Unapokwenda kununua kitu sehemu kuna jinsi unataka kuhudumiwa wewe, vile unavyotaka ,sasa ikitokea umehudumiwa tofauti au kuna kitu ulikuwa unakitegemea utakipata na ukakikosa basi utaona kwako imekuwa ni kama kero. Kila mtu kuna kitu anakipenda na anatamani akienda ahudumiwe vile anavyotaka yeye.

Katika kanuni ya dhahabu inasema mtendee mwingine kama unavyopenda kutendewa wewe. Sasa ukichukulia kanuni hii katika kumhudumia mteja wako  ni kama vile unavaa viatu vyake. Yaani wewe ndiyo unavaa uhusika wa mteja wako sasa unavuta picha wewe ndiyo mteja halafu unahudumiwa je ile huduma wewe unaridhika nayo? Kama huridhi nayo kwanini sasa unamhudumia mwingine?

Michango

Kitu ambacho wewe hupendi kufanyiwa na unaona ni kero kwako basi usimfanyie mteja wako, hakuna mtu ambaye anapenda kutoa hela yake halafu hapati ile hadhi ya kuthaminiwa. Usijali tu fedha ya mteja wako jali je mteja anaridhika na kile unachompa?  Kuna sehemu nyingine ukienda kupatiwa huduma unasema huendi tena kwa sababu ni kama vile wewe ndiyo unajipendekeza badala wewe mteja upewe thamani lakini mhudumu anakuona huna thamani.

Kila mtu anapenda kuthaminiwa hivyo usipopata kile unachokitaka katika sehemu uliyoenda kupata huduma kamwe huwezi kurudi tena. Badala ya kutumia kanuni hii tu ya dhahabu ya kumtendea mwingine kama unavyotaka kutendewa wewe sasa kwa mteja inaweza kuwa tofauti kwani tumetofautiana kihisia hivyo kuna kitu ambacho mimi napenda na wewe hukipendi. Kwa mfano, mtoa huduma yeye hapendi kusikiliza lakini mteja wewe unapenda kusikilizwa.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Psychology Of Selling (Jinsi Ya Kuuza Zaidi, Kwa Urahisi Na Haraka Kuliko Unavyodhani.)

Kwa mfano, wewe ni mtoa huduma ya kinyozi na mteja amekuja anataka umnyoe nywele. Anakupa maelekezo naomba uninyoe staili hii lakini wewe unamkatalia mteja unamwambia nyoa staili hii hapa hiyo ni mbaya hapo moja kwa moja utakua umemkwaza mteja kwa sababu yeye kila siku ananyoa vile anavyotaka yeye halafu wewe leo unakuja kumwambia nyoa vile lazima utamkwaza kitu unachopenda wewe siyo wote wanakipenda hivyo ni vizuri kumsikiliza mteja kile anachokitaka yeye na siyo kile unachokitaka wewe.

Hatua ya kuchukua leo, tumia kanuni ya almasi katika kumhudumia mteja wako ambayo inasema hivi mtendee mwingine kile ambacho anapenda kutendewa yeye. Kwahiyo, kama mteja wako anapenda kitu fulani basi mtimizie kadiri anavyopenda yeye. Kila mtu ana kitu chake anachokipenda ndiyo maana kanuni hii inaenda mbali zaidi kwa sababu mteja anataka kile anachotaka yeye hivyo ili kuteka au kuendana na saikolojia yake basi msikilize na mtendee vile ambavyo anataka kutendewa yeye.

SOMA; Usikubali Mtu Yeyote Akushinde Kwenye Maeneo Haya Kumi(10) Muhimu Kwa Mafanikio Ya Maisha Yako.

Kwahiyo, unatakiwa kuheshimu hisia za mteja wako, usiangalie tu fedha bali jali kutoa huduma ambayo mtu ataridhika na atabaki salama akiwa anaona kweli hela yake imeenda kihalali na siyo vinginevyo. Usipendelee mtu anaondoka kwako huku akinung’unika na kulalamika huku akiona kama vile hela yake imeenda na maji. Watu wanapata shida kupata fedha hivyo hakikisha unamtendea mteja vile anavyotaka yeye. Mteja haitaji sababu bali anahitaji kupata kile anachotaka yeye ndiyo maana ukaambiwa mteja ni mfalme.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net au  unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku  ambayo ni www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana !