Habari za leo rafiki yangu?

Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo. Kila unapopata nafasi ya kuiona siku nyingine mpya, kitu cha kwanza kufanya ni kushukuru, kwa sababu wapo wengi walikuwa na mipango mikubwa kwa siku hii ya leo lakini hawapo. Ila wewe upo, ni jambo la kushukuru sana. Lakini pia ni wajibu mkubwa kwako, kutumia siku hii vizuri, kwa sababu ni nafasi ambayo haitajirudia tena.

Kwenye makala ya leo nakwenda kukushirikisha umuhimu wa kujiwekea viwango vikubwa sana kwako binafsi na kwa wengine pia.

Walioshindwa

Kitu kimoja ninachojua na nina uhakika nacho, ni kwamba kila mtu anapenda kuwa na maisha bora, kila mtu anapenda mafanikio. Wewe hapo ulipo, unataka sana kuwa bora zaidi ya hapo ulipo. Iwe ni kwenye kazi, unahitaji kipato zaidi ya ulichonacho sasa, kadhalika kwenye biashara.

Hakuna mtu anayeamka asubuhi na kusema leo nakwenda kuwa hovyo kabisa na nategemea kila mtu anichukulie hovyo, watu wanidharau na hata wasinilipe, ni sawa kabisa. hayupo mtu mwenye akili timamu afanyaye hivyo. Kila mmoja wetu anaamka akiwa na matumaini kwamba leo inakwenda kuwa siku bora.

SOMA; Jinsi Ya Kupika Supu Ya Mawe; Njia Ya Kuanza Biashara Bila Ya Kitu Na Kuweza Kufikia Mafanikio Makubwa.

Pamoja na matumaini haya makubwa, wengi bado siku zao zinakwenda hovyo, na maisha yao hayaendi vile walivyotaka yaende. Zipo sababu nyingi zinapelekea hilo, lakini moja kubwa kabisa ndiyo tunakwenda kuijadili hapa leo.

Ninachoamini ni kwamba, watu wengi wanashindwa kupiga hatua na kufanikiwa, kwa sababu hawathubutu kujiwekea viwango vikubwa sana kwao binafsi na wale wanaowazunguka. Wanakubali kupokea kila kinachopatikana, kwa kuhofia kwamba wakiweka viwango vikubwa watakosa kabisa hata kile kidogo walichokuwa wanapata.

Ninaposema kujiwekea viwango vikubwa, namaanisha kuhakikisha kila unachofanya unakifanya kwa ubora wa hali ya juu sana, kila unachopanga unafanya na kila unayejihusisha naye, anatimiza kweli kile ambacho ameahidi kutimiza.

Labda kama bado huelewi vizuri nikupe mifano kadhaa;

Ni mara ngapi umepanga kuamka asubuhi na mapema, ukaweka mpaka sauti ya kukuamsha, sauti ikalia kweli lakini ukaendelea kulala?

Mara ngapi umepanga kufanya jambo fulani, na muda ukaweka kabisa, lakini muda ule ukafika na hukufanya, na wala hukutumia kwa jambo la maana. Labda ulitumia muda huo kupiga soga na wengine, au kupezuri mitandao?

Mara ngapi mtu amekudanganya mara moja, akakukwamisha, halafu akaja kwako tena akakudanganya tena?

Mara ngapi watu wamekuahidi watafanya kitu fulani, hawafanyi, wanakukwamisha, wanakuja kukuahidi tena wakati mwingine, unakubali na wanakukwamisha tena?

Yapo mambo mengi yanayotokea kwenye maisha yetu, ambayo yalipaswa tujifunze, lakini hatujifunzi na hili linaendelea kutukwamisha kwenye maisha yetu.

Changamoto nyingi tunazokutana nazo kwenye maisha, ni kama somo la maisha, ambazo tunapaswa kuzitatua ili kufaulu somo hilo. Lakini wengi hatutatui, tunabaki pale tulipo.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; BE OBSESSED OR BE AVERAGE (Chagua Kupenda Sana Kile Unachofanya Au Chagua Kuwa Kawaida).

Sasa ninaposema kujiwekea viwango vikubwa kwako binafsi namaanisha nini?

Unapopanga kitu kifanye, hata kama utaumia, kifanye, usiwe mtu wa kuvunja mipango yako mwenyewe, utajidharau na hutaweza kufanikiwa.

Unapoahidi kitu timiza, hata kama ulikosea kuahidi, wewe timiza hata kama itakugharimu kiasi gani, unapaswa kuwa mtu wa kuishi kwa maneno yako. Kama huna uhakika, ni bora usiahidi kuliko kuahidi halafu usitimize. Ni rahisi watu kusahau watu waliowasaidia, lakini kamwe hawasahau watu waliowaumiza.

Kitu chochote ambacho unaruhusu mikono yako ishike, basi kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana. Fanya kadiri ya uwezo wako. Usifanye kitu kwa sababu tu unafanya, bali fanya kuweka alama yako pale. Kila unachoshika, kigeuze kuwa dhahabu, weka ubora mkubwa, chini ya hapo ni kupoteza muda wako.

Jijengee tabia nzuri sana unapohusiana na wengine na hata kwako binafsi. Tabia zako ndiyo zitakazokubeba au kukuangusha. Kamwe usifanye jambo lolote ambalo litachafua tabia yako, hata kama lina manufaa ya muda mfupi.

Ninaposema uweke viwango vikubwa kwa wengine namaanisha nini?

Usikubali mtu yeyote awe na maamuzi ya mwisho kwenye maisha yako. Ninaposema mtu yeyote, namaanisha yeyote kweli. Kama umri wako umeshazidi miaka 21, basi hata mzazi hapaswi kuwa mwamuzi wa mwisho. Watu wanapaswa kukushauri na kukuelekeza, lakini maamuzi ya mwisho kabisa yafanye wewe. Na matokeo yoyote utakayoyapata kulingana na maamuzi yako, yapokee na ishi nayo, usimlaumu yeyote.

Usikubali kununua matatizo na hofu za wengine. Watu wenye hofu wanapendwa kuzungukwa na watu wenye hofu. Watu walioshindwa wanapenda kuzungukwa na watu walioshindwa. Usikubali kabisa kubeba hayo ya watu, yako tayari yanakutosha.

Wape watu nafasi chache na wajue hilo. Kwa mfano mtu akikudanganya mara moja, kwenye jambo ambalo hakupaswa kukudanganya, na uongo wake ukawa na madhara kwako, huna haja ya kumwamini tena wakati mwingine. Na mweleze wazi kabisa ya kwamba kwa kuwa alikudanganya, tangu sasa hutachukulia ukweli chochote atakachokuambia mpaka utakapodhibitisha mwenyewe. Kwa njia hii watu watajifunza kuwa wa kweli kwako na hutadanganyika kirahisi.

Jihusishe na watu ambao wanaishi kwa misingi ya maadili, hata kama jambo unalofanya nao halihusishi maadili hayo, kwa sababu mtu anapokosa maadili, hatashindwa kukuangusha na wewe pia. Kwa mfano kama unataka kushirikiana na mtu kwenye biashara, lakini mtu huyo siyo mwaminifu kwenye mahusiano yake, usishirikiane naye kwenye biashara. Kama amekosa uaminifu kwenye mahusiano yake, pia atakosa uaminifu kwenye biashara na ipo siku atakuumiza. Hivyo angalia kila tabia ambayo mtu anayo, hata kama haihusiani na kile mnachofanya pamoja, jua upo wakati itaathiri.

SOMA; Usimtafute Mtu Mwaminifu Bali Kuwa Mwaminifu Wewe, Wengine Watajifunza Kwako.

Wafanye watu watimize kile ambacho wamekuahidi, usikubali kabisa mtu aahidi kitu halafu asifanye, na wewe umchukulie kirahisi tu. Washikilie watu kwa ahadi zao. kama hatotimiza wakati mwingine usipokee ahadi yake. Hata kama ni kazi, mtu alikuambia itakuwa tayari baada ya muda fulani, muda umepita haijawa tayari, anakupa sababu ambazo unaona kweli zina mashiko, anakupa tena muda mwingine, bado hakamilishi, usifanye naye tena kazi.

Kama mtu kila mnapopanga kukutana amekuwa anachelewa, huna haja ya kuendelea kukutana naye tena. Haheshimu mkutano mnaopanga, na anakupotezea muda wako. Wafundishe watu thamani ya muda wako, ili wauchukulie kwa umakini.

Haya ni baadhi ya maeneo ambayo unapaswa kuyawekea viwango vikubwa kwako na kwa wengine. Kadiri unavyoyafanyia kazi, ndivyo unavyozidi kuona mengine zaidi ya kujiwekea viwango vikubwa.

Najua unaweza kufikiria sasa nikiweka viwango hivi maisha yangu si yatakuwa magumu sana? Si nitakosa kabisa watu wa kufanya nao kazi na maisha yangu kuwa magumu? Majibu yangu kwako ni siyo kweli, ni hofu tu hizo zinakufanya uone hivyo. Utakapoanza kujiwekea viwango vikubwa, wale watu wa viwango vidogo watapotea kwenye maisha yako na utaanza kuwavutia watu wa viwango vya juu. Na wapo wengi sana, wewe huwaoni tu kwa sababu umezungukwa na wengi wa viwango vya chini.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

fb instagram

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog