Rafiki yangu mpendwa,

Mafanikio ni matokeo ya hatua ambazo mtu unachukua. Upo hapo ulipo leo kwa sababu ya hatua ulizochukua jana na siku zilizopita. Hatua unazochukua leo ndiyo zinatengeneza matokeo yako ya kesho.

Hii ndiyo sababu nimekuwa nakusisitiza sana kufanya, haijalishi unajua kiasi gani, kama hufanyi, kujua kwako hakuna maana wala msaada kwako.

Pamoja na umuhimu wa kufanya na kuchukua hatua, siyo kila hatua ambazo watu wanachukua zinaweza kuwaletea mafanikio makubwa. Na ndiyo maana kuna watu wanaonekana wanaweka juhudi sana, lakini hawapati matokeo mazuri.

Kwenye makala hii ya leo tutajifunza ngazi nne za kuchukua hatua na kiwango halisi cha hatua unachopaswa kuchukua ili kufanikiwa.

MIMI NI MSHINDI

Kuna ngazi kuu nne zakuchukua hatua.

Ngazi ya kwanza; kutokuchukua hatua kabisa.

Hii ndiyo ngazi ya chini kabisa kwenye kuchukua hatua, ambapo mtu hakuna hatua yoyote anayochukua, licha ya kujua kwamba anapaswa kuchukua hatua. Hapa mtu anakaa tu, hakuna hatua yoyote anayochukua, na sababu kubwa inakuwa uzembe, uvivu na kukosa nidhamu.

Wale ambao wanaendesha maisha yao kwenye ngazi hii hakuna makubwa yanayotokea kwenye maisha yao, wanaendesha maisha kwa mazoea pekee na hawana msukumo wowote wa kupata mafanikio makubwa. Wengi wanaweza kuwa wamezungukwa na mazingira yanayowakatisha tamaa na ndiyo maana hawachukui hatua kabisa.

Ngazi ya pili; kuchukua hatua za kujilinda.

Ngazi ya pili ya kuchukua hatua ni kuchukua hatua za kujilinda. Hapa mtu anachukua hatua, lakini siyo za kupata kitu kipya, bali kuzuia kupoteza kile ambacho tayari mtu anacho. Kwenye uchukuaji huu wa hatua, mtu hajisumbui kujaribu mambo mapya, wala hana mpango mkubwa anaofanyia kazi. Ila inapotokea hatari ya kupoteza kitu ambacho tayari anacho, mtu anachukua hatua haraka kuepuka kupoteza alichonacho.

Wale wanaochukua hatua za kujilinda huwa hawapati mafanikio makubwa, kwa sababu wanachokwepa ni kupoteza, hivyo hata kama hawatapoteza kweli, bado hakuna hatua wamepiga. Wanazidi kurudi nyuma kwa sababu hawaendi mbele.

Ngazi ya tatu; kuchukua hatua za kawaida.

Hapa sasa ndiyo ngazi ambayo wengi wapo, kuchukua hatua za kawaida. Hapa mtu anafanya kile ambacho amezoea kufanya, kile ambacho kila mtu anafanya na kimezoeleka. Ukichukua hatua kwenye ngazi hii, hakuna unayemshangaza, maana kila mtu amezoea kiwango hicho cha hatua.

Ubaya wa kuchukua hatua kwenye ngazi hii ni kwamba huwezi kupata matokeo makubwa. Ukifanya kawaida unaishia kupata matokeo ya hovyo kabisa. Kwa sababu kama kila mtu anaweza na anafanya, matokeo utakayopata hayana cha kukutofautisha na wengine na hivyo yanakosa thamani.

SOMA; Mafanikio Makubwa Huwa Yanaenda Kwa Watu Wenye Sifa Hizi Saba, Zijue Na Ujijengee Ili Uweze Kufanikiwa Zaidi.

Ngazi ya nne; kuchukua hatua kubwa sana.

Hii ndiyo ngazi ya juu ya kuchukua hatua, ambapo mtu anachukua hatua kubwa sana kwenye maisha yake. Hapa mtu anachukua hatua ambazo hazijazoeleka, na yeye mwenyewe hajawahi kuzichukua. Katika ngazi hii ya kuchukua hatua, watu wanakuwa na hofu kubwa lakini wanachukua hatua licha ya hofu hizo.

Ngazi hii ya kuchukua hatua ndiyo inayoleta mafanikio makubwa, lakini siyo ngazi rahisi. Siyo ngazi rahisi kwa sababu watu wengi hawajazoea kuchukua hatua kubwa, hivyo unapoanza kuchukua hatua kubwa, unakuwa tishio kwao, hivyo watakupinga na kukukatisha tamaa. Pia unapochukua hatua kubwa, unajaribu mambo mapya na makubwa ambayo hujayazoea, hivyo unakuwa kwenye hatari kubwa ya kushindwa.

Hizi ndiyo ngazi nne za kuchukua hatua, kuanzia ya chini kabisa mpaka ngazi ya juu.

Kiwango sahihi kwako cha kuchukua hatua ili kufanikiwa.

Kama unachotaka kwenye maisha yako ni kupata mafanikio makubwa, basi unapaswa kujua kipi kiwango sahihi cha kuchukua hatua kwako, na kiwango hicho ni ngazi ya nne ambayo ni kuchukua hatua kubwa sana.

Chochote unachotaka kufanikiwa kwenye maisha yako, jiandae na chukua hatua kubwa sana. Angalia nini umezoea kufanya, angalia wengine wamezoea kufanya nini, kisha chukua hatua kubwa zaidi ya hapo, nenda hatua ya ziada, fanya vitu ambavyo havijazoeleka na havijawahi kuonekana.

Nimekuwa nasema, kama kwa unachofanya hakuna mtu anapata wasiwasi na wewe, anakuambia haiwezekani au utashindwa, basi hakuna makubwa unayofanya na mafanikio kwako yatakuwa ndoto.

Kiashiria kwamba unachukua hatua kubwa ni jinsi wengine wanavyokuchukulia. Kama watu wanakuchukulia kawaida, basi unachukua hatua za kawaida. Kama watu wanakushangaa, wanajaribu kukushawishi upunguze hatua unazochukua, wanakupa mifano ya walioshindwa, basi jua hapo upo kwenye njia sahihi ya mafanikio.

Kama unachofanya sasa hakuna wanaokushangaa, hebu jaribu kuanza kufanya mara kumi zaidi. Kila lengo unalofanyia kazi sasa, lizidishe mara kumi, na ongeza hatua unazochukua, ongeza mara dufu. Kabla hata hujaanza kupata matokeo makubwa, utaanza kupata fikra za tofauti ambazo zitakupa hamasa ya kuchukua hatua zaidi.

Mara zote chukua hatua kubwa kabisa, hicho ndiyo kiwango sahihi kwako kuchukua hatua na kitakachokufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji