Rafiki yangu mpendwa,

Kila mtu anapoianza safari ya mafanikio, huwa anakuwa na malengo na mipango mikubwa sana.

Malengo hayo na mipango vinampa hamasa kubwa ya kuweka juhudi kubwa zaidi ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Juhudi hizi kubwa ambazo wengi wanaziweka mwanzoni zinawaletea mafanikio kwa kiwango kidogo, na tungetegemea mafanikio hayo madogo yawe ndiyo kichocheo zaidi cha mafanikio makubwa.

Lakini hicho siyo kinachotokea, wengi baada ya kupata mafanikio madogo wanashindwa kabisa kuendelea. Mafanikio madogo wanayokuwa wamepata yanakuwa sumu kubwa kwa mafanikio makubwa zaidi.

cropped-mimi-ni-mshindi

Wengi ambao hawajui sababu ya hili, hufikiri labda watu hao wamehujumiwa, au walipata mafanikio hayo kwa njia zisizo sahihi. Japo wapo wanaokuwa na sababu hizo, lakini wengi wanaopata mafanikio madogo na wanashindwa kupata mafanikio makubwa zaidi wanakuwa wanazuiwa na sababu kubwa tatu.

Sababu ya kwanza ni kulinda mafanikio waliyopata.

Mtu anapoanzia chini kabisa, akiwa hana chochote, anakuwa hana cha kupoteza. Hivyo anakuwa tayari kuchukua hatua ambazo zinaweza kuwa hatari sana, na hatua hizi ndiyo zinazomwezesha kupiga hatua kubwa.

Lakini anapopata mafanikio madogo, anaanza kulinda mafanikio yale yasipotee. Hivyo anaacha kuchukua hatua kama alizokuwa anachukua awali, anaogopa kujaribu mambo ambayo ni hatari ili kuepuka kupoteza kile ambacho ameshapata.

Kwa kuogopa kupoteza mafanikio madogo ambayo tayari mtu ameshayapata, ni sababu kubwa kwa wengi kushindwa kufanikiwa zaidi.

Kama ambavyo nimekuwa nakuambia kwa mfano wa mchezo wa mpira, kama timu itaingia uwanjani ikishambulia ina nafasi kubwa ya kupata magoli. Lakini timu unapoingia uwanjani kwa lengo la kuepuka kufungwa, haishindi na mara nyingi inaishia kufungwa.

Kuondokana na kikwazo hiki, endelea kuchukua hatua kama vile ndiyo siku ya kwanza. Usijiweke kwenye hali ya kulinda, bali mara zote kuwa kwenye hali ya kushambulia. Usiogope sana kupoteza kile ulichopata, kama ulipata kihalali basi jua hata ukipoteza utapata tena. Mafanikio makubwa yanahitaji kuendelea kuchukua hatua ambazo ni hatari, usiogope kuchukua hatua hizo.

SOMA; Sababu Hizi Saba Ndiyo Zinakuzuia Kupata Mafanikio Makubwa Licha Ya Wewe Kuwa Na Juhudi Kubwa Kwenye Kazi Zako.

Sababu ya pili ni mazoea.

Watu wanapoanza kitu kipya wanakuwa na hamasa ya kuweka juhudi, kujaribu vitu vipya, kuwa wabunifu na kwenda hatua ya ziada. Lakini wanapoanza kupata mafanikio madogo, wanaanza kufanya kwa mazoea. Wanaanza kujiona wameshaijua siri ya kupata wanachotaka. Wanaanza kujiona wao siyo wa kuteseka tena kama wale wanaoanza. Wanaanza kujiweka kwenye daraja la juu.

Na popote unapoona mtu aliyeanzia chini anajiambia ameshafika juu, kuwa na uhakika hapo ndiyo mwisho wa ukuaji wake, hawezi kwenda juu zaidi. Kwa sababu njia pekee ya kwenda juu ni kutokufika wakati ukajiambia tayari upo juu.

Hata kama umeshazoea kiasi gani, chukulia kila nafasi kama nafasi mpya kwako, jifunze, jaribu vitu vipya, nenda hatua ya ziada na hayo yatakuwezesha kupiga hatua zaidi.

Kuondokana na kikwazo hichi, kila siku kuwa mtu mpya, kuwa mtu unayeanza na kamwe usijiambie umefika kwenye kilele cha jambo lolote lile. Kila siku jifunze na kuwa tayari kufundishika na kila mtu. Usijipe madaraja yoyote, endelea kuweka juhudi kama vile ndiyo siku yako ya kwanza, na utaweza kupiga hatua zaidi.

Sababu ya tatu ni kusahau nafasi ya bahati.

Nimekuwa nakuambia kwamba bahati ni pale maandalizi yanapokutana na fursa, na hilo ni kweli. Lakini pia kwenye maisha yetu na kazi zetu, kuna vitu ambavyo huwa vinatokea ambavyo hatukutegemea kabisa vitokee na vinatuwezesha kupiga hatua zaidi. Vitu hivyo havikuwa kabisa kwenye mipango yetu, lakini kutokea kwake kunakuwa manufaa kwetu.

Chukua mfano labda umenunua kiwanja mahali kwa lengo la kuja kujenga baadaye, lakini muda mfupi baada ya kununua kiwanja kile, anakuja mwekezaji anahitaji eneo lile na yupo tayari kukulipa mara mbili ya fedha uliyonunulia. Hiyo kwa hakika ni bahati, kwa sababu hukuwa na mipango ya kupata mwekezaji wa kumuuzia.

Sasa wengi wamekuwa wanasahau nafasi ya bahati kwenye mafanikio yao na kuona kila kitu wamepata kwa ujanja wao wenyewe na juhudi zao. Wanaanza kuona kama wana uwezo mkubwa kuliko wengine. Kwenye mfano wa kiwanja hapo juu, mtu anaweza kuanza kujiambia alijua hilo litatokea, wakati hata hakuwahi kulifikiria.

Shida ya bahati ni kwamba, matokeo kama hayo yanapotokea, watu wanakazana kuyatengeneza zaidi, na hapo ndipo wanaposhindwa. Yaani kitu kinakuwa kimetokea kwa bahati, lakini mtu anajiambia ni kwa ujanja wake, na hapo anajaribu kutumia ujanja huo zaidi na ndipo anaposhindwa vibaya kabisa.

SOMA; Hii Ndiyo Njia Pekee Ya Kukuwezesha Wewe Kufanya Kazi Zaidi Ya Wengine Na Kufanikiwa Zaidi.

Kuondokana na kikwazo hichi, kumbuka siyo kila kinachotokea ni kwa ujanja na juhudi zako. Jua kuna vitu vingine vinatokea kama bahati na huwezi kuvirudia vikatokea kama vilivyotokea. Hivyo jua kipi kipo ndani ya uwezo wako kuathiri na kufanyia kazi na kipi ambacho kipo nje ya uwezo wako kisha uachane na vile vilivyo nje ya uwezo wako.

Rafiki yangu, usikubali kabisa mafanikio kidogo unayoyapata yawe kikwazo kwako kupata mafanikio makubwa zaidi. Kila siku mpya kuwa kama ndiyo unaanza upya safari yako ya mafanikio. Sahau kabisa mafanikio ya jana na leo anza upya. Kila siku kuwa tayari kujifunza na usijiambie kwamba tayari unajua kila kitu. Na mwisho kabisa, jua kuna vitu vinatokea kwa bahati, usichanganye bahati hizo na ujanja au juhudi zako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Usomaji