekea kukata tamaa katika maisha yako badala ya kusonga mbele. Sema asante, hesabu Baraka ulizonazo katika maisha yako au mazuri ambayo Mungu amekujalia kulingana na mapenzi yake. Acha kuhesabu shida, matatizo au madhaifu uliyonayo. Shukuru kwa kila jambo, shukuru kwa kile ambacho unapata ndio sasa ndio utapata hamasa ya kusonga mbele zaidi.
Kila binadamu ana udhaifu wake, na udhaifu ni daraja linalotuvusha kuelekea sehemu yenye ukamilifu, tunajifunza katika udhaifu na udhaifu wako utakufanya kuwa na furaha kama ukiwa ni mtu wa kujifunza kupitia udhaifu wako. Unatakiwa kushukuru hata kwa udhaifu wako kwani udhaifu wako utakupa faraja. Changamoto au udhaifu ndio zinatufundisha tuwe bora na kupita njia sahihi.
Kuwa na shukurani inabadili kabisa maisha yako. Kusema asante huwa inawafanya watu kuwa wenye furaha. Huwa inaimarisha uhusiano, inaboresha afya, inapunguza msongo wa mawazo lakini pia shukurani inakupa shauku, inakupa uwezo wa kupambanua au kufanya utambuzi. Na kitendo cha kusema shukurani kinaongeza kiwango cha furaha maradufu. Sema asante hata kwa zawadi ya uhai kwani uhai ndio utaweza kutimiza dhumuni lako hapa duniani.
Unahitaji kutafuta furaha katika vitu vidogo badala ya kusubiria mafanikio makubwa mpaka uwe na kitu Fulani. Mfano kuna watu wengine wamekosa kabisa shukurani katika maisha yao utasikia kauli kama hizi, nikiwa na nyumba nitakuwa na furaha, nikioa au kuolewa nitakua na furaha, nikiwa na mtoto nitakuwa na furaha nikiwa na gari nitakua na furaha au nikipata kazi nitakua na furaha na mengine mengi yanayohusiana na haya. Chanzo cha furaha ni kuwa na shukurani katika kile ambacho unacho sasa na maisha yako ya kila siku na siyo vinginevyo.
Sema asante, kuwa na shukurani na maisha unayoishi yatakusaidia kuweka mambo yako katika mtazamo sahihi. Muda mwingine mambo hayawezi kwenda kama vile unavyotaka utakumbana na wakati mgumu. Lakini wakati mgumu huwa inabeba mbegu ya faida. Kwa kila jambo au changamoto jiulize nini kizuri kuhusu kitu hicho? Nini unaweza kujifunza kupitia kitu hiko? Nini unaweza kufaidika na kupitia kitu hiko au jambo hilo?
Anza mazoezi ya kuwa na shukurani kwa kuandika orodha ya mambo kumi (10) kila siku ambayo umekuwa na shukurani nayo. Fanya zoezi hili asubuhi au usiku kabla ya kwenda kulala. Kuna watu wengi pengine katika maisha yako wamekua msaada kwako au wamekua chachu ya maendeleo katika maisha yako au kuna mtu alikupa au anakupa ushawishi chanya katika maisha yako na hukuweza kumshukuru vema anza leo zoezi la kumuandikia barua mtu ambaye amekupa ushawishi chanya katika maisha ambayo unayo sasa. Najua huwezi kukosa mtu hata kama kuna mwandishi anagusa maisha yako kupitia makala, vitabu na mafunzo mbalimbali mwandikie barua ya shukurani. Ukiwa ni mtu kufanya hivi utaona jinsi maisha yako yanavyobadilika.
’ if the only prayer you said in your whole life was thank you that would suffice’’– Meister Ekhart Kama asante/shukurani ndio ilikuwa sala uliyokuwa unasema katika maisha yako yote basi hiyo inatosha. Kwa hiyo shukurani ni kama sala katika maisha yako.
‘’ Be thankfull for what you have, you’ll end up having more. If you concentrate on what don’t have, you will never, ever have enough’’ – Oprah Winfrey
Kuwa na shukurani katika kile ulichonacho,utaishia kuwa na vingi zaidi. Ukiendelea kufikiria katika kile ambacho huna, kamwe hutoweza kupata kinachokutosheleza.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com