Hongera sana rafiki yangu, juma namba 19 la mwaka huu 2018 linamalizika.

Imani yangu ni kwamba limekuwa juma bora kabisa kwako, juma la kujifunza na kukufanya kuwa bora zaidi kwa mwaka huu 2018 na miaka mingi ijayo.

Naamini yapo mengi uliyojifunza kwenye juma hili, ambapo kwa kuyazingatia, utaweza kupiga hatua zaidi. Na hili ndiyo lengo kuu la maisha, kama wanavyosema wastoa, lengo la maisha ni kujifunza jinsi ya kuishi. Yaani unavyoishi kila siku, ndiyo unajifunza jinsi ya kuishi.

Karibu sasa kwenye tano za juma hili la 19, ambapo nakushirikisha mambo matano niliyojifunza kwenye juma hili, ambayo kwa kuyafanyia kazi utaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako pia.

#1 KITABU NILICHOSOMA; SHERIA 12 ZA MAISHA, MBADALA WA VURUGU NA MACHAFUKO.

Maisha ni mfululizo wa mipangilio inayoenda sawa na isiyoenda sawa, yaani vurugu na machafuko. Pale unapopanga kitu na kikaenda kama ulivyopanga, mambo yanakuwa mazuri. Lakini kitu kinavyokwenda tofauti na ulivyopanga, hapo ni vurugu, ni machafuko.

Mwanasaikolojia Dr Jordan Peterson anatushirikisha sheria 12 za maisha, ambazo tukiziishi siyo kwamba tutaondokana na hali ya vurugu kabisa, ila tunapunguza hali hizo za vurugu na pia kupunguza vurugu kwenye maisha yetu.

Matatizo mengi tunayokutana nayo kwenye maisha, ni sisi wenyewe tunayasababisha, kwa uzembe au kutokujua, au kupuuza baadhi ya misingi ambayo ipo wazi kabisa.

Hapa nakushirikisha sheria 12 ambazo Dk Jordan anatupa kwenye kitabu chake cha 12 RULES FOR LIFE, kwa uchambuzi wa kina zaidi utausoma kwenye makala ya uchambuzi nitakayoweka kwenye AMKA MTANZANIA.

SHERIA YA KWANZA; SIMAMA WIMA, MABEGA NYUMA.

Jinsi unavyouweka mwili wako, kuna maana kubwa sana kisaikolojia na hata wengine wanavyokuchukulia. Unaposimama wima ni dalili ya kujiamini na kuwa na nguvu, ukiinama ni ishara ya kutokujiamini. Kusimama wima pia ina maana ya kuchukua majukumu ya maisha yako.

SHERIA YA PILI; JICHUKULIE KAMA MTU AMBAYE UNA WAJIBU WA KUMSAIDIA.

Watu wengi hujitoa sana pale wanapowasaidia wengine, lakini inapokuja kwao binafsi, wanapuuza. Mifugo yako ikiumwa haraka utaitafutia matibabu na kuhakikisha inapata matibabu, lakini wewe ukiumwa huhangaiki sana, na hata ukipewa dawa hutumii kwa umakini kama unavyoelekezwa.

SHERIA YA TATU; TENGENEZA URAFIKI NA WALE WANAOTAKA UWE BORA ZAIDI.

Watu unaojihusisha nao, wana mchango mkubwa sana wa wapi unafika. Kama unajihusisha na watu waliokata tamaa na maisha yao, hutaweza kupiga hatua kwenye maisha yako.

SHERIA YA NNE; JILINGANISHE NA ULIVYOKUWA JANA, NA SIYO NA JINSI MWINGINE ALIVYO LEO.

Haijalishi unafanya nini kwenye maisha, kuna mtu ambaye ni bora kuliko wewe, ukikazana ukawa na baiskeli, kuna wenye pikipiki, ukiwa na pikipiki kuna wenye magari, ukiwa na gari kuna wenye ndege. Hivyo kujilinganisha na wengine ni kujiumiza, jilinganishe na ulivyokuwa jana, kama leo uko bora kuliko ulivyokuwa jana basi unapiga hatua, haijalishi wengine wapoje.

SHERIA YA TANO; USIWARUHUSU WATOTO WAKO WAFANYE KITU AMBACHO KITAKUFANYA UWACHUKIE.

Watoto wa zama hizi wanakua hovyo bila ya malezi bora, wazazi wanaogopa kuwaadhibu watoto kwa kuhofia kuchukiwa na watoto hao. Lakini kitu chema ambacho mzazi anaweza kufanya kwa mtoto ni kutoa adhabu sahihi kwa makosa ambayo mtoto amefanya. Na kama mzazi hatafanya hivyo, kwa kufikiri anampenda mtoto wake, anamwandaa kuja kuadhibiwa na dunia, na dunia haina huruma, inaadhibu kikatili sana.

SHERIA YA SITA; WEKA NYUMBA YAKO SAWA KABLA HUJAKOSOA DUNIA.

Kila mtu anaweza kukosoa, kila mtu anaweza kutoa maoni yake namna gani mambo yanaweza kwenda vizuri zaidi, lakini kila mtu kuna kitu ambacho hafanyi kwa usahihi kwenye maisha yako. Kabla hujapoteza muda wako kuhukumu au kukosoa wengine, hebu kwanza angalia maisha yako kama kila kitu unafanya kwa usahihi. Kama siyo, tumia muda huo kurekebisha maisha yako badala ya kukosoa wengine.

SHERIA YA SABA; FANYA KILE CHENYE MAANA KWAKO, NA SIYO KILICHO RAHISI.

Kuna njia rahisi ya kupata chochote ambacho unataka kwenye maisha, lakini njia rahisi siku zote huwa zinakuja na madhara yake baadaye. Hivyo kwa chochote unachotaka kwenye maisha, tumia njia sahihi na fanya kitu chenye maana kwako, siyo kwa sababu kila mtu anafanya.

SHERIA YA NANE; SEMA UKWELI, AU ANGALAU USIDANGANYE.

Watu hupenda kutumia uongo kuwahadaa wengine ili kupata chochote wanachotaka. Imefika hatua watu mpaka wanajihadaa wenyewe. Njia bora ya kuishi maisha ni kuwa mkweli, au kutokudanganya wengine au kujidanganya mwenyewe.

SHERIA YA TISA; CHUKULIA KWAMBA MTU UNAYEMSIKILIZA KUNA KITU ANACHOJUA WEWE HUJUI.

Kusikiliza ni kazi ngumu, inahitaji kuwa mtulivu, kuacha vitu vingine vyovyote, kitu ambacho wengi hawawezi. Njia bora ya kuwa msikilizaji ni kuchukulia kwamba kila unayemsikiliza kuna kitu muhimu anajua ambacho wewe hujui. Na ukweli ni kwamba, kuna cha kujifunza kwa kila mtu.

SHERIA YA KUMI; KUWA MAKINI KWENYE KAULI ZAKO.

Sema kile unachotaka kusema, sema kwa njia ambayo unaeleweka. Usitoe maelezo ambayo hayaeleweki au yanapingana. Ukiwa makini kwenye kauli zako, utajiepusha na matatizo mengi.

SHERIA YA KUMI NA MOJA; USIWASUMBUE WATOTO WAKIWA WANACHEZA MICHEZO INAYOONEKANA NI HATARI.

Zama hizi, watoto wamekuwa wanalindwa sana, michezo mingi imekuwa inazuiwa kwa sababu ya hatari zake. Lakini licha ya kuondoa hatari hizo, bado watoto wamekuwa wakitafuta njia hatari za kucheza. Ili kuwakuza watoto ambao wanajiamini na kuyaelewa maisha, wanahitaji kujihusisha na mambo hatari, hayo yatawafundisha sana.

SHERIA YA KUMI NA MBILI; MBEMBELEZE PAKA UKIKUTANA NAYE.

Kuna vitu vidogo vidogo kwenye maisha ambavyo huwa hatuvipi mkazo, lakini kwa kuvifanya vinakuwa na maana kubwa sana kwetu. Angalia ni vitu gani vidogo vidogo umekuwa unavichukulia poa na anza kuvifanya kwa umakini.

Hizo ndiyo sheria 12 za maisha, ambazo ukizifuata kwa kina, utajiepusha na matatizo mengi kwenye maisha yako.

Pata kitabu hichi na kisome, zijue sheria hizi, kwenye kitabu Dk Jordan ametoa mifano na hadithi nyingi sana kufafanua sheria hizi. Ni kitabu ambacho kila aliye makini na maisha anapaswa kukisoma.

#2 MAKALA YA WIKI; HATUA YA KWANZA YA KUELEKEA KWENYE UTAJIRI.

Watu wanapenda utajiri, wanapenda fedha, ila hawana kanuni sahihi ya kuelekea kwenye utajiri wanaotaka. Watu wanakazana na mambo ambayo kwa nje yanaonekana kuleta utajiri, lakini msingi mkuu wa utajiri hawaujui. Kinachotokea wanapata fedha kidogo, halafu fedha hizo zinakuwa kikwazo kikubwa kwao kuendelea zaidi.

Kwenye makala ya wiki hii nilieleza hatua ya kwanza na muhimu sana ya kuelekea kwenye utajiri. Kama hukusoma makala na kuelewa hatua hiyo, unaweza kuisoma hapa; Hatua Ya Kwanza Muhimu Sana Ya Kuelekea Kwenye Utajiri, Ambayo Wengi Wanaipuuza Na Inawagharimu Sana.

(https://amkamtanzania.com/2018/05/11/hatua-ya-kwanza-muhimu-sana-ya-kuelekea-kwenye-utajiri-ambayo-wengi-wanaipuuza-na-inawagharimu-sana/)

#3 TUONGEE PESA; MAMBO MAWILI MUHIMU KUHUSU FEDHA.

Grant Cardone, mwandishi wa kitabu cha 10X RULE ni mmoja wa watu ambao huwa najifunza mengi sana kutoka kwake kuhusu fedha. Kwenye moja ya mafunzo yake Grant anasimulia hadithi ya utotoni. Anasema fedha ya kwanza kupata akiwa na miaka nane, ni baba yake alimka sarafu ya dola senti 25. Grant anasema alifurahia sana hela ile, alienda kwenye maduka akiwa anaruka ruka na kuangalia hela yake, anaiweka mfukoni na kuitoa, anasema hakuwahi kuwa na raha kama siku ile. Sasa akiwa eneo la maduka, akaenda chooni akiwa na hela yake, sasa wakati anaiangalia angalia, mara ikaangukia kwenye tundu la choo. Anasema furaha yake ilikatika ghafla, akarudi nyumbani akiwa amenyong’onyea, huku matumaini yake ya kununua vitu alivyopenda yakiwa wamekufa.

Alipomwelezea baba yake kilichotokea, baba yake alimwambia kitu kimoja; USICHEZE NA HELA. Akiwa bado anafikiria kile alichoambiwa na baba yake, babu yake alimwita na alipomweleza kilichotokea, babu alimwambia, USIENDE MAHALI UKIWA NA SENTI 25 TU.

Grant anasema haya ni masomo mawili makuu kuhusu fedha ambayo amekuwa akiyaishi maisha yake yote, na yamemletea mafanikio makubwa kifedha.

Hivyo tuzingatie haya mawili;

USICHEZE NA HELA, kuwa makini  na hela zako, zisimamie vizuri na wekeza sehemu salama unayoweza kuifuatilia kwa umakini.

USIENDE MAHALI NA FEDHA UNAYOTAKA KUTUMIA TU. Kwa kifupi kwenye kaisha usiwe na kiasi cha fedha unachohitaji kwa matumizi tu, unahitaji kuwa na kiasi cha fedha kwa ajili ya dharura. Kila mara yanatokea mambo ambayo hatukutegemea yatokee, kama hujaweka fedha ya dharura, utapata shida na kujikuta unaingia kwenye madeni.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; NINGEPENDA KUKUTANA NA KILA MTU, LAKINI NI VIGUMU.

Kadiri kazi ya uandishi na kufundisha ninayofanya inavyozidi kukua, ndivyo watu wengi zaidi wanapenda kukutana na mimi. Wanapenda tukutane kwa ajili ya ushauri zaidi, wengine wanataka tushirikiane kwenye mambo mbalimbali. Wengine wamekuwa wakiniweka kwenye makundi yao ya wasap lakini nimekuwa naondoka mara moja, bila hata ya kutoa maelezo. Wengine amekuwa wakipiga simu hazipokelewi au kutuma ujumbe lakini wasipate majibu.

Ningependa sana kukutana na kila mtu, kuwasiliana na kila mtu, lakini hilo haliwezekani. Muda ni mchache na majukumu ni mengi. Ndiyo maana nina huduma nzuri sana kwa wale wanaopenda kuwa karibu na mimi kupitia mafunzo ninayotoa. Na huduma hiyo ni KISIMA CHA MAARIFA.

KISIMA CHA MAARIFA kuna kundi maalumu la wasap ambapo kila siku tunakuwa karibu na kujifunza. Na unapokuwa na lolote la kuuliza, unaweza kuuliza moja kwa moja na ukapata majibu na msaada kutoka kwa watu zaidi ya 200 ambao wamejitoa kwa ajili ya kufanikiwa zaidi.

Hivyo kama hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, karibu sana tuwe pamoja. Tuma ujumbe kwa njia ya wasap 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na  nitakutumia maelekezo ya kujiunga.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KITU KIMOJA KITAKACHOKUFANYA USIZUILIKE.

“Believe in yourself and you will be unstoppable.” – Emily Guay

Utakapojaribu kufanya kitu chochote kikubwa kwenye maisha yako, ndiyo utaujua uhalisia wa dunia, kila kitu kitaibuka kukupinga na kukuzuia. Vitaibuka vikwazo ambavyo hata hukuwahi kuvifikiria. Hata ndugu na jamaa wa karibu watakuwa kikwazo kikubwa kwako. Nguvu ya kukupinga itakuwa kubwa kiasi kwamba huwezi kabisa kupiga hatua. Unaweza kuwa unajua hili vizuri kama umeajiriwa na ukawahi kuwaambia watu wa karibu yako kwamba unataka kuacha kazi ujiajiri.

Sasa kipo kitu kimoja ambacho kinaweza kukufanya usizuilike, pamoja na vikwazo na mapingamizi ya wengine, ukaweza kuchukua hatua na ukafanikiwa zaidi baadaye. Kitu hicho NI KUJIAMINI WEWE MWENYEWE. Unapojiamini na ukaamini kwenye kile unachofanya, bila ya kutetereka, hata dunia nzima ikikupinga, utaweza kuishinda.

JIAMINI NA AMINI KWENYE NDOTO YAKO KUBWA NA KILE UNACHOFANYA.

Rafiki yangu, jiandae vyema kwa juma namba 20 tunalokwenda kuanza. Panga yale muhimu ambayo ungependa kuyakamilisha na weka muda na nguvu zako kwenye hayo, na kwa hakika utapiga hatua. Usisahau kuishi SHERIA 12 ZA MAISHA, itakusaidia kupunguza changamoto mbalimbali kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji