Miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mwamko mkubwa sana wa watu kuingia kwenye biashara. Hii imetokana na hali ya uchumi kuwa ngumu na kipato kimoja, hasa cha mshahara kutokutosheleza mahitaji ya msingi ya maisha. Pia kumekuwa na fursa nyingi za mahitaji ya watu na hivyo watu kuchukua nafasi kutimiza mahitaji hayo na wao kujipatia faida.

Kumekuwa na watu wengi ambao wanafungua biashara ndogo za uchuuzi, na wengine uzalishaji wa bidhaa za vyakula na mavazi. Wapo pia ambao wameingia kwenye kilimo cha kibiashara, na kulima mazao ya matunda na bustani, ambayo yanachukua muda mfupi kulimwa na pia yana uhitaji mkubwa. Fursa zote hizi zimetoa nafasi kwa watu kujiongezea kipato kupitia biashara.
 

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA HAPA.


Licha ya kuwepo kwa fursa hizi nzuri za uhitaji wa watu, na licha ya wengi kuingia kwenye biashara hizi, kumekuwa na changamoto moja kubwa sana ambayo imekuwa inaua biashara nyingi ndogo zinazoanzishwa. Tumekuwa tunaona watu wengi wanaanzisha biashara zao wakiwa na hamasa kubwa ya kufanya vizuri, lakini haipiti miezi sita biashara hiyo inakuwa imefungwa. Tunaona watu wanakwenda shambani wakiwa na hamasa kubwa ya kupata faida kwenye kilimo wanachokwenda kufanya, lakini inapofikia wakati wa kuvuna, uzalishaji unakuwa mdogo tofauti na mategemeo, au bei ya soko inakuwa ndogo kuliko gharama mtu alizoingia.

SOMA; Kuanza Biashara Kwa Mtaji Kidogo, Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kuikuza.

Biashara nyingi zimekuwa zikipata hasara na kupelekea kufungwa kutokana na changamoto hii ambayo inawakumba wafanyabiashara wengi. Leo kupitia makala hii tutakwenda kuichambua changamoto hii kwa kina, ili uweze kuondoka na kitu cha kufanyia kazi, na unapoanzisha au kukuza biashara uliyonayo sasa, usiingie kwenye makosa ambayo umekuwa unafanya miaka yote.

Changamoto ambayo imekuwa inaua biashara nyingi ndogo hapa Tanzania, ni namna ya kufikiri ambayo wafanyabiashara wanayo. Watu wengi wanaingia kwenye biashara wakiwa hawana taarifa kamili. Wanaingia kwenye biashara wakiwa na taarifa za upande mmoja pekee wa biashara, na hivyo kupata shida pale wanapokutana na changamoto za upande mwingine wa biashara. Kwa kifupi, watu wengi wanaingia kwenye biashara wakiwa na wazo moja tu, nikizalisha watu watanunua, au nikiuza, watu watakuja kununua. Hii ni mbinu ambayo ilikuwa na mafanikio zamani, wakati wachache ndiyo walikuwa wanafanya biashara, ila kwa sasa karibu kila mtu anafanya biashara, unahitaji mbinu za ziada ili kuweza kuikuza biashara yako.

Watu wengi wamekuwa wakiingia kwenye biashara baada ya kuona wengine wanafanya, na kwa kuwa wanaona watu hao wanafanya na wana wateja, basi moja kwa moja wanahitimisha kwamba biashara hii ina wateja wengi na inalipa, wacha na mimi niingie kwenye biashara hii. Wengine wamekuwa wanaingia kwenye biashara baada ya kusikia watu wanasema biashara hiyo inalipa, wanahamasika kupitia maneno wanayosikia, na kujikuta wameshaingia kwenye biashara ambayo hawakuijua vizuri. Kwa kuangalia kwa nje, kila biashara inalipa, kwenye hesabu za makaratasi, kila biashara inalipa. Nimekuwa nawaambia watu, sijawahi kuona mchanganuo wa biashara ambao una hasara, lakini karibu kila biashara ina hasara. Kwa kuangalia upande huu mmoja wa biashara, wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiingia kwenye biashara na kujikuta kwenye wakati mgumu.

SOMA; Changamoto Ya Matumizi Mazuri Ya Fedha Za Biashara.

Hapa nakushirikisha mambo matatu muhimu ya kuzingatia kabla hujaamua kuingia kwenye biashara yoyote ile, iwe ni kuuza bidhaa, huduma au kufanya kilimo cha kibiashara.

Moja; fanya utafiti wa biashara kabla hujaingia kwenye biashara hiyo. Usiingie kwenye biashara kwa sababu unaona watu wanafanya na wana wateja, au kwa sababu umesikia kila mtu anaimba kilimo fulani kinalipa. Jipe muda na fanya utafiti, na utafiti huu ninaokuambia ufanye siyo wa kwenda kutafuta na kusoma kwenye mtandao au vitabu, badala yake watembelee wale wanaofanya biashara hiyo. Fanya nao urafiki na jifunze mengi kutoka kwao, namna wanavyo endesha biashara zao, changamoto wanazokutana nazo, na hata wanavyozitatua. Pia fanya utafiti kwa wateja wa biashara hiyo, wanapatikana wapi, mahitaji yao ni yapi na uwezo wao wa kumudu gharama za biashara husika.

Mbili; ifikirie biashara kwa ujumla, ifikirie kama mfumo na siyo kama kitu kimoja. Biashara yoyote, kwa kiwango cha chini kabisa inahitaji kuwa na angalau mifumo mitatu, usimamizi, uzalishaji na masoko/uuzaji. Wengi wanaoingia kwenye biashara huwa wanafikiria uzalishaji pekee, usimamizi na masoko/uuzaji huwa wanafikiri ni vitu vinavyokuja vyenyewe pale biashara inapokuwa imeshaanza. Matokeo yake ni watu wengi kuingia kwenye biashara na baadaye kukosa soko. Unapoingia kwenye biashara, jua kwa kina kuhusu usimamizi wa biashara hiyo, unachozalisha na soko lako na namna unavyolifikia soko hilo.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuingia Kwenye Biashara Baada Ya Kumaliza Masomo Ya Chuo.

Tatu; jitofautishe na wafanyabiashara wengine. Japo kwa sehemu kubwa wazo lako la biashara utakuwa umelipata kutoka kwenye mawazo ya wengine, usifungue biashara inayofanana na wengine kwa kila kitu. Tafuta njia ya kujitofautisha, hata kama biashara mnayofanya inafanana. Lazima uwe na kitu ambacho wateja wanakipata kwako tu na siyo kwa wengine. Kama biashara zinafanana, basi toa huduma bora zaidi ya wanazotoa wengine. Mteja anapokuwa kwenye biashara yako, ajisikie tofauti kabisa na akienda kwenye biashara nyingine. Njoo na mbinu tofauti za ufanyaji wa biashara yako, kama wengine wanasubiri wateja waje kwenye biashara zao, wewe unaweza kuwafuata wateja kule walipo.

Ni hatari sana kuingia kwenye biashara ambayo hujaijua vizuri, hakikisha umefanya utafiti, kujua biashara nzima na kujitofautisha na wengine. Kwa kufanya hivi utaondokana na changamoto inayoua biashara nyingi. Kila la kheri.

TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)