Uchumi wa nchi yoyote ile duniani, unategemea sana kwenye biashara ndogo. Hii ni kwa sababu ni biashara ambazo watu wanaweza kuanzisha, wakajiajiri wao na hata kuajiri wengine na pia zikachangia kwenye kulipa kodi.

Njia ya uhakika ya kuwawezesha watu kuondoka kwenye umasikini, ni biashara ndogo. Hii ni kwa sababu biashara hizi zinawapatia kipato ambacho hakina ukomo iwapo watakuwa tayari kuweka juhudi na kutoa thamani kwa wengine.

Sehemu kubwa ya wafanyabiashara kwenye jamii zetu wanafanya biashara ndogo, hizi ni biashara ambazo mtu anaendesha mwenyewe, au ameajiri watu wachache, chini ya kumi ambao wanamsaidia kwenye biashara yake hiyo.

Maendeleo ya kiteknolojia yamebadili sana biashara. Kwenye zama hizi, mtu anaweza kuwa na biashara ndogo, anayoiendeshea nyumbani kwake lakini akaweza kuuza dunia nzima. Anaweza hata kuingia kwenye ushindani na makampuni makubwa yanayofanya biashara ya aina moja.

Kuanzisha na kukuza biashara ni jambo ambalo wengi wanapenda, kutokana na ule uhuru wa kuendesha kitu chao wenyewe. Lakini pia ni moja ya mambo magumu sana kufanya na hili linadhibitishwa na wingi wa biashara zinazokufa na nyingi ambazo zimedumaa.

Hayo na mengine mengi yalimfanya mwandishi Steven Strauss kuandika kitabu ambacho anakiita BIBLIA YA BIASHARA NDOGO. Na baada ya kukisoma, nimekubali kweli hii ni biblia ya biashara ndogo, kwa sababu kitabu hichi kina kila kitu kuhusu biashara, kuanzia wazo la biashara, mpango wa biashara, kupata mtaji, kuanza biashara, masoko, uuzaji, usimamizi wa fedha, rasilimali watu na chochote unachoweza kufikiria kuhusu biashara, kipo ndani ya kitabu hichi.

Ni kitabu ambacho kila mtu ambaye yupo kwenye biashara anapaswa kukisoma. Na kama ilivyo kwa Biblia ya kwenye dini, ni kitabu kikubwa, ambacho utapaswa kukisoma kila siku. Kila siku unachagua kitu unachotaka kujifunza na kukisoma. Kwa njia hii utaweza kujifunza na kuendesha biashara yako vizuri.

small business bible

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hichi, ambao ni sehemu ndogo sana ya yale mengi yaliyopo kwenye kitabu hichi. Nakusihi usome uchambuzi huu kama sehemu ya kuanzia na kupata hamasa, lakini pata kitabu chenyewe na kisome taratibu taratibu. Kama utasoma kitabu kimoja tu kwenye maisha yako, basi hichi ndiyo kitabu unapaswa kukisoma. Na kama ukichagua kusoma kurasa kumi tu za kiabu hichi kila siku, kitu ambacho unaweza, utakimaliza ndani ya miezi miwili.

Hivyo karibu kwenye uchambuzi, na mwisho nitakupa utaratibu wa kupata kitabu hichi, pamoja na utaratibu mzuri wa kusoma vitabu zaidi.

  1. Hakuna anayeweza kukuhakikishia chochote kwenye biashara.

Watu wengi huingia kwenye biashara wakiwa na hamasa kubwa ya kuwa matajiri wao wenyewe, kufanya kazi kama wanavyojisikia na kuwa na uhuru wa kifedha. Lakini hayo yote huwa hayatokei kama watu wanavyotegemea yatokee. Mambo huwa magumu, changamoto hujitokeza.

Lakini mtu anapokuwa na uelewa sahihi juu ya biashara, akaanza biashara sahihi kwake, ambayo anaipenda, na akaweka juhudi kubwa, mwisho huwa na biashara nzuri na yenye mafanikio.

  1. Swali sahihi kuuliza kuhusu ujasiriamali.

Watu wengi wamekuwa wanajiuliza swali iwapo ujasiriamali unawafaa kama sehemu yao ya kuingiza kipato. Hili siyo swali sahihi. Swali sahihi ni je wewe unaufaa ujasiriamali? Kwa sababu kinachofanya mtu afanikiwe au kushindwa kwenye ujasiriamali siyo biashara anayoanzisha, bali yeye kama yeye.

Je upo tayari kwa msongo wa mawazo unaotokana na ujasiriamali? Je upo tayari na hali ya kutokuwa na uhakika wa jambo unalofanya? Vipi kuhusu kukosa uhakika wa kipato? Haya ni maswali muhimu kujiuliza ili uone kama ujasiriamali unakufaa. Kama haukufai usione aibu, badala yake fanya kile unachoweza na kinachokufaa.

  1. Njia tano za kupunguza hatari ya kushindwa kwenye biashara.

Kuanzisha biashara ni jambo la hatari, unaweza kupata hasara, ukapoteza kila kitu na maisha yakawa magumu sana. Lakini wafanyabiashara waliofanikiwa licha ya hatari hii, walizingatia mambo haya matano muhimu ambayo wewe pia unapaswa kuyazingatia ili kupunguza hatari kwenye biashara;

Moja; jua namba zako vizuri, jua kiasi gani cha mtaji unahitaji kuanza, na jua kiasi gani cha mauzo kinakuwezesha kuendelea kuwepo kwenye biashara.

Mbili; fanya utafiti, jaribu mambo kabla hujayafanyia kazi, angalia wengine wanafanya nini pia na ujifunze.

Tatu; endesha biashara kama kampuni, hii italinda mali zako zisifilisiwe iwapo biashara itafilisika.

Nne; kuwa na bima, ili mambo yanapokwenda vibaya, uwe na pa kusimamia.

Tano; omba msaada wa wengine, unahitaji kuajiri watu wa kukusaidia, na pia kupata ushauri kutoka kwa ma menta na wataalamu wengine.

  1. Kosa wanalofanya wanaoingia kwenye biashara wanazopenda.

Ni muhimu mtu kuingia kwenye biashara inayohusisha kitu anachopenda au ambacho ana uzoefu nacho. Lakini lipo kosa moja ambalo wengi wanafanya na linawagharimu. Kosa hili ni kujua zaidi kile ambacho wanafanya kuliko kujua biashara yenyewe.

Kwa mfano kama mtu anajua na anapenda kupika mikate, basi anaanzisha biashara ya mikate, na kuendelea kujifunza kuhusu mikate. Hapa anakutana na changamoto nyingi kwa sababu hajui kuhusu biashara, bali anachojua ni kuhusu mikate.

Kuondokana na changamoto hii, unapaswa kujifunza upande wa biashara. Hata kama unajua sana kile unachofanya, jifunze kuhusu biashara, vitu kama masoko, mauzo, mzunguko wa fedha, hesabu za fedha na kadhalika. Vitakusaidia kuendesha biashara yenye mafanikio.

  1. Elimu haijakamilika kama hakuna vitendo.

Hata kama ungesoma vitabu vingi kiasi gani, ukahudhuria kila aina ya mafunzo kuhusu biashara, elimu yako ya biashara bado haijakamilika kama hujajifunza kwa vitendo. Elimu hii kwa vitendo unaweza kuipata kwa njia mbili, kama bado hujaingia kwenye biashara.

Njia ya kwanza ni kupata nafasi ya kufanya kazi kwenye biashara za wengine, kwa lengo la kujifunza. Unaomba kazi eneo ambalo lina biashara kama unayotaka kufanya, na hapo unajifunza mengi kuhusu biashara yako, bila hatari ya kufanya makosa.

Njia ya pili ni kuongea na wanaofanya na kuwaangalia kwa karibu. Njia hii siyo nzuri kama ya kwanza.

SOMA; Hatua Tano (05) Muhimu Za Kuchukua Kuokoa Biashara Inayokufa.

  1. Biashara ni kama mtoto.

Unapoanza biashara unapaswa kuelewa jambo hili muhimu sana, biashara yako itageuka kuwa mtoto wako. Na inapokuwa changa haina tofauti kabisa na mtoto mchanga. Itahitaji muda wako mwingi, mapenzi yako kwa biashara hiyo na pia itahitaji fedha.

Kama ambavyo siku za mwanzo za mtoto ni hatari, ndivyo pia ilivyo kwa siku za mwanzo za biashara. Jua hili unapoanza biashara ili uweze kujitoa kisawasawa.

  1. Wazo la biashara lina mchango mdogo sana kwenye mafanikio (asilimia moja).

Wapo watu ambao hufikiri wakipata wazo moja bora kabisa la biashara basi mafanikio ni uhakika. Nina habari mbaya kwa watu hawa. Wazo bora la biashara siyo kitu kwenye mafanikio ya biashara, lina mchango sana, asilimia moja pekee.

Asilimia 99 ya mafanikio ya biashara, yanatokana na juhudi, ubunifu, mtazamo sahihi, uvumilivu na kutokukata tamaa. Hivyo kama unaangalia biashara ipi itakuletea mafanikio, anza kuangalia kwanza kama wewe unazo tabia zinazoweza kuipeleka biashara kwenye mafanikio.

  1. Kununua biashara inaweza kuwa bora kuliko kuanzia chini.

Kuanzia biashara chini kabisa kuna hatari kubwa kuliko kununua biashara ambayo tayari imeshaanzishwa na inajiendesha yenyewe.

Kwa kununua biashara ambayo tayari imeshaanza, unaondokana na hatari ya kifo cha biashara mwanzoni. Lakini pia unaanza na wateja ambao tayari walikuwa wanaijua biashara, tofauti na unapoanza bila ya mteja kabisa.

  1. Mambo ya kuzingatia pale unaponunua biashara.

Watu wengi wanauza biashara zao siku hizi. Wapo ambao wanaanzisha biashara kwa lengo la kuja kuziuza na wapo ambao wanaziuza baada ya kushindwa kuziendesha. Unapoamua kununua biashara, angalia mambo haya muhimu;

Moja; kwa nini mmiliki anauza biashara hiyo. je ni kwa sababu anakwenda kwenye mambo mengine au ni kwa sababu imemshinda? Kwa kujua hilo kunakuwezesha kujua hata bei sahihi ya kununulia, na kujua changamoto zake pia.

Mbili; pata taarifa za kutosha kuhusiana na biashara hiyo, kutoka kwa watu wengine na siyo yule anayekuuzia. Anayekuuzia anaweza kukuambia vitu ambavyo siyo sahihi, ili kukuhamasisha kununua.

Tatu; jua washindani wa biashara hiyo na walipo ukilinganisha na biashara hiyo.

Unapoamua kununua biashara, hakikisha unanunua biashara ambayo itakutengenezea faidia na siyo kupoteza fedha.

  1. Mchanganuo wa biashara ni muhimu.

Watu wengi huingia kwenye biashara wakiwa hawana mchanganuo (business plan). Wengi hufanya hivyo pale wanapohitaji kuomba mkopo au kupata ruzuku ya mtaji.

Lakini mchanganuo wa biashara ni muhimu siyo tu kwa mkopo, bali hata kukuwezesha wewe kuijua biashara yako vizuri na kuweza kupima ukuaji wa biashara yako.

SOMA; KITABU; IJUE BIASHARA YA MTANDAO (NETWORK MARKETING), Miliki Biashara Kubwa Kwa Kuanza Na Mtaji Kidogo.

  1. Chagua njia ya kuanza biashara.

Zipo njia nyingi za kuanza biashara, zifuatazo ni tatu muhimu za kuzingatia.

Moja; unaweza kuanza biashara kama mtu binafsi, hii ni rahisi kwenye maamuzi lakini hatari kwa mali zako binafsi.

Mbili; ni ushirikiano na mtu mwingine, hii ina msaada kwenye kupata kile ambacho huna na mwingine anacho, labda utaalamu au fedha.

Tatu; ni kampuni, hapa biashara inajiendesha kama kampuni, ambayo inajitegemea yenyewe. Kampuni ina urasimu kwenye kufanya maamuzi, lakini ni salama kwa mali zako binafsi.

  1. Kushirikiana kwenye biashara ni sawa na ndoa.

Moja ya njia za kuanza biashara pale ambapo una mtaji kidogo au huna uzoefu ni kushirikiana na mtu mwingine. Watu wengi wamekuwa wakishirikiana na ndugu, jamaa au marafiki kwenye kuanza biashara zao.

Kitu ambacho wanakuwa hawajajua ni kwamba, ushirikiano wa kibiashara ni sawa na uhusiano kwenye ndoa. Hii ni kwa sababu mnakuwa pamoja kwa muda mwingi, na makosa ya mtu mmoja yanaigharimu biashara nzima.

Hivyo kabla hujaingia kwenye ushirikiano wa kibiashara na mtu, fanya tathmini kama ni mtu unayeweza kwenda naye. Epuka sana ndugu na marafiki kadiri inavyowezekana, kwa sababu biashara ikifa na mahusiano yanavunjika. Je upo tayari kukosa biashara na ndugu au rafiki?

  1. Njia za kupiata mtaji wa kuanza biashara zipo nyingi.

Watu wengi watakuambia hawajaingia kwenye biashara kwa sababu hawana mtaji. Ukiwauliza ni njia zipi wametumia mpaka kufikia kuona hawajapata mtaji watakutajia mbili tu, hawana akiba na hawajapata mkopo.

Zipo njia nyingi ukianza na akiba binafsi, mtu unaweza kujiwekea akiba kwa lengo la kuja kuanza biashara.

Pia unaweza kupata michango kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Unaweza pia kupata ruzuku kutoka kwenye taasisi mbalimbali zinazofanya hivyo.

Unaweza kupata mtaji kutoka kwa wawekezaji, iwapo utaweza kuwavutia kupitia mchanganuo wako wa biashara.

Unaweza pia kuchukua mkopo kutoka kwenye taasisi za kifedha.

Njia zipo nyingi na kadiri unavyoijua biashara yako vizuri, ukiwa na mchanganuo mzuri na kujaribu njia mbalimbali, huwezi kukosa mtaji wa biashara.

  1. Mambo ya kuepuka kwenye kutafuta mtaji wa biashara.

Moja; epuka sana kuchukua mkopo kwenda kuanzisha biashara mpya, ni hatari, bora kuanza na njia nyingine.

Mbili; epuka sana kuchukua mkopo kutoka kwa ndugu au watu wengine ambao mna mahusiano ya karibu, hasa unapoenda kuanza biashara. Mnaweza kuishia kugombana na uhusiano ukavunjika.

Tatu; unapochukua mkopo wa biashara, epuka kutumia nyumba yako au ya biashara kama dhamana ya mkopo. Si vyema kukosa biashara na mahali pa kulala pia.

  1. Sababu saba kwa nini biashara nyingi ndogo zinakufa.

Utafiti uliofanywa na Hector Barreto umegundua biashara ndogo zinazokufa zina mambo haya saba;

Moja; mtaji mdogo.

Mbili; biashara isiyofaa kwa eneo na wakati husika.

Tatu; mmiliki kukosa hamasa na kujitoa kuikuza biashara.

Nne; mmiliki kukosa maandalizi ya kutosha.

Tano; biashara ina wafanyakazi wabovu.

Sita; mmiliki hajui jinsi ya kutumia teknolojia kwa maendeleo ya biashara.

Saba; mmiliki hajui ambacho hajui na hayupo tayari kujifunza.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; BE OBSESSED OR BE AVERAGE (Chagua Kupenda Sana Kile Unachofanya Au Chagua Kuwa Kawaida).

  1. Mambo saba ya kufanya ili kukuza biashara yako.

Moja; bidhaa itatue changamoto au kutimiza mahitaji ya wateja.

Mbili; bidhaa iwe na ubora wa hali ya juu, kwa bei ambayo wateja wanaiweza.

Tatu; kuwa mwangalifu kwenye fedha.

Nne; mzunguko wa fedha ni eneo la kusimamia vizuri.

Tano; linda fedha zako vizuri kwa upotevu na utapeli.

Sita; ongeza soko la biashara yako.

Saba; uza, hii ndiyo injini ya biashara.

  1. Eneo la biashara ni muhimu kulingana na biashara.

Kama biashara unayofanya inahitaji watu wanaopita waione, basi unahitaji kuiweka kwenye eneo ambalo watu wakipita wanaiona. Lakini kama una njia nyingine ya kuwawezesha wateja kujua biashara yako ilipo, itakuwa bora zaidi. Hii ni kwa sababu maeneo yanayoonekana kodi zake huwa kubwa, huku eneo la pembeni likiwa na kodi ndogo.

Kwa maendeleo ya sasa ya teknolojia, unaweza kuweka biashara yako popote na ukawafikia wateja unaowalenga.

  1. Biashara yako ni jina unalojenga.

Wafanyabiashara wengi huchukulia jina la biashara kirahisi, lakini hilo lina thamani kubwa sana kwenye biashara. Jina la biashara (brand) ni kitu kinachoweza kukuza au kuua biashara yako. Ili kufanikiwa kwenye biashara, lazima ujenge jina lako kibiashara.

Jina la biashara (brand) linatengenezwa kutokana na sifa ambazo biashara inakuwa nazo kwa wateja wake. Hivyo mtazamo na mpokeo wa wateja ndiyo unaojenga jina la biashara.

Katika kujenga jina la biashara yako, kwanza ipe jina linaloeleweka na linalohusiana na unachofanya, toa bidhaa au huduma bora kabisa, kuwa na msimamo kwenye yale unayofanya. Wateja wakishazoea kile wanapata kwako, wanakuwa tayari kuwaambia wengine kuhusu biashara yako, na hivyo ndivyo jina linavyokua.

  1. Faida kwenye biashara ndogo ipo kwenye kununua au kuzalisha.

Biashara nyingi ndogo huwa ni za reja reja au za kuzalisha bidhaa ambazo hazina tofauti kubwa kwa nje. Hivyo bei huwa hazitofautiani sana. Hii hupelekea ushindani kuwa mkali kwenye bei, kila mtu anaweka bei itakayovutia wateja na hilo kusababisha faida kuwa ndogo.

Ili kupata faida nzuri, unahitaji kuangalia kwenye manunuzi, ukiweza kupata unaponunua kwa bei ya chini na kuweza kuuza bei ya kawaida, utaongeza faida. Pia ukiweza kupunguza gharama za kuendesha biashara, bila ya kuathiri huduma na ubora, pia utaongeza faida.

  1. Usishindane kwenye bei, shindana kwenye ubora.

Ushindani kwenye biashara ni mkali, lakini ushindani kwenye biashara ndogo ni mkali zaidi. Hii ni kutokana na uharaka wa kufanya maamuzi wa biashara ndogo. Ni rahisi kuona ukipunguza bei utapata wateja zaidi, lakini ukishafanya hivyo, washindani wako nao wanapunguza, na wanaweza kupunguza chini kuliko wewe. Hapo mnaumia wote na kukosa faida.

Njia sahihi ya kushindana siyo kupunguza bei, bali kuongeza ubora zaidi. Ongeza ubora wa bidhaa au huduma ambazo mteja anapata kutoka kwako. Mpe kitu ambacho hawezi kupata kwa wengine, na hutajali kuhusu bei.

Kama nilivyokuambia rafiki, haya nimekushirikisha ni machache mno ukilinganisha na mengi yaliyopo kwenye kitabu hichi. Wito wangu kwako ni soma kitabu hichi, kisome kila siku kama upo kwenye biashara.

Kama unapata changamoto ya kukosa muda wa kusoma vitabu, nimekuandalia programu maalumu ya kukuwezesha kusoma angalau kitabu kimoja kila mwezi. Kupata maelezo zaidi kuhusu programu hii, nitumie ujumbe kwenye wasap 0717 397 253 wenye maneno PROGRAM YA KUSOMA KITABU KILA MWEZI na nitakutumia maelekezo.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz