Rafiki yangu mpendwa,

Kama kuna kitu kikubwa sana nilichokuahidi basi ni kuandika kila siku.

Kwa mara ya kwanza kabisa nilianza kushirikisha mawazo yangu kwa njia ya maandishi zaidi ya miaka kumi iliyopita, mwaka 2007 wakati nipo kidato cha tano.

Baadaye nilifungua blog yangu ya kwanza mwaka 2009 ambayo sikuandika kwa muda mrefu. Baadaye mwaka 2010 na mwaka 2011 nilianzisha blog nyingine lakini hazikudumu kwa muda mrefu, zilipotea haraka.

Mwaka 2012 nilianzisha blog nyingine, nayo pia haikudumu muda mrefu. Ni mpaka mwaka 2013 nilipoanzisha AMKA MTANZANIA, ndipo niliamua kuweka umakini zaidi kwenye uandishi wangu. Na hapo ndipo nilipoanza kuona namna uandishi wangu unawasaidia wengi sana.

Mwaka 2014 nilianzisha KISIMA CHA MAARIFA, baada ya kuona wengi wanajifunza kwenye AMKA MTANZANIA, na bado wanataka zaidi. Hivyo KISIMA CHA MAARIFA ikawa ni sehemu ya kupata zaidi hasa mtu anaponufaika na makala anazosoma kwenye AMKA MTANZANIA.

Katika kipindi hicho cha uandishi nimeweza pia kuandika vitabu nane, ambavyo wengi wamekiri vimewasaidia sana. Vitabu kama KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIYO TAJIRI, BIASHARA NDANI YA AJIRA NA MIMI NI MSHINDI, vimekuwa msingi kwa wengi waliovisoma na kufanyia kazi yale waliyojifunza.

Japokuwa tangu mwaka 2013 nilikuwa naandika mara kwa mara, bado nilikuwa sijatengeneza kanuni muhimu ya uandishi. Nilikuwa naweza kuandika makala hata tano kwa siku moja, halafu zikapita siku tatu bila ya kuandika. Naweza kusema nilikuwa naandika pale ninapojisikia na nisipojisikia siandiki.

MIMI NI MSHINDI

Ni mpaka tarehe 01/01/2015 ndipo nilipoamua kuandika kila siku ambayo nitakuwa hai. Na katika kudhibitisha hilo, nilianzisha mfumo wa makala fupi za KURASA, ambapo kila siku mpya naandika ukurasa mpya na kuweka kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Kwa sasa ni zaidi ya kurasa 1280 ikimaanisha kwa siku zaidi ya elfu moja na mia mbili, nimeandika kila siku, bila kuacha hata siku moja, hata iweje.

Rafiki yangu, utanisamehe kwa utangulizi huo mrefu, najua umekuja hapa kwa sababu sana za mimi kuandika kila siku, lakini utangulizi huo ulikuwa muhimu ili tuwe sawa unapopitia sababu hizi saba za uandishi wangu.

Nakushirikisha sababu hizi saba kwa sababu mbili kubwa;

Moja wapo watu ambao wamekuwa wananilalamikia nawatumia email nyingi sana za makala ninazoandika, wapo ambao wanasema kwamba nawafanya washindwe hata kufanya kazi zao. Leo nitawapa jibu hapa na jinsi ya kuondokana na usumbufu wa mafunzo ninayotoa.

Mbili nimekuwa nawashauri sana watu waandike, kila mtu anapaswa kuandika, anapaswa kuwa na blog na anapaswa kuandika kitabu kuhusu maisha yake. Lakini wengi wamekuwa wanasema hawana muda au hawajui wanawezaje kuandika. Kupitia makala hii, naamini wengi wataweza kupata msukumo wa wao kuandika pia.

Rafiki, zifuatazo ni sababu saba kwa nini naandika kila siku na nitaendelea kufanya hivyo kwa kipindi chote cha maisha yangu;

  1. Kwa sababu kuna ukweli ambao umefichwa kwa muda mrefu.

Tumezaliwa na kukuzwa kwenye jamii ambazo zimekuwa zinaficha ukweli muhimu sana kuhusu maisha yetu na mafanikio. Karibu kila mmoja wetu amekuwa anaambiwa ni vitu gani hawezi kufanya au akifanya atashindwa.

Lakini hakuna mtu amewahi kuambiwa yapi makubwa anaweza kufanya na maisha yake, ambayo wengine hawawezi kabisa kuyafanya. Jamii imekuwa inatulazimisha tuwe kama wengine walivyo, ambayo ni kanuni ya uhakika ya kushindwa.

Naandika kila siku kukupa ukweli huu, kwamba WEWE NI WA KIPEKEE, WEWE UNA UWEZO MKUBWA SANA NDANI YAKO NA UNAWEZA KUFANYA MAKUBWA kuliko ambavyo umekuwa unaambiwa.

Nitakuandikia ukweli huu kila mara na kila unapokutana na kazi yangu, lazima nisisitize hilo. Unapaswa kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yako ili kuweza kufanikiwa kwenye maisha yako.

  1. Kwa sababu dunia itakuwa sehemu bora sana kupitia uandishi wangu.

Kama kila mmoja wetu ataanza kuishi uwezo mkubwa uliopo ndani yake, kama kila mmoja wetu atatumia utofauti aliozaliwa nao, dunia itakuwa sehemu bora sana kwa kila mmoja wetu.

Maisha yanakuwa magumu kwa wengi kwa sababu wanafanya vitu ambavyo hawavipendi au hawavijali kwa sababu tu wameambiwa ndivyo wanapaswa kufanya. Pale kila mtu anapofanikiwa, pale kila mtu anapopiga hatua, dunia inakuwa sehemu bora kwa kila mmoja wetu kuishi.

  1. Kwa sababu njia za zamani hazifanyi kazi tena.

Kama ulipata nafasi ya kusoma hata darasa moja, kuna wimbo ambao walimu wako na hata jamii ilikuwa inakuimbia. Soma kwa bidii, faulu, utapata kazi nzuri na kuwa na maisha bora. Na wengi wakafuata njia hiyo, wakakamilisha kila walichoshauriwa, lakini mwisho wa siku, matokeo yakawa tofauti na walivyoambiwa watapata.

Njia ya zamani, ya kusoma kwa juhudi, kufaulu basi watapata ajira ya uhakika na mafanikio makubwa, ni njia ambayo kwa sasa haifanyi kazi. Ni njia iliyopitwa na wakati na wengi wanateseka kwenye njia hiyo.

Moja ya vitu ambavyo nasisitiza na nimeandika kitabu kabisa kwenye eneo hilo ni kuwa na mifereji mingi ya kipato. Kama umeajiriwa unapaswa kuwa na njia nyingine za kukuingizia kipato. Kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA nimeeleza hayo kwa kina.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

  1. Kwa sababu uandishi wangu utawasaidia wengi.

Wachache wanaposema makala na vitabu ninavyoandika vimewasaidia, najua wapo wengi zaidi watanufaika na kazi hizi. Hivyo nitaendelea kuandika kila siku, kwa sababu najua kila atakayekutana na kazi zangu, na akachukua hatua, hatabaki pale alipo sasa.

  1. Kwa sababu nahitaji kutengeneza kipato.

Naweza kusema asilimia 99 ya uandishi ninaofanya ni bure kabisa, na asilimia 1 pekee ndiyo unayolipia. Lakini ukifikia hatua kwamba unapaswa kulipia, basi utalipia gharama ambazo kwako utaziona ni kubwa, tofauti na ulivyozoea kulipia maarifa mengine.

Natumia muda mwingi kujifunza, kujaribu vitu vingi na hata kuandika makala kama hizi ambazo kila mtu anaweza kusoma na kujifunza. Lakini pia muda ninaotumia kuandika ni muda ambao siwezi kuutumia kwa shughuli nyingine, hivyo lazima nipate kipato kwa muda na juhudi ninazoweka.

Kwa kusema hivyo, nikuambie tu kwamba, huduma zote ninazotoa, gharama zake zimeongezeka mara mbili. Kwa mfano KISIMA CHA MAARIFA ada ya kujiunga ilikuwa elfu 50, kuanzia sasa ni laki moja. Gharama za PERSONAL COACHING, GAME CHANGERS na LEVEL UP pia zimeongezeka mara mbili.

Na usiwe na shaka, huduma utakazozipata pale unapolipia zitazidi kuwa bora zaidi na zaidi.

  1. Kwa sababu nimechoma moto madaraja mengi nyuma yangu.

Kuna vitu vingi sana ambavyo nimekataa kufanya kwenye maisha yangu, ili nipate muda mwingi wa kufanya yale ninayotaka kufanya, niweze kutumia uwezo wangu mkubwa kufanya makubwa zaidi.

Vitu vingi sana ambavyo nilikuwa nafanya kwenye maisha yangu, na nafasi nyingine ambazo nilikuwa nazipata nimeachana nazo nyingi ili nipate muda na nguvu za kutosha ili kuweza kuandika.

Sasa kama nimejinyima na kukataa vitu vizuri kwangu, nikiacha kuandika hata siku moja, sitakuwa nimejitendea haki.

  1. Kwa sababu hamasa niliyonayo haiwezi kuzuilika.

Kila kitu ninachokutana nacho kwenye siku yangu, huwa najiuliza nimejifunza nini na mtu mwingine anaweza kujifunza nini, na hapo hapo naandika wazo hilo chini kwa ajili ya kuandika makala zaidi baadaye. Program ambayo naitumia kuandika mawazo haya ya uandishi kwa sasa ina mawazo zaidi ya elfu moja.

Hivyo nina mawazo mengi sana ya kuandika kiasi kwamba sijui kama nitaweza kumaliza kuandika yote. Hamasa ya mimi kuandika mawazo haya yote ni kubwa sana kiasi kwamba siwezi kuacha kuandika.

Rafiki yangu, hizi ndiyo sababu saba kwa nini naandika kila siku, na kwa nini nitaendelea kuandika kila siku ya maisha yangu. Kama unanufaika na uandishi ninaofanya, endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na fanyia kazi yale unayojifunza. Unapoyafanyia kazi na ukapata matokeo bora, karibu ulipie huduma zaidi ninazotoa ili uweze kufikia uwezo mkubwa zaidi uliopo ndani yako.

Karibu sana tuendelee kuwa pamoja rafiki yangu, na kama umesoma mpaka hapa, sina shaka kwamba kuna uliyoondoka nayo, basi nenda kayafanyie kazi.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji