Habari za leo rafiki?

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Kila mtu anapenda mafanikio, lakini changamoto zipo kwenye njia yetu ya mafanikio. Hatupaswi kukimbia changamoto hizi, kwa sababu bila ya kutatua hazitaondoka. Kwenye kipengele hichi tunapena mbinu na mikakati ya kutatua changamoto tunazokutana nazo.

Changamoto ya mtaji wa kuanza biashara imekuwa inawasumbua wengi. Wapo watu wengi wanaosema wangependa sana kuingia kwenye biashara lakini hawana mtaji wa kufanya hivyo. Nimekuwa nasema mara zote kwamba mtaji siyo kikwazo kwa yeyote aliyeamua kuingia kwenye biashara, badala yake ni sababu kwa wale ambao hawataki kujituma.

Nitakwenda kudhibitisha hilo tena leo kwa kuonesha namna mtu anaweza kuanza biashara bila ya mtaji kwa kutumia elimu au utaalamu alionao.

kuanza biashara

Kabla hatujaangalia hatua zipi za kuchukua, tusome maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kutuomba ushauri kwenye hili;

Nina elimu ya diploma ya uhasibu, changamoto yangu kubwa natamani sana kufanya biashara ila upatikanaji wa kipato/mtaji kwangu imekuwa ni changamoto na biashara ya kufanya nawaza ni ipi? – Kelvin M. J.

Kama alivyotushirikisha Kelvin hapo, wapo wengine pia ambao wapo kwenye hali kama yake. Wamesoma na kuhitimu, kazi hawajapata na wakifikiria kuanza biashara hawana mtaji wa kuanzia.

Kwenye makala hii nakwenda kushauri wapi pa kuanzia, nitatumia mfano wa taaluma ya uhasibu ya Kelvin lakini unaweza kutumia ushauri huu kwa taaluma yoyote uliyonayo,  iwe ni ualimu, udaktari, kilimo na kadhalika.

Kwanza kabisa naomba nikusaidia kuondoa uongo ambao umekuwa unajipa kila siku. Uongo huo ni kwamba huna mtaji. Mtaji unao, mtaji kila mtu anao, sema watu wengi hawajui aina ya mtaji walionao na hawajui jinsi ya kuutumia.

Tunaposema mtaji, watu wengi wanafikiria kuhusu fedha pekee. Lakini ipo mitaji mingine mingi muhimu inayohitajika ili biashara iweze kufanikiwa, ambayo siyo fedha.

SOMA; USHAURI; Biashara Tano (05) Unazoweza Kuanzisha Kama Huna Mtaji Wa Kuanza Biashara.

Mfano wa mitaji hiyo ni nguvu binafsi ambazo mtu anazo, uzoefu ambao mtu ameupata, elimu au taaluma ambayo mtu anayo, na hata watu ambao mtu anafahamiana nao. Yote hii ni mitaji ambayo mtu akiweza kuitumia vizuri, ataweza kupiga hatua kwenye maisha yake.

Kama tayari una taaluma ambayo umesomea, huo ni mtaji ambao tunakwenda kuangalia unavyoweza kuutumia kuanza biashara. Tutachanganya mtaji huu wa taaluma na nguvu zako binafsi katika kuanza biashara bila ya mtaji wa fedha.

Biashara ambayo unakwenda kuanza ni biashara ya kutoa huduma, ambayo inatokana na taaluma ambayo mtu unayo, au uzoefu ambao mtu umeupata.

Kwa taaluma ambayo mtu unayo, angalia ni kwa namna gani inaweza kuisaidia jamii. Angalia ni watu gani ambao wana changamoto, ambao unaweza kuwasaidia kutatua changamoto hizo kupitia taaluma uliyoipata.

Kwa mfano kwa taaluma ya uhasibu, zipo biashara nyingi ndogo ambazo zinapata changamoto kubwa kwenye mambo ya kuweka vizuri kumbukumbu za kifedha na uhasibu pia. Wengi wamekuwa wakiamini wanaohitaji huduma za uhasibu ni biashara kubwa na makampuni makubwa. Lakini wangepata elimu sahihi, wangeweza kutumia huduma za uhasibu kujua kama biashara zao zinakua na hata kuweka mipango sahihi ya kibiashara.

Hivyo angalia ni namna gani unaweza kuwasaidia watu kwa taaluma hiyo ya uhasibu. Angalia changamoto ya wafanyabiashara katika mahesabu ya fedha na kuweka kumbukumbu za kibiashara. Wengi wanatumia njia ambazo siyo za kiteknolojia, ambazo ni ngumu na hawawezi kuzifanyia kazi kila siku.

Wewe angalia ni kwa jinsi gani unaweza kuwarahisishia njia hizo wanazotumia. Labda unaweza kutafuta programu nzuri ya kompyuta au ya siku, ambayo itawawezesha kuweka sawa kumbukumbu zao za kibiashara. Hapo unawarahisishia zoezi la kuchukua na kutunza kumbukumbu.

Unaweza pia kuwasaidia kuandaa mahesabu ya kibiashara, ambayo wataweza kuyatumia sehemu mbalimbali.

Biashara nyingi pia zinasumbuka sana na mambo ya kodi, wafanyabiashara wengi hawaelewi sheria na utaratibu wa kodi, wamekuwa wakikadiriwa kodi kubwa kuliko uwezo wa biashara zao. unaweza kutumia elimu yako kuwasaidia wafanyabiashara kupangiwa kodi sahihi na hata kuwasaidia kupanga muda mzuri wa wao kulipa kodi ili kuepuka usumbufu wa kupewa adhabu pale wanapochelewa kufanya hivyo.

Hata kama hujasajiliwa kuwa mhasibu ambaye anakagua hesabu za biashara, bado taaluma yako ya uhasibu inaweza kuwasaidia watu, na wao kuwa tayari kukulipa kulingana na huduma unayowapatia.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Vijana Wanaotafuta Ajira, Walioajiriwa Lakini Ajira Haziwaridhishi Na Waliojiajiri Lakini Wanaona Mambo Hayaendi.

Hapo tumeangalia mtaji mmoja ambao ni taaluma uliyonayo, sasa kuna mtaji mwingine wa nguvu zako binafsi ambao nimekuambia utautumia pia.

Mtaji wa nguvu zako binafsi utautumia kuweza kuwafikia watu wengi ambao wana uhitaji wa huduma uliyochagua kutoa. Ukweli ni kwamba, utakapoanza kutoa huduma zako siyo kila mtu atakubali kuwa mteja wako. Wengi watakukatalia, wengine hawataona umuhimu wa huduma zako. Hivyo unahitaji kuongea na watu wengi sana, unahitaji kuwashawishi wengi ili kupata wachache wanaokubali kufanya kazi na wewe.

Unahitaji pia kuweka nguvu katika kuzifuatilia biashara kabla hata hujaongea na wahusika. Fuatilia uone changamoto zake ni zipi, na wewe unawezaje kuwasaidia ili kupiga hatua zaidi. Hapo unapata kitu cha kuwashawishi wajaribu kufanya kazi na wewe.

Unahitaji kuweka nguvu sana kwa sababu mwanzoni utahitaji kufanya kazi bure, unahitaji kuwahudumia wale wachache wanaokubali huduma zako, kwa gharama za chini kabisa au hata bure. Hii ndiyo njia itakayojenga jina lako na watu kuona msaada wako ndipo wawe tayari kulipia huduma zako.

Mambo mengine ambayo yatahitaji nguvu zako ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa huduma za uhasibu. Hapa unajitoa kufundisha jamii kuhusu umuhimu wa huduma hizo, unaweza kufanya hivyo kupitia mitandao ya kijamii na muhimu zaidi, unapaswa kuwa na blogu ambayo unaitumia kutoa mafunzo yanayohusiana na huduma za uhasibu.

Taaluma yoyote uliyonayo, uzoefu wowote ambao umewahi kuupata na kitu chochote ambacho unapenda kufuatia, unaweza kukitumia kuanza biashara ya huduma, na hiyo ikakuwezesha kutengeneza jina lako na hata kipato pia. Na hapo inaweza kuwa hatua ya kwanza ya wewe kuingia kwenye biashara na hata kukua zaidi kibiashara.

Kama hujaingia kwenye biashara kwa kisingizio kwamba huna mtaji, siyo kweli kwamba mtaji ndiyo unakuzuia, ila wewe hujajitoa kuingia kwenye biashara, na unatumia mtaji kama sababu. Ukijitoa kweli, hakuna chochote au yeyote anayeweza kukuzuia. Kwa sababu mtaji mkubwa ni wewe mwenyewe, ukishakuwa tayari, kila kitu kinakaa sawa.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog