Habari rafiki? Nina imani uko vizuri na mambo yako yanaendelea kwenda vizuri kutokana na juhudi unazoendelea kuweka kila siku.
Karibu kwenye kipengele chetu cha ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zinatuzuia kufikia yale maisha ya ndoto zetu. Wote tunajua ya kwamba changamoto ni sehemu ya maisha, hatupaswi kuzikimbia wala kuzilalamikia, badala yake tunahitaji kuzitatua.

PATA KITABU HIKI KITAKACHOKUWEZESHA KUANZISHA NA KUKUZA BIASHARA YAKO UKIWA BADO UMEAJIRIWA. BONYEZA HAPA KUKIPATA.

 
Leo tutakwenda kuangalia changamoto ya kuanza biashara kwa mtaji kidogo na mambo ya kuzingatia ili biashara hiyo uweze kukua na kumfikisha mtu kwenye maisha ya ndoto yake. Lakini kabla hatujaingia kwenye hilo kiundani tupate maoni kutoka kwa msomaji mwenzetu ambaye amekutana na changamoto hii;

Mimi ni kijana ninayeishi katika mazingira ya hali ya chini nimebahatika kumaliza elimu ya sekondari ila sikufanikiwa kuendelea na elimu ya juu hivyo niliamua kwenda kujiunga na elimu ya utalii. Sikubahatika kuajiriwa sehemu yeyote, nimefanya shughuli mbalimbali nikabahatika kupata kiasi cha shilingi laki mbili ambazo nilikuwa nawaza nianzishe biashara ndogo itakayonisaidia kuendesha maisha ila mpaka sasa hivi sijajua nianzishe biashara ipi. Hivyo ninaomba msaada wenu tafadhali kwa sasa nipo dar es salaam maeneo ya sinza.
D. L Nestory.

Kama ambavyo tumeona kwenye maelezo ya msomaji mwenzetu, ana mtaji kidogo na anataka kuanza biashara ambayo itamsaidia kuendesha maisha yake.
Kabla sijamshauri msomaji mwenzetu kuhusu biashara gani afanye, kuna mambo muhimu nahitaji ayajue na kuyazingatia sana kwenye biashara yoyote atakayokwenda kufanya;

1. Kwa kuanza biashara na mtaji kidogo atahitaji kuweka juhudi kubwa sana kwenye uendeshaji wa biashara hiyo.
Kadiri biashara inavyoanza kwa mtaji kidogo, ndivyo uendeshaji wake unavyokuwa mgumu na changamoto zinakuwa nyingi. Hivyo mtu unapoingia kwenye biashara kwa mtaji kidogo unatakiwa kujiandaa kiasi cha kutosha. Utahitajika kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja, kitu ambacho kitakuchosha sana.
Pia unatakiwa kuelewa kwamba kwa kuanza biashara na mtaji kidogo itakuchukua muda mrefu zaidi mpaka kufikia yale mafanikio ambayo umepanga kuyafikia kibiashara.
Ni muhimu kujiandaa kwa hili ili mambo yanapokuwa magumu usikate tamaa, badala yake ujue ndiyo kitu ulichotegemea kukutana na cho na hivyo kuongeza juhudi zaidi.

SOMA; Huyu Ni Kijana Wa Kitanzania Aliyeanza Biashara Kwa Mtaji wa Milioni Nne na Baada Ya Miaka Mitatu Ana Zaidi Ya Milioni Mia Moja.

2. Biashara haijali umetokea wapi au umepitia magumu kiasi gani.
Msomaji mwenzetu ametueleza changamoto alizopitia na maisha ya chini ambapo ametokea. Hii ni nzuri katika kuweka maelezo yako ya kuomba ushauri, lakini ni kitu cha kuweka mbali pale unapoanza biashara. Watu wengi wamekuwa wakifikiri kwamba kwa sababu wamepitia maisha magumu basi biashara inapaswa kuwa rahisi kwao. Unachotakiwa kujua ni kwamba biashara haijali umetokea wapi au umepitia mambo magumu kiasi gani.
Biashara itakuja na changamoto zake kama ilivyo kwa watu wengine. Hivyo unahitaji kuweka hadithi yako ngumu pembeni na kujiandaa kupambana na biashara. Usiingie kwenye biashara ukiwa mnyonge, ingia ukiwa unajiamini ya kwamba unaweza kufanya makubwa na hupo tayari kukata tamaa hata kama mambo yatakuwa magumu kiasi gani.

3. Huna uhuru mkubwa wa kuchagua.
Unapoanza biashara kwa mtaji kidogo, huna uhuru mkubwa wa kuchagua ni biashara ya aina gani unataka kufanya, badala yake unahitaji kuingia kwenye biashara yoyote ambayo inaweza kukuletea faida mapema. Ukishapata biashara ya aina hii unaweka juhudi zako na biashara inapokua ndipo unaanza kuwa na uhuru wa kuingia kwenye zile biashara ambazo unazipenda.

Biashara unazoweza kuanza na mtaji kidogo wa tsh laki mbili.
Kwa msingi huo ambao tumeujenga hapo juu sasa tuangalie biashara ambazo msomaji mwenzetu anaweza kuzianza na mtaji kidogo wa laki mbili. Kuna biashara nyingi ndogo ndogo hasa kwa maeneo ya mjini kama dar es salaam ambazo mtu anaweza kuanza kwa mtaji usiozidi laki mbili. Unaweza kuangalia kwenye eneo ulilopo watu wana changamoto gani au mahitaji gani ambayo ni makubwa na kuweza kuwasaidia watu kuyatimiza.

Zifuatazo ni baadhi ya biashara ambazo mtu anaweza kuanza kwa mtaji kidogo kwa dar es salaam.

1. Kuuza nguo kwa kutembeza mitaani.
Hii ni biashara ambayo unaweza kuianza kwa mtaji kidogo. Kwa biashara hii unahitaji kwenda kwenye masoko makubwa ya nguo au viatu, iwe ni mtumba au ‘special’ chagua nguo nzuri na kisha kuzunguka mitaani kuuza nguo hizo. Kadiri unavyopata nguo nzuri na jinsi unavyoweza kuwa na kauli nzuri ndivyo unavyoweza kufanya mauzo makubwa. unahitaji kuweza kuongea vizuri na watu, na kuwa na ushawishi kwa nini mtu anunue. Nguo za wanawake na watoto zina wateja wengi zaidi ukilinganisha na za wanaume.

2. Kuuza genge au matunda.
Biashara nyingine ambayo mtu anaweza kuianza kwa mtaji kidogo ni kufungua genge la mahitaji ya msingi ya nyumbani kama mboga mboga au kuuza matunda. Haya ni mahitaji ya msingi sana ambayo bado wengi hawayapati vizuri. Kama ukiweza kupata bidhaa zilizo bora na kuwauzia watu kwa bei nzuri wanayoweza kumudu, unaweza kutengeneza biashara nzuri. Na kama kwa fedha kidogo uliyonayo haikutoshi kukodi eneo la kuuzia unaweza kuja na mbinu mpya ya kuuza kwa mfano kuwa na mkokoteni mdogo ambao unazunguka nao mtaa kwa mtaa kuuza bidhaa zako.

3. Kutoa huduma za maji safi kwa maeneo ambayo maji bado ni tatizo.
Kuna maeneo mengi ya dar es salaam ambapo watu bado hawapati maji masafi. Au maji hayo yanapatikana mbali na hivyo wengi kushindwa kuyapata, unaweza kutumia fursa hii kuwasambazia watu maji masafi. Unahitaji kuwa na mkokoteni na madumu yako ya maji, kujua eneo ambapo utapata maji safi na kuweza kuwasambazia wateja wako.

MUHIMU; Pata vitabu vya biashara na mafanikio kwa bonyeza na kutembelea MOBILE UNIVERSITY.

4. Kubeba takataka kutoka kwenye makazi ya watu.
Licha ya kuwepo kwa mifumo ya uzoaji taka kama magari na majalala makubwa, bado watu wengi hawafikiwi au hawatumii mifumo hii. Hivyo hapa kuna fursa ambapo mtu unaweza kuingia na kufanya biashara. Unahitaji kuwa na mkokoteni ambao unaweza kubeba taka na unahitaji kujua sehemu ya kwenda kuzimwaga. Hapa unaweza kupita kwenye mitaa, nyumba kwa nyumba na kuwapatia huduma ya kuzoa taka zao kwa bei ambayo wanaweza kuimudu.
Hizo ni baadhi ya biashara unazoweza kuanza kuzifikiria na hata kuzifanya. Unaweza kuchagua moja na kuiboresha zaidi kulingana na mazingira uliyopo. Au unaweza kufikiria biashara nyingine kwa mazingira ambayo upo. Kikubwa usianze kuchagua na kuona kuna biashara inayokufaa au ipi haikufai, unapoanza biashara kwa mtaji mdogo huna nafasi kubwa ya kuchagua.

Kuwa na msingi imara wa kibiashara na chagua biashara, weka juhudi zako zote na hakuna kinachoweza kukuzuiakufanikiwa.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.