Habari rafiki? Ni matumaini yangu uko vizuri sana na unaendelea kuwa bora kadiri siku zinavyozidi kwenda. Kama ndiyo basi hongera sana kwa sababu maisha ni mwendo, kadiri unavyokwenda ndivyo unavyotakiwa kuwa bora. Ukiacha kuwa bora maana yake umechagua kurudi nyuma.
Wote tunajua ya kwamba kuna changamoto nyingi sana kwenye maisha, hasa pale unapochagua kuishi maisha ya mafanikio. Kuna changamoto ambazo zinaanzia ndani yako mwenyewe, ambazo ndizo changamoto nyingi sana. Na pia kuna changamoto zinazotoka nje yako.
Na pia tumeshajifunza sana na tunajua ya kwamba njia bora ya kupambana na hizi changamoto siyo kuzikimbia, au kuomba zisitokee, bali kuweza kuzitatua na kupata majibu bora. Ni kupitia majibu haya ndiyo tunakua zaidi na kuongeza ufanisi wetu kitu ambacho kinatupeleka kwenye mafanikio makubwa.
Lakini pia siyo changamoto zote zipo ndani ya uwezo wetu kutatua. Na mara nyingi unapokuwa na changamoto hisia nazo zinaingilia katikati na hivyo kushindwa kufanya maamuzi sahihi ya hatua gani uchukue. Na hapa ndipo unapohitaji msaada wa watu wengine, hasa kwa njia ya ushauri.
Katika jambo lolote lile, vichwa viwili ni bora zaidi yakichwa kimoja, ila kama vichwa hivi vitakuwa vinaelewa kweli ni kitu gani hasa kinaendelea na ni wapi ambapo mtu anatakiwa kufika. Hivyo katika changamoto na hata kwa yale makubwa ambayo mtu unachagua kufanya, ushauri ni muhimu sana ili kufanikiwa. Na hapa ndipo inakuja changamoto juu ya changamoto.

 
Kwenye mazingira yetu ya Kitanzania, hakuna kitu rahisi mtu kupata kama ushauri. Yaani anza tu kuongea na kabla hata hujamaliza kujieleza tayari watu wameshaanza kukushauri. Na ushauri huu ni bure kabisa, mpaka pale utakapoanza kuutekeleza, ndipo utakapoona gharama kubwa ya ushauri wa aina hii.
Kuna changamoto kubwa sana ya kupata ushauri bora katika mazingira yetu ya Kitanzania. Katika makala hii ya leo tutaona jinsi unavyoweza kupata ushauri bora na utakaokuwezesha kufikia mafanikio makubwa. Katika kipindi hiki kumekuwa na watu wengi sana ambao wanatafuta ushauri bora, na hivyo makala hii itakusaidia kama na wewe ni mmoja wa watu hawa.
Kwa kuanza jua ya kwamba siyo kila mtu anaweza kukushauri kwa jambo lolote unalochagua kufanya. Na kwa kuwa wazi zaidi sehemu kubwa ya watu wanaokuzunguka hawawezi kukushauri vizuri, hii ni kwa sababu wao wenyewe wana hofu zao nyingi hivyo hawana muda wa kuongeza na hofu zako, hivyo wataishia kukuambia kile ambacho ni rahisi kufanya. Hivyo ni muhimu sana ujue ni mtu gani sahihi wa kukushauri. Wakati mwingine ukitaka kumwomba kila mtu ushauri utaishia kukata tamaa kwa sababu wengi watakuonesha kwamba haiwezekani au unakosea. Hivyo ni muhimu uchague kwa makini ni watu gani ambao unaona wanafaa kukushauri. Na hapa angalia mambo mengi, angalia mtazamo wa mtu huyo kwenye maisha kwa ujumla, je ni mtu ambaye anaona mambo yanawezekana (optimist) au ni mtu ambaye anaona mambo hayawezekani (pessimist). Angalia utendaji wa mtu kwenye mambo yake mwenyewe, hata kama unachomwomba ushauri siyo anachofanya, angalia kile anachofanya, je anasimamia misingi gani? Unapompata mtu ambaye anasimamia misingi mizuri, bila ya shaka atakupa ushauri mzuri.
SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kupata Ushauri Bora Kwa Mafanikio Ya Biashara Yako.
Kitu cha pili kuzingatia kwenye ushauri ni upate mtu wa kukusikiliza, bila ya kukuhukumu au kuamua kuelewa anavyotaka yeye mwenyewe. Unahitaji mtu akusikilize kwa kile unachoongea, na aelewe kwa kile unachopitia. Bila ya mtu kukusikiliza vizuri, hawezi kukupa ushauri ambao ni bora kwako. Na kwa bahati mbaya sana, jamii ya sasa watu wanaosikiliza wameadimika sana. Kila mtu yuko bize, na kumpata mtu ambaye atakusikiliza wewe unajieleza kwa nusu saa, ni vigumu sana. Yaani nusu saa ipite mtu hajaangalia wasap, facebook au instagram? Ni adhabu kubwa kwa wengi. Unahitaji kupata mtu atakayeweka mambo yote pembeni na akusikilize wewe ili aweze kuelewa vizuri na kukupa ushauri ambao ni bora.
Kitu cha tatu na muhimu kuzingatia unapotaka ushauri ni uwe tayari kugharamika. Ni lazima uwe tayari kulipia ushauri kama unataka kupata ushauri bora na utakaokuwezesha kufikia mafanikio. Kumpata mtu ambaye ana mtizamo chanya wa kuona mambo yanawezekana na ambaye yupo tayari kusikiliza bila ya kuhukumu, siyo kitu rahisi. Kwa sababu watu wa aina hiyo tayari wapo bize na mambo yao mengine. Hivyo ili upate muda wao ni lazima uwe tayari kulipa gharama. Najua unaweza kushangaa hili kwa sababu umezoea kupata ushauri wa bure huko mitaani. Lakini nataka nikuambie hili moja na kama hutalichukua utakuja kulikumbuka, USHAURI WA BURE HAUTAKUGHARIMU CHOCHOTE, MPAKA PALE UTAKAPOANZA KUUTUMIA. Ushauri wa bure ni ushauri wa juu juu ambao unamfaa kila mtu, sasa wewe huhitaji ushauri unaomfaa kila mtu, badala yake unahitaji ushauri unaokufaa wewe kutokana na kile unachopitia au kule unakotaka kufika. Na ushauri huu una gharama ambazo unatakiwa kulipia.
SOMA; USHAURI; Taratibu Za Kupata Ushauri Bora Na Gharama Zake.
Hayo ndiyo mambo muhimu ya kuzingatia kama unataka kupata ushauri bora na utakaokuwezesha kufikia mafanikio makubwa. Yazingatie ili ushauri unaoupata uweze kukusogeza mbele na siyo kukurudisha nyuma.
Karibu sana kwa jambo lolote ambalo unahitaji ushauri, tunaweza kuzungumza kwa pamoja na kuona ni hatua zipi muhimu kwako kuchukua ili kupata matokeo bora zaidi.
Nakutakia kila la kheri katika kufanyia kazi haya uliyojifunza leo,
TUPO PAMOJA,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz