Yapo mambo katika maisha yako ambayo ukishindwa kupambana nayo mapema, yanakupa tiketi moja kwa moja ya kuwa maskini hata bila kuuliza. Mojawapo ya jambo hilo ambalo wengi naweza sema wanalo ni uvivu.

Uvivu ni adui mojawapo mkubwa sana wa mafanikio yako. Unapokuwa mvivu kwa namna yoyote ile ni rahisi sana kuanza kutengeneza anguko kubwa la maisha yako pasipo wewe kujua kwamba sasa unatengeneza kushindwa kwa maisha yako.

Watu wengi hujikuta wakiingia katika mtego wa uvivu pasipo kujua. Hujikuta wakianza kutengeneza vitu vidogo vidogo kama kuchelewa kuamka, kutegea kazi fulani au kutokuifanya kwa uhakika, mwisho wa siku uvivu huanza.

mafanikio yanahitaji mudaKwa asili ya binadamu au jinsi mwili ulivyo, huwa una tabia fulani hivi ya uvivu au naweza kusema ‘ka uvivu’ kanaweza kakawepo kwa kila mtu kwa namna fulani. Utakuta mtu anaona ‘aaah kufanya jambo hili mbona ni kazi sana,’wakati ukiangalia jambo hilo linamsaidia hata yeye.

Na tunapozungumzia uvivu upo wa aina mbili, kuna ule uvivu wa kupindukia kabisa ambao mtu hafanyi kazi yoyote yeye ni kulala tu na kuna ule uvivu wa kutegea vitu vidogo vidogo yaani hutaki kujituma sana upo upo tu, lakini ieleweke wote ni uvivu na ni hatari kwako.

Inapofika mahali uvivu ukawa sehemu ya maisha yako bila kujali una uvivu mkubwa au uvivu kidogo basi hapo ndipo unapoanza kutengeneza njia ya kushindwa sana kwenye maisha yako. Siku zote hakuna mshindi katika maisha ambaye ni mvivu.

Kila mtu ambaye unamwona kafanikiwa adui wa kwanza ambaye amefanikiwa kumtupa mbali ni uvivu. Unapoamua kuondoa kila aina ya uvivu ndani mwako si rahisi sana kuweza kujionea huruma kwamba eti mambo hapa nitafanyaje.

Ni lazima utajituma kwa kila namna kutafuta matokeo unayotaka pasipo kujali wengine wanasema nini au matokeo ya upande wa pili yanataka nini kwako. Kikubwa utakachokuwa ukijali ni kuhitaji matokeo na hakutakuwa na sababu nyingine.

Kwa sababu sasa tumeshajua kwamba uvivu ni adui mkubwa wa mafanikio yako, ni kipi kifanyike ili uweze kumshinda adui huyu na wewe uweze kuishi maisha ya uhuru na mafanikio kwa kumfutilia mbali adui huyu?

Amka asubuhi na mapema.

Kuamka asubuhi na mapaema ni dawa mojawapo ya kukusaidia kukutoa kwenye uvivu. Unapoamka asubuhi na mapema tuchukulie kabla  ya saa kumi na moja, kisha ukafanya mazoezi kidogo na kusali, utaiweka akili yako sawa kuondokana na uvivu wowote ule.

Pia kuamka sasubuhi na mapema inakusaidia kupitia siku yako mapema na kujua ni majukumu yako mapema ambayo unatakiwa uyatekeleze kwa siku husika. Hiyo yote kwako itakusaidia pia kuweza kukuondolea uvivu ulionao.

Andika.

Kwa namna yoyote siri nyingine ya kuondoa uvivu ni kuandika. Kila wakati andika malengo na mipango yako ikaonekana, andika makala na andika chochote kila unachokiona kinakusaidia kisha kipitie.

Kupitia kuandika huko, hiyo inakuondolea msongo wa mawazo kwanza kwako. Pia haitoshi kuandika kunakufanya kukupa hamasa ya kuondokana na uvivu kwa sababu kila wakati malengo yako yanakuwa yanaonekana.

Tafuta mazingira mengine ya kukuhamasisha.

Njia nyingine ya kukuondolea uvivu ni kutoka eneo ulipo ambalo umezoea na kwenda eneo lingine mbalo linaweza likakuhamasisha na kukupa nguvu kubwa sana ya kuweza kufanikiwa kwako.

Eneo hilo linaweza likawa ni kujifunza nje ya mji uliopo na hata kwa marafiki wa karibu yako. Kupitia mazingitra mapya kuna nguvu kubwa fulani ambayo itaingia ndani mwako na kuweza kukuhamsisha vya kutosha.

Hivyo ndivyo unavyoweza kumshinda adui huyu mkubwa uvivu na kuwa mshindi katika maisha yako.

Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku kujifunza maisha na mafanikio.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

Ni wako rafiki katika mafanikio,

Imani Ngwangwalu,

Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,

Tovuti; www.amkamtanzania.com

Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

Email; dirayamafanikio@gmail.com