Biashara siyo kuuza na kununua pekee, wengi wanaoingia kwenye biashara kwa mtazamo huu wa kuuza na kununua huwa hawafiki mbali. Na wala biashara siyo kuwa na wazo na mtaji pekee, wengi wamekuwa na mawazo mazuri na mtaji wa kutosha, lakini walipoingia kwenye biashara hawakuweza kufika mbali.

Biashara na ujasiriamali ni kitu ambacho kinategemea mambo mengi kutoka kwa mwendeshaji. Na moja ya vitu vinavyostawisha au kuua biashara ni tabia ambazo mtu anayeendesha biashara anakuwa nazo. Biashara inabeba zile tabia ambazo mwanzilishi wa biashara ile anakuwa nazo. Na hata mfanyabiashara anapoajiri, hata wafanyakazi wake wanaishia kufanya kazi kama anavyofanya yeye.

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Hivyo kabla hujalalamika kwa nini biashara yako haiendi vizuri, ni vyema ukajichunguza kama tabia zako zinachangia kuikuza au kuiua biashara yako. Kupitia makala hii ya leo tunakwenda kuangalia tabia za wafanyabiashara ambazo zinaiwezesha biashara kufanikiwa.

Kuwa tayari kuweka juhudi kupita kawaida ni moja ya tabia ambazo zinawezesha biashara kukua. Biashara siyo rahisi hata kama mtu una wazo bora na una wasaidizi wengi. Wewe kama mwendeshaji na mmiliki wa biashara unahitajika kuweka juhudi kubwa kwenye biashara yako. unahitaji kujua kila kitu kinachoendelea kwenye biashara yako na kuona kama maamuzi yote yanayofanywa ni sahihi. Unapoona biashara yoyote inakufa, jua kuna uzembe ulikuwa unajitokeza kwa muda mrefu mpaka imefikia hatua ya kuleta hasara. Iwapo mmiliki wa biashara anakuwa karibu na biashara yake, na kuweka juhudi kubwa, atakuwa ameshaona mapema tatizo lolote linalojitokeza.

Kama wewe ni mfanyabiashara au unapanga kuingia kwenye biashara, basi jua unahitaji kuweka juhudi kubwa sana kwenye biashara yako. Unahitaji kuijua biashara yako nje ndani, jua kila kinachoendelea kwenye biashara hiyo ili uweze kuchukua hatua mapema pale changamoto zinapotokea.

SOMA; Jinsi ya kugeuza kipaji chako kuwa biashara inayokuingizia kipato.

Kuwa tayari kujifunza kila siku ni tabia nyingine ambayo inasaidia biashara nyingi kukua. Kwa dunia ya sasa mabadiliko yanatokea kwa kasi kubwa sana, biashara unayofanya leo hii kuna uwezekano miaka kumi ijayo isiwepo kabisa. Tumeona jinsi ambavyo maendeleo ya sayansi na teknolojia yalivyoweza kuua biashara nyingi. Kwa mfano kwa sasa kila mtu anaweza kutumia intaneti kwenye simu yake ya mkononi, kwa namna hii biashara ya mikahawa ya intaneti imekufa. Ili kuweza kuona mabadiliko ya aina hii kabla hayajaleta madhara kwenye biashara, ni lazima mfanyabiashara awe tayari kujifunza kila siku kuhusu biashara yake na biashara kwa ujumla. Ni muhimu ajue mwenendo wa kibiashara upoje na hatua zipi muhimu za kuchukua. Kwa dunia ya sasa ni hatari sana kufanya biashara kwa mazoea.

Kwa wafanyabiashara wote ni muhimu kujifunza kuhusu biashara yako na biashara kwa ujumla kila siku. Jifunze mbinu bora za kuikuza biashara yako, kuongeza mkopo, kuajiri na pia kusimamia biashara yako ili uweze kuikuza.

Uaminifu ni tabia muhimu mno kwenye ukuaji wa biashara yoyote ile, bila ya uaminifu hakuna biashara. Kwa dunia ya sasa, hata kama mteja anahitaji kununua kwako mara moja tu, kama hujawa mwaminifu kwake kwa kumpa kile kweli anachohitaji, ana nafasi kubwa ya kukunyima wateja wengi zaidi. Watu sasa wana nguvu kubwa ya kuweza kuwasiliana na watu wengi ndani ya muda mfupi kwa kutumia mitandao ya kijamii. Jambo lolote ambalo limewakera watu watashirikishana kupitia mitandao hii. Hivyo kama mteja hakuridhika, ni rahisi kuwaambia wengine na hivyo kukunyima wateja wengi zaidi. Uaminifu ni nguzo muhimu sana kwenye biashara, kwa sababu hakuna biashara kama hakuna wateja na hakuna wateja kama hakuna uaminifu.

Unapoamua kuingia kwenye biashara, kuwa mwaminifu, ahidi kile unachoweza kutekeleza na tekeleza kile unachoahidi. Usiongeze chumvi ili kuuza, unaweza kuuza mara moja na ikawa ndiyo mwisho wako kumuuzia mteja huyo na wengine wanaofahamiana naye. Kama kuna kitu ambacho bidhaa au huduma yako haiwezi kufanya kuwa mkweli na mweleze mteja wako hivyo, atakuamini na mtafanya biashara pamoja kwa muda mrefu.

SOMA; Njia tano (5) za uhakika za kuweza kuikuza biashara yako na kufikia mafanikio makubwa.

Uvumilivu ni tabia nyingine ambayo imewezesha biashara nyingi kukua. Hakuna biashara ambayo haikutani na changamoto, hakuna biashara ambayo kila wakati tangu inaanza imekuwa inatengeneza faida tu. Kila biashara inapitia magumu, hasa mwanzoni. Kuna wakati biashara inakuwa inajiendesha kwa hasara, wakati mwingine wateja wanakuwa wasumbufu, bado pia wafanyakazi nao wanakuwa changamoto. Biashara yoyote inayoonekana kufanikiwa leo, imepitia changamoto nyingi huko nyuma. Ni uvumilivu wa waendeshaji wa biashara hizo ndiyo umewawezesha kufika pale walipo sasa.

Unapochagua kuingia kwenye biashara, jua unahitaji kuwa mvumilivu sana. Kama unaingia kwa lengo la kupata faida ya haraka, utakata tamaa mapema sana. Jiandae kuweka juhudi kubwa huku ukiwa mvumilivu na utapata matokeo bora kupitia biashara hiyo.
Mafanikio ya biashara yako yanaanza na wewe mwenyewe, biashara itakua au kufa kutokana na hatua unazochukua wewe mwenyewe. Chukua hatua bora ili biashara yako iweze kukua.

Nakutakia kila la kheri katika kufanyia kazi haya uliyojifunza.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
MUHIMU; Kama unataka ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu, bonyeza maandishi haya na utapata maelekezo. karibu sana tufanye kazi kwa pamoja.