Heri ya mwaka mpya 2018 kwako rafiki yangu na mwanamafanikio.

Hongera kwa nafasi hii ya kipekee sana ambayo tumeipata, nafasi ya kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye maisha yetu na yale tunayoyafanya ili tuweze kupiga hatua kubwa sana.

Kipindi cha mwanzo wa mwaka kama hichi ndiyo kipindi ambacho wengi hupoteza mwaka mzima kwa sababu ya kufuata mkumbo. Watu wengi huweka malengo ya kufuata mkumbo, ambayo siyo malengo yao na mwishoni wanashindwa kuyaishi.

Kila mwanzo wa mwaka huwa naendesha semina maalumu ya kuufanya mwaka kuwa bora sana kwetu, semina ya kuhakikisha mwaka unakuwa na tofauti kubwa kwetu. Na moja ya maeneo ambayo nimekuwa nahitaji watu wawe makini nayo, ni kwenye uwekaji wa malengo.

mwaka mpya 2018.jpg

Kwa kuwa marafiki zangu wengi hamtapata nafasi ya kushiriki semina ya mwaka huu, kulingana na uhaba wa nafasi za kushiriki, nimeona ni vyema kuwashirikisha yake muhimu sana, ambayo kama mtu atayafanyia kazi, tarehe 31/12/2018 ataangalia nyuma na kusema hakika mwaka 2018 UMENIFUNDISHA VITU VINGI.

Hivyo basi rafiki yangu, kabla hujaendelea kukimbizana na kuweka malengo ya kufuata mkumbo, yasome mambo haya 18 kwa kina, na yafanyie kazi kwenye maisha yako kama yalivyo kwa kipindi hichi cha mwaka 2018 na uone kama maisha yako yatabaki hapo ulipo.

Kabla hatujaingia kwenye mambo haya 18, nikukumbushe kitu kimoja muhimu sana. Maisha ya mafanikio ni mfumo ambao una viungo vingi. Watu wengi wanaposikia mafanikio hukimbilia kufikiria mali na fedha, hiyo ni sehemu ya mafanikio, ila mafanikio ni makubwa zaidi ya fedha na mali.

Kuna maeneo matano muhimu sana ya kufanyia kazi kwenye maisha yako ili uweze kuwa na mafanikio yanayogusa kila eneo la maisha yako. Hivyo mambo haya 18 ya kufanya, yamegawanyika katika makundi hayo matano.

Kundi la kwanza; Maendeleo binafsi.

Wewe kama mtu unahitaji kukua kila siku, kwa sababu chochote ambacho hakikui kinakufa, kwenye ukuaji hakuna kusimama.

Watu wengi wamekuwa hawafanikiwi kwa sababu wamekuwa hawakui, wanakuwa wamefikia hatua fulani na kuona wameshafika kileleni, na hapo ndipo wanapoanza kuanguka.

Katika kuhakikisha unakuwa na maendeleo binafsi na ukuaji kwa mwaka huu 2018 fanya yafuatayo;

  1. Kuwa na maono na ndoto kubwa za maisha yako.

Maisha ni zaidi ya kufanya kazi, kupata fedha, kutumia, zikiisha unakopa, halafu unafanya tena kazi, upate fedha, ulipe madeni na kuendelea. Unahitaji kuwa na kitu kikubwa ambacho kinakupa sababu ya kuamka kila siku. Kitu kinachokusukuma na kukufanya uweke juhudi zaidi, ujifunze zaidi na uache kufanya mambo kwa mazoea.

Kama tayari una maono makubwa jikumbushe maono hayo kila siku, kama bado huna usiendelee na mwaka huu kabla hujatengeneza maono hayo, kwa sababu utakuwa umechagua kupoteza mwaka huu 2018 wewe mwenyewe.

  1. Kuwa na misingi ambayo unaiishi, kuwa na falsafa ya maisha yako.

Kama huwezi kusimama kwa chochote, basi unaweza kuangushwa na chochote. Haya maisha ya sasa yana changamoto nyingi kuliko wakati wowote ule. Kuna fursa za kila aina, nyingine halali nyingine za utapeli. Watu watakuudhi na kukufanyia mambo ambayo hutegemei. Na pia utakutana na vishawishi vingi vya kukata kona na kufanya mambo yasiyo sahihi.

Kama hutakuwa na msingi unaouishi kwenye maisha yako, lazima utaanguka. Na tena hakuna hatari kubwa kama kufanikiwa bila ya misingi, kwa sababu mafanikio yako yatakuwa moto kwako.

Kama huna msingi wa maisha basi nakuazima huu, ishi kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, Hii itakuwezesha kufanya maamuzi bora ya maisha yako.

Pia tafuta falsafa unayoweza kuiishi, falsafa unayoendana na yale unayofikiri ni sahihi kwako. Falsafa zipo nyingi, mimi binafsi nimechagua kuishi falsafa ya Ustoa na imekuwa na mchango mkubwa sana kwenye maisha yangu. Unaweza kujifunza falsafa hii na kuiishi pia, bonyeza maandishi haya kuijua na kuiishi.

  1. Fanya tathmini ya kila siku na kila hatua unayopiga.

Hakuna kinachowapoteza watu kama mazoea, watu huanza kufanya kitu wakiwa na hamasa kubwa, lakini kadiri wanavyoenda wanazoea na kinachofuatia ni kufanya kwa mazoea. Chochote unachofanya kwenye maisha yako, epuka sana mazoea, usikubali kabisa kufanya kitu leo kwa sababu jana ulifanya. Jipe muda wa kufanya tathmini ya yale uliyofanya kwenye siku nzima na weka mpango wa kufanya kwa ubora zaidi siku inayofuata. Hii itakusaidia sana kuwa bora zaidi kadiri siku zinavyokwenda.

Sehemu ya pili; Kazi na biashara.

Lazima uwe na kitu unachofanya ambacho kinakuingizia kipato, iwe ni kazi ya kuajiriwa au kujiajiri, au unafanya biashara, unahitaji njia ya kukuingizia kipato. Katika eneo la kazi na biashara fanya yafuatayo;

  1. Toa thamani zaidi kwenye kile unachofanya.

Mwaka huu 2018 angalia namna ya kuongeza thamani zaidi kwenye kile unachofanya. Angalia matatizo au changamoto ambazo watu wanazo na angalia namna gani unaweza kuyatatua kupitia kile unachofanya wewe. Dunia imejaa matatizo, kadiri unavyoyatatua ndivyo unavyofanikiwa zaidi. Mwajiri wako ana matatizo, wateja wako wana matatizo, je ni yapo unaweza kuyatatua kwa ubora zaidi? Yajue kisha yatatue.

  1. Acha alama kwenye kila unachogusa.

Mteja akipata huduma yako, asikusahau kamwe, mwajiri wako akiona kazi yako, asikusahau kamwe. Na kama leo utaacha kufanya biashara yako, au kuacha kazi yako, basi watu wakumbuke ulikuwepo, wakose uwepo wako, waone kwa namna fulani maisha yao yamepungukiwa kwa wewe kutokuwepo. Usifanye chochote kwa kawaida, fanya kwa upekee wa hali ya juu sana.

  1. Nenda hatua ya ziada.

Kuna vitu ambavyo watu wanategemea kutoka kwako, sasa wewe usiwape wanachotegemea, nenda hatua ya ziada, wape zaidi ya wanavyotegemea. Mteja anapolipia bidhaa au huduma yako, mfanye aamini kwamba amekuibia, yaani apate thamani kubwa kuliko fedha aliyotoa. Kadhalika kwenye ajira, mfanye mwajiri wako akutegemee kwenye kile unachofanya, fanya zaidi ya unavyotegemewa. Nenda hatua za ziada kwenye kila unachofanya, na mwaka 2018 utakuwa wa kipekee sana kwako.

Eneo la tatu; Fedha.

Hapa ndipo patamu, na kila mtu anapopanga mipango yake, fedha ndiyo kitu muhimu. Hilo halina ubishi, fedha ni muhimu sana, ukiondoa hewa tunayovuta kila siku, basi fedha ni kitu cha pili kwa umuhimu wake kwenye maisha yetu.

Kwenye eneo la fedha, mwaka huu 2018 fanya yafuatayo;

  1. Jilipe wewe mwenyewe kwanza, angalau sehemu ya kumi ya kipato chako.

Kosa kubwa ambalo watu wengi wamekuwa wanafanya ni hili, wanakazana sana kufanya kazi, wanapata fedha, halafu wanamlipa kila mtu isipokuwa wao. Wanalipa bili mbalimbali kama za maji  na umeme, wananunua vyakula, wananunua mpaka nguo, halafu wanabaki hawana hata senti moja. Huku ni kutengeneza utumwa.

Kwa mwaka 2018, kila fedha utakayoipata, kabla hujafanya matumizi yoyote, tenga sehemu ya fedha hiyo na iweke pembeni. Hii ni sehemu ambayo umejilipa wewe mwenyewe kwanza. Unaweza kuanza na asilimia kumi ya kipato chako, kama huwezi hiyo anza hata na asilimia 5 au hata moja. Muhimu ni usitumie fedha yote unayopata, weka kiasi pembeni, iweke akiba mahali ambapo huwezi kuitumia kwa haraka na baadaye unaiwekeza.

Sehemu ya kipato chako unayojilipa ndiyo mbegu ya kupanga utajiri, hili ni eneo unalopaswa kuwa nalo makini sana kwenye maisha yako.

  1. Kuwa na vyanzo vingi vya kuingiza kipato.

Hakuna utumwa wa kujitengenezea kama kuwa na njia moja tu ya kuingiza kipato. Kama umeajiriwa na mshahara wako ndiyo kipato pekee, upo kwenye mtego mbaya sana. Mwajiri wako anakuwa kama Mungu kwako, akitishia kukufukuza kazi unaona kama maisha yamefika ukingoni, hasa pale mahitaji yako yote ya maisha yanategemea ajira yako.

Tengeneza vyanzo vingi vya kipato. Mwaka huu 2018 ongeza chanzo cha kipato, iwe ni biashara mpya au huduma yoyote unayoweza kutoa, fanya hivyo.

Pia soma kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA, kitakusaidia sana kujua mifereji nane ya kipato unayopaswa kuwa nayo. Kukipata tuwasiliane kwa wasap 0717 396 253.

Kama huwekezi, unajitengenezea umasikini kwenye maisha yako. Iko hivi rafiki yangu, nguvu ulizonazo za kufanya leo, siyo nguvu utakazokuwa nazo miaka 20 mpaka 50 ijayo. Lakini mahitaji yako yanaendelea kukua kadiri unavyokwenda.

Hivyo unahitaji njia ya kuhakikisha kipato chako kinaendelea kuwa kikubwa hata kama hufanyi kazi. Na njia pekee ya kukamilisha hili ni uwekezaji. Mwaka 2018 wekeza, nunu ardhi, fanya kilimo cha muda mrefu, nunua hisa, nunua vipande vya UTT, anzisha biashara, wekeza kwenye majengo, na njia nyingine za uwekezaji zinazopatikana kwenye mazingira yako.

Eneo la nne; Afya.

Afya yako ni muhimu sana kwenye mafanikio yako, bila ya afya, huwezi kuchukua hatua unazopaswa kuchukua ili kufanikiwa. Hivyo weka kipaumbele kikubwa kwenye afya yako.

Na afya imegawanyika kwenye maeneo matatu;

Afya ya mwili.

Katika kuimarisha na kulinda afya yako ya mwili, fanya yafuatayo;

  1. Kula vyakula vyenye afya, hii itakuepusha na maradhi yanayotokana na ulaji uliopitiliza. Kazana kupata na kula vyakula asili, epuka vyakula vinavyoandaliwa kwa haraka kama chipsi. Kula kwa viwango maalumu na mlo uliokamilika.
  2. Fanya mazoezi, zama tunazoishi wengi tunafanya kazi zinazohusisha kukaa kwa muda mrefu, hivyo vyakula tunavyokula vinahifadhiwa kama mafuta na hii inapelekea kuwa na uzito uliozidi. Unahitaji kufanya mazoezi ili kuwa imara na kupunguza uzito.
  3. Pata muda wa kupumzika, hata kama una hamasa kiasi gani ya kufanikiwa, kufanya kazi muda wote bila kupumzika kutakufanya uchoke kabisa na kushindwa kuendelea. Panga ratiba zako vizuri upate muda wa kupumzika, hasa muda wa kutosha wa kulala.

Afya ya akili.

Akili yako ni mtaji muhimu sana kwa mafanikio yako. Kila unachotaka, kitaanzia kwenye akili yako. Hivyo akili yako inapaswa kuwa kwenye hali bora sana wakati wote. Zingatia haya kuiweka akili yako kwenye ubora.

  1. Lisha akili yako chakula safi cha ubongo ambacho ni kujisomea vitabu vizuri. Soma sana, soma angalau kitabu kimoja kila mwezi, na ukiweza kitabu kimoja kila wiki. Ukifika vitabu viwili kwa wiki utakuwa umepiga hatua kubwa zaidi. Muhimu sana, soma angalau kurasa 10 kila siku, na utapiga hatua kubwa. Kama una changamoto ya kushindwa kusoma, karibu kwenye kundi la KUSOMA KURASA KUMI ZA KITABU, niandikie kwenye wasap 0717396253.
  2. Epuka watu na habari hasi, hizi zinachafua akili yako na kuvutia mambo hasi. Epuka sana habari, usianze siku yako kwa magazeti, kuangalia tv au kusikiliza redio. Achana kabisa na habari, hutakosa chochote cha maana. Ondoka kwenye mitandao ya kijamii pia, inakupotezea muda wako mwingi na kukujaza mambo hasi.

Afya ya Roho.

Imani ni sehemu muhimu sana kwenye mafanikio yako. Kama hujiamini wewe mwenyewe na huna imani kwenye yale unayofanya, huwezi kupiga hatua, utaishia kuwa na wasiwasi na kukata tamaa. Kuimarisha afya yako ya kiroho fanya yafuatayo;

  1. Kulingana na imani uliyonayo, pata muda wa kusali kila siku, huu ni muda wa kujumuika na nguvu kubwa kuliko wewe, ambayo inakupa wewe imani ya kuendelea kupiga hatua zaidi.
  2. Tahajudi, fanya meditation kila siku, pata dakika chache za kutuliza akili yako na kuweza kuishi kwenye wakati uliopo. Tumekuwa tunajitesa kwa mambo ambayo yapo nje ya uwezo wetu, mambo yaliyopita na ambayo hata hayajatufikia. Kwa kufanya tahajudi, tunajikumbusha kuishi sasa, kuishi pale tulipo na kuona umuhimu wa wakati tulionao sasa.

Eneo la tano; Mahusiano.

Wewe siyo kisiwa, hakuna unachoweza kufanya wewe peke yako. Unahitaji msaada wa watu wengine ili kufanikiwa. Na chochote unachotaka, kinatoka kwa wengine. Hivyo bila ya mahusiano bora, huwezi kufanikiwa.

Katika kuboresha mahusiano yako, fanya yafuatayo;

  1. Pata muda wa kukaa na wale wa muhimu kwako.

Familia ni watu muhimu sana kwetu, hawa ndiyo watu watakaoendelea kuwa na sisi hata kama tutashindwa na kufanya mabaya kiasi gani. Lakini wengi tumekuwa tunasahau familia na kuzipa kipaumbele cha mwisho. Mwaka 2018 weka kipaumbele cha kwanza kwenye familia. Pata muda wa kuwa na watu hawa wa karibu kwako, saidianeni kutatua changamoto mbalimbali ambazo kila mtu anapitia. Kadiri mahusiano yanavyokuwa mazuri, ndivyo akili yako inavyoweza kutulia na kuweka juhudi kwenye kazi zako nyingine.

Marafiki na jamaa ni watu muhimu sana pia, hawa ni watu ambao wanaendelea kukuthamini na kukupa moyo hata pale unapopitia magumu. Tenga muda wa kuimarisha mahusiano haya ya kirafiki na kindugu, ili kuweza kupiga hatua zaidi.

  1. Kuwa mtu wa shukrani.

Hakuna kitu rahisi kama kulalamika na kulaumu wengine kwa lolote linaotokea kwenye maisha ya mtu. Lakini kulalamika na kulaumu hakubadili chochote zaidi tu ya kuhamishia majukumu kwa mtu mwingine.

Mwaka 2018 kuwa mtu wa shukrani, shukuru kwa kila jambo na mshukuru kila mtu kwa namna wanavyokusaidia hata kama ni kwa mambo madogo. Nakuambua watu watakuwa tayari kukusaidia zaidi, shukrani inakaribisha tabia bora zaidi.

Hayo ndiyo mambo 18 ambayo nakushauri wewe rafiki yangu uyafanye kwa mwaka huu 2018 ili uwe bora sana kwako. Fanya kila jambo kama nilivyoelekeza hapa, usitake kubadili kwanza, anza kufanya halafu utaendelea kuboresha kadiri unavyoanza.

Kwa wale watakaopata nafasi ya kushiriki semina yetu ya kuanza mwaka huu 2018 tutakwenda kuongeza mengine muhimu zaidi ambayo tutayaishi kwa pamoja mwaka huu 2018 kupitia KISIMA CHA MAARIFA. Mpaka sasa nafasi zimejaa, lakini zinaweza kupatikana chache, hivyo kama utahitaji kupata nafasi pale inapotokea, nitumie ujumbe kwa wasap 0717396253. Karibu sana.

 

Rafiki yangu, nipo kwa ajili yako, na mwaka 2018 nimejipanga kukuandalia maarifa bora kabisa ya kukuwezesha kupiga hatua. Ninachokuambua ni tuendelee kuwa pamoja kupitia www.amkamtanzania.com na www.kisimachamaarifa.co.tz

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog