Mafanikio na utajiri ni kitu ambacho kila mtu aliye hai anakipenda. Ndiyo vitu vinatufanya tuchukue hatua mbalimbali ili maisha yetu yaweze kuwa bora sana.

Lakini pamoja na uhitaji huo wa watu, pamoja na juhudi ambazo wengi wanaweka, ni watu wachache sana ambao wanapata mafanikio na utajiri. Wengi wanaishia kuwa na maisha magumu licha ya kukazana sana na kutaka kufanikiwa.

Ukiacha hilo, ipo changamoto nyingine kubwa ya kiimani. Watu wengi wanaamini kwamba ili kuwa na imani nzuri, basi hupaswi kupenda mali na hata kuwa nazo. Hivyo watu ambao wamejitengeneza vizuri kiimani lakini maisha yao kifedha ni magumu sana.

Mwandishi James Arthur anakataa hali hiyo ya kutenga mafanikio ya mali na fedha na imani. Katika kitabu chake hichi cha HARMONIC WEALTH anatuambia kwamba, mafanikio na utajiri wa kweli, ni pale maeneo matano ya maisha yako yanapokwenda sawa.

harmonic wealth

Maeneo hayo matano ni FEDHA, MAHUSIANO, AKILI, MWILI NA ROHO/IMANI. James anasema mafanikio yoyote ambayo hayahusishi maeneo hayo manne hayawezi kuwa mafanikio. Kama una fedha nyingi lakini mahusiano yako ni mabovu, au afya yako ni mbovu, huwezi kufurahia maisha yako. Kadhalika kama una imani inayoweza kuhamisha milima, lakini ukawa huna fedha, imani hiyo haiwezi kuyafanya maisha yako kuwa bora.

Karibu kwenye uchambuzi huu wa kitabu cha HARMONIC WEALTH, James aweze kutushirikisha namna ya kuvuta mafanikio na utajiri kwenye maeneo hayo matano ya maisha yetu.

  1. Sayansi na imani sasa zinakubaliana kwenye utajiri.

Tunaishi kwenye zama bora kabisa ambapo kwa mara ya kwanza sayansi na imani zinakubalia kwenye jambo moja ambalo ni kuvuta maisha ambayo mtu anayataka. Zamani sayansi na imani ni kama zilikuwa zinapingana na kushindana, lakini sasa maeneo ya sayansi yameweza kufikia kile ambacho wanafalsafa na viongozi wa kiimani walisema miaka mingi iliyopita. Kwamba mtu anapata kile ambacho anakivuta kwa mawazo yake.

  1. Ulimwengu wote ni kitu kimoja, ni nguvu, ni mawimbi, ni mwanga.

Kitu kimoja ambacho kimekuwa kinajulikana tangu enzi na enzi ni kwamba, mawazo yetu yanaumba na kujenga. Kile ambacho mtu anafikiri kwa muda mrefu ndiyo kinatokea kwenye maisha yake. Na hii ni kwa sababu ulimwengu na vyote vijazavyo ni kitu kimoja, ni nguvu ya nishati, ambayo ipo katika mfumo wa mwanga na unasafiri kwa mawimbi. Mawazo tuliyonayo ni mawimbi, ambayo yananasa mawimbi mengine yaliyoujaza ulimwengu. Hivyo chochote unachofikiria kwa muda mrefu, kinatokea kwenye maisha yako kwa sababu unanasa yale mawimbi yanayoenda ana unachofikiri.

  1. Mafanikio ya kweli ni maelewano ya nguzo tano za maisha.

Ili kuwa na mafanikio ya kweli kwenye maisha, lazima kuwe na maelewano katika nguzo kuu tano za maisha, ambazo ni fedha, mahusiano, akili, mwili na roho. Maelewano haya yanafanya maisha yaweze kwenda na kwa pamoja ukapiga hatua. Kwa mfano unapokuwa na fedha, huku afya yako ikiwa imara, ni rahisi kujenga mahusiano mazuri na wengine, pia hilo linapelekea kuwa na imani nzuri. Kukosekana kwa nguzo moja katika mafanikio yako, kunaharibu maisha yako yote.

  1. Dunia tayari ina kila kitu, ni wewe kuituma na kuielekeza.

Dunia imekamilika kwa kuwa na kila ambacho kinahitajika kwa maisha ya mafanikio. Kinachotakiwa ili mtu kupata kile anachotaka ni kuiambia dunia anataka nini kupitia mawazo yake, kisha kuweka juhudi katika kupata kile anachotaka. Kama ambavyo tumeona kwamba ulimwengu wote ni kitu kimoja, na kila kitu kipo katika umoja huo. Ni wewe uchague kupokea kile unachotaka kwa kuielekeza dunia unataka nini na kuituma ikuletee kupitia kazi unayofanya.

  1. Tatu mara tatu ya kupata mafanikio ya kweli.

Kuna vitu vitatu ambavyo vinaendesha maisha yetu ya kila siku. Vitu hivi ni fikra, hisia na vitendo. Hivi ni vitu ambavyo vipo na wewe popote ulipo, na vinatokea ndani yako mwenyewe. Ili uweze kufanikiwa, lazima vitu hivi viende pamoja, viwe na maelewano. Fikra zako zinapaswa kuendana na hisia zako na vitendo unavyofanya vitokane na fikra na hisia zako. Iwapo chochote kitakuwa tofauti na vingine, huwezi kufanikiwa, kwa sababu utafikiri au kutenda tofauti na unachotaka.

  1. Huwezi kufikia mlinganyo katika mafanikio.

Moja ya kitu ambacho kimewapoteza wengi kwenye mafanikio ni kutafuta mlinganyo. Watu wengi wamekuwa wakitaka kutoa muda na uzito sawa kwenye kila eneo la maisha yao. Lakini ukweli ni kwamba maisha hayana mlinganyo, nyakati hazifanani. Kuna wakati utahitajika kuweka juhudi eneo moja zaidi ya eneo jingine. Hivyo acha kukimbizana na mlinganyo (balance) badala yake kazana na maelewano (harmony) kwenye nguzo kuu tano za maisha yako.

  1. Siyo kwamba hujakamilika, ni kwamba una nafasi ya kukua zaidi.

Mafundisho na vitabu vingi vya hamasa vimekuwa vinawajenga watu dhana kwamba hawajakamilika kama bado hawajafanikiwa au hawajapiga hatua fulani. Lakini ukweli ni kwamba kila mtu amekamilika, hapo ulipo tayari umekamika. Ambacho kinakosekana kama hujafika unakotaka ni kwamba bado hujachukua hatua kufika unakotaka kufika. Na hata ukishafika bado ipo nafasi ya wewe kukua zaidi. Kwa kujua hili, kunakupa wewe uhuru wa kukua zaidi na zaidi.

  1. Pamoja na kujua misingi hii, mafanikio siyo rahisi.

Moja ya mambo ambayo yamekuwa yanawapotosha watu ni dhana kwamba kwa kuwa mawazo yetu yanavuta kile tunachotaka, basi ukiwaza mambo mazuri wakati wote basi yatajitokeza kwenye maisha yako. Huo ni uongo na wengi wamepotea. Ni kweli kwamba mawazo yako yatavuta chochote unachotaka, lakini ipo gharama ya kulipa. Kwa chochote unachotaka kwenye maisha yako, ipo gharama ya kulipa sawasawa na ukubwa wa unachotaka. Unapotaka makubwa utahitajika kulipa gharama kubwa, utahitajika kuweka kazi kubwa, utahitajika kupitia maumivu makubwa. Usijidanganye kwamba mambo yatakuwa rahisi, lakini unapokuwa na msingi sahihi, juhudi unazoweka zinakulipa baadaye.

  1. Tatizo siyo dunia wala tatizo siyo watu, tatizo ni mawazo watu waliyokubali.

Pamoja na siri za mafanikio kuwa wazi kwa kila mtu, bado watu wengi hawafanikiwi. Ni rahisi kuona labda kutakuwa na tatizo na watu au dunia itakuwa na matatizo. Lakini ukweli ni kwamba, watu siyo wabaya, wala dunia siyo mbaya. Tatizo kubwa lipo kwenye mawazo ambayo watu wameyakubali. Huwa kuna mawazo na dhana ambazo zinakuwa zimebebwa na jamii nzima. Kwa mfano dhana kwamba kuna uhaba wa mafanikio, au huwezi kufanikiwa kama ni mwaminifu, na nyinginezo zimewazuia wengi kufanikiwa kwenye maisha yao.

  1. Kitu kimoja ambacho ni muhimu kuliko vingine.

Hakuna kitu muhimu hapa duniani kama kupanua na kukuza ufahamu wa mtu. Na hii inakuwa muhimu kwa sababu wengi wanafanya maamuzi yao kwa ufahamu duni, ambao wameambukizwa na wengine. Kadiri mtu anavyokuza ufahamu wake ndiyo akili yake inavyoweza kufanya kazi vizuri, ndivyo imani yake inavyokuwa imara na ndivyo anavyoweza kujitengenezea mafanikio makubwa kwenye maisha yake.

  1. Fedha ni muhimu sana, na inaathiri nguzo nyingine za maisha ya mafanikio.

Fedha ni muhimu, fedha ni muhimu sana kwa maisha ya mafanikio. Huwezi kutenganisha fedha na maisha, hasa kwa zama hizi ambazo kila kitu kinapimwa kwa fedha. Hivyo ule ufahamu kwamba fedha ni mbaya au fedha siyo muhimu, ni moja ya vitu unavyopaswa kuviacha mara moja. Ukikosa fedha afya yako inaweza kuwa matatani, mahusiano yako yanakuwa magumu na hata imani yako itakuwa ya mashaka. Kwa sababu bila fedha mawazo yako hayawezi kutulia, na hata ugomvi na changamoto baina ya watu na hata vikundi, msingi wake unaanzia kwenye fedha.

  1. Kupata fedha zaidi, unahitaji kuwa mkubwa zaidi na siyo bora zaidi.

Mtu ambaye kipato chake ni milioni moja kwa mwezi na mtu ambaye kipato chake ni milioni kumi kwa mwezi, unafikiri nani mwenye matatizo zaidi? Kwa haraka utasema ni mwenye kipato cha milioni moja, kwa sababu ni kidogo ukilinganisha na milioni kumi. Lakini ukweli ni kwamba, ambaye kipato chake ni milioni kumi ana matatizo zaidi ya yule ambaye kipato chake ni milioni moja. Kadiri kipato chako kinavyokuwa kikubwa, ndivyo kazi au biashara unayofanya inavyozidi kuwa ngumu, ndivyo changamoto zinavyokuwa kubwa na pia ndivyo hatari ya kushindwa inavyozidi kuwa kubwa.

Hivyo kama unataka kuongeza kipato chako, anza kuwa mkubwa wewe kwanza, anza kutatua matatizo makubwa, anza kuwa tayari kukutana na changamoto kubwa. Kama haupo tayari kwa hayo, hutaweza kuongeza kipato chako.

Na msisitizo zaidi muhimu ni ukubwa wa wewe kuweza kupambana na changamoto, na siyo ubora wa wewe kupambana na changamoto hizo.

  1. Sayansi ya yanayoonekana na yasiyoonekana.

Kwa miaka mingi sayansi ilikuwa ikiongozwa na sheria za Newton, ambazo ni sheria za vitu vinavyoonekana. Lakini sasa hivi kuna sayansi mpya ya mambo yasiyoonekana, sayansi inayohisisha mawazo yetu na imani zetu. sayansi hii inaitwa QUANTUM PHYSICS. Sayansi hii inaonesha kwamba kila kitu kinatokana na nguvu moja na mawazo yetu ni mawimbi ambayo yanakutana na mawimbi mengine. Hii ndiyo inayopelekea sisi kupata au kukosa kile unachotaka.

  1. Mawimbi ya kujenga na mawimbi ya kubomoa.

Kwa kuwa kila kitu hapa duniani kipo kwenye mawimbi, mawazo tunayotoa nayo yanaenda kwa njia ya mawimbi. Sasa mawimbi mawili yanapokutaka, kulingana na asili ya mawimbi hayo, yanaweza kujenga na kuwa makubwa zaidi au kubomoa na kupotea kabisa.

Mawimbi mawili ambayo ni chanya yakikutana yanajenga na kuwa wimbi kubwa zaidi. Wimbi hasi likikutana na wimbi hasi yanabomoa na matokeo kuwa sifuri.

Sasa hii inaenda hivi, wewe unataka utajiri, lakini mawazo yako yanafikiria umasikini na ulichokosa. Hatua unazochukua zinatengeneza mawimbi chanya, lakini mawazo yako yanatengeneza mawimbi hasi, hilo linapeleka mawimbi hayo yanapokutana kubomoka na ukakosa kabisa. Hakikisha mawimbi yako yote ni chanya, ili yaweze kujijenga na kuleta matokeo bora zaidi.

  1. Mambo matatu yanayotokea kwenye mawazo mapya.

Mambo tunayojifunza kwenye kitabu hichi huenda hujawahi kuyasikia popote, na ni kwa sababu watu wengi hawajaweza kuyasikia kwa sababu wengi hawayaelewi.

Katika historia ya dunia, wazo lolote jipya linapokuja, linaloenda kinyume na utaratibu uliozoeleka,  huwa linakutana na mambo haya matatu;

Kwanza linadhihakiwa na kuonekana ni kitu cha ajabu, kitu kisichowezekana au kisichofaa.

Pili linapingwa kwa nguvu kubwa sana. Watu wanapinga hata ushahidi ambao upo wazi.

Tatu wazo linakubaliwa na kuwa sehemu ya maisha, na hii huchukua muda, mpaka kile kizazi cha kupinga kiwe kimepita, kizazi kipya kinapokea kama ukweli.

  1. Maisha yanakua, kisichokua kinakufa.

Moja ya makosa ambayo watu wengi wamekuwa wanafanya ni kuridhika haraka na chochote wanachopata. Wengi huanza kwa juhudi kubwa kutafuta kile wanachotaka, wakishakipata wanaridhika na kuacha kuweka juhudi. Siri moja ya maisha na dunia kwa ujumla ni kwamba inakua zaidi, na chochote ambacho hakikui kinakufa, chochote ambacho hakiendi mbele basi kinarudi nyuma. Kwenye dunia hakuna kusimama, ni kwenda mbele au kurudi nyuma, kukua au kufa.

  1. Muda wote unao sasa.

Moja ya changamoto kwa wengi ni muda, na ni kwa sababu tumegawa muda kwenye makundi matatu, muda uliopita, muda uliopo na muda ujao. Hili limekuwa kikwazo kwa wengi. Ili kufanikiwa unapaswa kuelewa kwamba muda wote ulionao ni sasa, muda uliopo. Jana na kesho zote unazo sasa. Hivyo hatua yoyote unayotaka kuchukua, lazima uichukue sasa kama unataka kunufaika nayo.

Sasa hivi hapo ulipo, kuna vitu vingi unavyoweza kuvipa muda wako, na vikaleta matokeo kulingana na kile ulichochagua. Hivyo kama utaheshimu muda ulionao sasa, na kuuweka kwenye yale makubwa unayotaka, hayo ndiyo matokeo utakayopata.

  1. Vikwazo viwili vinavyokuzia kupata unachotaka.

Kwa haya yote unayojifunza, kwamba unaweza kupata chochote unachotaka, mawazo yako yanavuta chochote unachofikiria, unaweza kuhisi ni uongo kwa sababu labda wewe umejaribu lakini hujapata ulichokuwa unataka. Kama hivi ndivyo unavyofikiria, basi kuna vitu viwili vinakuzuia usipate kile unachotaka;

Moja; hujakomaa na kitu hicho kwa muda mrefu kiasi cha kuweza kupata unachotaka, huenda unakata tamaa haraka. Pamoja na kwamba inawezekana, haimaanishi utakipata kwa muda unaotaka wewe, upo muda unaopaswa kuwekeza ili kupata chochote unachotaka, na unaweza kuwa muda mrefu sana.

Mbili; hujiamini kama unaweza kupata unachotaka, na hiyo ikapelekea hata usijaribu kabisa.  Au umechukua hatua lakini umeweka nusu nusu, ukijaribu kama labda itatokea, hujaweka juhudi zako zote ukiamini kweli utapata.

Fanyia kazi mambo hayo mawili na utaweza kupata chochote unachotaka.

  1. Chochote ambacho hujajifunza kulipa gharama yake utakipoteza.

Kama umekuwa unajifunza kuhusu mafanikio kupitia wengine, utakuwa umegundua vitu hivi viwili muhimu;

Moja; watu wanaopata fedha za haraka na kwa mara moja ambazo hawajazifanyia kazi, huzipoteza haraka pia. Watu wanaoshinda bahati nasibu au kurithi mali, hurudi kwenye umasikini wao haraka sana.

Mbili; matajiri ambao wametafuta mali zao wenyewe, kuna kipindi huwa wanafilisika, lakini huwa wanarudi kwenye utajiri wao baada ya muda.

Somo kubwa ni kwamba, dunia huwa inatupa vitu, wakati mwingine kwa juhudi ambazo tumeweka na wakati mwingine kwa bahati tu. Lakini dunia pia huwa inatunyang’anya chochote ambacho hatutajifunza jinsi ya kukipata, hatutajifunza kulipa gharama zake. Jua gharama unayopaswa kulipa kwenye kila kitu na kuwa tayari kuilipa.

  1. Mafanikio ya kifedha yanakuja na matatizo makubwa pia.

Kuna picha moja isiyo sahihi kuhusu mafanikio ya kifedha ambayo jamii inayo. Picha hiyo ni kwamba mtu akishakuwa na fedha nyingi basi yeye hana matatizo tena. Hahitaji kuhangaika tena. Utasikia wengine wakisema mtu ana fedha lakini bado anahangaika, mimi ningelala na kula raha tu.

Fikra za aina hii ndiyo zinawafanya wengi kuendelea kuwa masikini. Mafanikio ya kifedha yanakuja na matatizo na changamoto kubwa. Kadiri unavyokuwa na fedha nyingi, ndivyo fursa za kupoteza fedha hizi zinavyozidi kuwa kubwa. Kuna ambao watajaribu kukuibia au kukutapeli fedha hizo. Kuna ambao watajenga mahusiano na wewe lakini hayatakuwa mahusiano ya kweli bali ya kunufaika na fedha. Hapo bado changamoto za kazi au biashara unayofanya.

Hivyo jiandae, kama milioni moja inakutoa jasho, jua milioni kumi zitakutoa machozi na huenda milioni mia zikakutoa damu.

Kwa kumalizia uchambuzi huu, nitoe angalizo muhimu, kitabu hichi kina maarifa ambayo ni mapya kwa wengi, maarifa ambayo yanaweza kukufanya uone kama imani yako inatikiswa. Lakini ni kitabu ambacho ukikielewa vizuri, basi imani yako itakuwa imara na itakuwa sahihi. Soma kitabu hichi na fanyia kazi yale ambayo umejifunza na kwa hakika utapiga hatua kuwa kwa kua na maisha yenye mafanikio kwenye nguzo zote tano za maisha.

Usomaji

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na kundi la kusoma vitabu, ambapo utaweza kusoma kurasa kumi kila siku na kumaliza kitabu kimoja kila mwezi fungua; www.amkamtanzania.com/kurasa