Biashara ya nyumba na uwekezaji wa majengo ya kisasa inaendelea kupata wadau wapya kila inapoingia siku mpya, pamoja na hali ya uchumi tuliyonayo lakini timu ya marafiki bado inaendelea kupanga na kutekeleza kila aina ya mipango katika kufikia malengo makuu ambayo kila mmoja wetu amejiwekea. Hakuna namna mpya zaidi ya kuendelea kupigania kile tunachoamini kuwa tutakipata kwa muda ambao tumejipangia. Ni safari ngumu sana lakini yenye kila aina ya uwezekano wa kushinda, silaha zetu pekee ni juhudi, nidhamu na maarifa. Pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa katika kuhakikisha kila mmoja wetu anapata mafanikio ya kweli kwenye maisha yake, lakini kuna baadhi ya marafiki wanashindwa kusonga mbele kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa nyakati tofauti. Lengo kuu la Makala hii ni kupeana maarifa kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia kabla hujauza nyumba yako ili uweze kujitathmini na kufanya maamuzi yaliyo sahihi.

majengo29

TATHMINI LENGO KUU LA KUUZA NYUMBA YAKO

Wakati tulionao biashara ya nyumba na uwekezaji wa majengo unafanyika kwa mbinu za kisasa ambazo ni matokeo chanya ya ukuaji wa sekta ya ujenzi na mapinduzi ya teknolojia mbalimbali duniani kote. Watu binafsi, kampuni na taasisi nyingi zimejitokeza kwa wingi kuzitumia fursa zinazoendelea kujitokeza kila siku kwenye biashara ya nyumba na uwekezaji wa majengo ya kisasa. Lengo kuu la kampuni hizo ni kujiendesha kibiashara, kupata mafanikio ya uhuru wa kifedha kwa watu binafsi na kutoa huduma za makazi na biashara kwa wadau mbalimbali walio nje ya sekta ya ujenzi. Lakini kuna baadhi ya marafiki wamejikuta wakiingia kwenye uuzaji wa majengo yao kutokana na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kwenye maisha. Ni muhimu sana ukajitathmini kama unauza nyumba yako kwa lengo la kibiashara au kutokana na msukumo hasi wa kufikiri katika namna ya kupambana na changamoto zinazotukabili kwenye maisha yetu. Kujitathmini kwako kutakufanya ufikiri vizuri ili kuepuka majuto kama hukuwa na lengo la biashara, hatua hii itakusaidia kufanya maamuzi yaliyo sahihi yatakayo kufanya ubaki na furaha wakati wote.

SOMA; Zifahamu Hatua Muhimu Za Uwekezaji Wa Ardhi Na Majengo, Je Upo Hatua Gani Kuelekea Mafanikio Yako?

TATHMINI BEI NA GHARAMA YA MAUZO

Ni muhimu sana kufanya uthamini kujua bei ambayo utaipeleka sokoni na kuleta ushawishi kwa wanunuaji wa nyumba yako. Hali ya uchumi na ukubwa wa soko la nyumba ndio utakao kuongoza katika kupanga bei ya mauzo, pia ni muhimu sana kuweka gharama za kuwalipa mawakala pamoja na kodi mbalimbali katika kukidhi sheria na taratibu zilizopo. Tathmini ya bei na gharama ya mauzo itakusaidia kujua kiwango halisi na kutathmini faida au mapato utakayopata kabla hujaingia sokoni. Hatua hii itakufanya usimame imara kwenye mashauriano ya gharama za mauzo dhidi ya mteja na wakala watakaojitokeza kuhitaji nyumba hiyo. Hatua hii itakufanya utathmini vigezo mbalimbali ambavyo utavisimamia katika kuinadi na kupanga bei ya nyumba yako kwenye soko. Kama hujiamini ni muhimu ukawatembelea mawakala wa nyumba wakusaidie namna ya kupata wateja ambao umewadhamilia, usisite wala kuhofia jambo lolote maana wapo kwa ajili ya kukuhudumia wewe.

TATHMINI MAZINGIRA YA NYUMBA YAKO

Muundo na muonekano halisi wa nyumba yako ni muhimu sana kuzingatia ili iwe kivutio kwa wanunuzi, hali ya usafi wa nyumba yako ina ushawishi mkubwa kwa wanunuzi, hali ya ubora na uchakavu ni jambo mtambuka linalopaswa kuzingatiwa, fikiria kuhusu miundombinu ya huduma za maji, umeme na mawasiliano kama inafanya kazi ipasavyo. Mazingira halisi ya nyumba yako ndio itakayoshawishi muda gani nyumba yako itakuwa sokoni kupigania wateja dhidi ya nyumba nyingine zilizopo sokoni. Mvuto wa nyumba yako ndio itakayokushawishi kutathmini bei nzuri utakayoipeleka sokoni na kununuliwa ndani ya muda mfupi tofauti na nyumba nyingine zenye vigezo zinazofanana au kushabihana. Yapo mambo mengi sana ambayo wateja huyapa kipaumbele wakati wakutafuta nyumba ya kununua, mambo hayo hutofautiana kutokana na matumizi yanayokusudiwa na mnunuzi, hivyo ni muhimu sana ukatathmini hali ya soko la nyumba na kujitahidi kuweka mazingira yenye ushawishi mkubwa tofauti na wengine.

SOMA; Hizi Ndizo Mbinu Bora Za Kuepuka Majanga Kwenye Uwekezaji Wako Wa Majengo.

TATHMINI HALI YA SOKO LA NYUMBA

Maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano imeongeza ushindani wa hali ya juu sana kwenye mbinu mbalimbali za masoko ya nyumba. Ni muhimu sana ukajitathmini namna utakavyotumia mbinu za kisasa katika kuwafikia wateja uliowakusudia. Unaweza kutumia tovuti, blogu, magazeti, majarida na mitandao ya kijamii kama njia ya kuwafikishia taarifa wanunuzi wa nyumba yako. Kutozingatia hali ya soko la nyumba kwa wakati huo kutaifanya nyumba yako ikose ushawishi na kukaa muda mrefu sokoni pasipo kupata wateja. Ushindani mkubwa wa biashara na uwekezaji wa majengo umesababisha kukua na kuboreshwa kwa hali za nyumba kabla hazijaingia sokoni, tathmini kama muundo na muonekano wa nyumba yako inaushawishi kwa kiasi gani tofauti na wengine. Mbinu zinabadilika kila inapoingia siku mpya, hali ya uchumi nayo siyo ya uhakika kutokana na kukua na kuporomoka mara kwa mara, sheria na sera nazo hazipo nyuma kwenye mabadiliko haya, jambo muhimu kwako ni kusoma alama za nyakati ili zikusaidie kutathmini maamuzi yako kabla nyumba yako hujaipeleka sokoni.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com