Karibu rafiki yangu kwenye makala yetu ya nyeusi na nyeupe ambapo tunakwenda kuuangalia ukweli kama ulivyo. Kupitia makala hizi tunajadili mambo ambayo mara nyingi watu hawapendi kuuangalia ukweli ulivyo, kwa sababu mara zote ukweli ni mchungu.



Leo tunakwenda kuangalia eneo la ufanyaji wa kazi, ambapo kumekuwa na dhana mpya inayopambwa sana siku za karibuni. Dhana hii ni kwamba huhitaji kufanya kazi kwa nguvu (WORK HARD) badala yake unahitaji kufanya kazi kwa akili (WORK SMART).

Ni kitu ambacho kinashangiliwa na wengi na kwa kuwa asili ya binadamu ni uvivu, kupenda kupata makubwa kwa juhudi kidogo, basi wengi wamebebwa na hii. Wapo ambao pia wametapeliwa sana kwa dhana hiyo, kwa kuaminishwa dunia imebadilika, hatuhitaji tena kuweka nguvu kwenye kazi, kinachohitajika ni akili tu.

Nakumbuka siku za nyuma nimewahi kuhudhuria kwenye mkutano mmoja wa fursa ya kibiashara, sasa ilivyoelezwa nikawa na mashaka kwamba huenda siyo biashara sahihi, kwa sababu kuu moja, sikuona kazi ambayo mtu anafanya mpaka alipwe kiasi kikubwa cha fedha ambacho kilikuwa kinaahidiwa mtu anapata. Nikauliza swali, mbona kama hapo sioni kazi, mbona kipato ni kikubwa bila ya kuweka kazi? Na aliyekuwa akinadi fursa ile, alitoa jibu ambalo sitalisahau kamwe, alisema tatizo Watanzania tumezoea kazi mpaka mtu atoke jasho, alime shamba kubwa ndiyo apate fedha. Sasa hivi dunia imebadilika, unahitaji akili tu, siyo nguvu. Basi nikaondoka na sikujiunga na biashara ile, kwa sababu haikuwa na msingi muhimu wa kazi, na haikuchukua muda biashara ile ikafungiwa na serikali.

Siku za hivi karibuni, mambo haya yamekuwa yanashamiri sana. Watu wanashawishiwa kuingia kwenye biashara wasizozielewa, wanapohoji wanaambiwa usitake kutumia nguvu, wewe tumia akili.

Na mimi ninachokuambia rafiki yangu, unapoambiwa kauli kama hiyo, tumia akili yako kuachana nayo haraka sana.

Hakuna namna yoyote unaweza kutumia akili pekee na ukazalisha kazi yenye thamani kwa wengine bila ya nguvu kuhusika. Ni kweli tunahitaji kufanya kazi kwa akili, lakini nguvu pia ni muhimu. Hivyo falsafa yangu siku zote ni kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Hapo unatumia akili nyingi na nguvu kubwa kuweza kutengeneza matokeo bora kabisa.

Watu wamekuwa wanatumia maendeleo ya teknolojia kama kigezo cha kutotumia nguvu na badala yake kutumia akili tu. Hili lilinishawishi kuwaangalia wanaozalisha teknolojia hizi, je wanatumia akili pekee bila nguvu?

Kilichonishangaza ni kwamba wanaozalisha teknolojia, wanatumia nguvu nyingi na akili nyingi kuliko hata watumiaji.

Nilisoma mahali kwamba wakati Bill Gates anaanzisha Kampuni yake ya Microsoft, alikuwa anafanya kazi kila siku, usiku na mchana. Hakuna na mapumziko ya mwisho wa wiki wala likizo. Anasema ndani ya jengo la kampuni palikuwa na kila kitu, hivyo mtu akichoka anaenda kulala kidogo, baadaye anarudi kwenye kazi. Alifanya hivyo kwa zaidi ya miaka kumi.

Labda hiyo inaweza kuwa hadithi ya zamani, labda enzi hizo teknolojia haikuwa kubwa kama sasa, ambapo kuna maroboti ya kufanya kazi. Basi nikaangalia wazalishaji wa teknolojia wa zama hizi. Nikakutana na mahojiano ya mmoja wa wajasiriamali wanaofanya mapinduzi makubwa sana. Huyu anaitwa Elon Musk, ana makampuni matatu makubwa, moja ni la kutengeneza magari ya umeme (TESLA) nyingine ya umeme jua (SOLAR CITY) na ya tatu ni ya kwenda kwenye anga la dunia (SPACE X). Kwa kipimo chochote huyu ni mjasiriamali mwenye ubunifu mkubwa sana. Viwanda vyake vinatumia ROBOTS kuzalisha, hasa magari. Lakini katika mahojiano yake alisema wakati wa uzalishaji wa magari, hasa toleo jipya, huwa anaweka meza yake mwisho wa mnyororo wa uzalishaji, na pembeni kunakuwa na godoro. Kila gari inayokamilika anahakikisha ameikagua yeye mwenyewe na kuridhika nayo.

Kwa mifano hii miwili, kati ya mingi, hebu niambie hiyo mnajidanganya ufanye kazi kwa akili na siyo nguvu mnaitoa wapi?

Mimi sielewi, watu wanadanganyikaje kwenye hili.

Maisha ya wanadamu na hata tabia zetu hazijabadilika sana. Misingi ya maisha na mafanikio ni ile ile tangu zama za mawe mpaka sasa. Kilichobadilika ni namna tunavyofanya tu.

Hata ije teknolojia bora kiasi gani, kazi lazima mtu aweke. Hata zije mashine zenye kujiongoza zenyewe, bado kazi itahitajika.

Na hivyo rafiki yangu, nikusihi sana, achana na watu wanaodanganyana kwamba hawahitaji kuweka nguvu, bali akili tu inatosha.

Ili kufanikiwa kwenye maisha, unahitaji kuweka vyote viwili, NGUVU NA AKILI, na unahitaji kuviweka zaidi ya wengine wanavyoweka. Unahitaji kwenda hatua ya ziada, kufanya zaidi na hii itakuweka mbele na kukuwezesha kupata zaidi.

Yeyote anayekuambia ipo fursa ya kufanikiwa bila ya kuweka kazi na badala yake uweke akili tu, stuka, kuna kitu anataka kukuuzia au anataka kukutapeli. Msingi wa maisha yetu hapa duniani ni mmoja, kuweka kazi.

Hata wale wanaowekeza fedha zao kwa wengine ili wazalishe, kujua ni sehemu ipi sahihi ya kuwekeza, lazima ufanye kazi. Lazima utafute taarifa za kutosha, lazima udadisi, yote hiyo ni kazi. Na hapo ndipo unapata sehemu ya kuwekeza. Na hata baada ya kuwekeza hukai miguu juu na kusubiria kuvuna, lazima ufuatilie uwekezaji wako kwa karibu ili ujue hatua gani muhimu kuchukua.

Mwekezaji maarufu na bilionea Warren Buffett, siku moja akiwa anaongea na wanafunzi, mwanafunzi mmoja alimuuliza afanye nini ili na yeye awe na mafanikio makubwa kwenye uwekezaji? Buffett alichukua karatasi nyeupe na kumwonesha akimwambia unaona hii, soma karatasi 500 kama hizi kila siku. Karatasi mia tano ni sawa na vitabu viwili, vya ukubwa wa kawaida. Hii ina maana ili uwe mwekezaji mzuri, lazima usome sana, usome vitabu, usome nyaraka mbalimbali, ufuatilie mambo yanavyoenda.

Sasa kama kusoma karatasi 500 kila siku ni KAZI YA KUTUMIA AKILI PEKEE, basi endelea kutumia akili. Lakini kwa ninavyojua mimi, inakuhitaji akili na nguvu, kukaa chini na kusoma kwa kiasi hicho, tena kila siku.

Nimalize kwa kukukumbusha zaidi rafiki yangu, usidanganyike kwa namna yoyote ile inapokuja swala la kazi. Kazi lazima ifanywe, inaweza kurahisishwa, lakini haiwezi kufutwa kabisa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.