Karibu rafiki kwenye makala ya ushauri wa changamoto, sehemu ambayo tunakutana kwa ajili ya kupeana ushauri kwa zile changamoto ambazo zinatuzuia kufanikiwa.

Changamoto ni sehemu ya maisha na changamoto ndiyo zinafanya maisha yetu yawe na maana. Bila ya changamoto maisha yanakuwa ya ajabu na yasiyo na msukumo wa kuchukua hatua. Hivyo unapokutana na changamoto furahi kwa sababu zinakusukuma na hata kukuwezesha kukua zaidi.

Kwenye makala yetu ya leo tunakwenda kushauriana juu ya hatua za kuchukua pale kila biashara unayotaka kufanya unaona imeshafanywa na watu wengine. Hili ni tatizo kwa wengi, umepita eneo fulani, ukaona fursa fulani ya biashara ambayo haipo, ukasema utaifuatilia hiyo, unaanza mipango, mara siku unapita pale unakuta mtu mwingine ameshaanza biashara kama uliyokuwa unafikiria. Hujawahi kuwa kwenye hali hiyo?

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Sasa kabla hatujaangalia ni hatua zipi za kuchukua, tupate maoni ya msomaji mwenzetu ambaye ameomba ushauri kwenye hili;

Mimi changamoto inayonizuia ni kwamba nikitaka kuanzisha kitu na nikaona mwingine tayari amesha kaanzisha huwa naogopa kwamba nitamuharibia au namuonea huruma kwamba nitakuwa nimemuingilia biashara yake nifanye kuondokana na fikra hizo? – Isacka A.

Kama umewahi kujikuta kwenye hali ya kutaka kuanzisha biashara mahali, halafu ukakuta mwingine ameshaanzisha na kuacha kuanzisha, una tatizo kama alilo nalo mwenzetu.

Na kama umewahi kuona kama utaendelea kufanya utaonekana umeiga au unamharibia mwenzako, basi una tatizo kubwa zaidi.

Iko hivi rafiki, hakuna mtu ambaye anaweza kufanya kitu cha peke yake hapa duniani. Chochote unachotaka kufanya, ni labda utaona wengine wanakifanya na wewe ukapenda kukifanya, au utakigundua, lakini wengine wakikuona unafanya, basi na wao watafanya, kitu ambacho huwezi kuwazuia.

Linapokuja swala la biashara, unapoiona fursa mahali, jua kabisa kwamba fursa hiyo huioni wewe peke yako. Kila mtu anayepita au kuishi eneo hilo anaiona fursa hiyo. Hivyo kinachowatofautisha watu siyo ujanja wa kuziona fursa, bali uharaka wa kuchukua hatua. Wale ambao wakiona fursa wanachukua hatua wanaonekana kuwa wajanja kwenye fursa. Lakini wale ambao ni wazito kuchukua hatua, wanaosubiri mpaka wawe tayari, siku zote wanachelewa na kuishia kushindwa kuanza hasa wengine wanapoanza.

Hivyo basi rafiki, nataka niongee mambo matatu hapa, ambayo yatakusaidia sana kwenye kuanza biashara hasa unapokuta wengine wameshaanza.

Moja; kuwa mtu wa kuchukua hatua mapema, usisubiri mpaka uwe tayari.

Ukishaiona fursa mahali, na ukajishawishi kabisa kwamba ile ni fursa ambayo unaweza kuifanyia kazi na inaendana na zile ndoto ulizonazo kwenye maisha yako, basi unapaswa kuchukua hatua mara moja. Usisubiri mpaka uwe tayari, usisubiri mpaka sijui upate nini. Anza mara moja na anzia pale ulipo sasa. Anza hata kama ni kwa hatua ndogo, hili litakuweka mbele na pia utaona njia bora zaidi za kuitumia fursa hiyo.

SOMA; USHAURI; Njia Tano Za Kupata Mtaji Wa Biashara Bila Ya Kuchukua Mkopo.

Mbili; acha uvivu.

Kitu kingine ambacho nakiona kwa watu ni uvivu na uzembe wa kutokuwa tayari kuingia kwenye biashara. Mtu unaiona fursa ya kibiashara, ambayo unaona kabisa ni fursa nzuri, lakini una uzembe hivyo huanzi, unajipa sababu hujawa tayari au unasubiri. Sasa wakati unasubiri, huku ukiwa hufanyi chochote, anatokea mtu na kuitumia fursa ile. Moyoni unajishukuru kwa uvivu na uzembe wako, kwa sababu hata hivyo siyo kosa lako, wewe ulikuwa unajipanga na kaja mtu kutumia fursa yako.

Ukishaona unaacha kufanyia kazi fursa fulani kwa sababu wengine wameichukua, jua wewe ni mvivu na mzembe lakini hutaki kukubali hilo. Ulichokuwa unafanya ni kutafuta sababu ya kuficha uvivu na uzembe huo, usionekane wewe ndiyo huchukui hatua, bali ionekane kwamba wengine wamekuwahi kuchukua hatua.

Tatu; biashara ni kama bahari, kila mtu anaogelea eneo lake.

upo usemi kwamba huwezi kuichunga bahari, wewe ukikazana kuwazuia watu wasiogelee ufukwe mmoja, kuna wengine wanaendelea kuogelea kwenye fukwe nyingine. Kadhalika ndivyo biashara zilivyo, hakuna mtu mmoja anayeweza kuwazuia wengine wasifanye biashara kwa sababu yeye anaifanya. Hasa kwa zama za sasa, ambazo ushindani umekuwa mkali na wateja wana nguvu kubwa ya kuchagua.

Hivyo kama ulikuwa na wazo la biashara, na ghafla ukaona mtu kaanzisha biashara ya aina hiyo, hilo lisikutishe. Chunguza ukubwa wa soko, angalia yeye anatoa nini na ona kipi ambacho unaweza kufanya kwa ubora kuliko wengine wanaofanya biashara kama yako. Mnaweza kuiona fursa moja wote, lakini kila mtu akawa na mpango tofauti wa kibiashara wa kutumia fursa hiyo.

Hivyo kama unajiamini una kitu unaweza kutoa kwa ajili ya wengine, na kama upo tayari kuweka juhudi kuhakikisha watu wanapata thamani, basi wewe ingia kwenye biashara, hata kama wengine wameshaingia. Halafu weka juhudi kuzalisha thamani kubwa, kutatua matatizo ya wateja wako na kwa hakika utapata wateja.

Kingine pia unaweza kuangalia upande mwingine wa fursa hiyo hiyo ambao bado haujafanyiwa kazi. Hakuna biashara moja unayoweza kufanya kila kitu vizuri, hivyo ukiwa mdadisi na mchunguzi, utaona maeneo ya fursa hiyo ambayo bado hayajafanyiwa kazi na unaanza kuchukua hatua mara moja.

SOMA; USHAURI; Hatua Tano(5) Za Kuanzisha Na Kukuza Biashara Kwa Wale Ambao Hawana Pa Kuanzia Kabisa.

Nimalize kwa kusema kwamba, kama unaacha kuanza biashara kwa sababu unawaonea huruma wale ambao wameshaanza biashara hiyo na kuona kama unawaingilia, kwa sehemu kubwa hujawa tayari kwa ajili ya kufanya biashara, ila tu unatafuta visingizio. Kama upo tayari kufanya biashara, ingia kwenye biashara, zalisha thamani na tatua matatizo ya watu, soko litaamua nani alipwe na nani asilipwe. Na soko huwa halina huruma, wateja hawaangalii nani alianza na nani amekuja baadaye, wanachoangalia nani anawapa thamani, na wanafanya biashara na huyo.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog