Rafiki yangu na mshirika katika safari ya maisha ya mafanikio,

Hongera sana kwa kuanza mwezi mpya, mwezi wa nne. Hongera zaidi kwa kumaliza robo ya kwanza ya mwaka 2018, zimebaki robo tatu mwaka huu uishe, hivyo kwa yale unayofanyia kazi mwaka huu, unahitaji kuwa umeshapiga hatua kiasi fulani. Na kama kuna ambayo hujaanza kabisa, ni vyema ukaanza sasa kwa sababu uwezekano mkubwa ni kwamba kadiri muda unakwenda, hutayaanza, halafu utakuja kujidanganya kwamba mwaka huu haiwezekani hivyo utafanya mwaka kesho.

Leo chukua muda wa kupitia yale yote uliyopanga kufanya au kufikia mwaka 2018, angalia kwenye kila jambo umefika wapi na kwa yale ambayo hujaanza kabisa, anza sasa.

Karibu kwenye TANO ZA JUMA, ambapo leo tunamaliza juma namba 13 la mwaka huu 2018.

Kila mwisho wa juma nimekuwa nakushirikisha mambo matano muhimu niliyokutana nayo, niliyojifunza na hata huduma mbalimbali ninazotoa ili wewe rafiki yangu upate maarifa sahihi ya kufanya maamuzi sahihi.

Karibu tujifunze kupitia yale matano ya juma hili la 13 tunalomaliza.

#1 KITABU NILICHOSOMA; SAA YA KUISHI NA SAA YA KUPENDA.

Kuna swali moja muhimu sana ambalo unapaswa kujiuliza kila mara, kama ungeambiwa una saa moja tu ya kuishi, saa moja tu na unaruhusiwa kupiga simu kwa mtu mmoja pekee, ungempigia nani simu? Fikiria hapo, dakika zinapungua kutoka 60, 59, 58… je nani ambaye ungempigia simu? Ukishapata jibu la swali hilo, swali linalofuatia sasa ni hili, unasubiri nini sasa hivi usimpigie simu mtu huyo na kumweleza kile ambacho ungemweleza kama ingekuwa saa yako ya mwisho hapa duniani?

Wote tunajua kabisa ya kwamba siku moja tutakufa, na kwa hakika wengi wetu hatutajua ni siku gani au saa ngapi na katika hali gani. Hivyo kama kuna kitu ambacho ni muhimu kufanya, kwa nini hatukifanyi sasa, wakati tukiwa na nafasi ya kufanya hivyo?

Mwandishi Richard Carlson na mke wake Kristine Carlson kwenye kitabu chao cha AN HOUR TO LIVE, AN HOUR TO LOVE, wanatuonesha umuhimu wa kutumia muda wetu kwa wale ambao ni wa muhimu kwetu. Kupitia kitabu hichi ambacho ni hadithi ya kweli ya maisha yao, wanatushirikisha jinsi nguvu ya upendo inavyoweza kujenga mahusiano bora, na hata kuwapa faraja familia pale mwanafamilia anapofariki. Wakijua ya kwamba kimwili hawapo pamoja, lakini kiroho, kupitia upendo wapo pamoja.

Sasa nataka mimi na wewe rafiki yangu tutumie dhana hii ya saa moja ya kuishi kwenye kila tunachofanya.

Unajua kila mtu utamsikia akisema hana muda, yupo bize na kadhalika. Lakini utakuta watu wanaangalia TV, wanasoma magazeti, wapo kwenye mitandao ya kijamii, wanalala mpaka usingizi uishe wenyewe na kadhalika.

Kwenye kitu chochote ambacho unakifanya, wakati unaanza jiulize je kama hii ingekuwa saa yangu ya mwisho kuishi hapa duniani, ningefanya kitu hichi? Kama jibu ni ndiyo basi fanya, kama jibu ni hapana basi acha usifanye.

Nakuambia rafiki yangu jaribu hilo, na utajikuta una muda mwingi wa kufanya yale muhimu kuliko unavyoweza kuutumia. Kwa sababu kuhalisia muda ni mwingi mno kama utaacha kufanya yale yasiyo muhimu.

hour to live

#2 MAKALA YA WIKI; NJIA KUMI ZA KUFANYA MAISHA YAWE RAHISI.

Maisha ni magumu, hilo halina ubishi, hata wale wanaosemaga kwamba fedha hainunui furaha, wanakuwa wamedanganywa kwamba ukiwa na fedha basi maisha yanakuwa rahisi. Wasijue kwamba kuna matatizo ya kutokuwa na fedha, halafu kuna matatizo ya kuwa na fedha. Na haya ni matatizo tofauti kabisa. Hivyo kama hukuwa na fedha na ukawa na matatizo, ukizipata siyo kwamba matatizo yataisha, bali yataondoka na kuja matatizo ya fedha.

Sasa watu tumekuwa tunayafanya maisha yawe magumu kuliko yanavyopaswa kuwa, kwa kutokujua baadhi ya misingi muhimu ya maisha. Kwenye makala ya wiki hii, nimeshirikisha misingi kumi ambayo ukiishi, utaacha kuyafanya maisha yako kuwa magumu kuliko yanavyopaswa kuwa. Kama hukusoma makala ya wiki hii, isome hapa; Njia Kumi (10) Za Kuyafanya Maisha Yako Kuwa Rahisi Bila Ya Kuyarahisisha. (https://amkamtanzania.com/2018/03/30/njia-kumi-10-za-kuyafanya-maisha-yako-kuwa-rahisi-bila-ya-kuyarahisisha/)

#3 NILICHOJIFUNZA WIKI HII; KAMA UNAZIJUA SIKU ZA WIKI, HUFANYI KAZI VYA KUTOSHA.

Wiki hii nilikuwa nasoma makala za waandishi mbalimbali, nikakutana na makala ya mwandishi mmoja ambaye alikuwa anaeleza ni kwa namna gani watu huwa wanasema hawana muda na wakati huo huo wanachezea muda.

Anasema unakuta mtu anasema, leo ni jumatatu, jumatatu husa siyo siku nzuri, au leo ni jumatano, tunakaribia wikiendi. Na balaa zaidi ni inapofika ijumaa, basi watu wanakuwa na furaha ya ajabu na kutumia neno TGIF (Thank God It’s Friday).

Mwandishi anasema kama unazijua siku za wiki, kwamba leo ni jumatatu na siyo siku nzuri, au ijumaa ni siku nzuri, jumamosi na jumapili ni siku za kupumzika, basi jua hufanyi kazi vya kutosha.

Nimekubaliana kabisa na mwandishi kwenye hili kwa sababu nimetafakari na kuona kuna tofauti gani kati ya jumatatu na ijumaa, hakuna, masaa ni yale yale, jua ni lile lile linachomoza na kuzama kama siku nyingine.

Sasa inakuwaje iwe vigumu kwako kuamka jumatatu wakati ijumaa unakuwa na hamasa kubwa? Hapo ndipo utajua kwamba umetengenezwa hivyo makusudi ili usifanikiwe, ili uendelee kutumika na wengine.

Kama unataka kujitumia mwenyewe, lazima uwe moto kila siku, wakati watu wanasema leo ni jumatatu au leo ni ijumaa, wewe sema leo ni siku ambayo nakwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa. Hili litakuwezesha kujituma hata pale unapoona mambo ni magumu.

Usihesabu siku na kuzipa majina, bali ishi kila siku kwa ukamilifu wake, kwa kujitoa hasa ili kupata kile unachotaka.

# 4 HUDUMA NINAZOTOA; KAMA HAUPO KWENYE KISIMA UNAKOSA…

Zipo sababu nyingi sana kwa nini kila anayefuatilia mafunzo ninayotoa anapaswa kuwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, katika makala hizi za TANO ZA JUMA, nitakuwa nakupa vile unavyokosa kama haupo kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

Kama haupo kwenye KISIMA CHA MAARIFA, unakosa fursa ya kujipima kila mwezi na kujua upo wapi na unaenda wapi.

Ni mwanafalsafa Socrates aliyenukuliwa kusema MAISHA AMBAYO HAYAPIMWI HAYANA MAANA KUISHI. Na hakukosea hata kidogo, angalia watu wengi, tarehe moja ya mwezi wa kwanza kila mwaka hushangilia mwaka mpya mambo mapya, wanajipangia mambo mengi, lakini baada ya hapo wanasahau kabisa, mpaka tena mwaka mwingine unapoanza wanarudia zoezi hilo. Siyo mimi nasema, bali tafiti zinaonesha mtu mmoja hurudia kujiwekea malengo yale yale kwa miaka kumi bila ya kuyafanyia kazi.

Je unataka hilo lisitokee kwako? Karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA, kwani kwa kuwa kwenye KISIMA, kila mwezi unapata maswali ya kupima unafanya nini, na unaelekea wapi kwenye malengo unayojiwekea. Maswali unayopata, ambayo unapaswa kuyajibu, yanakufanya uyatafakari maisha yako kwa kina na kuweza kuchukua hatua.

Kama bado hujawa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, unasubiri nini, lipa sasa ada ya mwaka ambayo ni TSH 50,000/= kwa MPESA 0755 953 887 AU TIGO PESA 0717 396 253 Kisha tuma majina yako na email kwa wasap namba 0717396253 na utaunganishwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

Usikose nafasi hii ya kipekee ya kuweza kuyapima maisha yako na kujua unaelekea wapi. Badala ya kusubiri ufanye hivyo mara moja kila mwaka, sasa utakuwa unafanya kila mwezi, na ikiwezekana kila wiki.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KIPAJI HAKINA THAMANI YOYOTE.

Talent is cheaper than table salt. What separates the talented individual from the successful one is a lot of hard work.  – Stephen King

Hivi unajua ya kwamba kila mtu ana kipaji fulani? Lakini huwa hatuoni watu wengi wakionesha vipaji vyao. Unajua kwa nini? Kwa sababu watu huwa wanajidanganya ukishakuwa na kipaji basi inatosha. Sasa Stephen King anatuambia kipaji ni rahisi kuliko chumvi ya mezani. Hivi unajua chumvi ni rahisi kiasi gani? Nenda nyuma yoyote na omba chumvi utapewa bila hata ya kuulizwa unataka kiasi gani, tena utapewa kopo na kuambiwa jipimie. Lakini omba sukari na watu wataanza kukuuliza maswali.

Thamani ya kipaji itaonekana pale ambapo kazi, nirudie KAZA, KAZI HASA inapowekwa. Hivyo usijidanganye kwamba una kipaji hivyo unaweza tu kufanikiwa kwa kipaji chako, unahitaji kazi, kazi ya maana. Kazi hasa. Hivyo jua kipaji chako na fanya kazi sana, na mafanikio hayataweza kujificha kwako.

Ni hayo matano kwa leo rafiki yangu, jifunze na chukua hatua.

Kabla hujaianza wiki ya 14 nikukumbushe kwamba pangilia wiki hiyo leo hii, jua yapi unakwenda kukamilisha, vitabu gani unakwenda kusomana hatua zipi unakwenda kuzifikia.

Una siku saba mbele yako, masaa 168 na dakika 10,080, tafadhali sana, isipotee hata dakika moja kwenye dakika hizo elfu kumi na themanini.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog