Rafiki yangu mpendwa,

Watu wengi wanaosema wanataka kuingia kwenye biashara lakini hawajaingia, huwa wanatoa sababu mbalimbali kwa nini hawajaanza biashara. Na sababu inayoongoza kwa kutumiwa na wengi ni kukosekana kwa mtaji.

Watu wengi watakuambia wanapenda sana kuingia kwenye biashara lakini kikwazo ni mtaji. Wengine watakuambia kinachowazuia wasiweze kukuza biashara zao ni kukosekana kwa mtaji.

Ukweli ni kwamba, watu ambao wanataka kweli kuingia kwenye biashara, huwa wanaingia na hawakubali sababu yoyote iwarudishe nyuma. Hii ni kusema kwamba wale wanaokubali sababu yoyote iwazuie, wale wanaosema hawajaweza kuanza biashara kwa sababu fulani, hawajajitoa kweli kuingia kwenye biashara. Badala yake wanatafuta sababu itakayoficha kutokujitoa kwao, na sababu rahisi ni kukosa mtaji.

Kama mtu umejitoa kweli, na upo tayari kuingia kwenye biashara, na usiruhusu chochote kikuzuie, hakuna kinachoweza kukuzuia. Sababu ya mtaji wala haijawahi kuwa sababu halisi, kwa sababu wapo watu wengi sana walioweza kuanzisha na kukuza biashara zao wakiwa hawana kitu kabisa.

Lakini huenda umekuwa unajipa sababu hii ya mtaji kwa miaka mingi, leo nakwenda kuivunja sababu hiyo, kwa kukupa njia saba unazoweza kutumia kupata mtaji wa kuanza biashara hata kama huna pa kuanzia kabisa.

Jifunze njia hizi saba na angalia njia ipi ambayo unaweza kuitumia kwenye maisha yako ili uweze kuanzisha biashara yako na uweze kupata uhuru wa maisha yako.

Kabla sijaingia kwenye njia hizo saba, napenda nikukumbushe kitu kimoja muhimu sana, uvumilivu na subira inahitajika sana pale unapoanza biashara na hasa unapoanzia chini kabisa ukiwa huna mtaji. Mawazo ya kulala masikini na kuamka tajiri yafute kabisa, itakuchukua muda kuanza mpaka kukuza biashara yako. Usitafute njia ya mkato, maana nyingi zitaishia kukupoteza zaidi.

Tumia njia hizi saba kupata mtaji wa kuanza biashara hata kama huna kitu kabisa.

  1. Kuwa na njia nyingine ya kukuingizia kipato.

Kama huna mtaji mkubwa wa kuanza biashara, basi njia bora kabisa kwako ni kuanza biashara kama kitu unachofanya pembeni. Au kama biashara ndiyo kitu kikuu kwako, basi kuwa na shughuli nyingine inayokuingizia kipato.

Kwa wale ambao wameajiriwa, anza biashara ukiwa bado upo kwenye ajira yako. Anza biashara yako kama kitu cha pembeni, huku ukitumia akiba zako kama sehemu ya mtaji wa kuanza biashara, unaianza kidogo na kuendelea kuikuza.

Kwa wale ambao hawana ajira, angalia shughuli yoyote unayoweza kuwasaidia watu wakakulipa, huku ukiendelea kukuza biashara ya ndoto yako.

Changamoto kwenye kuanzisha na kukuza  biashara siyo tu kukosa mtaji wa kuanza, bali kupata fedha ya kuendesha maisha. Maana hakuna kosa wanalofanya wengi na linaloua biashara nyingi kama pale mfanyabiashara anapoitegemea biashara changa kama chanzo chake cha kipato.

Hivyo hata kama una mtaji wa kuanza biashara, usiitegemee biashara yako mwanzoni, hasa miezi sita mpaka mwaka mmoja tangu kuianza biashara hiyo. Hakikisha una njia nyingine ya kukuingizia kipato cha kuendesha maisha yako.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

  1. Punguza sana gharama za maisha.

Haijalishi hali ya mtu ni ngumu kiasi gani, kila mtu kuna fedha nyingi sana anapoteza kwa kufanya mambo ambayo siyo muhimu sana. Fedha ambazo watu wanatumia kwenye starehe mbalimbali, kununua nguo ambazo hata hawazivai sana, kutumia vilevi na hata kutoa michango ya sherehe mbalimbali, ni fedha ambazo mtu angeweza kuzitumia vizuri na akapata mtaji wa kuanza biashara.

Kama mambo yako ni magumu na huna mtaji wa kuanza biashara, anza sasa kwa kuondoa gharama ambazo siyo za muhimu sana kwako. Kama usipofanya kitu hutakufa, basi hupaswi kukifanya.

Hivyo kama unanunua nguo kwa sababu watu wananunua au kwa sababu ni sikukuu, kama unachangia sherehe mbalimbali, kama unatumia pombe au soda mara kwa mara na unasema huna mtaji wa kuanza biashara, nakuambia wewe ni mwongo. Unachokosa siyo mtaji, bali unakosa uthubutu, ndiyo maana unakazana kupoteza fedha ili ujiridhishe kwamba huna fedha.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE SMALL BUSINESS BIBLE (Kila Kitu Unachopaswa Kujua Ili Kufanikiwa Kwenye Biashara Ndogo).

  1. Uza kitu cha mtu mwingine.

Njia rahisi kabisa ambayo mtu yeyote anaweza kutumia kuingia kwenye biashara ni kutafuta kitu cha mtu mwingine na kukiuza. Kama huna pa kuanzia, huna mtaji na hujui ni biashara gani ufanye, angalia ni kitu gani umewahi kununua na kutumia kwenye maisha yako na kikawa na manufaa kabisa. pia kitu hicho iwe wengi hawajakijua vizuri.

Unaweza kuingia kwenye biashara kwa kuuza kitu hicho. Unachofanya ni kununua kimoja au vichache kisha kuuza moja kwa moja kwa wanaoweza kunufaika nacho. Au unaweza kuongea na mfanyabiashara anayeuza, ukamwambia unamletea wateja wa kitu hicho na yeye akulipe kwa kamisheni kutokana na mauzo anayofanya kupitia wewe.

Hii ni njia bora kabisa inayoweza kutumika na yeyote, angalia kile unachokijua na kukiamini hasa, kisha kiuze kwa wale kinaoweza kuwasaidia.

  1. Tumia taasisi zinazowezesha wanaoanza biashara.

Kuna taasisi mbalimbali na ambazo zinaendesha mashindano mbalimbali ya mawazo ya biashara kisha wazo bora linafadhiliwa au mwenye wazo anapewa mtaji wa kwenda kuanza  biashara yake. Tafuta taasisi za aina hii na peleka wazo lako la biashara.

Hapa unahitaji kuandika wazo lako vizuri, kuwa na sababu na tafiti za kutetea wazo lako na kulenga wateja halisi ambao wana shida dhahiri. Elewa vizuri wazo lako na weza kulitetea, na ukishirikisha wazo hilo kwenye taasisi nyingi, hutakosa wa kukufadhili au kukupa mtaji.

  1. Changisha kama watu wanavyochangisha fedha za sherehe.

Kama umewahi kuombwa kuchangia sherehe mpaka ukasema wacha tu nitoe ili kupunguza usumbufu, basi jua na wewe unaweza kuwachangisha watu fedha na ukapata mtaji wa kuanza biashara. Siyo kitu kilichozoeleka sana kwenye mazingira yetu, lakini ni kitu rahisia, ambacho kama utakuwa na ung’ang’anizi na ubishi kama wachangishaji wa sherehe, utapata michango mingi.

Cha kufanya ni kuandika vizuri wazo lako la biashara, kueleza ni kasi gani unahitaji ili kuanza, kisha kuorodhesha idadi ya watu unaowajua kwenye maisha yako, ambao wanaweza kuchangia kiasi kidogo kwenye biashara yako, weka kiasi wanachopaswa kuchangia kisha mfuate kila uliyemworodhesha na ongea naye kuhusiana na wazo hilo, huku ukimwonesha orodha ya watu wote unaolenga kuongea nao, na kama wapo ambao tayari wametoa anaweza kuona pia.

Tumia njia hii vizuri na utapata mtaji wa kuanza biashara yako.

  1. Kupata wawekezaji kwenye biashara yako.

Amini usiamini, wakati wewe una wazo la biashara lakini unasema huna mtaji wa kuanza, kuna watu wana fedha na hawajui wafanye biashara gani, au hata hawajui wafanye nazo nini. Ila watu wa aina hiyo wanaogopa kuwapa wengine fedha zao kwa sababu walishalizwa huko nyuma.

Unahitaji kutumia fedha za wengine kuanza biashara yako kama wewe huna pa kuanzia kabisa. Hapa unahitaji kuandika vizuri wazo lako la biashara, kisha kuchagua unahitaji kuwa na wawekezaji wangapi, na kiwango cha mtaji watakachochangia.

Wawekezaji hao utahitaji kuwajumuisha kwenye umiliki wa biashara kulingana na kiwango cha mtaji walichochangia.

Pia unaweza kuanzisha au kujiunga kwenye kikundi ambacho kila mtu anachangia kiasi fulani cha fedha kwa muda fulani na mkaweza kuanzisha biashara.

SOMA; USHAURI; Njia Tano Za Kupata Mtaji Wa Biashara Bila Ya Kuchukua Mkopo.

  1. Mkopo kutoka vyanzo mbalimbali.

Njia hii ya saba nimeiweka mwisho kabisa kwa sababu siyo njia ninayoshauri watu wanaoanza biashara kuitumia. Ni njia inayoweza kuwa rahisi kwa wengi kutumia, hasa wanaofanya kazi au wenye mali mbalimbali wanazoweza kuweka kama dhamana. Lakini fedha ya mkopo ni chungu sana, wakati unaanza biashara ambayo hujawa na uhakika nayo, unahitajika kulipa mkopo na riba, kabla hata hujaanza kupata faida.

Hivyo isiwe njia ya kwanza kwako kufikiria, lakini kama umejaribu njia nyingine na zimeshindikana, na unaweza kupata mkopo, na upo tayari kujitoa sana kuhakikisha mkopo huo unakuwa na manufaa kwako, basi unaweza kutumia njia hii.

Omba mkopo ukiwa umeshapangilia kila senti unayopata kwenye mkopo huo unaitumiaje. Kuwa na nidhamu sana, usitumie fedha hiyo ya mkopo kwenye kitu chochote nje ya biashara. Na pia usitumie fedha yote kwenye biashara, badala yake weka pembeni sehemu ya mtaji huo kama akiba ya kuiokoa biashara pale mambo yanapokwenda tofauti na ulivyotegemea.

Rafiki yangu, hizo ndiyo njia saba unazoweza kutumia kupata mtaji wa kuanza biashara hata kama huna pa kuanzia kabisa. Tumia njia hizo, jitoe kupambana, kuwa mvumilivu, kuwa king’ang’anizi na hakuna kitakachoweza kukuzuia kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.

Kila la kheri.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha