Linapokuja swala la fedha, kila mtu ana hisia tofauti, na hisia hizi zinatokana na malezi ambayo tumepata kwenye jamii ambazo tumekulia. Na katika hisia hizi, nyingi huwa ni hasi, kwamba fedha ni kitu kibaya au kitu ambacho hakihitaji kujadiliwa mara kwa mara.
Kwa kusoma tu hiko kichwa cha habari kwamba kuna namna unaweza kuwa sumaku ya fedha, kuna watu tayari wameshakuwa hasi, kwamba kwa nini huyu Makirita anaandika kuhusu fedha, kwanza yeye anazo kiasi gani, na mengine mengi. Nakuelewa kama wewe ni mmoja wa watu wenye hisia hizi hasi, kwa sababu halikuwa kosa lako kuwa nazo, ila kama utasoma hapa mpaka mwisho na ukaendelea kuwa na hisia hizo, hapo sasa ni kosa lako.
Tutakachokwenda kujifunza hapa ni kwamba wewe unaweza kuivuta fedha ije kwako, na kwa njia za kawaida kabisa, wala sio kwa nguvu ambazo hazieleweki kama wengi wanavyodanganyana. Zipo njia zilizodhibitishwa kisayansi ambazo zinafanya kazi kwa watu wote bila ya kujali kiwango cha elimu, rangi, au unatokea familia gani.

http://www.amkamtanzania.com/p/kuwa-tajiri.html

 
Nina hakika umewahi kusikia usemi kwamba mwenye nacho huongezewa, ya kwamba tajiri ataendelea kuwa tajiri na masikini ataendelea kuwa masikini. Huu ni usemi uliowekwa na watu walioliona hilo likiendelea kwa wengi, lakini wakashindwa kulichimba kwa undani. Ukweli ni kwamba tajiri anaendelea kuwa tajiri kwa sababu ameshakuwa sumaku ya fedha, anajua jinsi ya kuzivuta zije kwake. Na masikini anaendelea kuwa masikini kwa sababu hajaijua mbinu ya kuzivuta fedha zije kwake. Je unataka kuzijua mbinu za kuvutia fedha zije kwako?
Karibu tujifunze mambo haya kumi unayoweza kuanza kufanya leo kwenye maisha yako na ukazivutia fedha kuja kwako.
1. Kuwa mkarimu, wasaidie wengine kwa chochote unachofanya.
Njia ya kwanza kabisa ya kuzivutia fedha kuja kwako ni kuwa mkarimu. Chochote kile ambacho unakifanya kwenye maisha yako, iwe kazi au biashara, hakikisha lengo la kwanza ni kuwasaidia watu. Unawasaidia watu kwa kuwapa huduma ambazo ni bora na zinawaondolea maumivu wanayopata sasa au kuwapatia mahitaji wanayokosa sasa.
2. Kuwa na shukrani kwa fedha ulizonazo.
Haijalishi ni fedha kiasi gani unapata, hata kama ni kidogo sana, kitu muhimu kabisa ni kushukuru. Shukuru kwamba umepata nafasi ya kupata kiasi hiko cha fedha, ukijua ya kwamba kuna wengine wengi ambao hawajapata nafasi kama yako. Ukikutana na shilingi mia njiani wakati unapita, iokote kwa furaha.
Unapokuwa mtu wa shukrani unakaribisha zaidi kile ambacho unashukuru. Wengi huwa walalamikaji kwa fedha kidogo wanazopata na hapa wanafukuza zaidi nafasi yoyote ya kupata zaidi. Kuwa mtu wa shukrani, utavutia fedha nyingi zaidi.
3. Usiwaonee wivu wengine.
Kama kuna watu wengine wenye fedha nyingi kuliko wewe, usiwaonee wivu, badala yake wabariki. Mafanikio ya wengine siyo sababu ya wewe kushindwa. Na unapojenga wivu dhidi ya wengine unaiambia akili yako kwamba kuwa na fedha siyo kitu kizuri na hivyo inazikimbia fursa za fedha. Lakini unapowabariki wale wenye fedha kuliko wewe, unaifungua akili yako na kuziona fursa nyingi zaidi za kifedha.
4. Usijione mwenye hatia kwa kuwa una fedha nyingi.
Moja ya vitu vinavyowafanya wengi kutokuvutia fedha ni kujiona kama wakiwa na fedha nyingi basi wale wanaowazunguka hawatajisikia vizuri. Huku ni kujiona mwenye hatia kama utakuwa na fedha. Na kujiona mwenye hatia kutaiambia akili yako iepuke mazingira yoyote yanayoweza kukuletea fedha zaidi. Jione kuwa wa msaada kama utakuwa na fedha nyingi zaidi, na utazivutia zaidi na zaidi.
5. Kuwa na mapenzi makubwa kwenye kile unachofanya.
Chochote unachofanya kwenye maisha yako, jambo muhimu kabisa ni ukipende sana. Penda kile unachofanya. Kuna usemi unasema kama kazi yako ni kitu unachopenda, hutafanya kazi kwenye maisha yako. Na mwingine fanya kile unachopenda na fedha haitakuwa tatizo kwako. Fanya kitu unachopenda kufanya, iwe ni kazi au biashara, na weka moyo wako wote kwenye kitu hiko na hakuna kitu kinaweza kukuzuia wewe kupata fedha zaidi.
Wengi wamekuwa wakifanya vitu ambavyo hawavipendi ili tu wapate fedha, na wanashangaa kwa nini hawazipati, jibu ni kwa sababu wanazifukuza wao wenyewe. Unapofanya unachopenda, unazivutia fedha kuja kwako.
6. Ukipoteza fedha, usijione mnyonge na kulalamika.
Pale unapopoteza fedha, na lazima utapoteza iwe ni kwa hasara au kudhulumiwa, usianze kulalamika kwa nini inatokea kwako tu, bali jifunze ni nini kimepelekea wewe kufikia kwenye hali hiyo. Na hakikisha hurudii tena makosa ambayo uliyafanya awali na yakakufikisha hapo. Labda unahitaji kuwa makini zaidi, labda unahitaji kuangalia wale unaowaamini na mengine mengi.
Ukiishia tu kulalamika na kuona wewe huna hatia, utaendelea kurudia makosa yale yale na kamwe hutazivutia fedha kuja kwako.
7. Siku zote timiza ahadi zako.
Fanya kile ambacho umeahidi utafanya, na kikamilishe kwa wakati na kwa ubora. Usiwe mtu wa kuahidi kwa maneno na wakati wa matendo huonekani. Timiza ahadi zako na utavutia fedha nyingi zaidi kwako. Iwe ni kwenye kazi au kwenye biashara, unachomwahidi mwajiri wako kitimize, na hatakuwa na jinsi bali kukuthamini zaidi. Chochote unachomwahidi mteja wako timiza, na atapata huduma bora zitakazomfanya awe mteja wako wa kudumu na kuwaambia wengine wengi zaidi.
8. Tegemea kuwa tajiri.
Haijalishi maana yako ya utajiri ni nini, tegemea kuwa tajiri. Na usiishie tu kutegemea bali kuwa na mpango kabisa wa jinsi gani utafikia utajiri wako, kipato chako kiwe kiasi gani, uwekeze kiasi gani ili uweze kufikia utajiri. Utajiri hauji kama ajali, ni zao la malengo, mipango na juhudi kubwa. Kama hutegemei kuwa tajiri huwezi kuvutia fedha kwako.
9. Amini kwenye wingi.
Kuna fedha nyingi sana kwenye dunia hii, nyingi mno, japo wengi wanakushawishi kwamba kuna uhaba wa fedha, siyo kweli. Amini kwenye wingi wa fedha na unachohitaji ni wewe kuja na wazo zuri la kuwasaidia watu na watakuwa tayari kukupa fedha zaidi na zaidi. Dunia haina uhaba wa fedha na mali, bali ina uhaba wa mawazo mazuri ya kuboresha maisha, njoo na mawazo mazuri na utavutia fedha zaidi na zaidi.
10. Kuwa mkweli kwako, kuwa halisi.
Linapokuja swala la fedha na utajiri, watu wengi sana sio wa kweli kwao binafsi na hata kwa wengine. Watu wengi sio halisi, bali ni feki, wengi wanaigiza maisha ya utajiri na wakati hali zao sivyo zilivyo. Wengi wanakazana waonekane kwa nje wana utajiri kumbe ndani yao mambo ni magumu. Watu wanaingia kwenye madeni makubwa ili tu kuonekana nao wapo. Hii sio njia nzuri ya kuvutia fedha zije kwako, badala yake utazikimbiza zaidi. Njia bora ya kuvutia fedha kuja kwako ni kuwa mkweli, na kuwa halisi. Ishi yale maisha ambayo ni yako, usitake kuleta maigizo, hakuna yeyote unayemfaidisha na badala yake unajiumiza mwenyewe.
Hizo ndiyo njia kumi za kuzivutia fedha zije kwako na hatimaye uwe tajiri. Wote tunajua fedha ni muhimu, na kadiri unavyokuwa nazo nyingi inakuwa rahisi kwako kupata mahitaji ya msingi ya maisha yako, na hata kuwasaidia wengine pia.
Njia zote hizi kumi zinaanza na wewe binafsi, haiangalii elimu yako ni kiasi gani, rangi ya ngozi yako, au kabila unalotokea. Pia haziangalii umri wako au umetoka familia ya aina gani. Ni wewe ufanye maamuzi leo na uanze kutekeleza hayo. Na ujue inachukua muda, siyo jambo la kutokea mara moja, hivyo kuwa mvumulivu.
Neno la mwisho kabisa ninalotaka kukushirikisha ni kukuambia uchukue hatua, iwe utayafanyia haya kazi, au utayakataa na kuendelea na maisha yako ya sasa. Maamuzi ni yako wewe mwenyewe. Lakini jua hakuna mtu atakayekuja kukutoa hapo ulipo, utajitoa wewe mwenyewe.
MUHIMU; Kuna sababu 25 ambazo zinawafanya watu wengi kushindwa kutoka kwenye umasikini na kuelekea kwenye utajiri. Unaweza kuzijua sababu hizo na jinsi ya kuondokana nazo kwa kubonyeza haya maandishi.
Nakutakia kila la kheri,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz