Uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo ni uwekezaji ambao umebadili maisha ya watu wengi duniani, idadi kubwa ya watu waliofanikiwa kuwa huru kiuchumi kwa kiasi kikubwa walitokana na kuwekeza fedha, nguvu na muda wao kwenye rasilimali ardhi na majengo katika kujihakikishia wanakua huru kifedha na kuishi maisha yenye mafanikio. Wengi wao ndiyo wenye nguvu kubwa kwenye uwekezaji wa hisa kwenye kampuni na taasisi mbalimbali zenye majina makubwa na uwezo wa hali ya juu kwenye uzalishaji na utoaji wa huduma kwa watu wengi duniani.

Hayo ni matokeo chanya ya fikra na nidhamu ya uthubutu kuelekea kwenye mafanikio ya uhuru wa kifedha. Malengo na juhudi zao kubwa zilikuwa ni kujihakikishia kuwa na kipato kisichokoma kwenye maisha yao na ndipo walipoamua kuwekeza kwenye rasilimali ardhi na majengo. Ukiwaondoa wabunifu wa teknolojia za habari na mawasiliano ambazo zinaendesha dunia kwa sasa, inasemekana kuwa matajiri wakubwa wa kizazi kijacho watatokana na ugunduzi wa teknolojia ya ujenzi. Utajiri wao utatokana na ubunifu wa teknolojia itakayo rahisisha mfumo mpya wa ujenzi na utakaosaidia watu wote duniani kukidhi mahitaji bora ya makazi kwa gharama nafuu na kwa haraka zaidi.

majengo 40

Gharama kubwa za ujenzi ni tatizo ambalo limesababisha kilio cha watu wengi kwenye dunia hii ambayo watu wake wapo kwenye mahangaiko ya kujikwamua ili waweze kukidhi mahitaji muhimu ya kijamii na kiuchumi. Tatizo kubwa hasa ni kugharimu kwa fedha nyingi kwenye hatua ya ujenzi, hali hii ndiyo imesababisha kuwa na utofauti wa gharama za nyumba za makazi na biashara baina ya sehemu moja na nyingine.  Makala hii itaeleza sababu chache ambazo zinachangia kuwepo kwa utofauti wa gharama za nyumba za kupangisha kwa matumizi ya makazi na biashara.

HALI HALISI YA UCHUMI

Hali halisi ya uchumi wa watu binafsi na taifa huwa ni kigezo kikubwa kinachochangia kupanda na kushuka kwa gharama za kupangisha kwenye nyumba za makazi na biashara. Watu wengi wanapokuwa kwenye hali nzuri kiuchumi husababisha kushamiri kwa shughuli mbalimbali za kibiashara na utoaji huduma mbalimbali kwa jamii husika, hali hii husababisha watu wengi kujimudu kimapato na kuwa na uhitaji mkubwa wa nyumba kwa matumizi mbalimbali. Hali ya biashara na uwekezaji inaposhamiri husababisha kupanda kwa gharama za nyumba endapo uhitaji utakuwa mkubwa tofauti na upatikanaji wa nyumba hizo.  Hali ya uchumi inapokuwa sio nzuri hufifisha shughuli nyingi za kibiashara na uwekezaji na baadhi husababisha kufungwa kabisa, hali hii ndiyo husababisha kushuka au kutoendelea kupanda kwa gharama za kupangisha nyumba kutokana na uhitaji kuwa hafifu tofauti na upatikanaji.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kukamilisha Ujenzi Kwenye Nyakati Ngumu Kiuchumi.

HALI HALISI YA KIWANGO CHA AJIRA

Kiwango halisi cha upatikanaji na uzalishaji wa ajira ni matokeo ya kiwango halisi cha hali ya uchumi inayoendana na matumizi ya rasilimali. Idadi kubwa ya watu wanapokuwa hawana ajira husababisha watu wengi kutokuwa na uwezo wa kujimudu kiuchumi na kuwa tegemezi kwa wale wachache wenye ajira katika kutumia rasilimali ikiwemo kwa baadhi kuendelea kurundikana kwenye nyumba za urithi. Hali hii husababisha watu wengi kuishi kwa hofu na wasiwasi kwa kuhofia maisha yao ya kesho kiuchumi, hatimaye husababisha kushindwa kuweka akiba na kutoweza kufanya uwekezaji wowote, pia hofu hiyo inawazuia watu kuendelea kupanga au kujenga nyumba kutokana na kutokuwa na uhakika wa kipato. Hali hii ndiyo husababisha kutoendelea kupanda au kuendelea kushuka kwa gharama za nyumba kutokana na wengi kushindwa kumudu gharama hizo. Vivyo hivyo idadi kubwa ya watu wanapokuwa na ajira husababisha gharama za nyumba kupanda kutokana na hali kubwa ya uhitaji.

UPATIKANAJI WA HUDUMA ZA JAMII NA MIUNDOMBINU

Nyumba nyingi zilizojengwa kwenye maeneo yenye huduma nyingi na bora za jamii huwa na uhitaji mkubwa wa watu. Maeneo yenye miundombinu bora huwa na mvuto kwa watu wengi tofauti na maeneo mengine yenye miundombinu hafifu. Maeneo yenye barabara nzuri, mifumo ya maji safi na salama, nishati za umeme, mawasiliano, hosipitali, bandari, vituo vikubwa vya usafirishaji, shule, vyuo mbalimbali, viwanda na miundombinu ya michezo na burudani huwa na gharama kubwa kwenye nyumba za kupangisha kutokana na kuwa na mzunguko mkubwa wa watu katika kufanya shughuli zao za kimaendeleo tofauti na maeneo yenye upungufu au ukosefu wa huduma hizo. Huduma hizi mara nyingi hupatikana kwenye miji mikubwa na athari za kushuka kwa gharama za nyumba huwa ni ndogo sana kutokana na uhitaji wake kuwa kwenye kiwango cha juu tofauti na maeneo mengine. Kwenye maeneo haya ni nadra sana kushuka kwa gharama za nyumba, mara nyingi gharama hubaki bila kupanda kwa muda mrefu hadi hali itakapokuwa nzuri na kuanza kupanda tena kulingana na uwezo wa watu kumudu gharama hizo.

USIMAMIZI WA SHERIA NA SERA

Uwepo wa sheria nzuri na sera zenye ubora hazitakuwa na maana yoyote endapo kutakuwa na usimamizi hafifu usiokidhi matakwa halisi ya huduma na uratibu wa nyumba na maendeleo ya makazi. Ni muhimu sana kuwepo kwa sera na sheria nzuri zitakazo wezesha watu wengi kumudu gharama za ujenzi, kwa kiasi kikubwa hali hiyo itasababisha kuongezeka kwa nyumba za makazi na biashara na hatimaye kuleta unafuu wa gharama za kupangisha kwa watu wengine. Pia kuwepo kwa mamlaka zinazoratibu hali ya soko la nyumba ili kuleta hali ya msawazo wa kupanda na kushuka kwa gharama za nyumba. Pia kuwepo kwa sera zinazotekelezeka na rafiki wa maendeleo ya kisasa huweka nguvu kubwa kwa kupeleka maendeleo yenye usawa kila mahali ikiwemo kujenga miundombinu na kupeleka huduma bora za jamii kwenye maeneo yote ili kupunguza ongezeko kubwa la watu kwenye eneo moja tofauti na uwepo wa rasilimali. Hali hii huwa na matokeo hasi ikiwemo kuwa na miji yenye makazi holela ambayo siyo rafiki kwa maisha ya binadamu.

SOMA; Haya Ndiyo Maswali Matano Kwa Mtaalamu Wako Kabla Hujaanza Ujenzi Wa Nyumba Yako.

NGUVU ZA TAASISI ZA FEDHA

Gharama kubwa za ujenzi wa nyumba ndiyo sababu kubwa inayowakwamisha watu wengi kutokuwa na uhakika wa kumiliki nyumba za makazi na biashara. Mara nyingi kuwepo kwa taasisi nyingi za fedha kumekuwa ni kichocheo kikubwa kwa ukuaji wa biashara na uwekezaji kwenye jamii husika. Endapo taasisi hizo zitakuwa rafiki, imara na madhubuti katika kutekeleza azma yake ya kuwa sehemu ya mafanikio ya kiuchumi kwenye jamii husika kutachochea watu wengi kupata mikopo kwa ajili ya kukua kiuchumi ikiwemo kuwa na uwezo wa kupangisha au kujenga nyumba kwa ajili ya makazi na biashara. Mabadiliko yoyote ya mfumo wa uratibu wa taasisi hizo za fedha kwenye utoaji wa mikopo na kiwango cha utozaji wa riba kutasababisha kuchochea au kufifisha kwa biashara na uwekezaji, mabadiliko hayo ndiyo yatakayosababisha kuongezeka au kupungua kwa nyumba za makazi na biashara. Endapo taasisi hizo za fedha zitaweka sera ambazo zitachochea ongezeko kubwa la nyumba kutasababisha kupungua kwa gharama za kupangisha au hata kuuza ama kununua kutokana na kuwepo kwa kiwango cha upatikanaji wa nyumba kinachoendana na uhitaji wa soko.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com