Rafiki yangu,

Leo napenda kusema na wale ambao wanapitia magumu kwenye maisha yao.

Wale ambao wamefikia hatua ya kujiuliza kama kweli wanajua wanachotaka na maisha yao.

Wale ambao mbele wanaona giza, wasijue kama wataweza kuvuka giza hilo na kubaki salama.

Hawa ndiyo watu ninaowataka hapa, na kama wewe siyo mmoja wao ila unapenda kuendelea kusoma soma, lakini mwishoni fikiria watu unaowajua wanaopitia magumu kisha watumie ujumbe huu muhimu sana kwao, ambao unaweza kuyabadili maisha yao kwa kiasi kikubwa sana.

Stay-Strong-Never-Give-Up

Kwa kuanza, nikukumbushe hili muhimu rafiki yangu;

Siku utakayotangaza au kujiambia kwamba unataka kuwa na mafanikio kwenye maisha yako, unataka kufanya makubwa na kupiga hatua, itakuwa ndiyo siku umetangaza vita na dunia nzima.

Utakuwa umetangaza vita kubwa sana, ambayo kwa upande wako unakuwa mwenyewe, lakini upande wa pili kuna dunia nzima, kuanzia asili yenyewe, wale wanaokuzunguka na hata dunia nzima.

Unapochagua kufanikiwa, unakuwa umetangaza vita na wewe mwenyewe, umetangaza vita na ndugu, jamaa na marafiki, umetangaza vita na tv, redio, magazeti, facebook, instagram na kila aina ya chombo cha habari na mitandao ya kijamii.

Sasa vita hii haitakuwa rahisi, kwa sababu unaopambana nao, wana mbinu nyingi za kukurudisha nyuma.

Kama ni ndugu wa karibu na hata wazazi watakuambia usijiumize, endelea na maisha yako ya kawaida na usikazane na makubwa. Kwa upande wa  marafiki na jamaa watakuambia usikazane sana, ili usiwaache wao. Dunia itakuonesha kila aina ya hatari iliyopo mbele yako kwa kile unachojaribu, halafu vyombo vya habari na mitandao ya kijamii itakuwa inafanya kila hila ya kupumbaza akili zako, ili usiweke muda wa kutosha kwenye kile unachofanya.

Rafiki, unaona sasa jinsi vita hii ilivyo ngumu?

Sasa ugumu bado hatujaufikia, ugumu halisi unakuja hapa; UTASHINDWA, UTAANGUKA. Na hapo ndipo dunia itakapokucheka zaidi, ndipo watakuambia si tulisema, tulikuambua huwezi, tulijua utashindwa. Utakuwa na mashahidi wengi watakaotoa kila aina ya ushahidi dhidi yako, wakionesha jinsi ambavyo huwezi na utashindwa.

SOMA; Sababu Moja Kwa Nini Kanuni Ya Mafanikio Haifanyi Kazi Kwako, Na Jinsi Ya Kuitumia Vizuri.

Huu ndiyo wakati ambao unahitaji kuwa imara sana, unahitaji kuwa na kitu kikubwa kinachokufanya uendelee na mipango yako, licha ya kupitia wakati mgumu.

Ninachotaka kukuambia leo rafiki yangu ni hichi, kila mtu unayemwona amepiga hatua na kufanikiwa, jua alipitia wakati mgumu. Jua alikutana na changamoto kubwa ambazo ziliwakatisha tamaa wengine lakini yeye aliendelea kuweka juhudi.

Rafiki, changamoto unazokutana nazo ni faida kwako, kwa sababu changamoto hizi zinawazuia wale ambao hawajajitoa kweli kufanikiwa, hivyo unabaki na uwanja mpana wa kuweza kufanikiwa kama utaweza kuvuka magumu unayokutana nayo.

Rafiki, pale unapojiona kwamba umefika ukingoni, pale unapoona hakuna tena namba ya kuendelea, hapo ndipo unapaswa kuendelea zaidi. Pale unapoona umefika ukingoni, jiambie unahitaji kuweka juhudi kidogo zaidi ya wengine.

Angalia kwenye mashindano ya riadha, tofauti ya mshindi wa kwanza na wa pili huwa ni sekunde kadhaa tu, lakini zawadi zina utofauti mkubwa.

Kwenye chochote unachojaribu kufanya, utakutana na magumu, utakutana na changamoto kubwa, na watu watakuwa tayari kukuambia huwezi na utashindwa. Usikubali kumsikiliza yeyote anayekukatisha tamaa, na usikubali ugumu wowote uwe kikwazo kwako kupata unachotaka.

Ubishi, uvumilivu, ung’ang’anizi ni muhimu sana katika kufikia malengo makubwa uliyojiwekea. Na kila unaposhindwa shukuru, maana kwenye kila unachoshindwa kuna somo muhimu sana unalopaswa kujua ili kufanikiwa zaidi.

Nimalizie kwa kusisitiza hili rafiki, mambo hayatakuwa rahisi, na watu hawatakuachia kirahisi ufanye unachotaka kufanya. Unahitaji mtu mmoja tu wa kukuruhusu wewe ufanye unachotaka, na mtu huyo ni wewe mwenyewe. Maana ukishajiwekea wasiwasi wewe mwenyewe, kila utakapokutana na kushindwa utakimbilia kuacha na kukata tamaa. Lakini kama umejitoa, na hujui kuhusu kushindwa, dunia itakuacha upate unachotaka, na wale wanaokukatisha tamaa watakuwa mashabiki wako.

Endelea kupambana rafiki yangu, wakati mgumu haudumu, ni kipindi kifupi cha kujifunza na kuwa bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji