Habari za leo rafiki?

Hongera kwa siku hii nyingine nzuri na muhimu sana ya leo. Nafasi ya kipekee kwetu kwenda kupiga hatua zaidi kuelekea kwenye maisha ya ndoto zetu, maisha ya mafanikio. Tutumie nafasi hii vizuri, kwa sababu muda ni mali adimu sana kwa kila mmoja wetu.

Karibu kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto ambazo zinatuzuia kuchukua hatua na kufanikiwa kwenye maisha yetu. Tangu nimeanza kazi hii ya uandishi na ushauri nimejifunza kitu kimoja muhimu sana, ambacho ni hakuna ushauri mdogo.

Yaani hakuna jambo ambalo ni dogo au la kitoto kama wengi wanavyoita. Kuna maswali mtu anaweza kukuuliza au ushauri mtu akakuomba ukaona ina maana kuna mtu hajui hili?

Nilichojifunza ni kwamba vitu ambavyo wewe unaweza kuona ni vya kawaida sana, kwa wengine ni mtihani mkubwa. Kitu ambacho wala hakikufikirishi mwenzako hapati usingizi.

Hii imenifanya kutoa uzito sawa kwa kila shida na kila changamoto ya mtu, hasa pale mtu anapochukua hatua ya kukushirikisha, kwa sababu mpaka anafanya hivyo, jua ameshasumbuka sana.

Kwenye ushauri wa leo, tunakwenda kuangalia kitu ambacho kwa wengi mnaweza kuona ni cha kawaida, lakini ni kizito mno. Na nitakwenda kutoa ushauri ambao utamsaidia kila mtu kwenye biashara.

Twende moja kwa moja kwenye maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili na kisha tuone hatua zipi za kuchukua;

Ni maeneo gani Tanzania unayoweza kuanzisha biashara ya nguo hususa ni mashuka na kupata masoko na faida mapema. – Enock G.

Mwanamafanikio mwenzetu Enock anataka kujua ni maeneo gani Tanzania anaweza kuanzisha biashara ya nguo na kupata masoko na faida mapema.

Na mimi nakwenda kumjibu moja kwa moja pamoja na kushauri mambo muhimu kwa kila mtu kuzingatia kwenye biashara ya nguo na biashara kwa ujumla.

Jibu la swali kuu ni kwamba, ENEO LOLOTE TANZANIA, ambalo lina watu wanaoishi ni eneo ambalo unaweza kuanzisha biashara ya nguo na mashuka. Kwa sababu mavazi na malazi ni mahitaji ya msingi ya watu, na karibu kila eneo watu wanavaa nguo.

Sehemu ya pili ya wapi ukifanya biashara hii utapata faida mapema ndipo panapohitaji umakini mkubwa. Kwa sababu yapo mambo mengi yanayochangia upatikanaji wa faida kwenye biashara.

mitumba

Hapa nakwenda kukushirikisha njia mbili za kuifikia faida na kuona ipi utaitumia kwa eneo unaloliweza. Katika njia hizi, nitagawa makundi mawili ya vipato pia.

Njia ya kwanza; kuuza kwa bei ndogo kwa watu wengi.

Njia ya kwanza ya kuangalia faida ni kupitia wanunuzi wengi. Hapa unauza bidhaa au huduma ya bei ndogo, ambayo watu wengi wanaweza kuimudu, unatengeneza faida kidogo, lakini kwa kuwa wanunuzi ni wengi, faida hizo ndogo ndogo zinajikusanya na kuwa nyingi.

Hii ni njia utakayoitumia pale unapolenga watu wenye uwezo wa hali ya chini na ambao biashara unayofanya ni kitu ambacho siyo kipaumbele kikubwa kwao.

Kwa hiyo kwenye biashara ya nguo, hapa unaweza kuangalia kuuza nguo za bei ya chini au mitumba, kwa watu wenye uhitaji huo ambao kipato chao ni cha chini, ukawauzia wengi na kuweza kutengeneza faida.

Mbinu hii unaweza kuitumia vijijini hasa kwenye magulio na kwenda na misimu hasa misimu ya mavuno ambapo watu wengi wanakuwa na fedha za kufanya matumizi.

Pia unaweza kuifanya maeneo ya mitaani ambapo unaweza kutembeza nyumba kwa nyumba au kuwa na eneo unalofanyia biashara ambapo unaonekana na kufikiwa na wengi.

SOMA; USHAURI; Mbinu Za Kuendesha Biashara Yenye Mafanikio Na Kuepuka Biashara Kufa.

Njia ya pili; kuuza kwa bei kubwa kwa watu wachache.

Njia ya pili ni kuwalenga wale wenye uwezo mkubwa, wale ambao wanajali ubora na utofauti, ambao wapo tayari kulipa gharama kubwa kupata kile wanachotaka.

Hawa wanakuwa wachache na hivyo unawapa kile ambacho ni bora kabisa, kwa bei ya juu. Unatengeneza faida kubwa kwa wateja wachache na kuweza kuendesha biashara yako.

Unapotumia njia hii, lazima biashara yako uifanye kwa hadhi ya juu, eneo la biashara liwe zuri kiasi kwamba mteja anapofika, kisaikolojia anajiandaa kulipa fedha kubwa. Pia bidhaa na huduma unazotoa lazima ziwe bora sana kuendana na gharama ambazo mteja analipa.

Kwa upande wa nguo, hapa unahitaji kuwa na nguo ambazo ni bora na za utofauti, ambazo mteja hawezi kuzipata kiurahisi kila mahali. Biashara hii inafaa sana maeneo ya mjini na nyakati ambazo ni za sikukuu au matukio maalumu.

Hivyo basi, wapi ufanye biashara ya nguo Tanzania ni popote ambapo unaona watu wanaishi.

Wapi ukifanya utapata faida, basi angalia uwezo wa wale wateja unaowalenga, kama ni watu wa chini na kati, basi wapelekee bidhaa wanayoweza kuimudu, lakini zingatia sana ubora wa bidhaa yako. Siyo kwa sababu wanalipa kidogo basi uwapelekee vitu vibovu au vibaya.

Kama watu unaowalenga wana uwezo wa kulipia kile wanachohitaji, jipange kuwapa kilicho bora na cha tofauti.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kupata Masoko Ya Biashara Yako Kwenye Intaneti Bila Ya Kutumia Gharama Kubwa.

Mengine muhimu sana ya kuzingatia kwenye biashara yoyote ile;

  1. Jali sana ile biashara unayoifanya, ijue vizuri, jua wapi unapata bidhaa zako na unazipata kwa ubora na gharama nzuri.
  2. Wajali sana wateja wa biashara yako, wape huduma bora kabisa, kipaumbele cha kwanza kiwe mteja na siyo wewe.
  3. Wafikie wateja kule walipo, mambo yanabadilika, usisubiri wateja waje kwenye biashara yako, bali nenda kule wataje walipo.
  4. Tumia mitandao ya kijamii kama sehemu ya kutangaza biashara yako na kuwafikia wateja wengi zaidi. Tengeneza mahusiano na wateja wako kupitia mitandao ya kijamii.
  5. Endesha biashara yako vizuri, isimamie vizuri, dhibiti mzunguko wa fedha, kuwa na nidhamu ya fedha, kuwa na mpango wa ukuaji wa biashara ambao unaufanyia kazi.

Zingatia mambo hayo matano kwenye mfumo wowote wa biashara uliochagua, na weka juhudi kuhakikisha mteja anapata kitu kizuri, ili aweze kuwa balozi mzuri wa biashara yako.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog