Kila mtu amezaliwa na uwezo mkubwa sana ndani yake, kila mtu ana vipaji vya kipekee na kila mtu anaweza kuwa mshindi kwenye maisha yake.

Lakini dunia imefanya kazi moja kubwa ya kutuaminisha kwamba siyo kila mtu anaweza kufanikiwa. Hivyo wachache wameweza kufanikiwa huku wengi wakiishia kuwa na maisha ya kawaida ambayo hawayapendi wala kuridhika nayo.

Kazi kubwa ambayo aliyekuwa mwandishi, mzungumzaji na mhamasishaji Zig Zigler aliifanya katika kipindi cha uhai wake, ni kuwapa watu maarifa sahihi na hamasa ya kuweza kuchukua hatua ili kuweza kufikia ushindi ambao upo ndani yao.

Ni katika kitabu hichi cha Born To Win ambapo Zig Zigler na mwanae Tom Zigler wanatushirikisha njia sahihi ya kila mmoja wetu kuweza kuwa mshindi kwenye maisha yake.

Zigler anasema kwamba umezaliwa kushinda, lakini ili uweze kushinda unahitaji kwanza upange kushinda, ujiandae kushinda kisha ndiyo utegemee kushinda.

Kitabu hichi kimegawanyika katika sehemu kuu tatu;

Sehemu ya kwanza ni kujipanga kushinda.

Hapa Zigler anatupa msingi muhimu wa kufikia ushindi ambayo ni kuwa na maono makubwa, kuwa na malengo na pia kuwa na shauku kubwa ya kushinda. Bila ya vitu hivyo huwezi kushinda kamwe.

Sehemu ya pili ni kujiandaa kushinda.

Hapa Zigler anatuambia vitu tunavyohitaji ili kuweza kufikia ushindi. Anatushirikisha ujuzi tunaopaswa kuwa nao, elimu tunayohitaji na hata ushauri tunaohitaji kutoka kwa wengine.

Sehemu ya tatu ni kutegemea kushinda.

Baada ya kupanga kushinda, kisha kufanya maandalizi ya kushinda, kinachofuata ni kufanyia kazi mpango wa ushindi na kutegemea kupata matokeo mazuri ya ushindi. Kuna nguvu kubwa sana kwenye matarajio, na hapa ndipo mtazamo chanya unapofanya kazi yake.

born to win

Karibu sana kwenye uchambuzi huu wa kitabu na panga pia kusoma kitabu hichi. Kila mshindi anapaswa kusoma kitabu hichi, kwa sababu kina mkusanyiko wa kazi zote bora za Zig Zigler.

  1. Shauku ni mama wa hamasa.

Ili uweze kushinda, unahitaji kitu kimoja muhimu sana, hamasa ya kuweza kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata kile unachotaka. Bila ya hamasa hutafika mbali, changamoto zitakuangusha mara moja.

Hamasa inatokana na shauku kubwa ambayo mtu anakuwa nayo juu ya kitu. Kama una shauku, una hamu kubwa kweli ya kupata kitu, basi lazima utakuwa na hamasa ya kuchukua hatua ili kukiupata.

Hivyo hatua ya kwanza kabisa ya kufikia ushindi ni kuwa na hamu na shauku ya kushinda.

  1. Maono makubwa yanatengeneza hamu na shauku.

Tumeona ya kwamba ili uweze kuwa na hamasa kubwa ya mafanikio, unahitaji kuwa na hamu na shauku kubwa. Lakini je shauku hii inatoka wapi? Je wapo watu ambao wamezaliwa na shauku na ndiyo maana wanafanikiwa?

Swali ni hakuna anayezaliwa na shauku, bali kila mmoja anaweza kuizaa shauku. Na shauku inazaliwa kutoka kwenye maono makubwa ambayo mtu anakuwa nayo.

Ili uweze kushinda, unahitaji kuwa na maono makubwa ambayo yanakupa shauku inayoleta hamasa ya kuweka juhudi ili ufanikiwe. Angalia wote waliofanikiwa, huwa wanaanza na maono makubwa.

  1. Kujitoa na ung’ang’anizi ni muhimu kwa ushindi.

Siyo kwamba ukishakuwa na maono makubwa, utakuwa na shauku halafu hamasa inakupeleka moja kwa moja kwenye mafanikio. Dunia haifanyi kazi hivyo. Pamoja na maono makubwa unayoweza kuwa nayo, pamoja na mipango mikubwa unayoweza kuweka, utakutana na changamoto nyingi mno kwenye safari yako ya ushindi.

Na hapa ndipo unapohitaji vitu viwili muhimu sana, kujitoa na ung’ang’anizi.

Lazima ujitoe kweli ya kwamba unataka kushinda na hakuna chochote cha kukuzuia wewe kushinda.

Lazima kia uwe king’ang’anizi, lazima uendelee kuweka juhudi licha ya kukutana na changamoto na hata kushindwa.

  1. Maeneo saba muhimu ya maisha ya mafanikio.

Watu wengi wanaposikia kuhusu mafanikio hufikiria fedha na mali. Tunakazana kupata fedha na mali nyingi tukiamini hayo ndiyo mafanikio. Lakini je yafaa nini iwapo utapata fedha nyingi halafu afya yako ikawa mbovu? Au ukawa na mali za kutosha lakini huna maelewano na familia yako?

Mafanikio ya kweli yanahusisha maeneo saba ya maisha, lazima ufanikiwe kwenye maeneo yote ili kuwa na mafanikio ya kweli.

Eneo la kwanza ni afya yako binafsi, lazima uijali na kuilinda.

Eneo la pili ni familia yako, hawa ni watu muhimu sana kwako.

Eneo la tatu ni akili, lazima uiendeleze vizuri.

Eneo la nne ni fedha, lazima uwe na uhuru wa kifedha.

Eneo la tano ni wewe binafsi, lazima ujijali na kupata yale muhimu kwako.

Eneo la sita ni roho, lazima uwe mtu wa imani.

Eneo la saba ni kazi/biashara, lazima ufanye kile ambacho kina mchango kwa wengine.

Ukifanikiwa maeneo machache na kushindwa mengine, huna maisha ya mafanikio.

  1. Mambo sita yanayojenga msingi wa maisha ya mafanikio.

Watu wengi wamekuwa wanataka kufanikiwa, lakini hawazingatii misingi. Hufikiri mafanikio ni kitu kinachoweza kutokea tu kama bahati. Hapa yapo mambo sita muhimu yanayojenga msingi wa mafanikio;

Moja; uaminifu, lazima uwe mtu wa kutekeleza kile ulichoahidi, kufanya kama ulivyosema.

Mbili; tabia, tabia yako lazima iwe njema na yenye kuwapendeza watu. Watu wajisikie vizuri kujihusisha na wewe kutokana na tabia zako nzuri.

Tatu; imani, lazima uwe na imani ya kwamba unaweza kufanikiwa na unaweza kufanya makubwa.

Nne; uadilifu, unachofanya mbele ya watu na unachofanya ukiwa mwenyewe, lazima viwe vinaendana. Usiwe na maisha ya aina mbili.

Tano; upendo, lazima upende unachofanya na uwapende wengine pia.

Sita; kutunza imani ya wengine kwetu. Unapaswa kuwafanya wengine wajisikie salama kukuamini kwamba utatunza imani waliyoiweka juu yako.

Bila ya msingi huu imara wa mafanikio, huwezi kuwa na maisha ya ushindi.

SOMA; KITABU CHA JULY; MIMI NI MSHINDI, Ahadi Yangu Na Nafsi Yangu.

  1. Malengo yanakuwezesha kukaa kwenye njia moja ya mafanikio.

Safari ya maisha ya ushindi ina vishawishi vingi. Pamoja na kuwa na maono makubwa, zipo njia nyingi ambazo zinaweza kukushawishi uzitumie kufikia maono yako. Kama utafuata kila njia, hutaweza kufanikiwa.

Hapa ndipo unapaswa kuwa na malengo ambayo yanaonesha ni njia ipi unachukua, kipi unafanya na kwa wakati gani. Unapokuwa na malengo ambayo unayafuata na kuyafanyia kazi, unakuwa kwenye njia sahihi na kuepuka vishawishi vinavyokupotezea muda.

  1. Unahitaji kuchukua hatua kila siku.

Watu wengi wamekuwa wakifikiri kwamba kuna kitu kimoja tu ambacho ukishakifanya basi unafanikiwa. Wengi wamekuwa wanakimbizana na siri za mafanikio, wakiamini kuna siri ambayo wao hawajaijua na wakishaijua basi hawatakuwa na haja ya kuhangaika tena.

Kama siri ipo basi ipo wazi kabisa, ya kwamba ili kufanikiwa, lazima uchague kile unachotaka, halafu uwe tayari kuchukua hatua kila siku, KILA SIKU. Mafanikio ni mkusanyiko wa mambo madogo madogo yaliyorudiwa rudiwa kufanywa na siyo jambo kubwa lililofanywa mara moja.

Hivyo chochote unachotaka kufanya na unataka kufanikiwa, kama hupo tayari kufanya kila siku kwa maisha yako yote, sahau kuhusu ushindi na mafanikio.

  1. Thamani na kusudi vitakupa kichocheo cha kufanya kila siku.

Kuweza kufanya kitu kila siku kwa maisha yako yote siyo rahisi, wengi hukata tamaa na kuacha baada ya muda.

Vipo vitu viwili ambavyo vinaweza kukupa kichocheo cha kuendelea kufanya kila siku;

Cha kwanza ni thamani unayotoa, unapoona thamani unayotoa na namna inavyowasaidia wengine, unapata hamasa ya kuendelea kufanya zaidi ili kuwasaidia wengi zaidi.

Cha pili ni kusudi, unapojua kusudi la maisha yako na kulifanyia kazi, utaendelea kufanya kila siku.

Jua ni thamani gani unatoa kwa wengine na pia jua kusudi la maisha yako. Hivi vitakuwezesha wewe kuweza kufanya kila siku.

  1. Swali muhimu la kujua kusudi la maisha yako na kutengeneza maono yako.

Swali hilo ni KWA NINI?

Kwa nini upo hapa duniani?

Kwa nini unafanya kile ambacho unafanya?

Swali la kwa nini linakupa fursa ya kujiangalia ndani na kupata sababu halisi ya kwa nini upo hapa duniani na kwa nini unafanya yale unayofanya. Unapoweza kujibu swali hili unapata kusudi la maisha yako na kuweza kutengeneza maono makubwa ya maisha yako.

  1. Upo tayari kushindwa?

Japokuwa umezaliwa kushinda na una kila kinachokuwezesha kushinda, maisha yako hayatakuwa ushindi pekee. Kuna wakati utakutana na kushindwa, hasa pale unapohitajika kujaribu mambo mapya, ambayo huna uzoefu wa kuyafanya.

Wale ambao wanaogopa kushindwa huwa hawajaribu mambo mapya, na hivyo kujizuia kabisa kushinda.

Wale wanaojaribu mambo mapya, na kuwa tayari kushindwa, hushindwa, lakini pia hujifunza na hivyo kushinda zaidi baadaye.

Usiogope kujaribu mambo mapya na hata yanayoweza kuonekana hatari kama unataka kushinda.

SOMA; NYEUSI NA NYEUPE; Kizazi Cha Alama A+ Na Zawadi Ya Kushiriki.

  1. Maamuzi mabovu yana madhara makubwa kuliko unavyofikiri.

Iwapo ungejua nguvu kubwa ya maamuzi unayofanya kwenye maisha yako, usingekuwa unafanya maamuzi kirahisi rahisi tu. Wengi hukimbilia kufanya maamuzi, ambayo huwa ni mabovu na yanawaharibia zaidi.

Kwa mfano, unapofanya maamuzi mabovu, unapata matokeo mabovu, matokeo hayo mabovu yanapelekea hali yako kuwa mbaya, na ukishakuwa na hali mbaya unakuwa huna namna, unaona hakuna tena unachoweza kufanya.

Lakini kwa upande wa pili, ukifanya maamuzi bora, unapata matokeo mazuri, ambayo yanafanya hali yako kuwa nzuri na kuona mambo mazuri zaidi ya kufanya.

Kuwa makini sana na maamuzi unayofanya.

  1. Chagua marafiki na wanaokuzunguka kwa umakini mkubwa.

Sababu kubwa inayowazuia wengi kufanikiwa ni maoni ya wale ambao wamewazunguka. Unaweza kuwa na mipango mikubwa sana ya mafanikio, lakini kama umezungukwa na watu waliokata tamaa, watakukatisha tamaa na hutaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Watu wengi ambao wana mtazamo hasi na waliokata tamaa huwa hawafanikiwi, hivyo chunga sana hawa wasiwe watu wa karibu kwako, maana hawatakuruhusu wewe ufanikiwe.

  1. Unahitaji elimu sahihi ya mafanikio.

Huwezi kufanikiwa kama hujielimishi kwa maarifa sahihi. Maarifa sahihi yanakuwezesha wewe kuona kule unakokwenda na kukuwezesha kuamka tena pale unapoanguka.

Katika safari ya mafanikio, kuanguka ni swala la kawaida, unahitaji elimu sahihi ili uweze kuinuka na kuendelea na safari.

  1. Elimu pia inayafungua macho yako kuziona fursa.

Jambo moja la kushangaza kuhusu fursa ni kwamba, zipo mbele yetu kila siku, tena pale pale ambapo tupo. Lakini wengi hatuzioni kwa sababu macho yetu hayajui jinsi ya kuziona fursa hizi.

Elimu sahihi inakuwezesha wewe kuziona fursa ambazo tayari zipo mbele yako. Kadiri unavyokuwa na ufahamu mkubwa juu ya jambo lolote, ndivyo unavyoweza kuziona fursa nyingi zaidi hata kama wengine hawaoni.

Hivyo chochote unachofanya, hakikisha unakijua vizuri sana. Hilo litakuwezesha wewe kuziona fursa nyingi zaidi.

  1. Kabla hujategemea kushinda, lazima uwekeze ndani yako kwanza.

Hakuna mafanikio bila ya uwekezaji ndani yako. Na uwekezaji tunaozungumzia hapa ni uwekezaji wa maarifa na taarifa sahihi za mafanikio.

Lazima uwe mtu wa kujifunza kila siku na kila wakati. Lazima usome vitabu, usome makala na machapisho yanayohusu kile unachofanya na mafanikio kwa ujumla.

Na muhimu zaidi, pale unapokuwa kwenye safari, geuza safari yako kuwa chuo cha kujifunza. Fanya hivyo kwa kusikiliza vitabu vilivyosomwa na hivyo kujifunza huku ukiendelea na safari yako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THINK LIKE A CHAMPION (Fikiri Kama Mshindi, Elimu Isiyo Rasmi Kuhusu Biashara Na Maisha.)

  1. Ubora unatokana na kufanya.

Huwezi kuwa bora kama hufanyi, huwezi kuwa bora kwa kujifunza na kupanga pekee. Hata kama ungejifunza na kujua kwa kiasi gani, unapoanza kufanya lazima utakosea. Lakini kadiri unavyoendelea kufanya, unazidi kuwa bora zaidi na zaidi.

Jua kipi unachotaka, na anza kuweka kwenye vitendo, kila wakati kazana kuwa bora zaidi ya wakati uliopita, hii itakupeleka kwenye mafanikio.

  1. Sehemu mbili za kupata uzoefu.

Uzoefu ni muhimu sana kwenye mafanikio, lazima kuwa na uzoefu wa mambo gani ya kufanya na yapi siyo ya kufanya ili kuweza kufanikiwa.

Tunaweza kupata uzoefu kutoka sehemu mbili;

Moja; kutokana na makosa yetu wenyewe, hapa inatubidi tufanye makosa na kujifunza. Uzoefu huu una gharama kubwa na unachukua muda kuupata, kwa sababu huwezi kujaribu kila kitu.

Mbili; uzoefu wa wengine, hapa unajifunza kutoka kwa wengine na kupata ushauri wao pia. Huu ni uzoefu usio na gharama na hauhitaji muda kuweza kuupata.

Changamoto ni kwamba watu wengi huwa hawapendi kupokea ushauri, wanaamini wao wanajua kuliko wengine na hivyo kurudia makosa ambayo yameshafanywa na wengine.

  1. Kuwa mchimbaji wa ushauri.

Japokuwa unahitaji ushauri ili kufanikiwa, siyo kila ushauri unakufaa wewe, hata kama unatolewa na mtu gani.

Kupata ushauri ni sawa na kuchimba dhahabu. Ili upate kilo moja ya dhahabu utachimba sehemu kubwa sana ya ardhi, utahitajika kuondoa uchafu mwingi mno, lazima ichomwe na kuchujwa ndiyo ipatikane dhahabu safi.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye ushauri pia, kuna ushauri mwingi unahitaji kuutupa ili kuweza kubaki na ule ushauri mzuri na wenye thamani kwako.

  1. Sifa saba za washauri wazuri.

Unahitaji kuwa na mshauri au mtu unayemsikiliza kwenye maisha yako. Huyu anaweza kuwa menta wako, kocha wako au hata mtu unayependa kuwa kama yeye.

Ili kupata mtu atakayekusaidia, angalia sifa hizi saba muhimu;

Moja; awe na tabia nzuri, ambayo upo tayari kuiiga.

Mbili; awe na historia nzuri ya mafanikio kwenye yale anayofanya.

Tatu; awe msikilizaji mzuri na siyo mtu wa kuongea pekee.

Nne; awe mtu wa kufanya maamuzi mazuri.

Tano; awe mtu ambaye anasema ukweli mara zote, hata kama unakuumiza.

Sita; awe na mahusiano mazuri na watu wengine.

Saba; awe anafurahia mafanikio ya watu wengine, asiwe na wivu pale wengine wanapofanikiwa.

Inaweza kuwa vigumu kumpata mtu mmoja mwenye sifa zote hizo saba, lakini kama mtu hana sifa hata moja kati ya hizo saba, usichukue ushauri wowote anaokupa, utakuangamiza.

  1. Baada ya kupanga na kujiandaa, sasa tegemea kushinda.

Wanaweza kuwepo watu wawili, wenye elimu sawa na wote wanafanya kazi au biashara ya aina moja. Baada ya muda unakuta mmoja kafanikiwa sana na mwingine akaishia kuwa kawaida. Tofauti kubwa huwa inaanzia kwenye mategemeo. Wale wanaoshinda huwa wanategemea kushinda. Baada ya kuwa wamejipanga vizuri kisha wakafanya maandalizi mazuri, wanajua lazima watapata matokeo mazuri kwenye maisha yao.

Ili kuwa na mategemeo ya ushindi, lazima uwe mtu chanya, ambaye una mtazamo chanya na kwenye kila jambo unaangalia upande chanya. Ukiwa mtu hasi unakata tamaa na huwezi kuendelea na safari ya mafanikio.

  1. Maeneo matatu unayohitaji kuyafanyia kazi kwa mafanikio yako.

Sisi binadamu tumegawanyika katika sehemu kuu tatu, zote ni muhimu na zinashirikiana sana katika kuwa na maisha ya mafanikio.

Sehemu ya kwanza ni mwili, hapa unahusisha afya yako ya mwili, ambapo unahitaji kuulisha mwili wako vizuri na kuulinda kiafya.

Sehemu ya pili ni akili, ambapo unahusisha fikra zako, hapa unahitaji kuzitengeneza vizuri, ziwe chanya na uendelee kujifunza.

Sehemu ya tatu ni roho, hapa unahusisha imani, lazima uwe mtu wa imani, uweze kukua kiroho ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha.

Bila ya maendeleo na ukuaji kwenye maeneo hayo matatu, huwezi kuwa na maisha ya mafanikio.

Kama nilivyokuambia rafiki, hichi ni kitabu muhimu sana kusoma kwa sababu kila mmoja wetu anapenda kuwa mshindi na kupiga hatua zaidi kwenye maisha yake. Pata muda usome kitabu hichi, utajifunza mengi ya kufanyia kazi kwenye maisha yako na kuweza kweli KUWA MSHINDI KAMA AMBAVYO UMEZALIWA KUSHINDA.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

MIMI NI MSHINDI

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz