Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

52dde-9-hard-times

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza sumu hatari inayokumaliza taratibu kisaikolojia. Je unajua ni sumu gani? Karibu tujifunze.

Watu wamekuwa na matatizo mengi ya ndani yanayowasumbua na matokeo yake mpaka yale maumivu ya ndani huwa yanajitokeza nje kama ugonjwa. Watu wanatembea lakini  ndani ya mioyo yao wamebeba mizigo mikubwa isyostahili hata kubebeka katika hali ya kawaida.

Rafiki, watu wamekuwa wanabega mizigo mingi katika maisha yao lakini mzigo mkubwa kuliko wote na wa kujitakia ni kutokubali kujisamehe wewe mwenyewe. Hapa ni pagumu kama mtu anashindwa kujisamehe yeye mwenyewe kwa makosa aliyofanya je ataweza kuwasamehe watu wengine waliomkosea?

SOMA; Huu Ndiyo Wakati Sahihi Wa Kutua Mizigo Tuliyobeba Kwenye Mioyo Yetu.

Kutojisamehe na kujilaumu kwa mambo uliyofanya hapo nyuma ni sumu hatari sana inayokumaliza taratibu. Wako watu ambao wanakusanya matukio mbalimbali aliyofanya au kufanyiwa na kushindwa kuyaachilia nje. Kumbe tunapojisamehe sisi wenyewe  katika maisha yetu tunakuwa tunaondoa sumu ndani ya nafsi zetu wenyewe.

Hakuna mtu ambaye hafanyi makosa ila inabidi ifikie mahali huna budi kuachilia uchungu uliombika ndani ya moyo wako kwa faida yako wewe mwenyewe. Jisamehe wewe mwenyewe ili maisha yako yaende huna haya yakuendelea kujilaumu kwa yale uliyotendewa au ulifanya.

Pale unapokataa kujisamehe unakuwa unaruhusu sumu iendelee kukutafuna katika maisha yako yote hatimaye unakufa kiakili, kimwili na kiroho. Watu wengi wanakusanya matatizo katika maisha yako kwa kuendelea kubaki na maumizo na uchungu ndani yao bila kujisamehe, wengine wanaingia na maumizo yao katika mahusiano hivyo anashindwa kufurahia uhusiano alionao na mtu mwingine kwa sababu ya ile sumu ya kutosamehe wengine na kutojisamehe binafsi.

Hatua ya kuchukua leo, huu ni wakati sasa wa kuachilia vinyongo na maumizo yote uliyonayo ndani yako na kuwa huru. Kutojisamehe ni kujifunga kifungoni na kushindwa kufanya mambo yako mengine, anza sasa leo kujisamehe kwa yale yote uliyotendea na anza kuchukua hatua na siyo kujilaumu tena.

SOMA; Hii Ndio Dayari Unayopaswa Kwenda Kuichoma Moto Leo Katika Maisha Yako.

Kwahiyo,ili tuweze kuwasamehe wengine wale waliotuumiza inabidi kwanza tuanze kujisamehe sisi wenyewe kwa faida zetu ili mambo mengine yaendelee. Kutosamehe ni mzigo mkubwa unaokunyima raha maisha yako yote na duniani tuko kwa muda sasa usipoamua kuishi sasa unasubiri maisha gani mengine hapa duniani? Usikubali kufa huku ukiwa na maumizo mbalimbali ya kutojisamehe wewe mwenyewe.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi kila siku. Asante sana.