Rafiki yangu mpendwa,

Udhibiti ni kitu ambacho kila mmoja wetu anapenda kuwa nacho. Tunapenda kuyadhibiti mazingira yetu, tunapenda kudhibiti wengine na tunataka kila kitu kiende kama tunavyotaka sisi wenyewe.

Na kwa hakika, hitaji hilo la udhibiti limewaumiza wengi sana. Kwa sababu hakuna kitu chochote kinachoweza kwenda kama ambavyo mtu unataka. Wewe unapanga hivi na yanayotokea ni mengine.

Sisi binadamu tuna udhibiti mdogo sana kwa kitu chochote ambacho kipo nje ya uwezo wetu. Kuanzia mazingira yetu, wale wanaotuzunguka na hata matokeo tunayotegemea kupata.

Hivyo jitihada zozote ambazo mtu unaweza kuamua kuweka kutaka kudhibiti vitu, ni jitihada ambazo unapoteza, na kama ungejua eneo sahihi la kuelekeza jitihada hizo, ungeweza kupiga hatua kubwa sana.

Leo nakwenda kukushirikisha maeneo matatu pekee unayoweza kuyadhibiti utakavyo kwenye maisha yako na ukaweza kupiga hatua kubwa sana kimafanikio. Kila unaposumbuka na udhibiti wa wengine, mazingira na hata matokeo unayotaka, jikumbushe ni upotevu wa jitihada na rudi kwenye yale maeneo matatu unayoweza kudhibiti.

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO

Eneo la kwanza; fikra zako.

Unakuwa kile unachofikiri, huu ni msingi ambao falsafa na dini zote zinakubaliana. Kwamba zile fikra zinazotawala akili yako, ndiyo mambo yanayotokea kwenye maisha yako.

Fikiria kushindwa mara zote na kila wakati utakutana na kushindwa. Fikiria ushindi mara zote na kila wakati utakutana na ushindi. Jiambie una kisirani au bahati mbaya na kila utakachofanya kitaishia kuleta matokeo mabaya.

Fikra zako ni eneo muhimu la maisha yako ambalo unaweza kulidhibiti wewe mwenyewe. Japo wengi watajaribu kukujengea fikra fulani zisizokuwa na manufaa kwako, bado unaweza kuzikataa na ukajenga fikra zenye manufaa kwako.

Usiruhusu kila aina ya fursa iingie na kutawala akili yako. Fikiri kile unachofikiri, usikubali fikra hasi zikatawala akili yako. Iweke akili yako bize kwa fikra chanya, fikra za mafanikio na hayo ndiyo yatakayotokea kwenye maisha yako.

Una uhuru wa kuchagua nini unataka kufikiria, kwa nini uutumie vibaya kwa kuruhusu fikra za hovyo kutawala akili yako? Shika udhibiti wa fikra zako na utaweza kuyadhibiti maisha yako.

SOMA; Hii Ndiyo Hofu Mbaya Uliyojitengenezea Wewe Mwenyewe Ambayo Inakutesa Na Kukuzuia Kuwa Na Maisha Bora.

Eneo la pili; mtazamo wako.

Mtazamo ulionao kwenye maisha yako, ni kitu ambacho unaweza kukidhibiti. Japokuwa sehemu kubwa ya mtazamo ulionao umejengewa na wengine, lakini bado ni eneo ambalo unaweza kushika udhibiti wake na ukatengeneza mtazamo ambao unakupa yale matokeo unayoyataka.

Ni wewe pekee unayechagua kama utakuwa na mtazamo chanya au mtazamo hasi kwenye maisha yako.

Ni wewe pekee unayeamua uwe na mtazamo wa ushindi au mtazamo wa kushindwa.

Japo wapo watu wanaokushawishi kwenye kujijengea mitazamo hiyo, lakini kama wewe hutatoa ruhusa, hakuna anayeweza kujenga au kubomoa mtazamo wako.

Kwa kuwa una uhuru wa kuchagua na kuweza kudhibiti mtazamo wako, hakikisha unajijengea mtazamo chanya, mtazamo wa ushindi. Ondoa kabisa kila aina ya mtazamo hasi, kaa mbali na wale wanaokujenga mtazamo wa kushinda na yaepuke mazingira yanayokwenda kinyume na kile unachotaka.

Kagua sana aina ya marafiki unaowaruhusu waingie kwenye maisha yako, achana kabisa na habari za udaku, umbea na habari zozote hasi. Ishi maisha yako kwa mipango yako na siyo kwa msukumo wa wengine.

Unao uhuru wa kuchagua na kudhibiti mtazamo wako, usiruhusu yeyote akujengee mtazamo utakaokuzuia usifanikiwe.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; 12 RULES FOR LIFE (Sheria 12 Za Maisha, Mbadala Wa Machafuko).

Eneo la tatu; hatua unazochukua.

Hatua unazochukua ni kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako na unaweza kukidhibiti utakavyo. Unaweza kuchagua kuchukua hatua kubwa na ukaweza kupata matokeo bora kabisa. Lakini pia unaweza kuchagua kuchukua hatua ndogo au za kawaida na ukapata matokeo ya kawaida, ambayo wengine wanapata pia.

Unaweza kudhibiti hatua unazochukua, lakini matokeo utakayopata huwezi kuyadhibiti. Hivyo badala ya kupoteza muda na nguvu zako kwenye kutaka matokeo fulani ndiyo uyapate, weka nguvu hizo kwenye kuchukua hatua kubwa zaidi. Matokeo yatakuja kama yanavyokuja, lakini juhudi chagua kuweka kubwa.

Chochote unachofanya, usifanye kwa ukawaida, usifanye kama vile hutaki, fanya au usifanye. Chagua kufanya kitu kwa kuchukua hatua kubwa, au kama huwezi kuchukua hatua kubwa ni bora usifanye kabisa.

Hatua unazochukua zipo ndani ya udhibiti wako, mara zote kazana kuchukua hatua kubwa.

Rafiki yangu, kila mara unapotamani kwamba ungeweza kuwadhibiti wengine, kila unapofikiria labda mazingira yangekuwa tofauti, kila unapotamani matokeo yangekuja kama unavyotaka, jikumbushe kwamba hayo yote yapo nje ya udhibiti wako. Na jikumbushe vitu vitatu pekee ambacho vipo ndani ya udhibiti wako ambavyo ni FIKRA, MTAZAMO NA MATENDO. Weka nguvu zako kwenye maeneo hayo matatu na hutahitaji kujali sana kuhusu mazingira, matokeo au wengine wanafanya nini.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL