Rafiki yangu,

Katika kutimiza umri wa miaka 30 ya maisha yangu hapa duniani, nilipata nafasi ya kuyatafakari maisha kwa kina. Nilipata pia nafasi ya kusoma vitabu vitano muhimu sana, ambavyo vimeniwezesha kuwa na mtazamo tofauti kabisa kuhusu dunia na maisha kwa ujumla.

Vitabu vitano nilivyosoma katika kuelekea kutimiza miaka 30 ya maisha yangu ni hivi vifuatavyo;

Moja; FACTFULNESS.

Hichi ni kitabu ambacho kinaelezea mambo kumi ya ukweli kuhusu dunia, ambayo huwezi kuyajua kama kila wakati unafuatilia habari na mitandao ya kijamii. Haya ni mambo kumi ya jinsi dunia inavyopiga hatua na maisha kuwa bora, lakini hakuna anayeyapa kipaumbele.

Pia kwenye kitabu hichi nilijifunza jambo moja kubwa sana kuhusu utajiri na umasikini. Siyo kweli kwamba dunia imegawanyika kwenye makundi mawili ya nchi tajiri na nchi masikini, bali kwenye kila nchi kuna ngazi nne za kipato ambazo zinafanana kwa kila nchi. Nimekichambua kitabu hichi vizuri sana, unaweza kusoma uchambuzi wake kwa kubonyeza maneno haya.

Mbili; SKIN IN THE GAME.

Kama hasara haikuumizi basi hupaswi kunufaika na faida, huu ndiyo msingi mkuu wa kitabu SKIN IN THE GAME. Hichi ni kitabu ambacho nimejifunza jinsi ambavyo dunia imekosa usawa, jinsi ambavyo baadhi ya watu na taasisi zimeitengenezea mfumo wa kutokuumia, kwamba faida ikipatikana basi wao wananufaika, lakini hasara ikipatikana haiwagusi.

Kitabu hichi kimechambua mambo mengi sana kuhusu maisha na jinsi hali ya kukosa usawa inawaumiza wengi na kuwanufaisha wachache. Uchambuzi wa kitabu hichi unaweza kuusoma kwa kubonyeza hapa.

Tatu; PERENNIAL SELLER.

Wapo watu ambao wanatoa kazi zao na zinadumu kwa muda mfupi baada ya hapo zinapotea kabisa. Lakini wapo ambao wanatoa kazi zao na zinadumu vizazi kwa vizazi. Kitabu PERENNIAL SELLER kimeeleza kwa kina ni jinsi gani mtu unaweza kuandaa na kutoa kazi ambayo itadumu kwa muda mrefu. Uwe ni mwandishi, mwanamuziki au hata mjasiriamali, unahitaji kuona matunda ya juhudi zako, hivyo kutoa kazi inayodumu kuna manufaa kwako.

Unaweza kusoma uchambuzi wa kitabu hichi kwa kubonyeza hapa.

Nne; OWN THE DAY, OWN YOUR LIFE.

Ili ufanikiwe, lazima uweze kuyamiliki maisha yako, na ili uyamiliki maisha yako, unahitaji kitu kimoja muhimu, kuimiliki kila siku unayoiishi. Watu wengi hatumiliki siku zetu, badala yake siku zinatumiliki. Tunaanza siku kama kuku aliyekatwa kichwa, tunahangaika na kila kinachopita mbele yetu, habari, mitandao ya kijamii na mengine. Tunakula vyakula bila ya kufikiri kwa kina madhara yake kwenye afya yetu na siku yetu inaisha bila ya kuona kikubwa tulichofanya.

Kuimiliki siku yako unahitaji kuanza siku kwa mipango yako, kula kwa umakini ukijua unakula nini na matokeo yake ni yapi, unahitaji kufanya kazi kwa kujituma na kupenda unachofanya. Unahitaji kufanya mazoezi, pia kufanya mapenzi bora na kulala vizuri.

Nimechambua vizuri kitabu hichi hapa.

Tano; 12 RULES FOR LIFE.

Sheria, kila dini ina sheria zake, kila nchi ina sheria zake, kila taasisi ina sheria zake na kila familia ina sheria zake. Lakini sisi binadamu hatupendi sheria, tunapenda kuendesha maisha yetu vile tunavyotaka sisi wenyewe, na asiwepo wa kutupangia nini tunaweza kufanya au hatuwezi kufanya.

Lakini kama nchi au taasisi zingeendeshwa kwa namna hiyo, kwa kila mtu kufanya anachotaka kufanya, zisingeweza kupiga hatua. Hivyo kuna sheria za kuwaongoza watu kwenye nini cha kufanya au kutokufanya.

Kutokana na umuhimu huu wa sheria, kila mmoja wetu anahitaji kujitengenezea sheria ambazo atazifuata kwenye maisha yake. Sheria ambazo zitayafanya maisha yake kuwa na msimamo, kuepuka na kutatua changamoto na kumzuia mtu kuingia kwenye matatizo yanayokwepeka.

Kitabu hichi kimeeleza kwa kina sana sheria kumi na mbili unazoweza kuishi nazo kwenye maisha yako na ukaweza kuwa na maisha yenye utulivu na mafanikio. Kusoma uchambuzi wa kitabu hichi, bonyeza maandishi haya.

Nimekupa muhtasari huo muhimu wa vitabu vitano nilivyosoma siku za karibuni, na ningependa sana kila mtu asome vitabu hivyo, maana vitakupa mtazamo wa tofauti kabisa kuhusu maisha.

golden_rules1

 

MAMBO 40 KUELEKEA MIAKA 40 YA MAISHA YANGU.

Katika kutimiza miaka 30 ya maisha yangu, nimekushirikisha makala ya NAJIWASHA MOTO, ambapo nimekugusia miaka kumi inayofuata ya maisha yangu, kutoka miaka 30 mpaka miaka 40 kuna mambo makubwa sana ambayo nakwenda kufanya.

Katika kujiandaa na miaka hii kumi, nilitafakari na kujifunza mengi sana. katika kujifunza, nilikutana na mambo 40 kutoka kwa mwandishi wa kitabu cha 12 RULES FOR LIFE.

Kwa ufupi, kabla mwandishi hajaandika kitabu hicho, kulikuwa na swali kwenye mtandao wa QUORA, huu ni mtandao wa maswali na majibu, ambapo mtu yeyote anaweza kuuliza swali lolote, na watu wakajibu kulingana na uzoefu au uelewa wao.

Swali liliuliza kuhusu mambo muhimu mtu kufanya kwenye maisha na mwandishi Jordan Peterson ambaye ni mwanasaikolojia aliandika mambo 40 muhimu ya mtu kufanya kwenye maisha yake. Jibu lake liliwavutia watu wengi, ambao walilipigia kura na kufanya kuwa jibu bora kabisa. Ni kuanzia hapo ndipo wazo la kitabu cha 12 RULES FOR LIFE lilizaliwa.

Nimeyapitia mambo hayo 40 mara kwa mara, nimeona mengi katika hayo ni mambo mazuri sana kufanya na kuzingatia kwenye maisha. Nakushirikisha mambo haya hapa, ili nawe ujifunze na kuweza kuyafanya maisha yako kuwa bora. Mimi binafsi nitakwenda kuyazingatia sana mambo haya 40 kwenye miaka 10 inayofuata ya maisha yangu.

Yafuatayo ni mambo 40 muhimu kuzingatia kwenye maisha kama alivyotushirikisha Jordan Peterson;

  1. Sema ukweli.

Nafikiri hili halina haja ya maelezo marefu, sema ukweli mara zote, usidanganye hata kama ni kitu kidogo kiasi gani, sema kweli na kweli itakuweka huru. Ukweli ni rahisi kukumbuka na ukweli utakuweka sehemu salama mara zote.

  1. Usifanye kitu unachokichukia.

Fanya unachopenda, penda unachofanya, huu ndiyo msingi wa maisha bora na ya mafanikio. Kama kuna kitu hutaki au hupendi kufanya usifanye, muda wako ni mchache na wa thamani, usiupoteze kwa yasiyo muhimu.

  1. Fanya kwa namna ambavyo utaweza kueleza ukweli wa ulichofanya.

Iko wazi hii pia, fanya kitu ambacho unaweza kukielezea kwa wengine, kama huwezi kuelezea kwa ukweli, usifanye.

  1. Fanya kile ambacho ni muhimu kwako, na siyo ambacho ni rahisi.

Kila mtu anataka kukata kona, kila mtu anatafuta njia ya mkato ya mafanikio, kila mtu anatafuta njia ya kupata fedha bila ya kufanya kazi. Usiwe katika watu hawa, fanya kile ambacho ni muhimu kwako, na siyo kutafuta kilicho rahisi. Kwa sababu mwisho wa siku maisha siyo fedha tu, unaweza kuzipata na bado ukaona maisha hayafai.

  1. Kama unahitaji kuchagua, kuwa mtu anayefanya mambo, na siyo mtu anayeonekana kufanya mambo.

Kila mtu anapenda kuonekana ni mfanyaji, lakini wengi ni wasemaji na walalamikaji, kuwa mfanyaji, acha wengine wawe watu wa maigizo, wewe fanya.

  1. Kuwa makini.

Chochote unachofanya, akili yako yote na mawazo yako yote yawe pale, kuna mengi utayaona kwa kuwa makini kuliko kukosa umakini.

  1. Chukulia kwamba mtu unayemsikiliza kuna kitu anachojua ambacho wewe hujui.

Ukweli ni kwamba kila mtu kuna kitu anajua ambacho wewe hujui, hivyo unapofanya mazungumzo na yeyote, sikiliza kwa makini sana. Mtu yeyote atakuambia chochote unachotaka kujua, kama utasikiliza kwa makini.

  1. Kuwa makini na watu unaowashirikisha habari zako nzuri.

Wengi unaofikiri wanakupenda na kukujali, wanaweza kugeuka watu wabaya sana pale wanaposikia habari zako nzuri.

  1. Weka juhudi kuimarisha mahaba kwenye mahusiano yako.

Mahusiano ni kazi na kila kazi inahitaji juhudi. Kuweza kuwa na mahusiano bora na mwezi wako, unahitaji kuweka juhudi katika kujenga mahusiano hayo.

  1. Kuwa makini na unaowashirikisha habari zako mbaya.

Wapo watakaoonekana kusikitika lakini moyoni wanafurahia unapokuwa kwenye matatizo, kuwa makini na unaowashirikisha habari zako mbaya.

  1. Fanya angalau kitu kimoja kuwa bora kila mahali unapoenda.

Usiende sehemu yoyote halafu ukaondoka hujabadili kitu chochote kikawa bora, itakuwa haina maana yoyote ya wewe kuwepo eneo hilo. Angalia kipi unaweza kuboresha zaidi popote ulipo, kisha boresha.

  1. Tengeneza taswira ya unataka kuwa nani, kisha weka juhudi kufikia taswira hiyo.

Watu wengi hawajui nini wanataka kwenye maisha yao hivyo wanajiendea tu. Usiwe wewe, jua unataka kuwa nani, unataka kufikia wapi, kisha kila siku weka juhudi kufika pale unapotaka kufika.

  1. Usijiruhusu kuwa na kiburi au hasira.

Hizi ni hisia mbili ambazo zitakuharibia sifa yako, kuvuruga mahusiano yako na wengine na kukuingiza kwenye matatizo makubwa, usikubali hisia hizo zikutawale.

  1. Jaribu kufanya chumba kimoja kwenye nyuma yako kuwa kizuri iwezekanavyo.

Kwenye nyumba unayoishi, kazana kufanya chumba kimoja kuwa kizuri sana kiasi kwamba kila wakati utapenda kuwa kwenye chumba hicho, kisha kifanye kuwa eneo lako la kupumzika au kutafakari maisha yako.

  1. Jilinganishe na ulivyokuwa jana, na siyo kujilinganisha na wengine walivyo leo.

Kosa kubwa unaloweza kufanya kwenye maisha yako, ni kujilinganisha na mtu mwingine yeyote, awe yupo juu yako, chini yako au sawa na wewe. Mtu pekee wa kujilinganisha naye ni wewe mwenyewe, kama leo umefanya kwa ubora kuliko jana unapiga hatua, kama umefanya kama jana unarudi nyuma, kama umefanya chini ya ulivyofanya jana hujui unachofanya.

  1. Weka juhudi kubwa uwezavyo kwenye angalau eneo moja kisha angalia nini kitatokea.

Kwenye maisha yako, chagua eneo moja ambalo utaweka juhudi kubwa sana, utakwenda hatua ya ziada, utafanya kila kinachopaswa kufanyika, kisha angalia matokeo utakayopata, yatakuwa matokeo bora, makubwa na ambayo yatakupa hamasa ya kuendelea na juhudi zaidi kwenye maeneo mengine ya maisha yako.

  1. Kama kumbukumbu za nyuma zinakufanya ulie, ziandike kwenye karatasi kwa umakini na ukamilifu.

Kumbukumbu tunazobeba, zinaweza kuwa mzigo mzito kwetu na unaoturudisha nyuma, tunahitaji kuutua. Kitendo cha kuandika kitu, unakuwa umekitua kutoka kwenye akili yako na kinaacha kuwa mzigo.

  1. Imarisha muungano wako na watu.

Unahitaji kuwa na mtandao wa watu ambao wanaweza kukusaidia kwenye maeneo mbalimbali na wewe pia unaweza kuwasaidia. Imarisha muungano na mahusiano yako na wengine.

  1. Usikebehi taasisi za kijamii.

Hata kama hukubaliani na mtu au watu, usiwakebehi, kuwadharau au kuwakosoa kwa namna ya kudhalilisha. Hii inakwenda kuanzia kwenye taasisi mbalimbali kama za kidini na hata kwa watu binafsi.

  1. Jichukulie kama mtu ambaye una jukumu la kumsaidia.

Tunapopewa kazi ya kuwasaidia wengine, tunafanya kazi nzuri sana, lakini kwetu sisi wenyewe hatufanyi kazi nzuri. Jichukulie wewe kama mtu uliyepewa jukumu la kumsaidia kisha msaidie hasa.

  1. Waombe watu wakusaidie kitu kidogo ili nao wakuombe uwasaidie kitu.

Maisha ni mahusiano, kadiri mahusiano yako na wengine yanavyouwa bora, ndivyo maisha yako yanavyokuwa bora. Na mahusiano yanaimarishwa kwa namna watu mnashirikiana na kusaidiana, waombe watu wakusaidie kitu, ili nao wawe tayari kukuomba uwasaidie kitu.

  1. Tengeneza urafiki na watu wanaotaka ufanikiwe.

Wale wanaokuzunguka wanaweza kuwa kikwazo kikubwa sana kwa mafanikio yako. Kama umezungukwa na watu waliokata tamaa, na wewe utakata tamaa.

  1. Usijaribu kumwokoa mtu ambaye hataki kuokolewa, na kuwa makini unapomwokoa mtu ambaye anataka kuokolewa.

Kuna sababu kwa nini mtu ameingia kwenye matatizo ambayo unamwona anapitia. Ukikazana kumwokoa mtu ambaye yupo kwenye matatizo, bila ya kujua sababu iliyomwingiza kwenye matatizo hayo, unajiingiza mwenyewe kwenye matatizo.

  1. Hakuna kitu kilichofanywa vizuri ambacho hakina maana.

Kitu chochote ambacho kimefanywa vizuri, hata kama ni kidogo kiasi gani, kina maana kubwa sana. Fanya kila kitu vizuri, hata kama ni kidogo.

  1. Iweke nyumba yako vizuri kabla hujakosoa dunia.

Kukosoa ni rahisi, lakini kuchukua hatua ni kugumu. Tunaishi kwenye dunia ambayo kila mtu anaweza kukosoa wengine, lakini yeye mwenyewe maisha yake yanamshinda. Nyoosha kwanza maisha yako kabla hujajipa jukumu la kuinyoosha dunia.

  1. Vaa kama mtu unayetaka kuwa.

Ukishajua unataka kuwa nani, angalia jinsi watu hao wanavaa kisha vaa hivyo pia. Hata kama hujafikia ngazi hiyo, wewe vaa kama watu hao, na hilo litawafanya watu wakuchukulie kama mmoja wao na kukusogeza karibu na mafanikio yako.

  1. Kuwa sahihi kwenye maongezi yako.

Sema kile unachotaka kusema kwa usahihi na kueleweka, bila ya kuficha kitu au kuona aibu.

  1. Simama wima, mabega nyuma.

Jinsi unavyouweka mwili wako, inaeleza wewe ni mtu wa aina gani. Ukisimama wima na mabega nyuma, unaiambia dunia kwamba wewe ni mtu unayejiamini na makini.

  1. Usiepuke kitu cha kutisha kinachokuzuia na usifanye mambo hatari yasiyo na umuhimu.

Kitu chochote kinachosimama kwenye njia yako ya mafanikio, na kukuzuia wewe kufika kule unakotaka kufika, unapaswa kukiondoa. Lakini pia kuwa makini usijiingize kwenye mambo hatari, ambayo hayana maana kwako.

  1. Usiwaruhusu watoto wako wafanye kitu kitakachokufanya uwachukie.

Kama una watoto, basi jua una jukumu la kuwalea vizuri kwenye msingi wa maadili, na hilo litahuisha kuwaadhibu pale wanapokosea.

  1. Usimgeuze mke wako kuwa kijakazi wako.

Watu wengi huishia kuwafanya wake zao kama wasaidizi wao wa kazi za nyumbani, hilo linapelekea mahusiano hayo kuwa na changamoto kubwa. Mke wako anapaswa kupata nafasi yake sahihi ya mke, ambayo ni mshauri na mshirika kwa kila unachofanya.

  1. Usifiche vitu ambavyo havihitajiki kwenye ukungu.

Kuna vitu ambavyo vinatokea kwenye maisha yako, ambavyo huvitaki, lakini badala ya kuvikabili, unavificha kwenye ukungu, na kujifanya kama havijatokea. Kadiri unavyoficha vitu hivyo vinakuwa na baadaye vinaleta madhara makubwa. Kama kitu kisicho sahihi kimetokea, kinapaswa kusahihishwa na siyo kufichwa.

  1. Fursa hujificha pale majukumu yanapokimbiwa.

Kama hujakubali majukumu yako na kujiandaa vyema kuyakabili, huwezi kukutana na fursa.

  1. Soma kitu kilichoandikwa na mtu mkuu.

Chagua waandishi au watu ambao unawakubali sana, kisha soma kazi zao.

  1. Mbembeleze paka unapokutana naye.

Maisha ni magumu, lakini kuna vitu vidogo vidogo kwenye maisha yetu ambavyo vina maana kubwa. Usikubali ugumu wa maisha ukuondolee manufaa ya vitu hivi muhimu.

  1. Usiwasumbue watoto wanapofanya vitu vinavyoweza kuonekana ni hatari.

Kama jamii tunawalinda sana watoto na kuwaondolea kila aina ya hatari, lakini hilo haliwasaidii katika kuwa watu bora. Watoto wanahitaji kujiweka kwenye mazingira ambayo ni hatari kwa kiasi, ili wanapokosea wajifunze kwa maumivu watakayopata.

  1. Usikubali anayekuonea aendelee na uonevu wake.

Usikubali kuwa mtu wa kuonewa na watu kuchukulia ni kitu cha kawaida, simamia utu wako na yeyote anayekuonea mfanye ajifunze kwamba uonevu siyo kitu sahihi.

  1. Andika barua kwa serikali kama unaona kitu ambacho kinapaswa kurekebishwa, na pendekeza suluhisho.

Hii ni bora kuliko kukaa na kulalamika kuhusu serikali inafanya au haijafanya nini. Andika barua kueleza kile ambacho siyo sahihi na pendekeza suluhisho, na hata kama barua yako haitafanyiwa kazi, basi mawazo yako ya kuisaidia serikali yatasikika na wengi.

  1. Kumbuka kile ambacho hujui ni muhimu kuliko ambacho tayari unajua.

Hivyo kila siku jifunze, kuna vitu vingi huvijui, na vinakuwa kikwazo kwako kufanikiwa zaidi.

  1. Kuwa bora licha ya mateso yako.

Maisha ni mateso, huu ni msingi wa dini na falsafa zote. Usisubiri mpaka mateso na changamoto zako ziishe ndiyo uwe mtu bora, havitaisha, kama huteseki wewe basi ni mtu wako wa karibu. Hivyo chagua kuwa bora kila siku, hata kama unapitia magumu kiasi gani.

Hayo ndiyo mambo 40 muhimu niliyojifunza kutoka kwa Jordan Peterson ambayo nitakwenda kuyaishi kwa miaka 10 ijayo. Nimekushirikisha wewe rafiki yangu ili uyaishi pia, kwa sababu yatafanya maisha yako kuwa bora na uweze kufika kule unakotaka kufika.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji