Kipimo sahihi cha maendeleo na mafanikio ya biashara ni ukuaji wa biashara. Tunategemea biashara iwe inakua kadiri siku zinavyokwenda. Ukuaji wa biashara tunaouzungumzia ni kuongezeka kwa idadi ya watu inaowafikia, kuongezeka kwa mauzo, kupata faida kubwa na kuweza kufungua matawi zaidi ya biashara hiyo.
Kukua kwa biashara ni ndoto ya kila mtu anayeingia kwenye biashara lakini ni wachache sana ambao wanaweza kukuza biashara zao. Wengi wamekuwa wanaendesha biashara zilizodumaa na wakati mwingine zinakufa kabisa. Hakuna bahati nzuri kwa wale ambao wanakuza biashara zao na wala hakuna bahati mbaya kwa wale wanaoshindwa kuzikuza. 

Tofauti pekee inaanzia kwenye maarifa waliyonayo watu kwenye ukuzaji wa biashara.
Wale ambao wanakuza biashara zao wanajua vitu ambavyo wengine hawavijui. Kwa kuwa vitu hivi siyo siri bali ni maarifa ambayo kila mtu anaweza kuyapata na kuyatekeleza, leo tutakwenda kuangalia njia tano za uhakika za wewe kuweza kukuza biashara yako na kufikia ndoto zako za kibiashara. Jifunze njia hizi na zitumie kwenye biashara yako ili uweze kufika mbali.

1. Tengeneza timu sahihi ya kibiashara.
Kwanza kabisa ni vyema ukajua biashara haiwezi kukuzwa na mtu mmoja, wewe mwenyewe huwezi kufanya kila kitu ambacho biashara yako inataka kifanywe. Unahitaji kuwa na watu ambao watakusaidia kwenye biashara yako na watu hawa ni vyema ukawa umewaajiri. Hapa kwenye kuajiri kuna changamoto kubwa sana kwenye biashara nyingi. Wengi wamekuwa wakiajiri mtu ambaye yupo tayari kupokea mshahara kidogo bila ya kujali ataleta mchango gani kwenye biashara.
Biashara ni kama timu ya mpira wa miguu, kadiri wachezaji wanavyoelewana vizuri na kusaidiana ndivyo timu inavyopata ushindi. Unahitaji kuwa na timu sahihi kwenye biashara yako. unahitaji kuajiri watu ambao wana uwezo na vipaji tofauti. Angalia ni maeneo gani muhimu ya biashara yako na ajiri watu ambao wanaweza kuyafanyia kazi maeneo hayo na kuleta majibu mazuri. Ajiri watu ambao wana vitu ambavyo wewe huna, hii itakunufaisha wewe kwa kukupa muda wa kufanyia kazi yale ambayo ni muhimu zaidi kwa biashara yako.

2. Wekeza sehemu ya faida kwenye biashara yako.
Watu wengi wanaoingia kwenye biashara wamekuwa wakifikiri kwamba biashara ikishaanza basi wao ni kuchuma faida na kuendesha maisha yao. Kwa njia hii wamekuwa wanatumia kila faida wanayoipata na hivyo kupelekea biashara kubaki pale ilipo au hata kurudi nyuma, yaani kupata hasara. Biashara haiwezi kukua kama hakuna uwekezaji endelevu kwenye biashara hiyo.
Tuchukulie biashara kama mfano wa ng’ombe, ng’ombe anapozaa ndama, unaweza kukamua maziwa na kuyatumia au kuyauza. Lakini pia ndama naye anataka maziwa ili aweze kukua, sasa kama utamsahau ndama na kufurahia maziwa, utashindwa kuendeleza ufugaji wako. Unatakiwa kuhakikisha ndama amepata sehemu yake ya maziwa na wewe ndiyo utumie maziwa yanayobaki.
Wafanyabiashara wengi wamekuwa hawana mpango wa uwekezaji kwenye biashara zao, wanachofanya ni kununua vitu pale vinapoisha. Kwa njia hii biashara haiwezi kukua, biashara inakua pale sehemu ya faida inaporudi kwenye biashara kama uwekezaji. Na unafanya hivyo ukiwa unajua kabisa kwamba nimeongeza kiasi fulani kwenye mtaji na nimefanya hivyo kwa kununua kitu fulani ambacho hakikuwepo awali, au nimeongeza mzigo ambao nimekuwa nanunua.

3. Kuwa tayari kubadilika.
Tunaishi kwenye kipindi ambacho mabadiliko yanatokea kwa kasi sana, kila siku kuna vitu vipya vinakuja na vitu vya zamani vinakosa thamani. Kuna biashara ambazo zilikuwa maarufu miaka kumi iliyopita ila kwa sasa hazipo kabisa, na kwa kipindi hiko cha miaka kumi pia zimekuja biashara ambazo watu hawakuwahi kuzidhania.
Mabadiliko yanatokea na yataendelea kutokea kila siku kwenye maisha na biashara zetu. Wale ambao wao tayari kwenda na mabadiliko wananufaika, wale ambao hawapo tayari wanaachwa nyuma na mabadiliko haya.
Kila siku jifunze kuhusu biashara yako na biashara kwa ujumla, jua kinachoendelea kwenye ulimwengu wa biashara, jua mbinu mpya za ufanyaji wa biashara na angalia jinsi teknolojia mpya zinaathiri biashara yako. pale unapoona mabadiliko yanaathiri biashara yako usisite na wewe kubadilika. Kung’ang’ania kile ambacho umezoea kufanya kwenye biashara kutakuchelewesha kufika mbali kwenye biashara yako.

KITABU; JINSI YA KUFAIDIKA NA MABADILIKO YANAYOTOKEA KWENYE MAISHA.

4. Toa huduma bora kabisa kwa wateja wako.
Wateja ulionao ndiyo sababu biashara yako ipo, kama hakuna wateja hakuna biashara, haijalishi una bidhaa au huduma bora kiasi gani. Hivyo katika mipango yoyote ya kuikuza biashara yako, wateja lazima wawe kipaumbele cha kwanza. Wateja wako wanaweza kuwa mabalozi wazuri au wabaya wa biashara yako. Wateja wanaoridhika na huduma wanazozipata wanakuwa mabalozi wazuri na watakuletea wateja wengi zaidi. Lakini wale ambao hawaridhishwi watakuwa mabalozi wabaya kwa kutoa taarifa ambazo siyo sahihi kuhusu biashara yako.
Ili kutoa huduma bora kwa wateja wako, wape ahadi kubwa halafu toa zaidi ya kile ambacho umeahidi. Na pia inapotokea mteja amepata changamoto kwenye biashara yako msaidie kuitatua. Kwa njia hii utatengeneza uhusiano mzuri na wateja wako kitu ambacho kitaiwezesha biashara yako kukua zaidi.

5. Epuka hatari zisizo za lazima.
Kwenye ulimwengu wa biashara, hatari ni kitu cha kawaida, kuna maamuzi mengi ya hatari ambayo unahitaji kufanya ambayo yanaweza kuleta faida kubwa kama yakifanikiwa. Lakini pia yakishindwa yanaleta hasara kubwa. Pamoja na kwamba biashara zipo kwenye mazingira ya hatari, bado siyo sahihi kuchukua kila hatari. Epuka zile hatari ambazo siyo za lazima kwenye biashara yako. Hapa unahitaji kufikiri vyema kabla ya kuchukua maamuzi. Na pia unahitaji kuilinda biashara yako dhidi ya hatari ambazo huwezi kuzizuia kwa kuikatia biashara hiyo bima. Kwa kuwa na bima una uhakika wa kuendelea na biashara hata kama kuna ajali iliyopelekea wewe kupoteza sehemu kubwa ya biashara yako.
Ukuaji wa biashara ni kitu ambacho kinawezekana kwenye biashara yoyote. Kinachohitajika ni mfanyabiashara kuwa na maarifa sahihi na ayatumie katika kukuza biashara yake. Tumia mambo haya matano uliyojifunza ili kuikuza biashara yako zaidi. Kila la kheri.
TUPO PAMOJA.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

MUHIMU; Kila siku naandika makala nzuri za KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO pamoja na kupata Tafarari nzuri za kila siku. Kuweza kusoma makala hizi na kupata tafakari za kila siku karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Kujiunga tuma ujumbe wenye neno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253. Karibu sana.