Rafiki yangu mpendwa,

Moja ya hitaji muhimu sana la maisha ya mafanikio ni uhuru. Wale wanaofanikiwa ni wale ambao wapo huru zaidi na maisha yao.

Changamoto kubwa ni kwamba, watu wengi wanafikiri wapo huru, wakati kwa uhalisia hawapo huru. Kwa sababu unaambiwa upo huru, kwa sababu unaishi kwenye nchi yenye uhuru, haimaanishi kwamba lazima na wewe utakuwa huru.

Uhuru siyo kitu cha kupewa, bali kitu cha kupigania, kitu cha kutafuta, kitu cha kuchukua. Hutakuwa huru kama unawasubiria wengine wafanye kitu fulani ambacho unataka wafanye.

Ubaya zaidi kwenye zama hizi za taarifa, ndiyo wengi zaidi wamepoteza uhuru wao. Sasa hivi, mitandao ya kijamii ndiyo inaendesha maisha ya wengi. Mitandao hii ndiyo inatawala watu wafikirie nini, wapende nini, wale nini na hata wavae nini.

Mitandao hii ya kijamii imefikia hatua ya kuwasukuma watu wafanye vitu wasivyopenda, wasivyoweza na hata wasivyojali, ili tu waonekane nao wanafanya, waweze kuweka picha na kusema kwenye mitandao kwamba nao wanafanya.

Rafiki yangu, haya maisha bila ya kuwa na uhuru kamili, ni vigumu sana kufanikiwa. Kwa sababu kama hutakuwa huru, watu watakutumia wewe kama mtumwa wao, watakutumia kama mtu wa kuwafikisha kwenye ndoto zao na watakutumia wewe kama mteja wao.

MIMI NI MSHINDI

Hivyo rafiki yangu, uhuru mkubwa na wa kweli kabisa kwenye maisha yako, ni kuweza kujitawala wewe mwenyewe. Kiwango chako cha mafanikio kitaendana na jinsi unavyoweza kujitawala wewe mwenyewe.

Kama unaweza kujitawala wewe mwenyewe, ukajisimamia na kujiadhibu, basi utaweza kufanikiwa sana. Lakini kama huwezi kujitawala wewe mwenyewe, huwezi kujiadhibu, huwezi kujinyima, utaendelea kuwa mtumwa wa watu wengine na hutaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Yapo maeneo matatu muhimu sana ya kujitawala wewe mwenyewe ili uweze kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Eneo la kwanza ni fikra zako.

Hili ni eneo muhimu sana kwa sababu kama tunavyojua, unakuwa kile unachofikiri. Fikra zetu zina nguvu kubwa sana kwenye maisha yetu. Kila ambacho kinaendelea kwenye maisha yetu, ni zao la fikra zetu.

Kama hutaweza kutawala fikra zako, huwezi kuyatawala maisha yako. kama utaruhusu akili yako ibebe kila aina ya fikra, kama utaruhusu kila aina ya habari iingie kwenye akili yako, jua utaishia kuwa watumwa wa watu wengine.

Dhibiti sana fikra zako, kila unachofikiri, hakikisha ni wewe umechagua na kinachangia wewe kufanikiwa zaidi na siyo kukurudisha nyuma au kukujaza hofu zisizo muhimu.

Eneo la pili ni hisia zako.

Sisi binadamu ni viumbe wa kihisia, tunafanya maamuzi yetu kwa kusukumwa na hisia na siyo kwa kufikiri. Hivyo watu wanaotutaka tuchukue hatua fulani, huwa wanateka hisia zetu, ili tukimbilie kufanya maamuzi kabla hata hatujafikiri kwa kina.

Dhibiti sana hisia zako kama unataka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Na hisia zako kwa sehemu kubwa zitatokana na fikra unazokuwa nazo.

Ongozwa na hisia za upendo, matumaini na hamasa wakati wote. Kaa mbali na hisia za chuki, hasira na hata wivu, maana hizo zitakupelekea ufanye maamuzi ambayo baadaye utayajutia. Pia epuka sana hisia za tamaa, hizo zinatumiwa na watu ili kukufanya kuwa mtumwa wao.

SOMA; VIDEO; Sababu Moja Inayokuzuia Wewe Kufika Pale Unapotaka Kufika Kwenye Maisha Yako.

Eneo la tatu ni hatua unazochukua.

Hatua unazochukua ndiyo zinaleta matokeo unayopata, ndiyo zinaamua kiasi gani utafanikiwa au kutofanikiwa.

Lazima uweze kudhibiti hatua unazochukua kama unataka kufanikiwa kwenye maisha yako. Lazima hatua unachochukua ziwe zinakusogeza karibu na malengo yako makubwa.

Kama hutadhibiti hatua unazochukua, utajikuta unafanya mambo mengi kwenye siku yako, siku inaisha umechoka, lakini hakuna kikubwa ulichofanya. Kama hutadhibiti kipi unafanya na kipi muhimu zaidi, kila wakati utajikuta una mengi ya kufanya na ambayo siyo muhimu kabisa.

Dhibiti hatua unazochukua kwenye maisha yako na utaweza kupiga hatua kubwa kwa kuweka vipaumbele kwenye yale unayofanya.

Rafiki yangu, hayo ndiyo maeneo matatu muhimu ya kudhibiti kwenye maisha yako kama unataka kuwa na maisha yenye uhuru na mafanikio makubwa.

Kumbuka uhuru unatafutwa, uhuru unatengenezwa, uhuru unapiganiwa na uhuru unachukuliwa, hata siku moja uhuru huwa haupewi. Hivyo safari yako ya kuelekea kwenye uhuru na mafanikio haitakuwa rahisi, lakini uzuri ni kwamba utawezekana. Hivyo kazana kila siku kufikia uhuru mkubwa wa maisha yako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha