Umefika ule wakati ambapo mwaka wa elimu kwenye elimu ya juu Tanzania unakwisha. Na katika mwisho wa mwaka wa elimu, kuna wanafunzi ambao wanakuwa wamemaliza masomo yao, wamehitimu tayari kwa kwenda kulitumikia taifa. Huu ni wakati wa furaha kubwa kwa wahitimu, ambao wamekuwa kwenye mfumo huu wa elimu kwa kipindi kisichopungua miaka 16, katika kipindi chote hiki, walikuwa wanaiangalia siku hii ya kuhitimu.

Kwanza kabisa nitoe pongezi kubwa kwa wahitimu wote, iwe umehitimu ngazi ya cheti, stashahada au shahada, kwa sasa wewe umeshapata elimu ambayo unaweza kuitumia kwenye maisha yako na maisha yako yakawa bora sana. Kuwepo kwenye mfumo wa elimu kwa miaka hiyo mingi, wengine 16 wengine mpaka miaka 20 siyo kazi ndogo. Najua kuna wakati ulikutana na magumu ambayo yalitaka kukukatisha tamaa, lakini uliendelea kupambana mpaka leo umefikia kuhitimu.

Baada ya pongezi hizi naomba niende kwenye barua ya leo ambayo nimeiandaa maalumu kabisa kwa marafiki zangu ambao wamehitimu masomo yao ya elimu ya juu. Nimekua nikiandika makala hizi kila mwaka kuwashauri wahitimu, kusoma ya mwaka 2013 bonyeza hapa, 2014 bonyeza hapa, na 2015 bonyeza hapa na kupata mfululizo wa makala kwa wahitimu bonyeza hapa.

Kwenye makala ambazo nimekuwa naandika kila mwaka kwa wahitimu, naona kama nimeshagusia kila kitu. Hivyo kwenye makala ya leo nataka kukuambia kile ambacho hujawahi kuambiwa na wala hujawahi kusikia lakini ni ukweli. Kama ambavyo unajua, ukweli mara nyingi huwa unakuwa mchungu na hivyo watu hawapendi kuusikia. Ninachokwenda kukueleza leo ni ukweli mchungu sana, hivyo kama roho yako ni nyepesi ni vyema usiendelee kusoma. Kama upo tayari kuujua ukweli ili uufanyie kazi, basi karibu uendelee kusoma.

SOMA; KABLA HUJAANZA KUZUNGUKA NA BAHASHA SOMA HAPA.

Ukweli unaopaswa kuujua ni kwamba una miaka kumi ya mateso mbele yako, huu ni ukweli ambao umekuwa unafichwa kwa miaka 20 iliyopita. Kwa miaka 20 iliyopita, tangu unakua umekuwa unaimbiwa wimbo mmoja, soma ili ufaulu na uwe na maisha bora. Walikupa tu robo ya hadithi, hadithi nzima siyo rahisi kama hivyo, na sasa ndipo unapokwenda kuujua ukweli wenyewe kwenye maisha halisi.

Miaka kumi ijayo ndiyo miaka ambayo itatoa mwanga kwenye maisha yako yote utakayoishi hapa duniani. Miaka hii kumi itakuwa miaka migumu sana kwako, kitakuwa ndiyo kipindi cha kuamua ni kitu gani unataka kwenye maisha yako na kujenga misingi ya maisha yako. ni kwenye miaka hii kumi unaweza kujenga maisha bora au ukaharibu kabisa maisha yako.

Tukianza kuuchambua ukweli huu hatua kwa hatua, hapo ulipo sasa huna chochote zaidi ya kipande cha karatasi (cheti) ambacho kinaonesha masomo uliyosoma na ufaulu uliopata. Kipande hicho cha karatasi kilikuwa na matumizi mazuri sana siku za nyuma, ila kwa sasa matumizi yake yanafikia kuwa sifuri, kwa changamoto za ajira zilipo, unaweza kukosa popote pa kutumia cheti chako. Una cheti pekee, huna uzoefu wowote, huna ushuhuda wowote wa watu ambao wanaweza kuwaambia wengine kuhusu wewe na hakuna anayekujua wewe ni nani.

Kwa miaka hiyo uliyokuwa shuleni ulikuwa unakula tu, hukuwahi kuzalisha. Umekuwa unalipiwa ada na kupewa fedha ya matumizi, ulikuwa unatumia kwa raha, ukinunua kila ulichokuwa unataka, yote hii ni kula na inaelekea ukingoni wakati huu ambao unahitimu masomo yako. sasa dunia inaanza kukutaka siyo ule tu, bali pia uzalishe, na nafasi za wewe kuzalisha ni chache, hapo ndipo changamoto inakuwa kubwa zaidi.

Miaka kumi ijayo ni miaka ambayo unahitaji kuchagua ni kitu gani unataka kufanya na maisha yako, na kuweka juhudi zako zote katika kufanya kitu hicho. Miaka hii kumi itakuwa migumu, utakutana na changamoto nyingi na kukatishwa tamaa, lakini ninachotaka kukuambia ni kwamba usikubali kukatishwa tamaa. Ukishajua ni kipi ambacho unataka kwenye maisha yako, weka juhudi ili kukifikia.

SOMA; Ushauri Muhimu Kwa VIJANA; Okoa Miaka Hii Kumi Ambayo Utaipoteza.

Kama ambavyo tayari utakuwa umeona mwenyewe, ajira ni changamoto, hivyo usipoteze muda kusubiri mpaka upate ajira, kaa chini na yapange maisha yako, chagua ni kipi unataka kufanya kwenye maisha yako, chagua ni jina gani unataka kuacha hapa duniani, na chagua ni kwa namna gani unataka kugusa maisha ya wengine, kisha anza kufanyia kazi ndoto yako mpya kwenye maisha.

Ninachotaka kukuambia ni kwamba chochote unachochagua kufanya, miaka kumi ijayo hakuna atakayejua kama hata upo, utakuwa ni wewe unateseka na kila unachofanya, lakini miaka hiyo kumi ikishapita, kila mtu atajua kuhusu wewe. Kila mtu atakuwa anakutafuta kwa sababu utakuwa umefanya makubwa sana, kama hutaishia njiani.

Kama utakuwa tayari kuteseka kwa miaka hii kumi ya maisha yako ya ujana, miaka mingi ijayo utaishi maisha bora sana kwa sababu utakuwa umejijengea misingi imara ya maisha yako. lakini kama utakwepa kuteseka sasa, utateseka maisha yako yote ya baadaye. Kwa sababu utafika wakati umri wa ujana umekwisha na huna tena nguvu za kuhangaika kujenga misingi imara.

SOMA; Ni Muda Kiasi Gani Unahitaji Ili Kufiki Mafanikio Makubwa? Soma Hapa Kujua.

Huu ndiyo wakati wa kuanzisha biashara bila hata ya kuwa na mtaji, huu ndiyo wakati wa kufanya kilimo, huu ndiyo wakati wa kuwatumikia wengine, kufanya maisha yao kuwa bora zaidi. Huu ni wakati mzuri kwako kuionesha dunia kwamba una kitu kikubwa kipo ndani yako, kitu hiki hakisemwi, badala yake kinaoneshwa, na unakionesha kwa kufanya. Hivyo weka maneno pembeni na fanya.

Mambo kumi muhimu ya kuzingatia kwenye miaka hii kumi na maisha yako yote kwa ujumla.
Kwenye miaka hii kumi ambayo unakwenda kujenga misingi ya makisha yako, na hata kwenye maisha yako yote, zingatia mambo haya kumi muhimu sana.

1. Kuwa mwaminifu na mwadilifu. Uadilifu ni kuwa na misingi yako ya maisha na kuisimamia. Uaminifu ni kutimiza kile ambacho umewaahidi wengine. Naweza kusema huu ndiyo mtaji pekee ambao kwa sasa unao kwenye maisha yako, usiupoteze.

2. Weka juhudi kubwa sana kwenye kazi, usikubali kuwa mvivu, usikubali kuwa mtu wa maneno, badala yake fanya kazi kwa juhudi kubwa na toa matokeo bora kwa wale wanaopokea unachofanya.

3. Uwekezaji pekee ulionao kwa sasa ni muda. Kuna vitu viwili tunavyoweza kuwekeza kwenye amisha yetu, fedha na muda. Kwa wahitimu walio wengi, fedha huna, hivyo kitu pekee unachoweza kuwekeza sasa ni muda. Wekeza muda wako vizuri kwenye mambo ambayo ni muhimu kwako na yatakulipa vizuri.

4. Ishi chini ya kipato chako, jijengee nidhamu ya fedha, usinunue vitu kwa mashindano. Haya ni mambo unayotakiwa kuyazingatia sana kwenye maisha yako ya kifedha, kwa sababu usipojijengea misingi mizuri sasa, utakuwa mtumwa wa fedha kwenye maisha yako yote. Epuka sana kitu kinaitwa madeni, hasa ambayo hayazalishi, unapoingia kwenye madeni mapema, ndivyo unavyouza uhuru wako kwa wengine.

5. Fanya maamuzi ambayo unaweza kuishi nayo. Pia jifunze kuwajibika kwa maamuzi uliyofanya. Huu ni wakati wa kuacha zile tabia za shuleni za kufanya kile ambacho kila mtu anafanya. Njia rahisi ya kushindwa kwenye maisha, ni kuiga wengine, kufanya kile ambacho kila mtu anafanya.

6. Usilalamike, usilaumu, ni kupoteza muda. Kama kuna kitu hukipendi kibadili, kama huwezi kukibadili basi achana nacho. Kumbuka muda wako ndiyo rasilimali pekee uliyonayo kwa sasa, ilinde sana.

7. Zungukwa Na watu wazuri, watu wanaojua ni wapi wanaenda, watu wenye tabia zinazoendana na zako. Tabia zinaambukizwa, ukizungukwa na watu wenye tabia mbovu watakuambukiza tabia hizo mbovu. Wewe ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka, mara zote hakikisha unazungukwa na watu sahihi.

8. Usimsikilize yeyote anayekuambia HUWEZI au HAIWEZEKANI, watu wote waliofanya makubwa kwenye dunia hii waliambiwa hawawezi au haiwezekani. Kama kuna kitu una ndoto nacho, hata kama ni cha kijinga kiasi gani, usikiue, bali kifanyie utafiti, uzuri wa dunia ya sasa ni kwamba taarifa zipo za kutosha hivyo utapata pa kuanzia. Mtu akikuambia huwezi au haiwezekani mpuuze mara moja, haijalishi ni mtu gani. Hata kama utajaribu na ukashindwa, hutabaki kama ulivyokuwa mwanzo, kuna mengi ambayo utajifunza.

9. Furahia ujana wako na tunza afya yako. ujana ni wakati ambao unakuwa na nguvu kubwa ya kuweza kufanya makubwa. pia unakuwa na uhuru wa kufanya mengi na kwenda mbali kwa sababu huna utegemezi mkubwa kwako. Utumie muda huu vizuri, lakini muhimu zaidi tunza afya yako, una miaka mingi mbele yako, usiiharibu kwa kuchagua maisha ya hovyo kama ya ulevi.

10. Jifunze kwenye kila siku ya maisha yako, soma vitabu kila siku, Soma AMKA MTANZANIA kila siku kwenye maisha yako, Soma KISIMA CHA MAARIFA kila siku kwenye maisha yako na karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA ambapo tutakuwa pamoja, bega kwa bega kwenye safari yako ya miaka 10 ya kujenga msingi bora wa maisha yako. Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe kwa njia ya wasap wenye neno KISIMA CHA MAARIFA, kwenda namba 0717396253 na utapewa maelekezo.

Nimalize kwa kusema kwamba unaweza kuitumia miaka hii kumi kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako, au unaweza kuitumia kwa kufanya yale ambayo kila mtu anafanya. Wewe ni mtu mzima sasa, maisha ni yako na maamuzi ni yako. Usiendeshe maisha ya kuiga kama ya shuleni, sasa unahitaji kufanya kile ambacho ni muhimu kwako, hata kama hakuna anayeamini kile unachofanya.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.
Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.